IBADA NA USHUPAVU
  • Kichwa: IBADA NA USHUPAVU
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 17:59:48 20-7-1403

 BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

IBADA NA USHUPAVU

SIFA YA PILI NI IBADA NA USHUPAVU

Wafuasi wa Imam Mahdi wanachukuwa kigezo kwa Imam wao katika kufanya ibada zao, usiku na mchana huumalizia kwa kumtaja Mola wao.

Imam Safiq (a.s) akiwazungumzia watu hao anasema hivi:-

"Usiku mpaka asubuhi huwa wanamuabudu Mola wao na mchana huumalizia kwa kufunga[1]" na katika maneno mengine anasema hivi:-

"Watu hawa wakiwa juu ya migongo ya farasi huwa wanamtaj Mola wao[2]

Dhikiri hizi za Mwenyeezi Mungu ndizo zilizowafanya wao kuwa kama ni vyuma katika ukakamavu wao, kiasi ya kwamba hakuna kitu chochote kile kinachoweza kuuvunja ukakamavu wao. Ima Sadiq (a.s) anasema:-

"Wafuasi hawa ni watu ambao nyoyoza utafikiria kipande cha chuma[3]".

SIFA YA TATU NI KUJITOLEA MUHANGA NA KUTAFUTA SHAHADA

Utambuzi wa hali ya juu wa wafuasi hao kuhusiana na Imam wao kumezifanya nyoyo zao zijae mapenzi ya Imam ndio maana katika uwanja wa vita wanamzunguka Imam ili kumkinga na mabalaa, na hujitolea muhanga kwa Imam wao, kwani yeye ni mfano wa kito katika pete.

Imam Sadiq (a.s) anasema:-

"Wafuasi wa Imam Mahdi katika uwanja wa vita humzunguka Imam wao na humuhifadhi kwa kujitolea muhanga roho zao[4]"

Imam anasema tena "Wao hutmani kufa katika njia ya Mwenyeezi Mungu[5]".

SIFA YA NNE NI USHUJAA

Wafuasi wa Imam Mahdi wana kigezo cha Imam wao katika ushujaa, na ni watu walio mashupavu, Imam Aliy (a.s) akiwasifu wafuasi hao anasema:- "Wao ni kama simba waliotoka vichakani mwao ikiwa watataka kuuvunja mlima basi wataung'oa kutoka sehemu yake[6].

SIFA YA TANO NI KUSUBIRI

Ni kitu cha wazi kuwa kupambana na dhulma ya kilimwengu na kusimamisha serikali ya uadilifu katika ulimwengu inabidi kwanza ukumbane na matatizo yaliyo makubwa lakini wafuasi wa Imam Mahdi katika kuhakikisha malengo ya Imam wao huyanunuwa matatizo hayo kwa roho zao, lakini kwa kutokana na ikhlasi walizonazo kufanya kwao hivyo hawakuhesabu kuwa ni kitu kikubwa.

Imam Aliy anasema :-

"Wao ni kikundi ambacho kwa kutokana subira zao mbele ya Mwenyeezi Mungu huwa hawamsumbulii Mola wao na kwa kutokana kwamba wao wamezitolea muhanga roho zao mbele ya Mola wao huwa hawajifaharishi na jambo hilo, na wala hawahesabu kuwa ni kitu kikubwa walichokifanya.

SIFA YA SITA NI UMOJA NA FUNGAMANO LA NYOYO ZAO

Imam Aliy (a.s) katika kusifu fungamano la roho zao na umoja walionao anasema hivi:-

"Wao ni moyo mmoja na wamefungamana kisawasawa[7]".

Fungamano hili lanyoyo ni kutokana na kwamba wao hawana kiburi wala hawayatilii maanani matakwa ya nafsi zao, wao kwa kutokana na imani sahihi wamekuwa jora moja na wana malengo mamoja, na hilo ndilo lililowafanya wasimame na kitu hichi ni moja kati ya sababu zenye kuwaletea ushindi.

