UTAFITI KATIKA KUFUTWA HUKUMU
  • Kichwa: UTAFITI KATIKA KUFUTWA HUKUMU
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 13:16:13 3-9-1403

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

NASIKH NA MANSUKH NDANI YA QUR_ANI.4

UTAFITI KATIKA KUFUTWA HUKUMU

Tukiendelea na mada yetu kuhusiana na Nasikh na Mansukh, katika makala iliyopita (makala no.3) tulielezea masharti ya kufutwa kwa baadhi ya hukumu na kuletwa hukumu nyengine, katika makala hii tutazungumzia umuhimu kuhusiana na ufutwaji wa hukumu hiyo.

Umuhimu wa kuzungumzia suala hili uko wazi kabisa kwani Mwanachuoni anapokuja na kupekuwa hukumu za Kifiqhi ndani ya Qur-ani, au Mwanachuoni anapokuja kutafuta elimu fulani katika Qur-ani ni lazima azielewe hukumu zilizofutwa ili asije akazitumia aya hizo katika kutoa fatuwa katika hukumu fulani.

Abu Abdi-Rahmani Sulamiy ambaye ni mtumishi wa Imam Ali (a.s) anasema kwamba Imam Ali (a.s) alipambana kimaneno na mmoja kati ya Maulamaa na Makadhi wa mji wa Kufa akamuuliza :-

“Jee hivi unazifahamu aya zilizofutwa hukumu zake na zile zenye kufuta hukumu zilizopita? Akamjibu hapana! Akamwambia basi katika hali hii utakuwa umejitokomeza wewe pamoja na wanaokufuata”,  

MAANA NA UHAKIKA WA UFUTWAJI WA AYA

Kwa kutokana na yale yaliyozungumziwa hapo juu, itakuwa imefahamika kwamba neno (Naskh) linamaanisha kubadilishwa hukumu iliyopita kwa kupitia hukumu mpya iliyoletwa, na jambo hili limefahamika hivyo kwa jinsi ya mtizamo wa watu tu, kwani Mwenyeezi Mungu alipoiweka hukumu ile ya mwanzo alikuwa ameiweka kwa kipindi cha mpito, lakini mtizamo wa watu hauwezi kugundua suala hilo, na ilipokuja hukumu ya pili iliyoifuta hukumu ya mwanzo ilionekana ni kama kwamba Mwenyeezi Mungu amebadilisha mtizamo wake, kiasi ya kwamba baadhi ya watu wameona kuwa mtizamo wa pili unabainisha kutokuelewa kwa Mwenyeezi Mungu, yaani (ni kana kwamba Mwenyeezi Mungu alikuwa haelewi masharti na manufaa ya watu katika zama zitakazokuja baadae), na pale zilipofika zama hizo na kumbainikia suala hilo ndilo alipoibadilisha ile hukumu ya mwanzo na kuleta hukumu nyengine badala ya ile aliyoiweka mwanzo, Naskh kwa maana hii tuliyoizungumzia hupatikana na kuonekana katika sheria zinazopangwa na watu, kwani mwanaadamu hawezi kuyafahamu manufaa na matokeo yatakayokuja baade, lakini Mwenyeezi Mungu Yeye ni Mjuzi wa yote yaliyopita na yajayo, kwa hiyo hatuwezi kulifasiri neno naskh katika Qur-ani kwa maana hii ya pili tuliyoielezea, kwa hiyo basi ufutwaji wa sheria za Mwenyeezi Mungu hauna maana ya neno hili kamili, bali kiudhahiri tu huonekana hivyo yaani ( Hukumu ya Aya ya mwanzo imefutwa na kuwekwa hukumu ya Aya nyengine badala yake).

Kwani Mwenyeezi Mungu toka alipoiweka hukumu ya Aya ile ya mwanzo alikuwa ameiwekea wakati maalumu, na ulipofikia wakati wake hukumu hiyo ikawa tayari imeshapitiwa na muda, lakini kwa kutokana na maslahi ya watu wa zama zile ilikuwa sio jambo la busara kuwapa hukumu nzito watu hao, bali hatua baada ya hatua. Kwa ubainifu uliopatikana sasa tunaweza kusema kuwa hakuna aya iliyofutwa bali kila aya ilikuwa na kipindi chake maalumu na kilipomalizika kipindi chake hukumu ya Aya hiyo ikamalizika.

MWISHO