BIBI FATIMAH ZAHARA (A.S) 7
  • Kichwa: BIBI FATIMAH ZAHARA (A.S) 7
  • mwandishi:
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 19:39:16 1-9-1403

HISTORIA YA MASUMIN (A.S)

MA'ASUMAH WA PILI

BIBI FATIMAH ZAHARA (A.S)

Sehemu ya nane

ELIMU YA FATIMAH ZAHARA as.

Na kati ya sifa zingine alizojipamba nazo bibi wa wanawake wa ulimwenguni (a.s) ambazo ni wajibu kwa waislamu waume kwa wake wachukue kigezo kwake (Fatimah), nayo ni elimu... Ambapo alikuwa mjuzi, kwani alikuwa anapata elimu kutoka katika mji wa elimu naye ni Mtume saww na kutoka katika mlango wa mji wa elimu naye ni Ally bin Abi Twalib (a.s).

Pale Mtukufu Mtume saww aliposema:

أنا مدينة العلم وعلي بابها فمن أراد المدينة فليأت الباب

Mimi ni mji wa elimu na Ally ni mlango wake anayetaka elimu basi aiendee kupitia katika mlango wake.

Fatimah alichukua elimu kupitia mlango alioamrisha Mtukufu Mtume (s.a.w.w).

Hivyo Fatimah (a.s) anamjua Mwenyezi Mungu na anajua uhakika wa ulimwengu na falsafa ya maisha kama ambavyo kuwa kwake karibu na Msikiti wa Nabii kulimpa fursa ya kufuatilia sheria za Mwenyezi na kusoma aya zake tukufu, hii ni pamoja na kwamba yeye alikuwa na elimu ya tabia njema.

Nafasi yake tukufu na elimu yake nyingi imemuwezesha kulea, kufundisha na kuelekeza wanawake wa ulimwengu katika kila mji na kila zama, hususan wanawake wa ulimwengu wake ambao walikuwa wakijufunza kwake na kuchukua elimu ya Kiislamu na walikuwa wanamuuliza kila kitu. Fatimah Zahara alikuwa mwalimu na mlezi hata kwa wanaume kwa kupitia kwa wanawake.

Kutoka kwa Imamu Hassan al Askari (a.s) amesema: Mwanaume alimwambia mke wake: "Nenda kwa Fatimah bint Rasulillah muulize juu yangu, kuwa mimi ni katika (Shi'ah) Wafuasi wao au sio katika (Shi'ah) Wafuasi wao?" Akamuuliza. Zahara (a.s) akasema: Mwambie kama anafanya tuliyomuamuru na anaacha tuliyomkataza basi yeye ni katika Shi'ah (wafuasi) wetu vinginevyo hapana."

Yule mwanamke akarejea na akampa habari. Akasema: "Ole wangu nani ataniokoa kutokana na dhambi na makosa? Hivyo mimi nitakaa motoni milele, kwani asiyekuwa katika Shi'ah (wafuasi) wao atakaa motoni milele". Mke wake akarejea na akamwambia aliyoyasema mume wake.

Fatimah as akasema: "Mwambie sivyo, Shi'ah (wafuasi) wetu ni kati ya watu bora mno peponi na kila anayetupenda na mwenye kuwapenda wanaotupenda na mwenye kuwachukia maadui zetu na mwenye kujisalimisha kwa moyo wake na ulimi wake kwetu.  Sio katika Wafuasi wetu kama watakhalifu maamrisho yetu na makatazo yetu.

Katika madhambi mengine, wao pamoja na hayo lakini wataingia peponi, lakini ni baada ya kutakaswa kutokana na madhambi yao kwa balaa na misiba au kwa adhabu ya kiyama kwa aina za mateso yake, au katika tabaka la juu la moto wa Jahannamu na adhabu zake, hadi tutakapowaokoa kwa mapenzi yetu kutoka kwayo na kuwaleta kwetu.