SIFA YA SABA NI KUIPA MGONGO DUNIA

Imam Aliy (a.s) katika kuwasifu wafuasi hao anasema hivi:-

"Imam Mahdi atachukuwa kauli kutoka kwao ya kwamba wao wasirimbike dhahabu wala fedha na wala wasiweke ghalani ngano wala shairi[8]".

 (Wao wana malengo makubwa na matumaini wanayotaka kuyahakikisha, na mali za kidunia hawatakiwi kuzifanya kua ndio malengo yao, kwa hiyo basi watu ambao hubakukwa na roho kwa kuona mali za dunia na hutetemekwa na nyoyo wao hawawezi kuwa wafuasi wa Imamu.

Yaliyopita ni baadhi ya sifa za wafuasi wa Imam na kwa kutokana na kwamba wao wana  sifa hizi maalum, ndio maana kuna hadithi nyingi zilizowasifu na kuwatukuza, na Maimamu wamewatukuza wafuasi hao.

Mtume Muhammad (s.a.w.w) katika kuwasifu watu hao amesema hivi:-

"Wao ndio wabora wa umma huu[9]".

Katika maneno mengine ya Imamu Aliy anasema hivi:-

"Baba yangu na mama yangu ni uhanga wa lile kundi dogo ambalo majina yake hayatambulikani katika ardhi[10]".

Wafuasi wa Imamu hupatikana katika matabaka tofauti, lakini ni kwa kuangalia sifa na kustahiki kwao kuwa na nafasi kama hiyo, imepokewa katika hadithi kuwa Imam Mahdi juu ya wale wafuasi maalum aliokuwa nao ambao ni watu 313 bado atakuwa na jeshi jengine la watu 10000, na waumini wengi watakuwa katika kumsubiri yeye.

D) MATAYARISHO YA KIJUMLA JUML

Katika zama tofauti za tarehe za Maimamu ilionekana kuwa watu hawakuwa na matayarisho ya lazima ili waweze kufaidika zaidi na kuwepo kwa Imamu, wao katika zama tofauti neema ya kuwepo Imam hawakuitambua, na hawakuweza kufaidika kama inavyostahiki na ule mto wa uongofu, ndio maana Mwenyeezi Mungu (s.w) Imamu wake wa mwisho akamficha mpaka zifikie zile zama ambazo matayarisho kamili yatakuwa yamepatikana hapo ndipo atapodhihiri Imamu ili awatowe kiu ya elimu ya kumtambua Mwenyeezi Mungu watu wote.

Kwa hiyo basi kupatikana matayarisho ni moja kati ya shuruti muhimu za kudhihiri kwa yule aliyeahidiwa kuja kutengeneza ulimwengu, kwani kwa kupatikana matayarisho ndio kutafikia natija ya mapinduzi yanayotakiwa kupatikana kwa kupitia kiongozi huyo.

Katika Qur-ani kumwzungumziwa kundi la bani Is-rail ambalo lilikuwa likidhulumiwa na Jalut ambaye ni kiongozi dhalimu, ambapo wana wa Is-rail walimtaka Nabii wa zama zao awachagulie kiongozi atakayewaongoza kwenda kupambana na Jalut, kisa hichi katika Qur-ani kimekuja hivi:-

"hivi hamjaona kundi miongoni mwa watu wa bani Israil waliokuja baada ya Mussa ambao walimwambia Nabii wao, tuchagulie kiongozi ili tuweze kupigana katika njia ya Mwenyeezi Mungu. Nabii wao akawaambia inawezekana mkapewa amri hiyo na msiitekeleze wakasema litawezekana vipi jambo hilo kwamba sisi tusipigane katika njia ya Mwenyeezi Mungu hali ya kwamba tumetolewa sisi na watoto wetu katika nyumba zetu, lakini pale walipoamrishwa kupigana wote wakakimbia isipokuwa wachache miongoni mwao, na Mwenyeezi Mungu anawaelewa madhalimu".

Kutaka kwao kiongozi watu hao katika vita ni moja kati ya ishara ya kujitayarisha kwao, ingawaje kundi kubwa lililegea miongoni mwao, na ni wachache miongoni mwao waliobakia mpaka mwisho wa vita.

