RUHUSA YA KUWALILIA WAFU
  • Kichwa: RUHUSA YA KUWALILIA WAFU
  • mwandishi: Rehani Yasini
  • Chanzo: kutoka:www. al-islam.org
  • Tarehe ya Kutolewa: 12:37:21 14-9-1403

RUHUSA YA KUWALILIA WAFU

Hapana shaka kwamba kuwalilia wafu Waumini ni jambo linalofaa katika Uislamu kutokana na dalili ya kitendo cha Mtume (s.a.w.w) kuhusu jambo hilo.

Mtume kulitenda tendo hili kumekaririka mara nyingi na pahala pengi kama ifuatavyo: Mara ya kwanza ni siku alipofariki ami yake na mlezi wake Bwana Abu Talib.

Ya pili ni siku alipouawa kishahidi ami yake Mtume Bwana Hamza katika vita vya Uhud.

Ya tatu siku alipopata Shahada (kuuawa) Bwana Jaafar Bin Abi Talib na Bwana Zaid Bin Harith na Bwana Abdallah Bin Ruwah, wote hawa waliuawa katika vita ya Muuta.

Ya nnei, ni siku alipofariki Bwana Ibrahim ambaye ni mtoto wake mwenyewe Mtume (s.a.w.w).

Mtume (s.a.w.w) alimlilia mwanawe huyu kiasi ambacho kilimfanya Bwana Abdurahman bin Auf amwambie Mtume (s.a.w.w): "Na wewe unalia Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu"?

Bwana Mtume (s.a.w.w) akasema: "Ewe mwana wa Auf hiyo ni alama ya Huruma".

Kisha Mtume akaendelea kulia na akasema: "Hakika jicho linatoa machozi na moyo unahuzinika, wala hatusemi isipokuwa yale anayoyaridhia Mola wetu, na hakika sisi kutengana nawe ewe Ibrahim Wallahi tunahuzunika".

Na mara ya tano, ni siku Mtume (s.a.w.w) alipozuru kaburi la mama yake Bibi Amina, alilia kiasi cha kuwaliza watu waliokuwa karibu yake.

Vitabu vinavyoashiria juu ya Mtume kuwalilia wafu ni vingi mno idadi yake siyo rahisi kuidhibiti.

Kadhalika mapokezi ya kauli ya Mtume (s.a.w.w) na kukiri kwake juu ya kufaa kulia kwa ajili ya wafu ni mengi. Mojawapo ni siku alipopata Shahada Bwana Jaafar bin Abi Talib (At-Tayyaar), Mtume (s.a.w.w) alikwenda kwa mkewe (Jaafar) Bibi Asmaa bint Umais ili kumpa faraja, naye Bibi Fatma aliingia pahala hapo huku analia na kusema:

"Ewe Ami yangu". Basi Mtume (s.a.w.w) akasema: "Na walie wenye kulia kuwalilia mashujaa mfano wa Jaafar."

Siku nyingine aliyowakubalia watu kuwalilia wafu ni siku alipofariki Ruqaiya binti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), wanawake wakawa wanamlilia (Ruqaiya), basi Omar bin al-Khatab akawa anawapiga kwa bakora yake, pamoja na kwamba Mtume alikwishawakubalia kulia, basi Mtume (s.a.w.w) akamwambia Omari: "Waache walie" kisha Mtume akasema: "Vyovyote iwavyo, huzuni itokayo Moyoni na jicho kulia, hayo ni kwa ajili ya huruma, ameyaweka Mwenyezi Mungu."

Pia kuna siku lilipitishwa jeneza mbele ya Mtume (s.a.w.w) ilihali kuna wanawake wanalia, Omar akawakemea, Mtume akamwambia Omar, "Waache walie ewe Omar kwani nafsi huhuzunika na jicho hutoa machozi."

Mapokezi ya hadithi kuhusu jambo hili yako mengi kiasi ambacho hatuna nafasi ya kuyakamilisha yote, lakini itoshe kwamba: Nabii Yaaqub bin Is-haq bin Ibrahim alimlilia mwanawe Yusufu pale Mwenyezi Mungu alipomuondosha Yusuf machoni mwake na akasema (alipokuwa akilia): "Ooo majonzi yangu kwa Yusufu!!! Na macho yake yakawa meupe kwa huzuni naye alikuwa amejawa na huzuni." (Qur'an 12:84).

Kutokana na kilio cha Nabii Yaaqub imefikia hadi kusemwa kwamba, "Hayakukauka macho yake (kwa kulia) tangu alipotengana na Yusuf (a.s) mpaka alipokuja kukutana naye, ukiwa umepita muda wa miaka themanini (vitabu vingine husema miaka arobaini).

Taz. Tafsirul-Kashaaf ya Az-Zamakhshari.

Basi je, palikuwa na nani aIiyebora mbele ya Mwenyezi Mungu katika zama hizo kuliko Nabii Yaaqub (a.s)?

Imepokewa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) kwamba yeye alimuuliza Jibril (a.s) yalifikia kiasi gani majonzi ya Yaquub (a.s) alipokuwa akimlilia mwanae"? Jibril akaseama: Yalifikia kiasi cha majonzi ya wanawake sabini waliopotelewa na watoto wao.

