BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
UHUSIANO BAINA YA UFALME NA HEKIMA ZA MWENYEEZI MUNGU
* Milki na ufalme wa Mwenyeezi Mungu uko katika hali gani?.
* Kuna uhusiano gani baina ya milki (ufalme) na hekima za Mwenyeezi Mungu?.
* Ufalme wa Mwenyeezi Mungu umedhihirika vipi katika uumbaji wake?.
* Hivi kweli hekima za Twaaghuuti na hekima za Mwenyeezi Mungu zisizo mpaka zinaendana sambamba?.
MILKI (UFALME) NA HEKIMA ZISIZO MPAKA ZA MWENYEEZI MUNGU (S.W.).
Milki na ufalme wa viumbe vyote duniani ni wa Mwenyeezi Mungu (s.w), na viumbe vyote duniani viko chini ya ufalme wake Yeye Mola Muwezi, hata mali na vitu vyote vinavyomilikiwa na wanaadamu ni amana kutoka kwake Yeye Allah (s.w). Kwa hiyo vitu vyote vinavyomilikiwa na wanaadamu kiuhakika sio milki yao, kwani milki ya uhakika ni yake Yeye Allah (s.w).
Milki na hekima isiyo mpaka ya Mwenyeezi Mungu ni dhati na ya uhakika, na vitu vyote duniani vilivyo na akili na visivyo na akili vinatii na kuheshimu amri zake Allah (s.w).
Kuna dalili nyingi zilizo wazi zinazothibitisha hekima za Mwenyeezi Mungu, na Yeye ndiye muaminifu katika kuhukumu kutokana na kanuni hizo. Na hii ni kwa sababu Mwenyeezi Mungu ni mwenye kujua uhakika na siri zote katika dunia, na anajua yale anayoyahitajia mwanaadamu katika maisha yake.
UFAFANUZI WA NENO MILKI NA HEKIMA:
Neno milki lina maana ya ufalme, na maana asili ya neno hilo ni kuwa na nguvu na kudra ya kilakitu.
Neno maalik, baadhi ya wakati lina maana ya mwenye nguvu na kudra ya mali. Mfano katika aya hii tukufu, Allah (s.w) anasema:-
اَوَلَمْ يَرَوْا اَنَّا خَلَقْنَا لَهُمْ مِمَّا عَمِلَتْ اَيْدِينَا اَنْعَاماً فَهُمْ لَهَا مَالِكُونَ[1]
Je! Hawaoni kwamba tumewaumbia kutokana na iliyo fanya mikono yetu wanyama wa mifugo, na wao wakawa wenye kuwamiliki.
Na baadhi ya wakati neno hilo lina maana ya mwenye uwezo na qudra katika kuhukumu kwa kila analolitaka , kama tunavyosoma ndani ya Qur-ani:-
قُلِ اللهُمَّ مَالِكَ الْمُلْكِ تُؤْتِى الْمُلْكَ مَن تَشَاء وَتَنزِعُ الْمُلْكَ مِمَّن تَشَاء وَتُعِزُّ مَن تَشَاء وَتُذِلُّ مَن تَشَاء بِيَدِكَ الْخَيْرُ إِنَّكَ عَلـٰيَ كُلِّ شَيْءٍ قَدِير[2]ٌ
Sema: Ewe Mwenyezi Mungu uliye miliki ufalme wote! Wewe humpa ufalme umtakaye, na humwondolea ufalme umtakaye, na humtukuza umtakaye, na humuangusha umtakaye. Kheri yote iko mikononi mwako.Hakika Wewe ni Muweza wa kila kitu.
Maana asili ya neno hukumu ni kuzuilia.
