BIBI FATIMAH ZAHARA (A.S) 2
  • Kichwa: BIBI FATIMAH ZAHARA (A.S) 2
  • mwandishi: Hassani Bussi
  • Chanzo: mailto:busihassan@gmail.com
  • Tarehe ya Kutolewa: 19:39:32 1-9-1403

HISTORIA YA MASUMIN AS

BIBI FATIMAH ZAHARA (A.S)

Sehemu ya pili

FATIMAH ZAHARA NDANI YA QURAN TUKUFU.

2. Ni aya ya tohara (kutoharishwa kwa watu wasifanye lolote ovu maishani mwao). Watu hao wanaitwa Maasumina.

Mwenyezi Mungu anasema:

إنما يريد الله ليذهب عنكم الرجس أهل البيت ويطهركم تطهيرا

Hakika Mwenyezi Mungu anatakakukulindeni na uchafu watu wa Nyumba ya Mtume na anataka kukutakaseni moja kwa moja.

Wanazuoni wa Ahlubaiti wamepokea kutoka kwa Fatimah (a.s) kuwa Aya hii 33:33 ilishuka kwa ajili ya kuonyesha utukufu na ubora wa Ahlubaiti Rasulallah zaidi ya viumbe vyote. Na aya hii inawahusu watu watano tu na kizazi chao kitukufu kupitia Hussein (a.s).

Kisa chenyewe ni: Kutoka kwa Jabir bin Abdullah Al Ansari kutoka kwa Fatimah Zahara as bint Rasulallah saww alisema:

Nilimsikia Fatimah akisema: Siku moja baba yangu Mtume wa Mwenyezi Mungu aliingia kwangu kisha akasema: Assalam alayki Ewe Fatimah!

Nikasema: waalayka salamu!

Mtukufu Mtume saww akasema: katika mwili wangu najisikia udhaifu.

Nikasema: Mwenyezi Mungu akulinde na udhaifu (wa aina yoyote) Ewe Baba.

Kisha akasema: Niletee kishali (kisaa) kutoka Yemen nifunike nacho.

Nikakileta kishali cha Yemen, nikamfunika nacho nikawa ninamwangalia mara nikaona uso wake unang'aa kama mwezi ung'aavyo usiku wa kumi na nne, haukupita muda isipokuwa muda mfupi mara nikamuona mtoto wangu Hassan as anakuja na akasema: Amani iwe juu yako Ewe mama!

Nikasema: Waalayka salamu Ewe tulizo la jicho langu na tunda la moyo wangu.

Hassan as akasema: Ewe mama! Hapa kwako mimi ninasusa harufu nzuri kama harufu ya babu yangu Mtume wa Mwenyezi Mungu saww.

Nikasema: Ndio Hakika babu yako yupo ndani ya kishali, Hassan akaelekea kwenye kishali na akasema: Asalamu Alayka Ewe Babu! Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, je, unaniruhusu na mimi niingie pamoja nawe katika kisaa (kishali)?

Mtukufu Mtume saww akasema: Waalayka salamu Ewe mwenye usuhuba na haudhwa yangu, Nimekuruhusu, kisha Hassan akaingia ndani ya kishali.

Haikuchua muda isipokuwa muda mfupi mara nikamuona mtoto wangu Hussein as anakuja na akasema: Asalamu Alayki Ewe mama!

Nikasema: Waalayka salamu Ewe mtoto wangu  tulizo la jicho langu na tunda la moyo wangu.

Kisha Hussein akasema: Ewe mama! Hakika hapa kwako ninanusa harufu nzuri kama harufu ya Babu yangu Mtume wa Mwenyezi Mungu.

Nikamwambia: Ndio Hakika Babu yako na ndugu yako wapo hapo ndani ya kisaa (kishali).

Hussein akasogea pale penye kisaa na akasema :Asalamu Alayka Ewe Babu! Asalamu Alayka Ewe uliye teuliwa na Mwenyezi Mungu! Je, unaniruhusu nami niwe pamoja nanyi ndani ya kisaa?.

Mtukufu Mtume wa Mwenyezi Mungu akasema: waalayka salamu Ewe mtoto wangu na muombezi wa ummah wangu! Nimekuruhusu.

Hussein akaingia pamoja nao ndani ya kisaa.

Baada ya hapo mara akaja baba Hassanaini Ally bin Abi Twalib (a.s) na akasema: Asalamu Alayki Ewe bint wa Mtume wa Mwenyezi Mungu!

Nikasema waalayka salamu Ewe Baba Hassan Ewe kiongozi wa waumini (Amirul Muuminina).

Kisha akasema: Ewe Fatimah! Hakika mimi ninanusa harufu nzuri kama harufu ya kaka yangu na bin'ami yangu Mtume wa Mwenyezi Mungu.

Nikamwambia: Ndio huyo hapo pamoja na watoto wako ndani ya kisaa.

