BIBI FATIMAH ZAHARA (A.S) 1
  • Kichwa: BIBI FATIMAH ZAHARA (A.S) 1
  • mwandishi: Hassani Bussi
  • Chanzo: mailto:busihassan@gmail.com
  • Tarehe ya Kutolewa: 19:51:25 1-9-1403

HISTORIA YA MASUMIN (A.S) 1

2. BIBI FATIMAH ZAHARA (A.S)

Sehemu ya kwanza

Kwa jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema mwenye kurehem.

Shukran zote zinamustahiki Mwenyezi Mungu Mtukufu ambaye katujaalia kuwa katika ummah wa Muhammad saww Sayyid (Bwana) wa Manabii

Na aliye tujaalia kushikamana na utawala wa Sayyid (Bwana) wa mawasii Ally bin Abi Twalib (a.s).

Shukran zote zinamustahiki Mwenyezi Mungu Mtukufu ambaye kupitia kwa mja wake mwema Mtukufu Mtume Muhammad saww ametuletea kiigizo chema kwa wanawake wote ambaye ni Bibi Fatimah (a.s).

Kwa hakika yeyote atakaye mfuata Bibi Fatimah as hatapotea kwa sababu yeye ndiye mwanamke bora wa kufuatwa na kuigwa.

Na ubora wa rehema na amani zimshukie Muhammad saww na kizazi chake kitukufu ambacho kimelindwa (kisifanye) uchafu (makosa) na kutoharishwa moja kwa moja. 33 :33 Qur-an.

Na rehema na amani ziwashukie Shi'ah (wafuasi) wao ambao wamesifiwa ndani ya Quran tukufu yenye hekima. 98:7 - 8 Qur-an.

Mwenyezi Mungu anasema :. Wape habari njema waja ambao wanasikiliza (wanasoma) maneno na kufuata mazuri yake nao ndio ambao Mwenyezi Mungu amewaongoza na wao hasa ndio wenye akili. 39 :18 Qur-an.

Jina :. FATIMAH (A.S).

Majina ya heshima :. Zahara, Swiddiqah Kubraah, Twahirah, Radhiah, Mardhiah, Batuli, Muhaddithah, Insiyah, Huriah.

Majina maaruufu :. Ummu Hassanain,(mama wa Hassani na Hussein), Ummu Abiha,(mama wa babake) Ummul Aimmah. Mama wa Maimamu 11)

Jina la baba yake : Muhammad bin Abdullah (s.a.w.w).

Jina la mama yake : Khadija bint Khuwaylid (a.s).

Tarehe ya kuzaliwa : Alfajiri ya ijumaa, 20 Jamadithan (mfunguo tisa) mwaka 5 Bi'ithah (tangu Muhammad (s.a.w.w) kupewa utume) A'amul Fili, mji mtukufu wa Makkah.

Kuuawa na : Maumivu makali kutokana na kipigo kutoka kwa maadui

Tarehe ya kufariki: 3 Jamadithan mwaka wa 11 Hijria, akiwa na miaka kumi na nane 18.

Bibi Fatimah as ni mwanamke bora kabisa katika Dunia hii na Akhera pia na yeye ni mfano mwema kabisa wa kuigwa.

Baba yake ni Mtukufu Mtume Muhammad saww na mama yake ni mwanamke mwema aitwaye Khadija bint Khuwaylid as. Hawa ni wazazi wa Bibi Fatimah as ambao ni viumbe bora zaidi katika Dunia hii na Akhera 98 :7 – 8.

Mtukufu Mtume Muhammad saww alikuwa akimpenda sana bint yake, na desturi yake ilikuwa kwenda kwa bint yake kwanza kabisa kila aliporejea kutoka safarini. Wakati huo akimbusu na kusema : "Fatimah ananukia harufu ya peponi".

Wakati wote uso wa Bibi Fatimah (a.s) hutoa nuru kama mwezi ung'aavyo.

Malaika nao walikuwa wanazungumza na Bibi Fatimah as hufurahi sana pindi wanapomuona.

Mtume Rasul alifurahia,Mwenyezi Mungu jalali kumbariki,Bint wa halali,Mwema wa tabia, Furaha faraha alishangilia.

Bibi Fatimah as ni zawadi kutoka kwa Mola. Yeye ndiye mwanamke mtakatifu asiyewahi kutenda Maovu duniani. Kwa hakika hakuna yeyote atakayejaaliwa kupata bint bora kama huyu.

Kwa binadamu wote wanaume na wanawake, Mwenyezi Mungu amewateua watu fulani fulani kuwa mfano (Viigizo) kwa wengine katika matendo yao. Katika ummah wa Kiislamu  Mwenyezi Mungu ameteua wanaume kumi na tatu (Muhammad bin Abdullah Mtume wa Mwenyezi Mungu, Ally bin Abi Twalib as kipenzi cha Mwenyezi Mungu (Waliiyullah), Hassan bin Aliy mteule wa Allah (al Mujtabaah) Hussein bin Aliy shahidi wa Karbala, Ally bin Hussein kipambo cha wachamungu, Muhammad bin Aliy sazo la elimu ya mitume, Ja'far bin Muhammad msema kweli, Musa bin Ja'far mficha hasira, Ally bin Musa mwenye kuridhia, Muhammad bin Aliy mtoaji sana, Ally bin Muhammad mchamungu, Hassan bin Aliy mfungwa gereza la jeshi, Muhammad bin Hassan anayengojewa. Mwenyezi Mungu amewateua hawa kuwa mfano (kiigizo) mwema kwa wengine katika matendo yao.