Hakimu huitwa yule mtu ambaye kutokana na hukumu anayoitoa au kumhukumu mtu, huwazuilia watu mahalifu kutokufanya mambo yanayoleta khilafu katika jamii. Kama inavyosema Qur-ani tukufu:-
سَمَّاعُونَ لِلْكَذِبِ اَكَّالُونَ لِلسُّحْتِ فَإِن جَآؤُوكَ فَاحْكُم بَيْنَهُم اَوْ اَعْرِضْ عَنْهُمْ وَإِن تُعْرِضْ عَنْهُمْ فَلَن يَضُرُّوكَ شَيْئاً وَإِنْ حَكَمْتَ فَاحْكُم بَيْنَهُمْ بِالْقِسْطِ إِنَّ اللّهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ[3]
Hao ni wasikilizaji kwa ajili ya kusema uwongo, na ni walaji mno vya haramu! Basi wakikujia, wahukumu baina yao au jipuuze nao. Na ukijipuuza nao, basi wao hawatakudhuru kitu. Na ukiwahukumu, basi hukumu baina yao kwa uadilifu. Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda waadilifu.
*Wakati mwengine huja Mayahudi hao kwa Mtume ati awahukumu yeye katika kesi zao, kwa kuwa yeye atawahukumu bila ya kuwapendelea – wala sio madhumuni ya hayo, basi anapewa Mtume hiyari hapa, kuwa akitaka awahukumu, na akitaka anaweza kuwakatalia, kwani sio makusudio yao kutaka la haki, wanataka wapate la takhfifu tu ijapokuwa silo.
UTUKUFU , MILKI NA HEKIMA ISIYO MPAKA YA MWENYEEZI MUNGU KATIKA NIDHAMU ZA KIMAUMBILE.
Kuumbwa na kubakia kwa vitu vyote duniani kunatokana na ufalme wake Allah (s.w), na kitu chochote kilichomo duniani kikiwa kimefichika au kimedhihirika, kikubwa au kidogo, vyote hivyo vimeumbwa na kumilikiwa na Allah (s.w). kama anavyosema Mwenyeezi Mungu Mtukufu:-
قُلِ ادْعُوا الَّذِينَ زَعَمْتُم مِّن دُونِ اللهِ لاَ يَمْلِكُونَ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ فِى السَّمَاوَاتِ وَلاَ فِى الاَرْضِ وَمَا لَهُمْ فِيهِمَا مِن شِرْكٍ وَمَا لَهُ مِنْهُم مِّن ظَهِيرٍ[4]
Sema: Waite mnao wadaia kuwa ni badala ya Mwenyezi Mungu. Hawamiliki hata uzito wa chembe hichi katika mbingu wala ardhi. Wala hawana ushirika wowote humo. Wala Yeye hana msaidizi miongoni mwao.
Milki na hekima isiyo mpaka ya Mwenyeezi Mungu imeenea katika nidhamu ya kimaumbile. Kama anavyosema Allah (s.w):-
إِنِّى تَوَكَّلْتُ عَلـٰي اللهِ رَبِّى وَرَبِّكُم مَّا مِن دَآبَّةٍ إِلاَّ هُوَ آخِذٌ بِنَاصِيَتِهَا إِنَّ رَبِّى عَلـٰي صِرَاطٍ مُّسْتَقِي[5]مٍ
Hakika mimi nimemtegemea Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wangu na Mola Mlezi wenu. Hapana kiumbe yeyote ila Yeye anamwendesha atakavyo. Hakika Mola wangu Mlezi yuko juu ya Njia Iliyo Nyooka.
* Nabii Nuhu (a.s) anawabainishia kuwa hao wanaowaabudu hawana lao jambo – hawawezi kudhuru wala kunufaisha. Na anawatia mori wamdhuru kama wataweza, na wewe wachalleng wanaokutishia kwa mizimu yao na mapango yao… wala usiogope.
[1] Surat Yaasin Aya ya 71
[2] Surat Al-Im-rani Aya ya 26
[3] Surat Al-Maidah Aya ya 42
[4] Surat saba Aya ya 22
[5] Surat Hud Aya ya 56
MWISHO