KUZALIWA KWA NABII MUSA NA NABII HARUUN.
  • Kichwa: KUZALIWA KWA NABII MUSA NA NABII HARUUN.
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 17:20:45 1-9-1403

KUZALIWA KWA NABII MUSA NA NABII HARUUN.

Siku moja Firauni aliota usingizini mwake ndoto ya moto umetoka Baitul Muqaddas ukielekea Misri kisha ukaunguza nyumba zote wanazoishi ndani yake Wamisri isipokuwa nyumba za Ma-Bani Israil. Mara tu alipoamka aliwaita haraka wachawi wake na wapiga ramli ili wamfasirie ndoto yake. Wakamfasiria wakamwambia, "Atatokea kijana miongoni mwa Ma-Bani Israil ambaye ndiye atakuwa sababu ya kuangamiza utawala wako na kubadili dini yako ewe mfalme!" Mmoja wao akamshauri Firauni ya kwamba, kila mtoto atakayezaliwa wa kiume wa Kibani-Israil auwawe.

Firauni lilimpendeza sana shauri hili. Ndio maana tokeya hapo Firauni aliwatuma askari zake wamchinje kila mtoto mchanga wa kiume wa Ki-Bani Israil. Lakini wakubwa wanaosimamia kazi za ujenzi wa majumba ya Firauni wakashtaki kwa Firauni wakamwambia wakasema: "Ukiwa mtindo huu wa kuwauwa watoto wakiume utaendelea baadaye watapungua wafanya kazi wanaume wa Ki-Bani Israil wanaotengeneza matofali ya kuchomwa."

Firauni alifikiri kisha alilikubali ombi lao akatoa shauri zuri la kuwaridhisha wajengaji akasema Firauni: "Mwaka mmoja nitasimamisha wasichinjwe watoto wakiume na mwaka mwingine wachinjwe ili wasizidi idadi yao. Na pia wakati ule ule watakuwa wanao wafanyakazi wa kutosha."

Kwa bahati nzuri mke wa Imraan akamzaa Nabii Haruun A.S. katika mwaka ule ambao wasiochinjwa watoto wa kiume wa Ki-Bani Israil. Hivyo hakufanywa kitu chochote kile. Lakini kwa bahati mbaya Nabii Musa A.S. alizaliwa katika ule mwaka ambao wanachinjwa watoto wa kiume.

Hivyo mama yake Musa hakujua jinsi ya kufanya ili kusudi amuokoe mwanawe. Lakini kwa kuwa Mwenyezi Mungu S.W.T. ni Mjuzi wa mambo yote yanayotokea mbinguni na ardhini, hivyo alimfundisha kwa ilhamu njia ya kumuokoa Nabii Musa, akamfunulia kwamba ikiwa atakhofia kumweka nyumbani kwake, basi amtiye mwanae kwenye kisanduku na kisha akitie katika mto wa Nile na Mwenyezi Mungu Mtukufu atapitisha jambo la kumuokoa. Akafanya hivyo kama alivyoamrishwa na Mola wake, kisha akakitia kisanduku kile mtoni kikawa kinachukuliwa na maji. Lakini hata hivyo wasiwasi ulimwingia moyoni mwake kumfikiria mwanae, kwa hali hiyo akamtuma dada yake Nabii Musa akifuatie kile kisanduku mpaka mahali kitakapofikia. Akaondoka kukifuata akawa akimwangalia kwa mbali na huku akijihadhari asitambulikane na Firauni na watu wake kama ni dada ya Nabii Musa. Kisanduku kile kikafika mpaka kwenye ufuko wa jumba la Firauni. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Surat Taha Aya ya 38 na ya 39,

إِذْ أَوْحَيْنَا إِلَى أُمِّكَ مَا يُوحَى * أَنْ اقْذِفِيهِ فِي التَّابُوتِ فَاقْذِفِيهِ فِي الْيَمِّ فَلْيُلْقِهِ الْيَمُّ بِالسَّاحِلِ يَأْخُذْهُ عَدُوٌّ لِي وَعَدُوٌّ لَهُ وَأَلْقَيْتُ عَلَيْكَ مَحَبَّةً مِنِّي وَلِتُصْنَعَ عَلَى عَيْنِي

Maana yake, "Tulipomfunulia mama yako yaliyofunuliwa. Ya kwamba mtie (mwanao kwanza) katika kisanduku, na kisha kitie mtoni, na mto utamfikisha ufukoni. Atamchukua adui yangu (Firauni) na adui yake. Na nimekutilia mapenzi yanayotokana Kwangu, na ili ulelewe machoni Mwangu"

Kwa bahati nzuri kisanduku kile kiliokotwa na wafanya kazi wa kike wa Bibi Asia mkewe Firauni, wakakhofia kukifungua wakidhani labda huenda kuna mali ndani yake wasije wakasingiziwa na mke wa Firauni kwamba wao wameiba.