Basi zama za kudhihiri Imam ni zile zama ambazo watu watakuwa ndani ya nyoyo zao ni wenye kutaka uadilifu wa kijamii, amani za kitabia, akili zilizo sawa na kuchanuwa mambo ya kimaana ndani ya nyoyo zao, kiu ya kutaka uadilifu itakuja katika zama ambazo watu watakuwa wamechoshwa na kutokuwepo uadilifu, ubaguzi, na pale watapoona kuwa haki za madhaifu zinachukuliwa na watu wenye nguvu, na nyenzo za kimaisha ziko mikononi mwa watu wachache, na katika zama hizi hizi watu wengi katika jamii watahitajia chakula,huku wengine wakiwa wanajijengea majumba ya kifakhari na katika mihafala yao wanatayarisha vyakula vya aina tofauti hali ya kuwa wengine hawana chakula cha kukila.

Zama ambazo ufisadi wa kitabia utakuwa umeenea katika aina tofauti na watu watakuwa wanashindana katika kutenda matendo yenye kwenda kinyume na maadili, na watakuwa wanajifakharisha kutokana na matendo yao maovu, au watakuwa wako mbali na misingi ya Mwenyeezi Mungu, na matendo yale yenye kwenda kinyume na ubinaadamu ndiyo yatakayofanywa kuwa kanuni za msingi, na kupelekea nidhamu za familia kupwaya, na watoto kutokuwa na kiongozi na kumiminika katika katika jamii, zama hizi basi ambazo watu watakuwa wanatamani kudhihiri kwa uongozi wenye amani utakaoleta tabia na matendo mema na kuzituliza akili, kupatikana Imam katika zama hizi kutakuwa ni zawadi kubwa kabisa, na matendo mema na amani itaenea katika kila pembe, kabla ya kudhihiri kwake watu watakuwa wameonja ladha tofauti lakini bado watakuwa hawajaridhika na maisha waliyokuwa nayo, na watakuwa wana kiu ya mambo ya kimaana atakayokuja nayo Imam (a.s), ni wazi kabisa kuwa matamanio ya kuonana na Imam yatafikia upeo katika zama ambazo watu watakuwa wameonja nidhamu tofauti za kiserikali zilizopangwa na wanaadamu na pale watakapofikia na kuelewa kuwa njia pekee ya kuokoka na maovu ni kumpata kiongozi anyetoka kwa Mwenyeezi Mungu ambaye ni Mahdi (a.s), ambaye ayawaletea watu njia pekee yenye maisha safi na miongozo ya Mwenyeezi Mungu.

Kwa hiyo basi watu wanatakiwa waelewe kwa undani umuhimu wa Imam na waelekee katika matayarisho ya kudhihiri na wajitahidi katika kutayarisha matayarisho hayo, na waondowe vikwazo ambavyo viko katika njia ya kudhihiri kwake, iwapo watu watafanya hivyo hapo ndipo Imam atakapodhihiri.

Mtume Muhammad (s.a.w.w) akisifu zama za mwisho na zama za kabla ya kudhihiri anasema:-

"Zama zitafika ambapo mtu muumini atakuwa hana ehemu ya kujificha kutokana na shari na dhulma, katika zama hizo basi Mwenyeezi Mungu atamdhihirisha kiongozi atakayetoka katika kizazi chetu[11]".

 

[1] Rejea yawmul-khalas, ukurasa wa 224

 

[2] Rejea Bukharul-an-war, juzuu ya 52, ukurasa wa 308.

 

[3] (Rejea Bukharul-an-war, juzuu ya 52, ukurasa wa 308).

 

[4] (Rejea kitabu kulichopita).

 

[5] (Rejea kitabu kilichopita).

[6] (Rejea kitabu Yawmul-khalas, ukurasa 224).

[7] (Rejea kitabu kichopita).

[8] Rejea kitabu Muntakhabul-athar.

[9] Rejea kitabu Yawmul-khalas, ukurasa wa 224.

[10] (Rejea kitabu Muujamu ahadiythi Imam Mahdi, juzuu ya 3, ukurasa wa 101).

[11] Rejea kitabu Iqdud-dirar, ukuirasa wa 73.

MWISHO