WATU WA 'UKHDUD' (MAHANDAKI)
  • Kichwa: WATU WA 'UKHDUD' (MAHANDAKI)
  • mwandishi: AMIRALY M.H.DATOO
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 18:1:29 2-10-1403


WATU WA 'UKHDUD' (MAHANDAKI)

Qurani Tukufu inatuambia: Sura Al-Buruj, 85, Ayah ya 4 - 9. Kuwa walioangamizwa walikuwa watu wa mahandaki. Ya Moto wenye kuni. Walipokuwa wamekaa hapo. Wakitazama yale waliyokuwa wakiwatendea waumini. Wao waliwatesa (hao) si kwa kingine ila hao walimwamini Allah, Mwenye kushinda (na) Mwenye kusifiwa. Ambaye ni Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi; na Allah ni Mwenye kuona kila kitu.

Imam wa tano, Muhammad ibni-'Ali Al-Baquir a.s. anasema kuwa siku moja Imam wa kwanza, Imam 'Ali ibni Abi Talib a.s. alimtuma mtu kwenda kwa wakuu wa dini ya Wakristo wa Najran kwa kuwauliza kuhusu watu wa Mahandaki --- na baada ya kupata majibu yao, aliwatumia ujumbe kuwa: "Kile mukihadithiacho kuhusu watu hao, si hadithi ya kweli na kwa hakika hadithi ya kweli ni kama ifuatavyo." Zu Nuwas alikuwa ni mfalme wa mwisho wa kabila la Hamir mwishoni mwa karne ya sita A.D. Yeye alikuwa ni mfuasii wa dini ya Juda ( dini ya Kiyahudi) na hivyo ilikuwa ndiyo dini ya Serikali. Dini hiyo ya Juda ilikuwa imeachwa na watu baada ya kuja Mtume 'Isa a.s. Lakini Zu Nuwas aliendelea kuwaadhibu vikali mno wale wote walioifuata dini ya Mtume 'Isa a.s. na alitumia mbinu mbalimbali na hila za kuimaliza dini hiyo katika kila sehemu za ardhi. Yeye alikuwa akiwapendelea mno Mayahudi na kuwatesa vikali mno Wakristo. Yeye aliwateketeza Wakristo popote pale walipoonekana katika ufalme wake. Yeye alikuwa ameamua kuusambaza Uyahudi katika kila sehemu za dunia hii huku akizimaliza na kuzifyeka dini zingine zote. Yeye hakubakiza juhudi zake zozote katika kufikia lengo lake hilo. Yeye vile vile alikuwa akizishambulia nchi zozote zile ambazo zilikuwa zikifuata dini mbali na dini ya Juda. Na vile vile alikuwa mwepesi wa kuzishambulia sehemu zozote zile zilizokuwa zikifuata dini mbali na dini ya Juda na hatimaye kuwalazimisha kuifuata dini yake.

Allah swt alimtuma Mtume mmoja wa Kihabeshi kwenda kuhubiri watu wa Habeshi. Mtume huyo alipambana sana na mfalme huyo ambaye alikuwa akiipigania dini yake ya Kiyahudi kwa hali na mali. Siku moja alipata habari kuwa wakazi wa Najran wamekubalia dini ya Mtume 'Isa a.s. isipokuwa Wayahudi wachache tu ndio waliokuwa wamebakia katika dini yao. Habari hizi zilimghasi na kumbughudhi mno huyo Zu Nuwas kiasi kwamba aliupoteza usingizi wake na kukosa raha kabisa na kufikia uamuzi wa kuishambulia sehemu hiyo kwa haraka iwezekanavyo. Na hivyo alilitayarisha jeshi kubwa mno na kuwapatia silaha nyingi zilizo nzuri na alijitolea mwenyewe kuongoza vita hivyo vya kuishambulia Najran. Kwa hakika alikuwa amewaghadhabikia mno wakazi wa Najran kiasi kwamba alikuwa anataka awarudishe wote kwa pamoja katika dini ya Kiyahudi kwa haraka iwezekanavyo.

