KUIELEWA QUR-ANI
  • Kichwa: KUIELEWA QUR-ANI
  • mwandishi: HADI MAARIFAT
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 13:17:10 3-9-1403

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KUIELEWA NA KUIFAHAMU ELIMU YA QUR-ANI

Qur-ani ni kitabu kimoja wapo katika vitabu ambavyo Mwenyeezi Mungu ameviteremsha kutoka mbinguni, kitabu hicho toka pale mwanzo ambapo kimeteremshwa, mpaka sasa hivi kimesalimika na hakijaharibiwa, kimehifadhika na kitaendelea kuhifadhika .
Mada muhimu ambazo zimo katika kitabu hichi kitukufu ni kumjua Mwenyeezi Mungu na kumfahamu ili tuwe karibu naye, kisha kuyaelewa maneno ambayo ameyazungumza katika kitabu hicho
    Kabla hatujaingia katika mada muhimu, kwanza kabisa kuna ulazima wa kuifahamu Elimu ya Qur-ani, na vipi tutaweza kupambanua baina ya elimu ya Qur-ani na taf-siri ya Qur-ani, kwa hiyo katika mada hizi ni muhimu na ni vizuri tukaelewa maana ya maneno hayo.

Ufahamu wa kuitambua Qur-ani umegawika katika sehemu mbili:- nazo ni kama ifuatavyo  a) Elimu zinazohusiana na Qur-ani, yaani elimu ambazo zinamsaidia mtu kuilewa zaidi Qur-ani 

b) Elimu zilizokuwemo ndani ya Qur-ani Kwa ibara nyengine tunaweza tukasema hivi.

1 -Sisi tunaingalia Qur-ani katika mitizamo miwili, kwanza kabisa tunaiangalia ni kama kitabu cha Mwenyeezi Mungu ambacho kuna uwezekano wa kukifanyia uchunguzi katika kuteremka kwake, na kimechukua muda gani katika kuteremka kwake au kimekusanywa vipi, na mengineyo yasiyokua haya, kama vile kupekua na kujiuliza je, kuna uhusiano baina ya Aya moja na nyengine ndani ya kitabu hichi au hakuna? Au kujiuliza, je hivi ndani ya kitabu hichi mna Aya ambazo zinazozichambua Aya nyengine? Au kufanya utafiti kuhusiana na Aya ambazo ni Naasikh na Aya ambazo ni Mansuukh n.k. Mtizamo huu basi ndio mtizamo ambao umebeba maana halisi ya neno (Ulumul- Qur-ani) lenye maana ya elimu zinazohusiana na Qur-ani, na huu ni mkusanyiko wa elimu tofauti, kama vile: elimu ya Tajuwidi, elimu ya Tafsiri, elimu ya Kisomo cha Qur-ani n.k.

2- Vilevile tuna mtizamo mwengine wa kuingalia Qur-ani, na mtizamo huu ni kule kukiangalia kitabu hichi kwa ajili ya kutaka kufaidika na mafunzo yaliomo ndani ya kitabu hichi na mtizamo huu unajulikana kwa jina la (Tafsiri ya Qur-ani), na tafsiri hutimia kwa kupitia mfumo maalum, moja kati ya elimu ambazo Mfasiri wa Qur-ani anatakiwa kuzielewa ni (Ulumul- Qur-ani) Kwa maelezo ambayo tuliyoyaelezea hapo juu, itakua imeshaeleweka kua (Ulumul- Qur-ani) ndio hatua ya mwanzo kabisa ambayo mtu anatakiwa kuielewa, kabla hajaingia katika uwanja wa Tafsiri, kwa kutokana na siri hii basi, ndio maana mapema kabisa baada tu ya Mtume (s.a.w.w) kufariki, walijitokeza miongoni mwa Masahaba waliopiga hatua katika fani ya Qur-ani. Na kwa kutokana na kwamba Imamu Ali (a.s) ndiye mtu wa mwanzo aliye watangulia Masahaba wote katika kupiga hatua katika suala hili, ndio maana Jalalu Dini Suyutiy akasema: (mtu wa mwanzo miongoni mwa Makhalifa ambaye amepokea hadithi nyingi zaidi zinazohusiana na Qur-ani ni Ali bin Abii Taalib). Na baada ya Imamu Ali (a.s) wanafuatilia miongoni mwa Masahaba ni Abdullahi bin Abbaas, Abdullahi bin Masoud, na Ubayya bin Ka’ab, hawa ndio watu wenye daraja ya mwanzo katika fani hii ya Qur-ani.

