BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
MALENGO YA MITUME YA MWENYEEZI MUNGU NO.1
* Mitume Mitukufu ya Mwenyeezi Mungu imekuja kuwalingania wanaadamu katika kitu gani?.
MITUME (A.S) IMESHIRIKIANA KATIKA MALENGO YAO.
Tukitupilia macho elimu ya Tarekhe tutafahamu kuwa katika kipindi chote kilichopita elimu ya Tarekhe inathibitisha kuwa Mitume yote imekuja ikiwa na malengo mamoja, nayo ni kuwalingania wanaadamu kwa kuwataka wamuabudu Mola mmoja, na hii ni katika sunna zake Allah (s.w). kama alivyosema:-
إِن يَمْسَسْكُمْ قَرْحٌ فَقَدْ مَسَّ الْقَوْمَ قَرْحٌ مِّثْلُهُ وَتِلْكَ الايَّامُ نُدَاوِلُهَا بَيْنَ النَّاسِ وَلِيَعْلَمَ اللّهُ الَّذِينَ آمَنُواْ وَيَتَّخِذَ مِنكُمْ شُهَدَاء وَاللّهُ لاَ يُحِبُّ الظَّالِمِينَ[1]
Kama yamekupateni majaraha, basi na hao watu wengine yamewapata majaraha mfano wa haya. Na siku za namna hii tunaweletea watu kwa zamu, ili Mwenyezi Mungu awapambanue walio amini na awateuwe miongoni mwenu mashahidi. Na Mwenyezi Mungu hawapendi madhaalimu.
*hapa wanakumbushwa misukosuko iliyowafika siku ya vita vya Uhudi, na kuwa kama walivyosibiwa wao ndivyo wao nao walivyowasibu maadui zao, na kuwa mambo ndivyo vivi hivi.
Basi huo ni uhakika ulio wazi kabisa kwamba Mitume yote imekuja ikiwa na madhumuni mamoja na imewalingania wanaadamu kwa lengo moja, na mlolongo huo wa Mitume umekuja na alama tofauti zinazothibitisha kuwa wao ni Mitume ya haki, basi kwa wale wanaotafuta haki wataiona haki hiyo na wataongoka kupitia Mitume hiyo, na hao watakaoongoka wataajenga mlolongo wao wakikabiliana na wale walio batili, na mataghuti ambao wamejenga serikali na kuwahukumu watu kwa dhulma.
Basi kwa wale ambao wamejenga mlolongo na wanasonga mbele kwa kupigania haki watavuna matunda mazuri, na watapata malipo mema kutoka kwa Mola wao, kwa hiyo Mitume na wafuasi wao ni sidikisho la Aya hii tukufu:-
اَلَمْ تَرَ كَيْفَ ضَرَبَ اللّهُ مَثَلاً كَلِمَةً طَيِّبَةً كَشَجَرةٍ طَيِّبَةٍ اَصْلُهَا ثَابِتٌ وَفَرْعُهَا فِى السَّمَاء. تُؤْتِى اُكُلَهَا كُلَّ حِينٍ بِإِذْنِ رَبِّهَا وَيَضْرِبُ اللّهُ الاَمْثَالَ لِلنَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ[2]
Hebu hukuona vipi Mwenyezi Mungu alivyo piga mfano wa neno zuri? Ni kama mti mzuri, mizizi yake ni imara, na matawi yake yako mbinguni.
Hutoa matunda yake kila wakati kwa idhini ya Mola wake Mlezi. Na Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano ili wapate kukumbuka.
*Hapa inapigwa mfano kheri namna inavyotanda vizuri ikaleta nafuu kila upande.
*Katika Aya hizo kumepigwa mifano ya mti mzuri ambao mizizi yake iliyo imara ni mlolongo wa Mitume na wafuasi wake ambao utathibiti milele. Na kwa upande mwengine kwa wale walio batili wamepigiwa mfano wa mti ambao hauna mizizi na kamwe hautothibiti katika dunia hii. Kama anavyosema Allah (s.w):-
وَمَثلُ كَلِمَةٍ خَبِيثَةٍ كَشَجَرَةٍ خَبِيثَةٍ اجْتُثَّتْ مِن فَوْقِ الاَرْضِ مَا لَهَا مِن قَرَارٍ[3]
Na mfano wa neno ovu ni kama mti muovu, ulio ng'olewa juu ya ardhi. Hauna imara.
* Inapigiwa mfano shari namna inavyotanda juu tu – kama miti ya kutambaa – kisha ikasukulikia mbali ikapotea.
Mitume ni Makhalifa wa Mwenyeezi Mungu katika dunia, na wamekuja kuiongoza jamii ya wanaadamu ili wafikie katika kheri na saada, ili wanaadamu wajitakase na kumuabudu Mola wao na wabaki mbali na ujahili. Vile vile Mitume imekuja kukataza kuabudu masanamu, na kuwataka watu wajiepushe na kufanya dhulma. Na kwa sababu hiyo basi Mitume yote inashirikiana katika madhumuni yao, na malengo yao ni mamoja katika kuwalingania wanaadamu. Katika makala ijayo tutatupilia macho malengo muhimu wanayoshirikiana Mitume katika kuwalingania wanaadamu.
kila mmoja wetu anaweza kujiwa na suala kama hili lililonojia mimi binafsi, ya kwamba ikiwa Mitume yote imekuja na malengo mamoja tu, basi kwa nini duniani kuna dini tofauti na madhebu tofauti?. kwa upande mwengine, kwa nini kila wafuasi wa dini wanadai kuwa dini yao ndio dini ya haki?, kwa mfano Mayahudi na wakiristo wanadai kuwa sio dini ya Kiislamu tu ndio dini ya haki,bali dini zote ni dini za haki, na wanathibitisha hayo kutokana na Aya za qur-ani takatifu.
Kwa upande mwengine Waislamu wanadai kuwa ni dini ya Kiislamu tu ndio dini ya haki, na wao vile vile wanathibitisha hayo kutokana na aya za Qur-ani takatifu, lakini kwa sababu wakati hauniruhusu tutaendelea kutafiti masuala kama hayo katika makala inayofuata, ili tupate ufumbuzi wa madai hayo ya Mayahudi na manasara kuwa dini zao pia ni dini za haki na zinazoridhiwa na Allah (s.w). Tunategemea tutakuwa tumefaidika na ukumbusho huo, na tunamuomba Mola kutupa nguvu na uwezo ili kukumbushana zaidi, inshaallah tuwe pamoja na wale walioridhiwa na Yeye Mola muwezi na Mitume yake na Ahlulbayt wake.
[1] Surat Al-Imrani Aya ya 140
[2] Surat Ibrahim Aya ya 24-25
[3] Surat Ibrahim Aya ya 26
MWISHO