Kwa hivyo wakakiacha kama kilivyokuwa kimefungwa wakakibeba mpaka kwa Asia mkewe Firauni. Mke wa Firauni akakifungua kisanduku kile akakuta ndani yake mtoto mzuri wa kiume aliyekamilika kwa umbo, hana dosari yoyote ile, na Mwenyezi Mungu S.W.T. aliutia mapenzi moyo wa mke wa Firauni kumpenda mtoto yule. Kwa bahati mbaya wachinjaji wakasikia wakaja haraka kwa mke wa Firauni wakimtaka awape yule mtoto ili kusudi wamchinje. Mke wa Firauni akawazuia akasema, "Mwacheni! Hakika huyu ni mmoja tu hawezi kuzidisha hesabu ya Ma-Bani Israil wala kupunguza hesabu yao, ngojeni kwanza mpaka nimshauri jambo hili Firauni. Ikiwa Firauni atang`ang`ania achinjwe basi mtamchinja, na ikiwa atanikubaliya niwe naye basi atabaki kwangu." Akaja mke wa Firauni kwa mumewe akamwambiya kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Suratil Qasas Aya ya 9, "

وَقَالَتْ امْرَأَةُ فِرْعَوْنَ قُرَّةُ عَيْنٍ لِي وَلَكَ لا تَقْتُلُوهُ عَسَى أَنْ يَنفَعَنَا أَوْ نَتَّخِذَهُ وَلَدًا وَهُمْ لا يَشْعُرُونَ

Maana yake, "…Atakuwa kiburudisho cha macho kwangu na kwako. Msimuuwe! Huenda akatufaa, au tumpange kuwa mtoto (wetu). Wala wao hawakutambua (kuwa atakuwa adui wa Firauni)."

Lakini Firauni alimjibu akasema, "Kwangu mimi sina haja naye ama kwako wewe kama unavyotaka mwenyewe." Firauni alipomkubalia mkewe basi mtoto yule aliachwa hai bila kuchinjwa. Mke wa Firauni alimpeleka kwa wanawake wanyonyeshaji, wakajaribu kumnyonyesha lakini wapi! Alikataa kabisa kunyonya ziwa la kila mwanamke aliyejaribu kumnyonyesha mpaka alipokuja dada yake Nabii Musa akawaambiya, "Jee, nikuonesheni watu wa nyumba watakayemlea kwa ajili yenu, na pia watakuwa mwema kwake?" Kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Surat Taha Aya ya 40, "
إِذْ تَمْشِي أُخْتُكَ فَتَقُولُ هَلْ أَدُلُّكُمْ عَلَى مَنْ يَكْفُلُهُ فَرَجَعْنَاكَ إِلَى أُمِّكَ كَيْ تَقَرَّ عَيْنُهَا وَلا تَحْزَنَ…
Maana yake, "Dada yako alipokwenda na akasema: "Jee! Nikujulisheni mtu wa kuweza kumlea? Basi tukakurejesha kwa mama yako ili macho yake yaburudike, wala asihuzunike..."

Akaletwa mama yake akampa ziwa akakubali kunyonya. Mke wa Firauni akafurahi sana kisha akamwambiya mama yake Nabii Musa akae pamoja na mwanae katika jumba la Firauni ili apate kumnyonyesha. Lakini mama yake Nabii Musa alikataa kabisa shauri hilo bali alisema, "Mimi siwezi kuacha nyumba yangu ikaharibika, ikiwa unataka nitamnyonyesha nyumbani kwangu na wakati wowote ule ukimhitajia uje umchukue." Mke wa Firauni alilikubali shauri hilo, kwani Mwenyezi Mungu S.W.T. alimuahidi mama yake Nabii Musa ya kuwa atamrudisha mwanawe kwake salama salimini na atamfanya miongoni mwa Mitume.

MWISHO