Mtume akasema: "Je alipata malipo kiasi gani?" Jibril akasema: "Alipata ujira wa mashahidi mia moja.."

Taz. Tafsirul-Kashaaf.

Mimi nasema: "Basi ni mtu gani atakayechukizwa na madhehebu yetu sisi (Shia Ithnashari) katika suala la kulia kutokana na huzuni, baada ya kuwa jambo hili limethibiti toka kwa Manabii. "Ni nani anayechukizwa na mila ya Ibrahim (a.s)? Hakuna, isipokuwa yule anayeitia nafsi yake katika upumbavu. " (Qur'an, 2:130).

Kwa hakika sera ya Maimamu juu ya maombolezo na kulia iliendelea zama baada ya zama, na wakawaamuru wafuasi wao kudumisha mikusanyiko ya huzuni juu ya Imam Husein (a.s).

Amesema Imam Jaafar as-Sadiq (a.s): "Hakika Ali bin Husein (a.s) alimlilia baba yake maisha yake yote, hapakuwekwa chakula mbele yake ila hulia, na wala hakuletewa kinywaji isipokuwa hulia.

Kutokana na kulia kwake huko, mmoja wa wafuasi wake alimwambia: "Mimi niwefidia kwako, acha kulia hakika nachelea kwamba utakuwa miongoni mwa wenye kuangamia kwa kulia sana."

Imam Ali bin Husein (a.s) (Zainul Abidin) akajibu: "Hapana jambo lolote (linaloniliza sana) isipokuwa mimi nashitakia huzuni zangu kwa Mwenyezi Mungu nami nayajua yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu ambayo ninyi hamuyajui."

Na katika mapokezi mengine Imam Ali bin Husein (a.s) alisema kumwambia mmoja katika wafuasi wake, "Ole wako hakika Yaaqub (a.s.) alikuwa na watoto kumi na wawili, macho yake yalibadilika na kuwa meupe kwa ajili ya kulia sana (kumlilia Yusuf (a.s) na mgongo wake ulipinda kutokana na huzuni nyingi, hali yakuwa mwanawe yu hai hapa duniani, lakini mimi nalia sana kiasi hiki kwa sababu niliwaona na kuwashuhudia, baba yangu (Imam Husein (a.s), ndugu zangu, ami zangu na watu kumi na saba miongoni mwa watu wa nyumba yangu wakiwa wamenizunguka hali wamechinjwa!!!"

Pia Imam Ali bin Husein (a.s) alikuwa kila anapochukuwa chombo ili anywe maji, hulia mpaka chombo kile akakijaza damu.

Akiulizwa kuhusu hali hiyo hujibu: "Basi ni kwa nini nisilie wakati ambapo baba yangu alinyimwa maji ambayo yalikuwa hayana kizuizi chochote kwa wanyama.........? "

Na imepokewa hadithi toka kwa Bwana Rayyan bin Shubaib amesema: "Nilingia nyumbani kwa Imam ar-Ridha (a.s) katika siku ya kwanza ya Muharram. Imam akaniambia: "Ewe mwana wa Shubaib, hakika Mwezi wa Muharram (Mfungo nne) ni mwezi ambao watu wa zama za Jahiliya (kabla kuja Uislamu) walikuwa wakiharamisha dhulma na mauaji kutokana na utukufu wa Mwezi huu lakini watu wa Ummah huu (wa Kiislamu) hawakuheshimu Utukufu wa Mwezi huu wala heshima ya Mtume wao (s.a.w.w), kwani walikiua kizazi chake ndani ya Mwezi wa Muharram, na wakawateka wanawake wa kizazi cha Mtume wao, na wakapora vyombo vyao.

Ewe mwana wa Shubaib, ikiwa wewe utakuwa ni mwenye kulia, basi mlilie Husein (a.s) kwani yeye alichinjwa kama anavyochinjwa kondoo, na aliuawa yeye pamoja na watu kumi na nane katika watu wa nyumba yake, ambao hawalinganishwi na yeyote hapa duniani kwa ubora, na kwa hakika Mbingu Saba zililia kwa kuuawa Husein (a.s)."

Imepokewa hadithi kutoka kwa Abu Ammarah Al-Munshid amesema: "Hakutajwa Imam Husein (a.s) mbele ya Abu Abdillah as-Sadiq (a.s) katika siku yoyote isipokuwa (siku hiyo) hakuonekana kuwa na furaha mpaka usiku."

Na amesema Abu Ammarah, "Abu Abdillah as-Sadiq (a.s) alikuwa akisema: Mauaji aliyouliwa Husein (a.s.) ni jambo la kumpa mazingatio kila Mu'umini.

Na imepokewa kutoka kwa Imam Jaafar as-Sadiq (a.s) amesema: "Imam Husein (a.s.) alisema, mimi nitauawa ili yapatikane mazingatio kutokana na mauaji hayo, hatanikumbuka (kwa kunitaja) Mu’umini yeyote bali atapata mazingatio.