Mwanzo wa utafiti wa Qur-ani na uandishi wa Tafsiri, ulianza katika karne ya pili Hijiria, mtu wa mwanzo aliyelianzisha suala hili ni (Yahya bin Ya’amir) ambaye ni mwanafunzi maarufu wa (Abul-Aswadi Addualiy), ambaye amefariki mwaka (89 Hijiria Qamaria), mwanaffunzi huyu ameandika kitabu cha fani ya visomo vya Qur-ani (Qiraa-aat) ambacho ndani yake mna aina mbali mbali za visomo ambavyo vilikua ni maarufu katika zama alizokua akiishi yeye, na baada yake ni Hasani Al- Basriy ambaye amefariki mwaka (110 Hijiria Qamaria) yeye ameandika kitabu chenye kuzungumzia adadi za Aya za Qur-ani, baada ya hapo kukaadikwa vitabu vyengine tofauti vinavyohusiana na fani ya elimu za Qur-ani (Ulumul-Qu-ani), vitabu hivi vilikua vikiandikwa ima ni kando ya Qur-ani, au wakati mwengine vilikua vikiandikwa vikiwa ni kama utangulizi wa Tafsiri ya Qur-ani, mpaka katika fani hii kukapatikana athari zenye thamani kubwa na zilizokusanya kila kitu ndani yake, ambazo zimebakia milele hadi hivi sasa, na miongoni mwa athari hizo ni kitabu kijulikanacho kwa jina la (Al-burhaan) na cha pili ni (Al-itqaan), vitabu ambavyo vina nafasi maalum katika fani hii.

Kitabu (Al-burhaani) mtunzi wake ni Imamu Badrud-diin Zarkeshiy ambaye ni Mwanazuoni mwenye daraja ya juu katika karne ya nane Hijiria Kamaria, naye amezaliwa mwaka (745 Hijiria Qamaria) katika mji wa Misri na akakulia katika mji huo huo, na ameweza kufikia ulingo katika fani tofauti za elimu ya Qur-ani (Ulumul-Qur-ani). Kitabu chake (Al-burhaan) miongoni mwa vitabu vya (Ulumul-Qur-ani) vilivyoandikwa ndicho kitabu kilichokusanya mada mama za elimu hii kwa vizuri zaidi kuliko vitabu vyengine, kitabu hichi kina ibara zilizoshonana ambazo zimebeba na kukusanya ndani yake ufafanuzi kwa ufupi, na ndani yake kimekusanya mada arubaini na saba, kiasi ya kwamba ndani yake kimekusanya kila kile kinachohitajika kuelezewaKitabu cha pili katika fani hii ni (Al-itqaan fii-ulumil-Qur-ani), kilichotungwa na Jalalud-diin Abdur-Rahmaan Suyutiy, naye amezaliwa katika kitongoji cha Assuyuutiy huko Misri katika mwaka (894 Hijiria Qamaria) na amefariki katika mji wa Cairo Misri. Mwanazuoni huyu ameandika vitabu vyenye thamani kubwa katika fani zote za Hadithi, na katika elimu nyengine za kiislamu. Yeye katika kitabu chake Al-itqaan cha (Ulumul- Qur-ani), ameweza kukusanya ndani yake mada zifikazo thamanini ambazo zinahusiana na fani hii. Na leo hii kitabu hichi kinahesabiwa kua ndio kikubwa kilichoikusanya fani na ndio marejeo mukuu ndani ya fani hii na ndicho kitabu kinachorejelewa na watafiti pamoja na wapekuzi wa fani hii.

Katika zama hizi za karibuni kuna wengi miongoni mwa Wanazuoni, wakiwemo wanazuoni wa madhehebu ya Shia ambao wametunga vitabu vinavyohusiana na fani hii, nasi basi hatuna budi kukitaja kitabu kilichotungwa na Sayyid Khui (Rahmatu-Llahi Alaihi) ambacho ni kitabu pekee katika zama zake kijulikanacho kwa jina la (Al-bayaan). Katika kitabu hichi kuna utafiti wa hali ya juu unaohusiana na fani hii, na mpaka hivi sasa kitabu hichi ndio moja kati ya vitabu muhimu vinavyotumika ndani ya Chuo kikuu pamoja na Hauza za kielimu.

MWISHO