KUANGAMIZWA KWA WATU WA NABII LUUT
  • Kichwa: KUANGAMIZWA KWA WATU WA NABII LUUT
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 17:18:43 1-9-1403

KUANGAMIZWA KWA WATU WA NABII LUUT.

Nabii Ibrahim alipojua makusudio ya Malaika waliokuja kumbashiria kwa kuzaa mtoto atakayeitwa Is-haaq ya kutaka kuwaangamiza watu wa Nabii Luut alianza kujadiliana nao, kwamba kuna idadi ya Waislamu katika kaumu Luut; lakini Malaika walipochungua walikuta ni nyumba moja tu ya Waislamu nayo ni nyumba ya Nabii Luut peke yake. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Surat Dh-dhariyaat aya ya 36, "

فَمَا وَجَدْنَا فِيهَا غَيْرَ بَيْتٍ مِنْ الْمُسْلِمِينَ

Maana yake, "Lakini hatukupata humo (katika kaumu ya Nabii Luut) ila nyumba moja tu (ya Nabii Luut) yenye Waislamu.

Ssuddiyy kasema: "Malaika hao walipotoka kwa Nabii Ibrahim waliendelea na safari yao moja kwa moja mpaka karibu na kijiji cha kaumu ya Nabii Luut, wakaufikia nusu ya mchana, walipofika katika mto wa Sodom wakamkuta mtoto wa kike wa Luut anateka maji kwa ajili ya ahli yake. Na Nabii Luut alikuwa na watoto wawili wa kike, Wakamuuliza "Ewe msichana! Jee, una nyumba?" Akawajibu: "Msiuingie mji huu mpaka kwanza nikuijieni." Kwani aliwakhofia kaumu yake wasije wakawachukua kisha wakawafanyia mambo machafu, kwa sababu kaumu Luut walikuwa ni watu ambao wakiwaingilia wanaume wenzao. Msichana akamjia baba yake akamwambia: "Ewe baba yangu! Wanakutaka vijana kwenye mlango wa mji; sijaona watu wenye sura nzuri kabisa kama wao, nami nakhofia wasije wakachukuliwa na watu wako kisha wakawafedhehesha. Na kabla ya hapo watu wa Luut walimkataza Mtume wao asimkaribishe mgeni yeyote yule. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Suratil Hijr aya ya 70, "

قَالُوا أَوَلَمْ نَنْهَكَ عَنْ الْعَالَمِينَ

Maana yake, "Wakasema: "Jee! Sisi hatukukataza (kukaribisha) watu wa (nje)?"

Mtume wa Mwenyezi Mungu Luut A.S. akawaendea mpaka pale mahali walipo hao vijana kwenye mlango wa mji. Naye hakuwajua kama ni Malaika, kwa hivyo akaanza kuwahadithia mambo ambayo yatawachukiza kuuingia mji huo ili kusudi wasiuingie. Lakini hata hivyo hawakumsikiliza bali walikwenda naye mpaka nyumbani kwake. Inasemekana hawa wageni walikuwa: Malaika Jibriil na Mikaiil na Israfiil waliokuja kwa umbo la binadamu wenye sura nzuri kabisa mtihani na ushahidi kwa watu wa Luut. Mara tu mke wa Luut alipowaona hao wageni wamefikia kwao akatoka mbio kwenda kuwapasha khabari watu wa mji ule; na akawajulisha akawaambia: "Katika nyumba ya Luut kuna wanaume ambao sijawahi kuona katika maisha yangu watu wenye sura nzuri kama wao."

Wakaja mbio mbio kutoka kila upande mpaka kwa Nabii Luut wakimtaka awape hao wageni wanaume ili wawatendee machafu. Na huo haukuwa uovu wa mwanzo bali walikuwa daima wakitenda maovu kama haya. Nabii Luut alipowaona wanaelekea kwake akaufunga mlango wa nyumba yake. Wakajaribu kutaka kuuvunja ule mlango. Na wakati huo ulikuwa wakati wa usiku na Nabii Luut alikuwa akiwakinga na akiwakataza kaumu yake kuwafikia wageni wake na huku akiwaambia: "Waendeeni hao wake zenu walioko majumbani kwenu."

