MWENYEEZI MUNGU NI WALII KWA WAJA WOTE
  • Kichwa: MWENYEEZI MUNGU NI WALII KWA WAJA WOTE
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 17:18:15 1-9-1403

 KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

MWENYEEZI MUNGU NI WALII KWA WAJA WOTE

Uwalii wa Mwenyeezi Mungu kwa waja wote, na uwalii Wake kwa waja makhsusi na maalumu.

Mwenyeezi Mungu Mtukufu aliyeumba vitu na viumbe vyote duniani ndiye Walii na mlinzi wa kuongoza na kusimamia mambo ya viumbe wote duniani, na Mwenyeezi Mungu ndiye Mlinzi wa kuwasimamia waja hao, hakuna shaka kuwa nidhamu ya kimaumbile na kuendelea kwa maisha ya wanaadamu iko chini ya ulinzi wake Allah (s.w), na ulinzi huo huitwa (wilayat takwiniyah) – yaani uwalii wa kimaumbile - Na uwongofu wa wa wanaadamu unaonyesha (wilayat tashriiyyah) – yaani uwalii usio wa kimaumbile – Mwenyeezi Mungu huwapa waja wake wote wilayat tashriiyah, yaani Mwenyeezi Mungu huwaongoza na kuwasimamia waja wake wote, na uwalii huu ni manufaa kwa waja wote duniani. Isipokuwa kwa baadhi ya wale ambao waliochagua chaguo baya katika kumchagua Mola wao. – yaani wanaabudu asiyekuwa mola anayestahiki kuabudiwa – na wakamfanya mungu wao huyo ndiye muongozi na msimamizi wa mambo yao. Kama anavyosema Allah (s.w):-

اَمِ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ اَوْلِيَاء فَاللهُ هُوَ الْوَلِيُّ وَهُوَ يُحْيِى المَوْتَي وَهُوَ عَلـٰي كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ[1]

Au wamechukua walinzi wengine badala yake! Lakini Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi khasa. Na Yeye ndiye anaye huisha wafu. Na Yeye ndiye Mweza wa kila kitu.

Ama kwa wale ambao wamemchagua Mwenyeezi Mungu wa haki kuwa ni Mola wao na msimamizi wao anayeweza kuwaongoza katika maisha yao, na wakabakia katika imani yao hiyo, ijapokuwa hawataamini uwalii wake Mwenyeezi Mungu kwa dalili mbali mbali ikiwa kwa kughafilika au kwa sababu nyengine yoyote ile,Mwenyeezi Mungu huwapa rehema watu hao, na huwaondoa katika giza la kijahili, na huwaokoa na kuwaepusha na kufanya maasi, na huwaonyesha nuru inayowaongoza wao katika imani. Huu basi huitwa uwalii wa Mwenyeezi mungu anaowajaalia waja wake makhasusi, kama inavyosema Qur-ani takatifu:-

اللّهُ وَلِيُّ الَّذِينَ آمَنُواْ يُخْرِجُهُم مِّنَ الظُّلُمَاتِ إِلَي النُّوُرِ وَالَّذِينَ كَفَرُواْ اَوْلِيَآؤُهُمُ الطَّاغُوتُ يُخْرِجُونَهُم مِّنَ النُّورِ إِلَي الظُّلُمَاتِ اُوْلَـئِكَ اَصْحَابُ النَّارِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ[2]

Mwenyezi Mungu ni Mlinzi wa walio amini. Huwatoa gizani na kuwaingiza mwangazani. Lakini walio kufuru, walinzi wao ni Mashet'ani. Huwatoa kwenye mwangaza na kuwaingiza gizani. Hao ndio watu wa Motoni, na humo watadumu.

Uwalii wa Mwenyeezi Mungu na uwalii wa shetani (iblisi).

Mwenyeezi Mungu ameumba viumbe wake, na akaweka nidhamu katika dunia, na kuwapa wanaadamu nguvu na uwezo utakaowafikishia wao kufanikiwa katika mambo yao, na akampa mwanaadamu hiyari ya kuchagua katika mema na mabaya, na kushukuru au kukufuru. Baadhi ya wanaadamu wenye imani kwa kuukubali uwalii wa Mwenyeezi Mungu na kumshukuru katika neema zake wamefanikiwa na wako katika himaya yake yeye Allah (s.w). Qur-ani takatifu inasema kumwambia Mtume Muhammad (s.a.w.w).

قُلْ اَغَيْرَ اللهِ اَتَّخِذُ وَلِيّاً فَاطِرِ السَّمَاوَاتِ وَالاَرْضِ وَهُوَ يُطْعِمُ وَلاَ يُطْعَمُ قُلْ إِنِّيَ اُمِرْتُ اَنْ اَكُونَ اَوَّلَ مَنْ اَسْلَمَ وَلاَ تَكُونَنَّ مِنَ الْمُشْرِكَينَ[3]

Sema: Je, nimchukue rafiki mlinzi asiye kuwa Mwenyezi Mungu, ambaye ndiye Muumba mbingu na ardhi, naye ndiye anaye lisha wala halishwi? Sema: Mimi nimeamrishwa niwe wa kwanza wa wenye kusilimu. Na wala kabisa usiwe miongoni wa washirikina.

