HAKI ZA NDOA NDANI YA QUR_ANI
  • Kichwa: HAKI ZA NDOA NDANI YA QUR_ANI
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 17:29:5 1-9-1403

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

HAKI ZA NDOA NDANI YA QUR_ANI

UNASHIZA WA MUME

Mwenyeezi Mungu Mtukufu anasema:-

وَإِنِ امْرَأَةٌ خَافَتْ مِن بَعْلِهَا نُشُوزًا أَوْ إِعْرَاضًا فَلاَ جُنَاْحَ عَلَيْهِمَا أَن يُصْلِحَا بَيْنَهُمَا صُلْحًا وَالصُّلْحُ خَيْرٌ وَأُحْضِرَتِ الأَنفُسُ الشُّحَّ وَإِن تُحْسِنُواْ وَتَتَّقُواْ فَإِنَّ اللّهَ كَانَ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرًا[1]

Na mwanamke akichelea kutupwa au kutojaliwa na mumewe, basi si vibaya kwao wakisikizana kwa suluhu. Na suluhu ni bora. Na nafsi zimewekewa machoni mwake tamaa na choyo. Na mkifanya wema na mkamchamngu basi hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari za yote mnayo yatenda.

Maelezo kuhusiana na Aya:

Mambo ya kuachana yanavunjwa nguvu sana katika sharia za kiislamu, na watu wengine mara huchokana wakaona tabu kutekelezeana haki zao za ndoa.

Ima mke hamkamilishii mume haki zake, au mume hamkamilishii mke haki zake.

Basi inataka yule asiyekamilishiwa asipande mori akaacha (akiwa mwanamume) au akataka kuachwa akiwa mwanamke, kwani subira yavuta kheri.

Lakini nyoyo zina ubakhili, kila mmoja hakubali kusamehe haki yake, basi kila mmoja anatakiwa apigane na moyo wake, na akubali kusamehe baadhi ya haki zake- bali hata zote pia. Na Mwenyeezi Mungu atampa thawabu kubwa, na wanawake ndio sana wasiopendwa kuonewa, basi ndiyo maana hapa akatajwa mke kuambiwa astahamili, basi na mume ndiyo vivyo hivyo.

Maelezo kuhusiana na Aya ya 129 ya suratun nisaa.

Imebainishwa katika maelezo ya  aya ya 3 ya suratun Nisaa kuwa ukewenza umenunjwa nguvu sana na Uislamu, ila ikiwa hapana budi ndiyo ufanywe, kwani moyo ni moyo, takriban ni muhali moyo kupenda vitu viwili sawa sawa, na kuvifanyia insafu sawa sawa, lazima utamili kumoja.

Basi hapa wanaambiwa hao waume wenye kuweka uke wenza, kuwa wakimili upande mmoja, wajitahidi mwisho wa jitihada zao wasimili kabisa kabisa, hata akawa huyo mwengine hajijui kuwa mke au si mke, anajiona katundukika kwa uzi, anasukumika huku na huku, hajijui kasimama wapi.

وَإِنْ خِفْتُمْ اَلاَّ تُقْسِطُواْ فِى الْيَتَامَي فَانكِحُواْ مَا طَابَ لَكُم مِّنَ النِّسَاء مَثْنَي وَثُلاَثَ وَرُبَاعَ فَإِنْ خِفْتُمْ اَلاَّ تَعْدِلُواْ فَوَاحِدَةً اَوْ مَا مَلَكَتْ اَيْمَانُكُمْ ذٰلِكَ اَدْنَي اَلاَّ تَعُولُواْ[2]

Na ikiwa mnaogopa kuwa hamtowafanyia mayatima uadilifu, basi oeni mnao wapenda katika wanawake, wawili au watatu au wane. na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu, au wale ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki. Kufanya hivi ndiko kutapelekea msikithirishe wana.

Maelezo Kuhusiana na Aya ya 3 ya suratun Nisaa

Wanavyuoni wote wa sharia ya Kiislamu wamekongamana kwamba Aya hii imeweka mpaka wa idadi ya wake ambao mtu aweza kuoa, na inakataza mtu kuwa na zaidi ya wake wanne wakati mmoja, hadithi za Mtume pia zinatilia nguvu kongamano hilo. Imehadithiwa kuwa Ghailan, mtemi wa Taif alikuwa na wake tisa aliposilimu, Mtume akamwambia abakishe wanne tu, na awataliki waliobakia, na naufal bin Muawiya ambaye aliposilimu, naye aliamrishwa na Mtume kumtaliki mmoja wa wake zake watano.