Lakini watu wake walimjibu: "Sisi hatuna haja ya wanawake na bila shaka unajua tunachotaka." Na hali ilipozidi kuwa mbaya na kukataa isipokuwa kuingia ndani tu akawatokea nje Malaika Jibril .A.S. akawapiga kwa bawa lake kisha akawapofua macho yao wakawa hawaoni njia ya kurejea kwao. Wakarejea nyumbani kwao kwa kupapasa kuta za nyumba na huku wakimtishia Nabii Luut kuwa ati ataona ikifika asubuhi. Lakini mara asubuhi lilipochomoza jua, Mwenyezi Mungu SW.T. aliwaangamiza wao kwanza. Kama alivyosema katika Surat Huud kuanzia aya ya 78 hadi 80, "

وَجَاءَهُ قَوْمُهُ يُهْرَعُونَ إِلَيْهِ وَمِنْ قَبْلُ كَانُوا يَعْمَلُونَ السَّيِّئَاتِ قَالَ يَا قَوْمِ هَؤُلاءِ بَنَاتِي هُنَّ أَطْهَرُ لَكُمْ فَاتَّقُوا اللَّهَ وَلا تُخْزُونِي فِي ضَيْفِي أَلَيْسَ مِنْكُمْ رَجُلٌ رَشِيدٌ * قَالُوا لَقَدْ عَلِمْتَ مَا لَنَا فِي بَنَاتِكَ مِنْ حَقٍّ وَإِنَّكَ لَتَعْلَمُ مَا نُرِيدُ * قَالَ لَوْ أَنَّ لِي بِكُمْ قُوَّةً أَوْ آوِي إِلَى رُكْنٍ شَدِيدٍ

Maana yake, "Wakamjia kaumu yake mbio mbio (nyumbani kwa Luut ili wawatendee machafu wale wageni). Na kabla ya haya walikuwa (daima) wakitenda maovu. (Nabii Luut) akasema: "Enyi kaumu yangu! Hao binti zangu (binti za umma wangu walioolewa katika nyumba zenu) ndio wametakasika kwenu (kuwaingilia; si wanaume wenzenu).

Basi mcheni Mwenyezi Mungu wala msinifedheheshe mbele ya wageni wangu. Jee, hamna hata mtu mmoja miongoni mwenu aliyeongoka?" Wakasema: "Bila shaka umekwishajua (haina haja ya kukueleza) hatuna haki juu ya binti zako, na unayajua tunayoyataka. (Nabii Luut) akasema: "Laiti ningalikuwa na nguvu kwenu (mimi mwenyewe) au nategemea katika nguzo yenye nguvu ili wanisaidie juu yenu)."

Pia Mwenyezi Mungu S.W.T. kasema katika Suratil Qamar aya ya 37, "

وَلَقَدْ رَاوَدُوهُ عَنْ ضَيْفِهِ فَطَمَسْنَا أَعْيُنَهُمْ فَذُوقُوا عَذَابِي وَنُذُرِ

Maana yake, "Na walimtaka awape (wageni) wake (ili wawafanye machafu) tukayapofua macho yao; (na tukawaambia): "Onjeni adhabu Yangu na maonyo Yangu." Pia Mwenyezi Mungu S.W.T. kasema katika Suratil Hijr aya 73 na ya 74, "

فَأَخَذَتْهُمْ الصَّيْحَةُ مُشْرِقِينَ * فَجَعَلْنَا عَالِيَهَا سَافِلَهَا وَأَمْطَرْنَا عَلَيْهِمْ حِجَارَةً مِنْ سِجِّيلٍ

Maana yake, "Mara adhabu ikawakamata lilipotoka jua. Na tukaigeuza nchi juu chini, na tukawanyeshea mvua ya mawe ya udongo wa Motoni." Nabii Luut hakujua kwamba alikuwa na nguzo yenye nguvu kabisa nayo ni nguzo ya Mola wa walimwengu wote pamoja na hao Malaika waliokuwa karibu yake. Hapo Malaika wakatoa siri yao na wakajitambulisha kwake wakasema: "Usiwe na khofu wala usihuzunike! Sisi ni wajumbe wa Mola wako, wala si binadamu kama tuonekanavyo na watu. Hawa watu wako hawatakutendea ubaya wowote ule wala hawatokudhuru. Basi ukifika usiku wenye giza toka wewe na watu wako.

