KANUNI ZA NDOA NA MAADILI YA FAMILIA
WAJIBU WA MWANAMUME.
Sehemu ya saba
MSIMAMIZI WA FAMILIA
USIWE NI MWENYE KULALAMIKA KUSIKO NA LAZIMA.
Matatizo ya maisha ni mengi. Hakuna mtu ambaye anayo furaha kamili na hali yake. Lakini baadhi ya watu ni wavumilivu zaidi kwa matatizo yao kuliko wengine. Hujaribu kuyaweka katika kumbukumbu ya akili zao na hawayataji isipokuwa kama ipo sababu ya kuyafichua.
Kwa upande mwingine, wapo watu ambao ni wadhaifu mno hivyo kwamba hawawezi kuishi na matatizo yao bila ya kuyafichua. Wanayo mazoea makubwa kulalamika hivyo kwamba kila wanapokutana na watu wengine, huanza kulalamika. Popote wendapo na wakati wowote wanapokuwa kwenye mikusanyiko, hulalamika kuhusu Matukio ya kila siku ambayo yameathiri maisha yao.
Inakuwa kama vile wametumwa kwenye misheni na shetani mwenyewe, kuharibu furaha ya wengine. Ndiyo maana marafiki wengi sana na ndugu hawependi kutiwa wasiwasi na watu wenye tabia hii na hujaribu kuwakwepa kadiri iwezekanavyo.
Lakini lazima watu wawasikitikie wake zao, na watoto wao ambao wanatakiwa kuvumilia tabia yao. Kwa sababu hakuna mtu mwingine ambaye yupo tayari kusikiliza malalamiko yake, watu hawa hutoa matatizo yao mbele ya familia zao.
Wakati mwingine hulalamika kuhusu matumizi yao, kodi marafiki zao na wakati mwingine hulalamika kuhusu wafanya kazi wenzao biashara zao, maradhi, madaktari na kadhalika.
Watu hawa ni wenye kuona kila kitu kuwa kibaya hawaoni chochote kizuri katika dunia hii. Wanateseka wao na wengine, pia na hususan familia zao huteseka pia.
Mpendwa bwana! Kuna maana gani kulalamika wakati wote? Unafanikiwa nini katika kulalamika? Kwa nini familia yako iteseke kwa sababu wewe umekasirishwa na dereva wa teksi, bajaji, na haisi? Kwa nini umlaumu mke wako kwa sababu biashara yako haiendi haraka?
Usisahau kwamba msimamo wako utaifukuza familia yako kutoka kwako. Watakukasirikia na kukata tamaa. Wanaweza hata wakakimbia kutoka kwako na inawezekana wakaangukia kwenye mtego wa uovu na ukhalifu.
Jambo la mwisho ni kwamba tabia hii huweka kovu la kiakili kwa watu wako.
Je, huoni kwamba sio jambo jema zaidi kutokuharibu furaha ya familia yako? Unaporudi nyumbani, jaribu kusahau matatizo. Furahia na familia yako. Kula nao cheka nao na furahia kuwa pamoja nao.
Pia Uislamu unachukulia uvumilivu na kutokulalamika kuwa ni tabia njema na hata uketenga thawabu (malipo ya baadae) kwa sifa hii.
Imamu Ally bin Abi Twalib as alisema: "Matatizo yanapompata Mwislamu, si vizuri alalamike kuhusu Mwenyezi Mungu kwa watu wengine, isipokuwa anachotakiwa kufanya ni kumpelekea Mwenyezi Mungu matatizo yake ambaye ndiye mwenye ufunguo wa matatizo yote."
Imamu Ally bin Abi Twalib as pia alisema: "Imeandikwa kwenye Taurati; yeyote anayelalamika kuhusu tatizo ambalo limempata kwa kweli atakuwa analalamika kuhusu Mwenyezi Mungu."
Mtukufu Mtume saww alisema: "Yeyote anayepata matatizo ya afya yake na halalamiki kuhusu jambo hilo kwa watu, basi ni wajibu Mwenyezi Mungu kumsamehe dhambi zake zote."
Fuatana nami Sehemu ya nane kanuni za ndoa na maadili ya familia.