Pia inapasa kuzingatia kuwa Aya hii, ingawa inatoa ruhusa kuoa mke zaidi ya mmoja, ni sharti awafanyie insafu (awagawie haki zao kwa usawa),kwa hiyo, mtu yoyote anayeitumia vibaya ruhusa hii kwa kuoa mke zaidi ya mmoja bila ya kufanya insafu, atakuwa anajaribu kumhadaa Mwenyeezi Mungu. Kwa sababu hii, mahakama ya nchi za Kiislamu yamepewa uwezo wa kulazimisha kufanywa insafu ili kurakibisha kosa alilofanyiwa mke au wake, pamoja na hayo, ni kosa kabisa kuchukulia kwamba, kwa kuweka sharti hiyo ya insafu, aya hii imekusudia kuondoa ruhusa ya kuoa wake wengi, hivyo sivyo inavyosema Qur-ani, wanaosema hivyo ni wale Waislamu ambao wametekwa akili zao na Wakiristo na nchi za Magharibi.

Wao husema kwamba:

“Qur-ani pia inapinga kuoa wake wengi, lakini haikuliondoa jambo hilo moja kwa moja kwa sababu haikuona kuwa ni jambo la busara kufanya hivyo wakati huo kwa vile ambavyo dasturi yenyewe ilikuwa imeenea. Badala yake inamruhusu mtu kuoa wake wengi maadam atawafanyia insafu,kwa kuwa sharti hii ni ngumu mno kuitekeleza. Pendekezo hapa ni kuoa mke mmoja, kwa hakika, fikira hizo husababishwa na kutawaliwa akili,kwa sababu kuoa wake wengi kuoa kwenyewe sio jambo ovu, kwani wakati mwengine huwa ni jambo la lazima ili kumzuia mja asipindukie mipaka ya Mwenyeezi Mungu. Kuna watu wengine, hata wakitaka hawatosheki na mke mmoja. Ruhusa ya kuoa wake mpaka wanne huwaepusha watu kama hao na madhara ya uhasharati usio na kifani, ndiyo Qur-ani ikawaruhusu watu kama hao kuoa mpaka wake wanne maadamu watawafanyia insafu.

Ama wale wanaoona kuwa ni ufisadi kuoa wake wawili mpaka wanne, ni hiyari yao kuipinga Qur-ani na kuibeza ruhusa hiyo, lakini hawana haki ya kuisingizia upotofu wa mawazo yao, maana Qur-ani imehalalisha jambo hili kwa lugha iliyo wazi bila ya kutumia neno lolote liwezalo kupinduliwa kwa namna yoyote ili liwe na maana kwamba Qur-ani imekusudia kukataza jambo hili.

Maelezo kuhusiana na aya ya 130

Na ikiwa hapana budi kabisa na waachane, kama Aya ya 130 inavyosema:

وَإِن يَتَفَرَّقَا يُغْنِ اللّهُ كُلاًّ مِّن سَعَتِهِ وَكَانَ اللّهُ وَاسِعاً حَكِيماً[3]

Ukimwacha wewe hatakuwa kaachwa na Mwenyeezi Mungu, atampa aliye bora kuliko wewe.

Ikiwa mke atahofia mumewe kuwa nashiza au kumtelekeza.

Unashiza unaweza kuwa kwa mke kwa kumnyima unyumba mumewe au kutoka nyumbani bila ya idhini ya mume.Yametangulia maelezo ya unashiza wa mke katika kufasiri Aya ya 34 ya Sura hii.

Pia unashiza unaweza kuwa kwa mume kwa kumuudhi mke na kuacha kumpa matumizi au kumnyima siku akiwa na mke zaidi ya mmoja. Aya hii inaelezea hofu ya mke kwa unashiza wa mumewe au kumtelekeza. Makusudio ya kutelekeza ni kumwepuka kwake kunakoonyesha kumchukia.

Ama kwenda kwenye shughuli zake na matatizo yake, lazima mke amvumilie na kumstahmilia madamu hamchukii.

Basi hapana vibaya juu yao kusikilizana kwa suluhu.

Ikiwa mke anahofia kuwa unashiza wa mumewe utasababisha talaka au kuwa katika hali ya kufungika - si kuwa na mume wala kuachwa, basi hapana ubaya kwa mume wala kwa mke kuafikiana wenyewe au kupitia kwa mtu. Waafikiane na kusikilizana, kuwa mume aache kumnyima haki zake, ili abakie katika hifadhi yake na waishi maisha ya utulivu.