Aliy (a.s) akaelekea kwenye kisaa na akasema: Asalamu Alayka Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Je, unaniruhusu niwe pamoja nanyi ndani ya kisaa?

Mtukufu Mtume saww akamwambia: Waalayka salamu Ewe kaka yangu, Ewe wasii wangu, Khalifa wangu na mshika bendera yangu, nimekurusu, Ally (a.s) akaingia ndani ya kisaa.

Fatimah as akasema: Na mimi nikaenda kwenye kisaa nikasema Asalamu Alayka Ewe Baba, Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Je, unaniruhusu na mimi niwe pamoja nanyi ndani ya kisaa?

Mtukufu Mtume saww akasema: Waalayki salamu Ewe mtoto wangu na sehemu ya mwili wangu, nimekuruhusu. Nikaingia ndani ya kisaa, tulipokamilika wote ndani ya kisaa, Babaangu  Mtume wa Mwenyezi Mungu alishika pande mbili za kisaa na akanyoosha mkono wa kulia kuelekea mbinguni na akasema:

اللهم إن هؤلاء أهل بيتي و خاصتي وحامتي، لحمهم لحمي،ودمهم دمي، يؤلمني ما يؤلمهم، ويحزنني ما يحزنهم، أنا حرب لمن حاربهم وسلم لمن سالمهم، وعدو لمن عاداهم، ومحب لمن أحبهم، إنهم مني و أنا منهم، فاجعل صلواتك وبركاتك ورحمتك وغفرانك ورضوانك علي وعليهم، وأذهب عنهم الرجس وطهر هم تطهيرا.

Ewe Mwenyezi Mungu! Hakika hawa ndio Ahlubaiti wangu wanaonihusu na watakaonilinda (pamoja na uislamu), nyama zao ni nyama zangu, damu yao ni damu yangu, huwa ninaumia pale wanapoumia, ninahuzunishwa na lile linalowahuzunisha, mimi ni adui kwa mwenye kuwafanyia uadui wao mimi ni mpenzi wa yule anaye wapenda wao, hakika wao wanatokana na mimi na mimi natokana nao, (Ewe Mwenyezi Mungu) shusha rehema zako, baraka zako, huruma zako, msamaha wako, na radhi zako juu yangu na juu yao. Na uwaepushe wao na uchafu na uwatoharishe moja kwa moja.

Fatimah (a.s) anaendelea kusema, mara Mwenyezi Mungu Mtukufu akajibu maombi ya Babaangu Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa kujifakharisha juu ya Malaika akasema: Enyi Malaika wangu! Enyi wakaazi wa mbingu zangu! Hakika mimi sikuumba mbingu madhubuti wala ardhi iliyotandaa, wala mwezi wenye nuru, wala Jua lenye kuangaza wala sayari (dunia) yenye kuzunguka wala bahari yenye mwendo wa mawimbi wala Jahazi zenye kuelea kwenye maji, isipokuwa ni kwa ajili ya kuwapenda hawa watano ambao wamo ndani ya kisaa (kishali).

Hapo Malaika mkuu Jibrilu as akasema: Ewe Mola wangu mlezi ni akina nani wapo ndani ya kisaa (ambao unajifakharisha kwao)?

Mwenyezi Mungu Mtukufu akawaambia: Hao ni watu wa Nyumba ya utume, na asili ya ujumbe.

Wao ni Fatimah, Baba yake, mume wake na watoto wao.

Kisha Jibrilu as akasema: Ewe Mola wangu mlezi unaniruhusu na mimi nishuke hadi duniani niwe wa Sita pamoja nao?

Mwenyezi Mungu akasema: Ndio nimekuruhusu.

Jibrilu as akashuka na akasema: Asalamu Alayka Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu!

Mwenyezi Mungu Mtukufu

(العلي الأعلى)

Anakutolea salamu na amefanya maamkizi na ukarimu khaswa kwa ajili yako, na anakwaambia: (Naapa) kwa cheo changu na utukufu wangu mimi sijaumba mbingu madhubuti, wala ardhi iliyotandaa, wala mwezi wenye nuru, wala Jua lenye kuangaza wala sayari (dunia) yenye kuzunguka, wala bahari yenye mwendo wa mawimbi wala Jahazi zenye kuelea kwenye maji, isipokuwa ni kwa ajili yenu na mapenzi yake kwenu, na ameniruhusu niingie pamoja nanyi,, je, unaniruhusu Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?

Mtukufu Mtume wa Mwenyezi Mungu akasema: Waalayka salamu Ewe mwaminifu wa ufunuo (wahyi) wa Mwenyezi Mungu! Hakika ndio nimekuruhusu.

Jibrilu as akaingia tukawa pamoja naye ndani ya kisaa.