" Nabii Luut akauliza: "Jee, nitaokoka mimi pamoja na watu wa nyumbani kwangu? Malaika wakamjibu: "Ndiyo, ila mkeo tu." Nabii Luut akauliza "Na miadi yao itakuwa lini?" Malaika wakamjibu: "Miadi yao ni asubuhi; na asubuhi si mbali." Kama ilivyobainika katika Surat Huud aya ya 81, "

قَالُوا يَا لُوطُ إِنَّا رُسُلُ رَبِّكَ لَنْ يَصِلُوا إِلَيْكَ فَأَسْرِ بِأَهْلِكَ بِقِطْعٍ مِنْ اللَّيْلِ وَلا يَلْتَفِتْ مِنْكُمْ أَحَدٌ إِلاَّ امْرَأَتَكَ إِنَّهُ مُصِيبُهَا مَا أَصَابَهُمْ إِنَّ مَوْعِدَهُمْ الصُّبْحُ أَلَيْسَ الصُّبْحُ بِقَرِيبٍ

Maana yake, "(Wajumbe) wakasema: "Ewe Luut! Sisi ni wajumbe (Malaika) wa Mola wako. Hawatakufikia (kwa baya lolote).

Na ondoka pamoja na watu wako katika pingapinga la usiku. Wala yeyote miongoni mwenu asitazame nyuma, isipokuwa mkeo, kwani yeye utamfika msiba utakaowafika hao. Hakika miadi yao ni asubuhi. Jee, asubuhi si karibu?" Ulipoingia wakati wa usiku wenye giza, Nabii Luut akatoka pamoja na ahli yake wakakimbilia mbali na mji wa Sodom. Inasemekana kwamba ilipofika miadi yao Alfajiri, Malaika Jibril A.S. aliinyanyua juu mbinguni miji ya kaumu Luut kwa bawa lake moja kati ya mabawa yake 600 kisha akaipindua ardhi hiyo juu chini halafu ikateremshiwa mvua ya changarawe za udongo mgumu uliokamatana kutoka Motoni. Na changarawe hizo zimetiwa kila moja alama kuonesha jina la mtu fulani. Na Mwenyezi Mungu S.W.T. amewaonya na kuwatahadharisha adhabu kali hiyo kuwa haiko mbali kwa watu wa umma huu wa Muhammad S.A.W. ikiwa watatenda kitendo kama hicho cha kaumu Luut.

Kama alivyotuhadharisha Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Surat Huud aya ya 82 na ya 83, "
فَل َمَّا جَاءَ أَمْرُنَا جَعَلْنَا عَالِيَهَا سَافِلَهَا وَأَمْطَرْنَا عَلَيْهَا حِجَارَةً مِنْ سِجِّيلٍ مَنْضُودٍ * مُسَوَّمَةً عِنْدَ رَبِّكَ وَمَا هِيَ مِنْ الظَّالِمِينَ بِبَعِيدٍ

Maana yake, "Basi ilipofika amri yetu, tuliigeuza nchi juu chini, na tukawateremshia mvua ya changarawe za udongo mgumu uliokamatana wa Motoni. Zilizotiwa alama kwa Mola wako (kila moja kuwa ya mtu fulani). Na (adhabu) hii haiko mbali na wenye kudhulumu wengineo (katika umma huu watakaotenda kitendo hiki)."

Na mpaka hivi sasa mji huo ulioangamizwa ungali umebakia ili kusudi iwe ni onyo na alama kwa watu watakaokuja (ambao ndio sisi); na mji huo ni bahari iliyokufa (Dead sea) ambapo haishi samaki wala kiumbe chochote kile. Na watu wanapita kila siku na wanaiona sehemu hiyo. Kama alivyosema Mola wa walimwengu wote katika Suratil Hijr aya ya 75 na ya 76, "

إِنَّ فِي ذَلِكَ لآيَاتٍ لِلْمُتَوَسِّمِينَ * وَإِنَّهَا لَبِسَبِيلٍ مُقِيمٍ

Maana yake, "Hakika katika (masimulizi) haya yamo mazingatio (makubwa) kwa watu wenye kupima mambo. Na (miji) hii (tuliyoiangamiza hivi) iko katika njia zipitwazo (nao kila wakati; wanaona alama hizo)."

Na pia kasema Mola wa walimwengu wote katika Surat Ssaaffaat aya ya 137 na ya 138, "

وَإِنَّكُمْ لَتَمُرُّونَ عَلَيْهِمْ مُصْبِحِينَ * وَبِاللَّيْلِ أَفَلا تَعْقِلُونَ

Maana yake, "Na hakika nyinyi mnawapitia wakati wa Asubuhi. Na usiku (pia). Basi jee! Hamyatii akilini?"

MWISHO