Lakini Mwenyezi Mungu ameteua mwanamke mmoja tu kuwa mfano (kiigizo) kwa wanawake wote na mwanamke huyo katika ule muda mfupi wa maisha yake, ameonyesha mfano ulio kama nyota imulikayo kwa muda wote ujao na alipofariki dunia, aliurithisha mfano huo kwa njia ya dalili za bint wake (Zainabu bint Ally bin Abi Twalib as) aung'arishe kwa mwangaza wa tabia za bint wa Mtukufu Mtume Muhammad saww mwenyewe.

Fatimah Zahara ndani ya Quran tukufu.

1. Aya ya kumsalia Mtume Muhammad saww. Sala ya Mtume inayotakiwa :.

Ilipoteremshwa Aya hii isemayo

إن الله وملائكته يصلون على النبي يا أيها الذين آمنوا صلوا عليه وسلموا تسليما

Hakika Mwenyezi Mungu na Malaika wake humswalia Mtume, Enyi Mulioamini mswalieni Mtume na muombeeni amani. 33:56 Qur-an.

Maswahaba walimuuliza Mtume tutakuswalia vipi?

Mtukufu Mtume saww akawaambia semeni Allahumma swali Alaa Muhammad wa A'ali Muhammad

 اللهم صل على محمد وآل محمد

Maneno haya kuna makubaliano kati ya Shi'ah na ahlisuna.

Mtukufu Mtume Muhammad saww alisema :. Msinisalie sala iliyokatika,

Masahaba wakamuuliza ni swala gani iliyokatika?  Mtume Muhammad saww akajibu: Mnasema Allahumma swali Alaa Muhammad, mnanyamaza; lakini semeni Allahumma swali Alaa Muhammad wa A'ali Muhammad.

Angalia : kusema, "Swalallahu a'layhi wa salama" ni batili, (japo imezoeleka) unatakiwa kusema : "Swalallahu a'layhi wa A'alihi"

Wanazuoni wa fiqihi wanasema swala ya Mtume pamoja na A'ali zake ni wajibu katika sala tano za wajibu na endapo utasema Allahumma swali Alaa Muhammad na usiseme waala A'ali Muhammad, sala zako za wajibu ni batili.

A'ali Muhammad kilugha ni wengi sana yaani hata A'ali Aqiil A'ali Abbasi, ni katika A'ali Muhammad.

Ama A'ali Muhammad kisheria ni watu watano na kizazi chao kitukufu, Muhammad saww, Fatima as, Ally a.s Hassan, Hussain na watu tisa katika kizazi cha Hussein as kama tutakavyoona katika aya zingine katika mfululizo wa historia ya Bibi Fatimah (a.s).

Kama wewe ni mtu wa swala tano, hakikisha unamswalia Fatimah pamoja na Baba Yake. Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanasisitiza asaliwe Fatimah baada Mtume kila siku mara tano au zaidi kwa wale tunao sali sala za suna.

Mwenyezi Mungu Katika hadithi qudsi anamwambia Mtume wake Mtukufu saww:

Ewe Muhammad! Kama siyo wewe nisingeumba sayari yoyote, na kama siyo Ally nisingekuumba wewe na kama siyo Fatimah nisingewaumba wewe na Ally.

Imamu Shafii anasema kuhusu A'ali Muhammad

 يا أهل بيت رسول الله حبكم فرض من الله في القرآن أنزله.

كفاكم من عظيم القدر أنكم من لم يصل عليكم لاصلاة له

"Enyi watu wa Nyumba ya Mtume, kupendwa kwenu ni faradhi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, katika Qur'aan ameteremsha 42:23.

Inatosha kwenu kuwa ni heshima kubwa, kwamba nyinyi, yeyote asiye watakia rehema, hana swala.

Tunamtakia rehema Mtume katika kizazi cha Hashim, na tunawaudhi watoto wake? Kwa kweli hilo ni ajabu.

Ikiwa kosa langu ni kuwapenda watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad, basi kosa (dhambi) hilo sitaliombea msamaha.

Wao (Ahlubaiti) ni waombezi wangu, siku ya kufufuliwa kwangu na siku ya hesabu yangu,

Na kumsakama Shafii (kwa msimamo wake huo) ni makosa.

"kama utapasuliwa moyo wangu, itaonekana katikati yake misitari miwili, imechorwa bila ya mwandishi.

Sheria na Tawhid kwa upande mmoja, na penzi la watu wa Nyumba ya Mtume kwa upande wa pili.

Ikiwa nitakuwa muongo katika haya niliyoyasema, basi laana ya Mwenyezi Mungu imshukie muongo. "

Rejea: 

Tafsir Basaair Jz 36 UK 653-672

Majmaul Bayan Jz 4 UK 369

Almizan fyitafsiril Qur-an Jz 16 UK 366

Alburhan fyitafsiril Qur-an Jz 3 UK 335

Tafsirus Safi Jz 4 UK 201

Rejea Yanabiul Mawaddah Jz 1 UK 6

Sawaiqul Muhriqa UK 146.

Al Tafsirl Kaashif juz.6 uk 237.

Twatiqul Huda UK 109

Lima dhakartu Madh'haba Shia UK 25

Anasaihul Kafya UK 224

Yanabiul Mawaddah UK 428

Diwani ya Imamu Shafii UK 86, 107 na 172.

Fuatana nami sehemu ya pili historia ya Maasumah Fatimah bin Muhammad (s.a.w.w).