Kisha akamwambia Babaangu: Hakika Mwenyezi anakufunulieni (ameleta wahyi kwenu) anasema:

 إنما يريد الله ليذهب عنكم الرجس أهل البيت ويطهركم تطهيرا.

Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukulindeni na uchafu (Enyi) watu wa nyumba ya (Mtume) na kukutakaseni moja kwa moja. 33 :33.

Aliy as akamwambia Babaangu: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu nipe habari kuhusiana na kikao chetu hiki ndani ya kisaa kina fadhila gani mbele ya Mwenyezi Mungu?

Mtukufu Mtume saww akasema: (Naapa) kwa yule aliye nituma kuwa Nabii wa haki na akaniteua kwa ujumbe wenye kuokoa, hazitajwi habari zetu hizi katika mahfali miongoni mwa mahfali za duniani katika mahfali hiyo kukawa na mashia (wafuasi) wetu na vipenzi vyetu isipokuwa rehema zinashuka juu yao na Malaika wanawazunguka na kuwatakia Istigh'far (msamaha) hadi watakapo tawanyika.

Aliy as akasema: Hivyo basi Wallahi tumefaulu na Shi'ah (wafuasi) wetu wamefaulu Naapa kwa Mola wa al Kaaba.

Kisha Babaangu akasema: Ewe Ally! Naapa kwa yule aliyenituma kuwa Nabii wa haki na akaniteua kwa ujumbe wenye kuokoa, hazitajwi habari zetu hizi katika mahfali miongoni mwa mahfali ya watu wa duniani, ndani ya hafla hiyo kukawa humo kuna mashia (wafuasi) wetu na vipenzi vyetu, na kisha kukawa na watu wenye matatizo isipokuwa Mwenyezi Mungu atatia faraja katika matatizo yake au mwenye kero isipokuwa Mwenyezi ataondoa kero zake wala mwenye haja(yoyote) isipokuwa Mwenyezi atamkidhia haja zake.

Aliy (a.s) akasema: Hivyo basi Wallahi tumefaulu na tumetukuka (tumekuwa watukufu) vile vile Shi'ah (wafuasi) wetu wamefaulu na wametukuka (wamepanda Daraja la juu la utukufu) katika Dunia hii na Akhera Naapa kwa Mola wa al Kaaba.

Aya hii ya Ahlul kisaa ni maaruufu na kuna makubaliano kwa waislamu wote Shi'ah na ahlisuna kuwa Aya hii inawahusu Ahlubaiti kisheria (kiistilahi) na siyo kilugha.

Msikie Ummu Salama (mke wa Mtume) anasema: Iliposhuka aya hii 33:33, Mtume saww alimwita Fatumah (bint yake) na Ally na Hassan na Hussein as akawafunika guo, kisha akasema: "Ewe Mola! Hawa ni watu wa Nyumba ya yangu, basi wakinge na uchafu na uwatakase moja kwa moja."

Mama Ummu salama alipotakakuingia pamoja nao katika guo hilo, Mtume alimzuia.

Kuonyesha mke wake wa Mtume siyo Ahlulbaiti kiistilahi.

Aisha mke wa Mtume saww anasema: Mtukufu Mtume saww alitoka asubuhi akajifunika guo, mara akatokea Hassan, akamwingiza, kisha akakaja Hussein akaingia pamoja (na kaka yake) kisha akaja Fatimah Mtume akamwingiza, kisha akaja Ally Mtume akamwingiza, ndipo Mtukufu Mtume aliposoma: "Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukukingeni na uchafu watu wa Nyumba ya (Mtume) na anataka kukutakaseni moja kwa moja.

Ibun Abbas anasema: Ayatut tat'hir imeshuka kwa ajili ya Mtume saww Ally bin Abi Twalib as Fatimah na Hassan na Hussein.

Mwana Aisha na ibn Abbas hawakuhusika kuingia humo. Bali Ummu salama, yeye alijaribu kuingia Mtume akamzuia.

Na aya hii ya tat'hir "imeshuka nyumbani kwa Ummu Salama mke wa Mtume.

Rejea:

 A'waalimul ulumi ya shekh Abdullah bin Nuru llahil Baharaniy.

Mafatihul Jinani UK 843-846.

Rejea Tafsirul Khazin Jz 5 UK 259

Tarekhul Baghdad Jz 9 UK 127

Fat'hulbary Jz 7 UK 172.

Rejea sahihi Muslim Jz 4 UK 1883.

Rejea Ihqaqul haqqi Jz 14 UK 53

Rejea Tafsirul Tabariy Jz 22 UK 7

Tafsirul Ibn Kathir Jz 3 UK 491

Adurrul Manthur Jz 5 UK 376.

Huyo ndiye Fatimah bint Muhammad (s.a.w.w) mwanamke pekee katika watu waliotoharishwa (Maasumah)

Fuatana nami sehemu ya tatu historia ya Maasumah Fatimah bint Muhammad (s.a.w.w).