Alipoukaribia mji wa Najran, aliwataka baadhi ya watu waliokuwa wameheshimika huko kuja kuwawakilisha wakazi wa Najran katika mazungumzo yao pamoja na Zu Nuwas. Wakati watu hao walipoletwa mbele yake, yeye aliwaambia: "Mimi nimekuja hapa baada ya kupata habari kuwa wakazi wote wa mji wenu wameiacha dini ya Kijuda na wamekubali dini ya Mtume Mtume 'Isa a.s. kwa sababu ya kudanganywa na kushawishiwa na Mkristo wa Kikatoliki aitwaye Dus. Hivyo mutambue kuwa mimi nimefika hapa pamoja na jeshi langu hili lililo kubwa sana ili kuirudisha dini ya Kijuda hapa Najran na kuutokomeza kabisa Ukristo. Swala hili la kuwaiteni nyinyi hapa ni kuwatakeni nyinyi murejee kwenu mukaongee na wazee wenu ili wote wakazi wa Najran warudie katika dini ya Kijuda na kuiachilia mbali dini ya Kikristo. Kuna mambo mawili tu yaliyo bayana mbele yenu. Ama mukubali kuingia katika dini ya Kijuda ama sivyo mujiweke tayarri kwa adhabu kali kabisa ambayo hayatakuwa chini ya adhabu ya kifo na maangamizo."

Wawakilishi hawa wa wakazi wa Najran walikuwa ni watu ambao walikuwa na imani thabiti ya dini yao na hivyo wote kwa pamoja walimwelezea wazi wazi mfalme Zu Nuwas kuwa: "Sisi kamwe hatutaki ushauri na uwakilishi wa mtu yoyote yule. Sisi tumeshatambua na kuipata njia ya haki na uongofu na hivyo tunafuata mafunzo na maamrisho yake. Sisi kamwe hatuogopi mauti. Sisi tupo tayari kukabiliana na hali yoyote ile itakayotokezea na tutakabiana nayo ipasavyo na hata kama itabidi kujitolea mhanga tutafanya hivyo ili kuilinda dini na imani yetu."

Zu Nuwas alikuwa hakutegemea kupewa majibu makali na yaliyo wazi kabisa kuhusu msimamo wa wakazi wa Najran, na hivyo alizidi kukasirika. Alifikia uamuzi wa kuwamaliza na kuwateketeza Wakisto wa Najran. Yeye aliwaamuru majeshi yake kuchimba mahandaki na kuyajaza kwa moto mkali kabisa. Yeye pamoja na majeshi yake walikaa kandoni kwa kuzunguka mahandaki hayo kwa kushuhudia hali mbaya kabisa. Baadaya ya hapo, alitoa amri ya kuwa waumini wote wa dini ya Kikristo waletwe mbele yake. Kwa kutolewa amri hiyo, majeshi yake yalitoka kuwatafuta Wakristo wote na kuwaleta mbele ya Zu Nuwas. Ikatolewa amri ya kuwatupa hao katika mahandaki hayo yaliyokuwa yakiwaka moto mkali sana. Wengi walisukumwa na kuchomwa hivyo na wengine walichinjwa. Vile vile walikuwapo wengine ambao walikatwa viungo vya mwili kama masikio, pua, mikono na miguu. Hivyo ndivyo Najran ilivyotokana na watu ambao waliikuablia dini ya Mtume 'Isa a.s. Inasadikiwa kuwa Zu Nuwas amewaua watu zaidi ya elfu ishirini (20,000) katika kulazimisha dini ya Kijuda.

Mmoja wa Wakristo alipoyaona mateso na maagamizo waliyokuwa wakitendewa wafuasi wenzake wa Kikristo, alifanikiwa kutoroka na kwenda mjini Roma akipitia majangwa na milima hadi kwa Czar, aliyekuwa mfalme, na kumpa habari zote zilizowafikia Wakristo wa Najran chini ya amri za Zu Nuwas na alitoa ombi la kupatiwa majeshi ili kuweza kulipiza kisasi na kumshinda.

Czar alikuwa Mkristo kwa dini na alihuzunika mno kwa kusikia unyama wa Zu Nuwas. Yeye alimwambia yule mtu kutoka Najran kuwa: "Kwa hakika nchi yenu ipo mbali mno na kwetu na hivyo mimi siwezi kuchukua hatua yoyote ile dhidi ya Zu Nuwas. Hata hivyo mimi ninamtumia risala maalum mfalme wa Habeshi, Najjashi (Negus) ambaye pia ni Mkristo. Ufalme wake upo karibu na Yemen, ufalme wa Zu Nuwas. Kwa hakika itakuwa rahisi kwa Najjashi kumshinda Zu Nuwas."