FATIMAH KATIKA MAISHA YA NDOA

Bibi Fatimah (a.s) aligawana majukumu ya maisha ya ndoa na Imamu Aliy (a.s) majukumu ya ndani ya Nyumba yalikuwa ni juu yake na ya nje yalikuwa juu ya mume wake. Kutoka kwa Abu Ja'far (a.s) amesema: "Hakika Fatimah alichukua dhamana kwa Ally ya kazi za nyumbani, kukanda unga, kuoka mikate na kusafisha nyumba, na Ally akachukua dhamana kwake kwa yaliyo nje ya Nyumba kuleta kuni na chakula.

Siku moja Ally alimwambia:" Ewe Fatimah je, unachochote? Fatimah (a.s) akasema: Hapana... Naapa kwa aliye tukuza haki yako hatukuwa na chochote tangu siku tatu tunachoweza kukukirimu kwacho."

Imamu Aliy (a.s) akasema: Kwa nini hukuniambia?

Fatimah (a.s) akasema: "Mtume wa Mwenyezi Mungu alinikataza kukuomba chochote. Aliniambia usimuulize mtoto wa ami yangu chochote, akikuletea chochote pokea vinginevyo usimuulize".

Abu Ja' afar (a.s) akasema: Imamu Aliy (a.s) alitoka akakutana na mtu na akamkopa dinari kisha akarejea nayo na wakati wa jioni umeishaingia, akakutana na Miqdad bin al Aswad akamwambia Miqdad: "Nini kimekutoa katika wakati huu? Akasema: "Njaa, Naapa kwa yule aliye tukuza haki yako ewe Amirul Muuminina."

Mpokezi amesema: "Nilimuuliza Abu Ja'far Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa hai? Akasema: " Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa hai. Imamu Aliy (a.s) akamwambia Miqdad: "Mimi pia njaa imenitoa nimekopa dinari na nitakupa, akampa akarejea akamkuta Mtume wa Mwenyezi Mungu amekaa na Fatimah as anaswali na baina yao kuna kitu kimefunikwa, alipomaliza akaleta kile kitu wakakuta vipande vya mikate na nyama. Akasema: Ewe Fatimah hivi umevitoa wapi? Fatimah akasema: "Ni kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu anamruzuku amtakaye bila ya hesabu."

Mtume wa Mwenyezi Mungu akamwaambia nikuekeze aliye mfano wako na aliye mfano wa Fatimah? "Akasema: Nieleze, Akasema: Mfano wako ni mfano wa Zakaria alipoingia kwa Mariamu katika mihrabu akamkuta ana chakula, akasema: "Ewe Mariamu umekitoa wapi? Akasema: "Ni kutoka kwa Mwenyezi Mungu hakika Mwenyezi Mungu anamruzuku amtakaye bila ya hesabu.

كلما دخل عليها زكريا المحراب وجد عندها رزقا قال يمريم أنى لك هذا قالت هو من عند الله إن الله يرزق من يشاء بغير حساب 3:37.

Mtukufu Mtume Ally na familia yao wakala chakula hicho kwa muda wa mwezi mmoja nacho ni chakula anachokula Al Mahdi as nacho kipo kwetu (Ahlubaiti Rasulallah).

Kwa kweli Fatimah as alijitahidi kumridhisha Mwenyezi Mungu kupitia mume wake hadi Imamu Aliy (a.s) alisema siku Fatimah as alipofariki na kumzika:

اللهم إني راض عن إبنة نبيك اللهم إنها قد أوحشت فآنسها

Ewe Mwenyezi Mungu mimi nimemridhia Fatumah bint wa Nabii wako. Ewe Mwenyezi hakika nimemuacha peke yake kuwa naye karibu.

Fuatana nami sehemu ya tisa ya historia ya Maasumah Fatimah bint Muhammad saww.

Rejea:

Uyunul Akhbar UK 233

Kanzul Ummal Jz 6 UK 152.

Mustadrakul al Wasaail cha Mirza an Nuriy Jz 13 UK 25.

Tafsirul Ayashi UK 171 na 172

Al Khiswal cha Sheikh Suduq.