BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM
KUITAFAKARI QURANI
Kuna mambo matatu yanayosaidia kufanya tafakuri sahihi. La kwanza: kuyafikiria maisha ya kupita na mafupi ya hapa duniani na kuepukana na matazamio ya muda mrefu. La pili: kuizingatia Qur'an. la tatu: kuepuka madhambi yanayoudhuru moyo. Kuutambua muda mfupi wa maisha haya ya dunia na kuutambua ukaribu wa mtu na mauti ni mambo yanayounufaisha mno moyo na kumpa muumini msukumo wa kuutumia kwa manufaa kila muda wa maisha yake. Muumini huyu huelekeza mazingatio na tamaa yake katika Makazi ya Milele.
Hii humpa hamasa ya kufidia kile kinachokosekana katika maandalizi ya safari na kumfanya ajizuie kutamani starehe za maisha haya mafupi. Iwapo mtu atadumu na tafakuri hii, basi itamuwezesha kuuona undani halisi wa maisha haya. Ataona jinsi hicho kinachoachwa kilivyo kidogo kuliko hata kile kinachosalia kidoleni kwa mtu pale kidole hicho kinapochovya bahari ambapo bahari ndiyo Maisha ya Milele ya Akhera.
Jua la dunia hii ndio hilo limezama tena na kana kwamba linazamia chini ya vilele vya milima. Hali na dalili zilizobashiriwa pale zifikapo zama za mwisho zimejitokeza. Mauti na wewe ni kama marafiki wawili walionjiani kwenda kukutana ambapo muda wowote mtakutana na kukumbatiana. Itoshe basi kuyakumbuka maneno haya ya MwenyeziMungu; -"Na (wakumbushe) siku atakayowakusanya (waone) kama kwamba hawakukaa (duniani) ila saa moja tu ya mchana...." (10:45). -Siku watakapokiona (Kiama) watakuwa kama kwamba hawakukaa (ulimwenguni) ila jioni moja au mchana wake (kwa kishindo kitakachowafika)." (79:46).
Siku litakapopigwa baragumu na Tukawakusanya wakosa siku hiyo, hali macho yao yatakuwa ya buluu (kwa hofu), watanong'onezana wao kwa wao (wakisema): "hamkukaa (ulimwenguni) ila siku kumi tu. Sisi Tunajua sana watakavyosema, watakaposema wabora wao katika mwendo: "nyinyi hamkukaa ila siku moja" (20: 102-104). Wakati mmoja Mtume wa Allah aliwaambia Maswahaba pale jioni ilipokuwa inakaribia kuingia na jua likiwa juu ya milima, "(Muda) uliobaki katika dunia hii kulinganisha na ule uliopita si chochote ila ni kama muda uliosalia wa siku ya leo kulinganisha na muda uliopita." (Ahmad).
Kuitafakari Qur'an
Tafakuri ya Qur'an hutekelezeka pale moyo unapoona maana ya maneno yake, na akili inapozingatia maana na lengo la kufunuliwa kwake. Usomaji mtupu wa Qur'an usiokuwa na mazingatio hautoshi (hauleti tija). MwenyeziMungu Anasema: -"(Na hiki) Kitabu; Tumekiteremsha kwako chenye baraka nyingi ili wapate kuzitafakari Aya zake na wenye akili wawaidhike" (38:29).
-"Je! Hawaizingatii hii Qur'an? Au katika nyoyo zao kuna kufuli?" (47:24)
-"Tumeifanya katika Lugha ya Kiarabu ili upate kuielewa." Al-Hasan aliisherehesha Aya hii hivi: "Ameifunua Qur'an ili itafakariwe na kuzingatiwa na kutekelezwa." Hakuna jambo lenye faida kwa mja wa Allah katika maisha ya dunia na Akhera kama kuyatia akilini maneno ya MwenyeziMungu, kuyatafakari kwa muda mrefu, kuhudhurisha kichwa (fikra), moyo (hisia, hamasa na mapenzi) katika maneno haya.