*Hapa wanazinduliwa wale wanaowacha kumuabudu Mwenyeezi Mungu Ambaye baadhi ya sifa zake ni hiyo iliyo katika Aya ya 13, wakaomba mizimu na mapango na makaburi na mapepo, yana jambo gani hayo mapepo, si upotofu wa akili tu huo? Bali na ukafiri pia kuwaomba. Mwislamu kamili hasubutu kusema hivi. Kufanya hivyo ni namna ya ushirikina, basi na tujiepushe na chembe hii ya ushirikina.

Na Mwenyeezi Mungu huwasaidia waja wake kupitia waja wake waumini, kama anavyosema Allah (s.w):-

وَإِن يُرِيدُواْ اَن يَخْدَعُوكَ فَإِنَّ حَسْبَكَ اللّهُ هُوَ الَّذِيَ اَيَّدَكَ بِنَصْرِهِ وَبِالْمُؤْمِنِينَ[4]

Na wakitaka kukukhadaa basi Mwenyezi Mungu atakutosheleza. Kwani Yeye ndiye aliye kuunga mkono kwa nusura yake na kwa Waumini.

Ama ikiwa baadhi ya wanaadamu watamkufuru Mwenyeezi Mungu na hawataukubali uwalii na ulinzi wa Mwenyeezi Mungu, Mwenyeezi Mungu ameiumba dunia katika nidhamu ambayoitawapelekea watu hao kukumbwa na adhabu ya shetani, kama anavyosema Allah (s.w):-

اَلَمْ تَرَ اَنَّا اَرْسَلْنَا الشَّيَاطِينَ عَلـٰي الْكَافِرِينَ تَؤُزُّهُمْ اَزّا[5]

Kwani huoni ya kwamba tumewatuma mashet'ani kwa makafiri wawachochee kwa uchochezi?

Katika hali kama hiyo basi waatu hao hawatopata msaada wowote kutoka kwa Mola wao, na Mwenyeezi Mungu anawambia watu hao:-

مَثَلُ الَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِ اللهِ اَوْلِيَاء كَمَثَلِ الْعَنكَبُوتِ اتَّخَذَتْ بَيْتاً وَإِنَّ اَوْهَنَ الْبُيُوتِ لَبَيْتُ الْعَنكَبُوتِ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ[6]

Mfano wa walio wafanya walinzi badala ya Mwenyezi Mungu, ni mfano wa buibui alivyo jitandia nyumba. Na hakika nyumba dhaifu mno kuliko zote ni jumba la buibui, laiti kuwa wanajua.

Kwa hiyo uwalii wa shetani kwa makafiri na wale wanaotenda matendo mabaya ni kutokana na nidhamu ya hekima ya Mwenyeezi Mungu na uwalii wa kimaumbile(wilayat takwiniyah) wa Allah (s.w).

Maelezo kwa ufupi kuhusiana na somo lililopita:

*kwa wale ambao wameharamika na uwalii wa Mwenyeezi mungu yaani wameharamika na mlinzi wa kuwasimamia na kuwaongoza wao katika mambo yao, na natija ya hayo watu hao watapata matatizo duniani wa watapata adhabu kali siku ya Kiama.

*Wanaadamu wote duniani hufaidika na Uwalii wa kijumla jamala wa Mwenyeezi Mungu. Ama uwalii makhsusi wa Mwenyeezi Mungu hufaidika wale waja wake waumini na wenye taqwa.

*Uwalii wa shetani ni kwa ajili ya makafiri na watenda maovu, ijapokuwa aili yake ni hekima zake Allah (s.w).

* shafaa, rehema, imani,n.k yote hayo ni natija ya kuukubali uwalii wa Mwenyeezi Mungu.

Masuala:

1. kwa mtazamo wa Qur-ani kwa nini watu ambao wanamuabudu asiyekuwa Mola wa haki wanapata madhara?.

2. Neno wilayat (walii) lina maana gani?.

3. Watu gani hukumbwa na uwalii wa shetani?.

4. Vipi mwanaadamu anakuwa mwenye utukufu kwa kuukubali uwalii wa Mwenyeezi Mungu?.

5. Ni watu wa aina gani watakaopata shafaa ya Mwenyeezi Mungu?.

6. Elezea kwa ufupi uwalii wa kijumla jamala wa Mwenyeezi Mungu na uwalii wake kwa waja wake makhsusi.

[1] Surat Shuura Aya ya 9

[2] Surat Albaqarah Aya ya 257

[3] Surat Al-An-aam Aya ya 14

[4] Surat Anfaal Aya ya 62

[5] Surat Maryam Aya ya 83

[6] Surat Ankabuut Aya ya 41

MWISHO