Mfalme wa Kiroma alimtumia risala maalum Najjashi akimtaka amng'oe Zu Nuwas na kuwakomboa Wakristo wa Najran. Mtu huyo aliichukua barua hiyo ya Czar na alikwenda Habeshi na akatoa habari zote za ukatili na mauaji wa Zu Nuwas aliyowafanyia Wakristo wa Najran. Najjashi alikubali kuishambulia Yemen na kuikomboa kutoka kwa Zu Nuwas. Zu Nuwas naye pia alijitayarisha na kujitolea kukabiliana na Najjashi. Hatimaye kulizuka vita vikali mno baina yao ambamo Najjashi alipata ushindi na Zu Nuwas aliuawa katika vita hivyo. Najjashi aliiunganisha Najran pamoja na ufalme wake na kuirudisha dini ya Kikristo huko ambayo ndiyo ikawa dini ya Watawala.

Vile vile kuna habari ifuatayo nimeipata katika utafiti mwingine: Kulikuwapo na mwanamke mmoja muumini pamoja na mtoto wake aliyekuwa mchanga mikononi mwake. Nao pia walikuwa watupwe ndani mwa mahandaki yenye moto mkali na pale alipoukaribia moto huo, mapenzi ya mtoto wake aliye mchanga, yalimfanya arudi nyuma. Mtoto huyo aliyekuwa bado yu mchanga, kwa amri za Mwenyezi Mungu akamwambia mamake kwa sauti kubwa "Ewe Mama yangu ! Ruka ndani mwa mahandaki yawakayo moto mkali pamoja nami kwani moto huu ni mdogo kabisa katika mtihani wa Mola wetu." Kwa hayo mwanamke huyo alijitupa motoni humo pamoja na mtoto wake huyo. Lakini kwa amri za Mwenyezi Mungu, Mtume, waumini wote, mwanamke huyo pamoja na mtoto wake walikuwa salama u salimini katika mahandaki hayo bila ya kudhurika hata kidogo.

Kwa kusoma kisa hicho kutoka Qur'an tukufu, kwa hakika nyoyo zetu zimejawa na majonzi na masikitiko kwa kuona udhalimu ulivyokuwa katika zama za ujahiliyya. Lakini hata katika zama hizi tunazoziita sisi za maendeleo, bado udhalimu huu unaendelea humu duniani kidhahiri na batini kwa kupitia njama tofauti tofauti. Mfano mmoja wa hivi karibuni ni wa Raisi Saddam wa Iraq, alivyowaua Mashia ambao ndio raia wake. Kila mtu mwenye akili na busara atakubaliana kuwa ni dhuluma tupu kuwatesa na kuwaua na kuwa teketeza watu ambao wamekuwa wakifuata madhehebu kwa mappenzi ya Ahlul-Bait ya Mtume Muhammad s.a.w.w. Someni vitabu vya historria na mutaona kuwa Mashia wameuawa kwa mamilioni wakiwemo wanaume, wanawake na hata watoto walio wachanga ati kwa sababu ni Shia wa Imam 'Ali a.s.

Katika Qur'an tukufu kuna mahala pengi panapoelezewa habari za waumini kuhukumiwa adhabu za kuuawa na kuchomwa moto. Wadhalimu watendaji hao wanapofanya hayo hushuhudiwa na watazamaji huku wakiona furaha. Kwa hakika Qur'an kwa uwazi kabisa unawalaani si wadhalimu tu bali hata wale wanaokaa kuyatazama dhuluma wafanyiwao waumini na wale ambao wanaangalia tu bila ya kujitahidi kufanya lolote ili waweze kuzuia hayo yasitokee. Ujumbe huu ni kwa watu wa Makkah ambao walikuwa wakiwahukumu kwa kuwaonea wale wote waliokuwa wameukubali Uislamu, na vivyo hivyo inatumika kwa ajili ya mateso na mauaji ya kikatili dhidi ya waumini ambao wanawafuata kikamilifu Ahlul-Bait a.s.

Na kwa sababu hii ndiyo maana imesemwa katika Ziyarat: "La'anallahu Ummatan Zahamatka wa La'anallahu Ummatan Sami'at bidhalika wa radhiat bihi." Yaani "Laana ya Allah swt iwe juu ya wale wote wasiotenda uadilifu kwako na walaaniwe wale wote waliosikia haya na wakaridhika nayo."

MWISHO