Na suluhu ni bora kuliko kutengana na talaka. Kuna Hadith isemayo: "Halali inayochukiza zaidi kwa Mwenyezi Mungu ni talaka." Ni vizuri tueleze kuwa anachokitoa mke kwa ajili ya talaka si halali ila kwa kuridhia nafsi yake. Mwenyezi Mungu anasema: "… Kama wakiwatunukia kitu katika hayo mahari, basi kuleni kwa raha na kunufaika.

Na nafsi zimewekewa mbele uchoyo.

Yaani uchoyo daima uko mbele katika nafsi haumwepuki hata wakati wa kutoa, ile hali ya jakamoyo anayoihisi mtoaji na kuificha wakati wa kutoa ndio uchoyo wenyewe na makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu "na nafsi zimewekewa mbele uchoyo." Mke haiachi haki yake kwa urahisi wala mwanamume hasamehi badali. Tusisahau kuwa Aya tukufu imezungumzia matatizo ya unyumba. Ama ikiwa unyumba hauna matatizo hakuna lolote la kuwajibisha kutoa kitu bali hakuna kati ya mume na mke anayeona kuwa kitu ni chake. Na mkifanya wema na mkajihifadhi basi Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa muyatendayo.

Huu ni mwito kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa mume na mke kufanya kila juhudi amfanyie wema mwenzake na ajichunge na sababu za kukosana na kutengana.

Wala hamtaweza kufanya uadilifu baina ya wanawake hata mkikamia.

Kufanya uadilifu baina ya wake kuko aina mbili: Kuna kule kunakowezekana, kama kufanya usawa katika matumizi na mazungumzo mazuri.

Na kuna ambako kuko nje ya uwezo wa binadamu, kama vile mapenzi ndani ya moyo na hata kujamii pia. Mume anaweza kusisimuliwa na mke,kiasi ambacho yule mwingine hamsisimui vile.

Uadilifu baina ya wanawake unaotakiwa ni katika matumizi ambao uko chini ya uwezo. Ama uadilifu katika mapenzi na mfano wake, mtu hakalifishwi nao. Na hii ndiyo inayotofautisha baina ya Aya hii na ile Aya ya tatu katika Sura hii isemayo: "Na kama mkihofia kutofanya uadilifu basi ni mmoja …"Imam Jafar as-Sadiq anasema: "Ama kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Mkihofia kutofanya uadilifu’ anakusudia kutoa matumizi; na ama kauli yake; 'Hamtaweza' anakusudia mapenzi.” Na sisi ni katika wale wanaoamini kabisa kuwa hakuna kitu kigumu kukipata kuliko uadilifu. Kwa hakika yake hasa na kiini chake ni kujikomboa na matamanio; kama ilivyoelezwa katika baadhi ya Hadith kwamba mwadilifu ni yule mwenye kuhalifu mapenzi yake na akamtii Mola wake. Wala hawi na haya ila aliyejitakasa. Basi msipondokee kabisa kabisa.

Kwa mke mnayempenda na mwingine mkamnyima haki zake.

Mkamwacha (mwingine) kama aliyetundikwa akawa si mke aliyeolewa anayepata haki zake, wala si mtalikiwa anayeweza kuolewa na mwingine anayemtaka.

Na watakapotengana, Mwenyezi Mungu atamtosheleza kila mmoja kwa wasaa wake.

Inatakikana kabla ya chochote mume na mke wajaribu kuondoa tofauti zao na mambo yanayosababisha kutengana. Kwa sababu suluhu ni bora.

Ikiwa haiwezekani, basi talaka ni bora kuondoa madhara zaidi; na fadhila ya Mwenyezi Mungu na riziki yake itawaenea wote, wawe pamoja au watengane. Mwenyezi Mungu anaweza kumpa mtalikiwa mume bora kuliko wa kwanza; na anaweza kumpa mtaliki mke bora kuliko wa kwanza.

Kwa ufupi ni kwamba yote yaliyotangulia yanazunguuka kwenye mzunguuko mmoja tu ambao ni "kushikana kwa wema na kuachana kwa wema." Kushikana ni bora ikiwa hakuna ufisadi na kuachana ni bora ikiwa kuna ufisadi; kama ambavyo Mwenyezi Mungu ameumba dawa ya kuponesha magonjwa ya mwili, vile vile ameweka dawa ya maradhi ya kijamii.

[1] Suratun Nisaa Aya ya 128-130

[2] Suratun Nisaa Aya ya 3

[3] Suratun Nisaa Aya ya 130

MWISHO