Tafakuri hii juu ya maana ya aya za Qur'an inampatia mtu elimu sahihi (tami'izi) ya kupambanua wema na uovu (haki na batili), inampatia elimu ya chimbuko la wema na uovu (haki na batili), njia zake na matokeo yake. Tafakuri hii ndiyo inayojenga msingi wa ngome ya Imani katika moyo wa mtu, ndiyo inayoinua kuta na kuimarisha nguzo zake. Tafakuri ya Qur'an ndiyo inayomuonesha mtu picha ya Pepo na Moto, inamuonesha yote yaliyomo humo kana kwamba yumo ndani ya jumba la makumbusho ya historia ya mwanadamu), inamuonesha kaumu zilizopita na watu wake na inaweka wazi masiku yao ya furaha na huzuni, inamuonesha mafundisho makubwa yaliyofichikana katika matukio na kumfanya atambue uadilifu na Rehema za MwenyeziMungu juu ya waja Wake.
Tafakuri hiyo ndiyo inayomwambia mtu habari za MwenyeziMungu, Majina Yake, Sifa Zake na Mambo yake. Ndiyo inayomuonesha mtu njia ya kumfikisha kwa MwenyeziMungu na inayomuonesha malipo yanayomsubiri yule anayepita njia hiyo kwa mafanikio. Inamtahadharisha juu ya wadanganyifu na misukosuko ya njia hiyo. Kwa ufupi wa maneno, tafakuri juu ya maana ya Qur'an ndiyo inayompatia mtu elimu sahihi juu ya MwenyeziMungu, njia ya kumfikisha Kwake, na Malipo makubwa ambayo Mola wake amemuandalia.
Inamjuza mtu kule anakoitia Shetani na njia inayomfikisha mtu huko na hizaya na adhabu iliyopo katika njia hiyo. Ni muhimu kwa mja kujua na kutafakari mambo haya tisa:
1. Kuitafakari Qur'an kunamuonesha mtu Akhera kama vile anaiona kwa macho yake na huishusha thamani dunia machoni mwake kama vile hayuko duniani.
2. Tafakuri ya Qur'an inampa mtu tamiizi ya kupambanua haki na batili katika kila jambo lenye khitilafu katika dunia hii, inamuonesha kuwa haki ni haki na batili ni batili.
3. Ujumbe wa Qur'an unavinjari katika dhana ya Tauhiid, dalili na ishara zake pamoja na Sifa nyinginezo za MwenyeziMungu ambapo zote hizo zikibainisha ukamilifu na ukwasi- kwamba Allah ni wa pekee (hana mfano).
4. Aidha tafakuri hiyo inajumuisha elimu ya kuwajua Mitume, dalili za ukweli wao, na haki zao kwa walimwengu ambao wanapaswa kuwaheshimu na kuwafuata.
5. Inazungumzia imani juu ya Malaika na Siku ya Mwisho.
6. Inazungumzia Uzito na ujio usioepukika wa Siku ya mwisho ambayo itaandamana na adhabu ya milele kwa baadhi ya watu na starehe na furaha ya milele kwa wengine.
7. Ujumbe wa Qur'an unamwita mja katika njia ya kumwelekea Mola wake kwa ahadi nono na unamtahadharisha juu ya adhabu. Qur'an inamvusha mtu katika njia zenye farka za rai (araa) na njia nusu-nusu, njia finyu za ndani ya Uislamu na nje yake na kumfikisha katika njia sahihi.
8. Ujumbe wa Qur'an unamkinga mtu dhidi ya njia za bidaa na upotevu. Unamuhimiza awe hadhiri katika kumshukuru Mola Wake mtukufu na kumlinda katika misukosuko na matatizo anayoweza kukumbana nayo katika njia ya Allah.
9. Ujumbe huu unamwita wakati wote, "sikiliza! Sikiliza! Shikamana na MwenyeziMungu, na muombe msaada...na sema, "Anatutosha MwenyeziMungu, naye ndiye Mlinzi bora aliyetakasika kabisa hasiye mshirika.
MWISHO