KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
KWA NINI IMAM HUSEIN (A.S) ALISIMAMA DHIDI YA UONGOZI WA YAZIDI?
Tungetaka kuchukuwa fursa hii kujaribu kutazama katika baadhi ya maswali ambayo watu wengi hujiuliza kuhusu tukio la Karbala na hususan msimamo wa Imam Hussein(as) kuhusu hali ilivyokuwa wakati huo mpaka ikambidi achukuwe msimamo aliyouchukuwa. Yako maswali mengi tu ambayo watu hujiuliza sana,na kwa kadri ya uwezo atakaotupa mwenyezi Mungu(swt) tutajaribu kuyajibu kulingana na utafiti uliyofanywa na wasomi na hadithi zilizo nukuliwa kuhusu tukio la Karbala na aliyoyaisema Imam Hussein(as).
Swali la kwanza ni: kwa nini Imam Huseni(a.s.) alitoka dhidi ya kiongozi na ufalme wa wakati huo?
Kwa nini hakuamua kutulia tu Madina kama walivyokuwa wakimshauri watu kuwa atulie tu?
Je hakuenda kinyume na aya ya Qur’an inayosema kuwa: tusijitie katika maangamizi? Kwa sababu Imam alijuwa atakufa na mbali na kufahamu hivyo bado akatoka?
Maswali haya yote tunaweza kuyajibu kwa jawabu moja tu ambalo litatosheleza maswali hayo yote yaliyoulizwa. Kwa kujibu maswali haya itabidi niingie kidogo katika historia ya Kabla ya tukio la Karbala na kuangalia ni nini kilimsababisha imam mpaka akasimama dhidi ya Yazid,kiongozi dhalimu wa wakati huo.
Imam Hussein(as) wakati akitoka madina kuelekea Makkah na baadaye Karbala,alikuwa akiyasema maneno haya yafuatayo:
“Hakika mimi sikutoka kwa ajili ya kutaka uongozi wala kufanya ufisadi,wala kufanya dhulma,bali nimetoka ili kutafuta suluhu katika umma wa babu yangu,nataka kuamrisha mema na kukataza maovu, na niyapeleke mambo kulingana na alivyoishi babu yangu mtume(saww) na baba yangu Ali bin Abi Talib(as)”
Kulingana na hadithi hii, yapo mambo yaliyojitokeza hapo, nayo ni kuwa kumbe imam (as) alitoka kwa ajili ya malengo Fulani,nayo ni kuamrisha mema na kukataza mabaya,na vile vile kuyapeleka mambo kulingana na jinsi mtume(saw) na Imam Ali(as) walivyoishi. Na kwa nini imam alisema kuwa anataka kuamrisha mema na kukataza mabaya? Hii ni kwa sababu hali ilivyokuwa wakati huo ilikuwa mbaya sana. Haki ilikuwa haitekelezwi tena na batili haikatazwi. Akithibitisha maneno haya katika hadithi nyingine iliyonukuliwa kutoka kwake kuwa:
“je,hamuoni kuwa haki haifanywi tena na batili haikatazwi?”
Hii inaonyesha ni jinsi gani umma wa mtume (saww) ulivyokuwa baada yake. Na kwa kutoka kwake imam dhidi ya kiongozi huyo dhalimu Yazid anasema kuwa baada ya kufuatwa na watu waliokuja ili kutafuta mkono wa imam kumbai(kuonyesha hali ya kukubali uongozi )alisema kuwa:
“yazid ni mtu fasiki,mnywa pombe,mwenye kuwauwa watu wasiyo na hatia,kwa hivyo mfano wangu hauwezi kukubali mfano wa mtu kama yazid”
Sasa ikiwa huyu ndiye aliyekuwa kiongozi wa wakati huo,je Uislamu wa mtume(saww) uliyo safi kutokana na aina yoyote ya makosa ungetufikia kweli sisi katika zama hizi? Kwa sababu kati ya mambo mtu mwenye kufikisha dini lazima awe nayo ni tabia njema na kuishi kulingana na uislamu unavyosema. Kuacha makatazo na kufanya maamrisho. Je sasa ikiwa mtu atafanya kinyume na maamrisho ya uislamu na kuyafanywa yanayokatazwa , atakuwa na nafasi ya kuufikisha uislamu ipaswavyo au itakuwa kinyume? Jawabu ni kuwa itakuwa kinyume tu na wala hakuna manufaa yoyote yatakayo patikana kutokana na mtu kama huyu. Na hivyo ndivyo alivyokuwa Yazid bin Muawiyyah. Kwani alizini na hata madada zake na kufanya aina ya uchafu ambao haukubaliki katika uislamu hata kidogo.
Ikiwa hali hivyo ndivyo ilivyokuwa, je kulikuwa na haja ya mtu kusimama na kupinga hali kama hiyo kuendelea ama hakukuwa na haja ya mtu kufanya hivyo? Jawabu ni kuwa bali ni lazima mtu apatikane wa kuweza kukataza mambo kama haya kuendelea. Kwa ahkamu za kifiqhi tunauita wajibu huu kwa jina(waajibul kifai)kwamba akisimama mmoja katika kutekeleza wengine wanakuwa wamesamehewa kwa jambo kama hilo. Sasa turudi katika sheria tuangalie inasemaje kuhusu kuitetea dini ya mwenyezi Mungu(swt),tunaona kwamba ni wajib kwa kila muislamu kuihami dini na yanayoambatanishwa nayo,mahala popote pale atakapo kuwa. Ndio maana hata makafri wanapoichezea Qur’an,waislamu husimama na kupinga kitendo kama hicho.
Sasa ikiwa hii ndiyo hali halisi,turudi katika zama za imam Hussein(as) zilivyokuwa na uislamu ulipofikia wakati wake. Hatuwezi fahamu ukweli wa hali hadi turudi katika maneno ya imam (as) alivyokuwa akiielezea zama aliyoishi. Na hali kama hiyo tumeibainisha hapo mbeleni. Ila katika kubainisha hali zaidi na msimamo wa imam,naomba tufaidike kutokana na hadithi ya imam Hussein(as) aliposema baada ya kufuatwa na wajumbe wa Yazid wakitaka awape bai’ah(kukubali uongozi),alisema:
“Na tuupungie uislamu mkono(kuuaga) ikiwa atapewa uongozi mtu kama Yazid bin Muawiyyah” hii inaonyesha kuwa hakukuwa na njia nyengine mbadala ya ile aliyoichukuwa imam (as) ambayo ni kusimama na kuipinga dhulma ambayo ilikuwa imekithirisha na Yazid malu’uni. Kwa hivyo tumeona kuwa laiti imam(as) hangesimama basi ndiyo ingekuwa kwaheri uislamu. Ladba mtu anaweza kuuliza swali kuwa; mwenyezi Mungu(swt) anaahidi kuwa yeye ndiye aliyeteremsha dhikri nay eye ndiye atakayeihifadhi,sasa ni vipi mtu adai kuwa uislamu ungepotea?
Jawabu ni kuwa,mwenyezi mungu(swt) anauhifadhi uislamu ,Qur’an na chochote kinachohusika nao kwa kupitia waja wake wema. Kwa sababu uislamu lazima uendelee katika kila zama. Na haipaswi ukosekane hata kidogo katika hii ardhi ili lengo la kuumbwa mwanadamu litimie kama asemavyo Mwenyezi Mungu katika Qu’an kuwa, “Na wala sikuwaumbeni wanadamu na majini ila tu waniabudu mimi” 1. Sasa inabidi uislamu ubaki katika ardhi ili upitishwe kutoka kwa kizazi hadi chengine ili watu waendelee kumwabudu mweyezi Mungu(swt). Ambaye ndiye mwenye kustahiki ibada, na wala asiyekuwa Mungu inakuwa shirki. Sasa ikiwa hiyo ndiyo hali halisi hivyo basi inakuwa ni wazi kuwa uislamu unahifadhiwa kwa kupitia kwa waja wema ambao ni wasomi wa kiislamu(maulamaa) ambao haijapita zama wakakosekana. Kama vile watu wanavyo jitahidi katika kuihifadhi Qur’an na hadithi za mtume(saw) katika vichwa vyao,hii ni njia moja wapo ya kuuhifadhi usilamu. Na katika njia za kuuhifadhi uislamu ni kusimama na kupinga yeyote Yule ama chochote kinachoweza kusambaratisha harakati za uislamu. Na Yazid alikuwa ni katika kundi la kusambaratisha uislamu. Na laiti angeachiwa yeye basi uislamu ungepotea,na ili ahadi ya Mungu itimie imam akasimama kuunusuru akisema kuwa :
“Ikiwa dini ya Muhammad(saw) haiwezi kusimama ila kwa kuuawa mimi basi enyi mapanga nichukueni” na kweli imam akafa kuutetea uislamu,na kwa kupitia yeye na maswahaba wake 72 uislamu umebaki hadi leo na utaendelea kubaki hadi siku ya mwisho ambayo mwenyezi Mungu ataamua mwenyewe kuwa hukumu isimame kwa waja wake(yaani siku ya kiyama).
1:Suratu Adhaariat, aya. 56.