FUNGA YA RAMADHAN, HUKUMU, FADHILA, ADABU ZAKE
UTANGULIZI
Sifa zote njema zinamstahikia Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) na sala na salamu zimfikie Mtume wake (Swalla Allahu alayhi Wasallam) pamoja na ndugu na maswahaba zake.
Baada ya kumshukuru Allah (Subhaanahu Wata’ala) na kumtakia rehma na amani Mtume Muhammad (Swalla Allahu alayhi Wasallam) pamoja na ndugu zake na maswahaba zake wote, basi kwa hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu (Subhaanahu Wata’ala) amejaalia kwa waja wake miongo [misimu] ya kuzidisha ndani yake matendo mema na Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) huzidisha pia malipo ya matendo hayo kwa waja wake, na miongoni mwa miongo hiyo ni huu mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Basi katika makala haya nitaelezea kwa ufupi juu ya funga na yale yanayoambatana nayo ikiwa ni pamoja na hukumu, fadhila na adabu zake.
Ninamwomba Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) awanufaishe Waislamu kwa yale nitakayoyaelezea, na aturuzuku ikh-laswi [kutaka radhi zake pekee] katika matendo yetu yote, amiiin. Kwake pekee ndiyo kwenye mafanikio ya dunia na akhera.
Maana ya Funga
Neno swaumu ambalo ni funga katika lugha ya Kiswahili, kilugha lina maana ya kujizuilia. Ama katika sheria, funga [swaumu] ni kumuabudu Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa kujizuilia na vyenye kufuturisha [kufunguza] kuanzia kudhihiri alfajiri [ya pili] mpaka kuchwa [kuzama] kwa jua na kwa kunuilia kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala).
Historia ya Funga
Kwa hakika funga si ibada ngeni, bali ni ibada iliyofaradhishwa kwa umati zilizotangulia na pia kufaradhishwa katika umati huu. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {{Enyi mlioamini! mmelazimishwa kufunga [saumu] kama walivyolazimishwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu}} (2:183).
Ama katika umati huu wa Muhammad (Swalla Allahu ‘alayhi Wasallam) funga ilifaradhishwa katika mwezi wa Shaaban mwaka wa pili baada ya Hijrah (2H).
Hukumu ya Funga
Funga ya mwezi wa Ramadhani ni nguzo katika nguzo za Uislamu, nayo ni wajibu kwa dalili ya kitabu (Qur-aan), Sunnah na Ijmai (makubaliano) ya wanavyuoni wote wa Kiislamu.
1: Amesema Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) : {{Enyi mlioamini mmelazimishwa kufunga (saumu) kama walivyolazimishwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha mungu. Siku chache tu ( kufunga huko)…(Mwezi huo mlioambiwa mfunge) ni mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa katika mwezi huo hii Qur-aani ili iwe uwongozi kwa watu, na hoja zilizo wazi wa uongozi na upambanuzi (wa baina ya haki na batili). Atakayekuwa katika mji katika huu mwezi (wa Ramadhani) afunge. …}(2:183-185) .
2: Na imepokewa hadithi kutoka kwa Abdullah ibn ‘Umar (Radhiya Allahu ‘anhuma) amesema: Nimemsikia Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi Wasallam) akisema: “Umejengwa Uislamu juu ya nguzo tano; kushuhudia ya kwamba hakuna Mola anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) na kwamba hakika ya Muhammad (Swalla Allahu ‘alayhi Wasallam) ni Mtume wa Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) na usimamishaji Swala na utoaji zakah na kuhiji katika nyumba (tukufu) ya Alkaaba na funga ya Ramadhani. (Al Bukhariy na Muslim).
Na kuna hadithi nyingine nyingi zinazojulisha wajibu huo, na wanavyuoni wote wamewafikiana juu ya uwajibu huo.
Inayemuwajibikia Funga ya Ramadhani
Funga ya Ramadhani inamuwajibikia kila Mwislamu, baleghe, mwenye akili, aliye katika mji wake (asiwe msafiri), mwenye siha (afya – asiwe mgonjwa), asiwe na mambo yanayozuia kuswihi kwa funga (kama hedhi na nifasi kwa wanawake).
Na inatakikana kwa wazazi kuwafundisha kufunga watoto wao wanapofikia umri wa miaka saba (7) na kuwalazimisha hadi ikibidi kuwapiga wanapofikia umri wa mika kumi (10), na hili inabidi pia kuzingatia afya na ukuaji wa mtoto.
Nyudhuru za Kufunga
Nyudhuru za kuacha kufunga zinatofautiana na kila udhuru una hukumu yake, na hapa nitazielezea nyudhuru hizo kwa ufupi.
1. Hedhi (damu ya mwezi) na nifasi (damu ya uzazi). Huu ni udhuru ambao unamlazimisha mwanamke kuacha kufunga, na inakuwa haramu kwake kufunga na iwapo atafunga haitosihi (haitokubaliwa) funga yake, na ni wajibu kwake kulipa funga hiyo.
2. Maradhi au safari. Na mwenye udhuru wa maradhi (yanayotibika kwa kawaida) pamoja na msafiri wanaruhusiwa kutokufunga na itawawajibikia kulipa. Amesema Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) :{{Atakayekuwa katika mji katika huu mwezi (wa Ramadhani) afunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi (atimize) hisabu (ya siku alizoacha kufunga) katika siku nyingine. Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito.. .}} (2:185). Na kama maradhi yatazidi au kumletea madhara iwapo atafunga basi itakuwa lazima kwake kutokufunga.
Ama safari ambayo inaruhusiwa kwa sababu yake kutokufunga, wanachuoni wengi wemesema: Ni safari ya siku mbili kwa ngamia au kwa mwendo wa miguu (mar-hala mbili) ambayo ni sawa na umbali wa takribani kilomita (85km). Na ruhusa hii inapatikana kwa msafiri anayesafiri kwa chombo cha aina yoyote atakachosafiria, ijapo kwa dhahiri safari hiyo haimpi uzito wowote.
3. Vizee (vikongwe) na wenye maradhi sugu (yasiotarajiwa kupoa). Na haya mawili iwapo yanamsababishia madhara, basi ni katika udhuru na ruhusa ya kuacha kufunga, na itamlazimikia atoe fidia kwa kumlisha masikini kibaba (mudi) cha chakula (ambacho ni sawa na uzito wa gramu 600 takribani) au chakula kinachomshibisha masikini mmoja kwa kila siku aliyoacha kufunga.
4. Waja wazito na wanaonyonyesha. Nao ni katika wenye ruhusa ya kutokufunga, na inawabidi kulipa siku walizoshindwa kufunga kwa sababu ya udhuru huo.
5. Iliyemzidia njaa au kiu na akahofia kuangamia, huu pia ni katika udhuru wa kuacha kufunga, bali wamesema wanachuoni kwamba yule mwenye kuhofia kuangamia inakuwa kwake ni wajibu kufungua, na itamuwajibikia kulipa kama mgonjwa.
Nguzo za Kufunga
Nguzo za kufunga ni tatu:
1. Kwanza ni kunuia. Nia ni kukusudia kufunga usiku wa kuamkia siku ya kufunga, kwa funga ya faradhi.
2. Kujizuilia na vyenye kufunguza (kufuturisha).
3. Muda wa kufunga (mchana kuanzia alfajiri mpaka kutwa (kuzama) kwa jua).
Unavyothibiti kuingia Mwezi wa Ramadhani
1. Kwa kukamilika siku thelathini (30) za mwezi wa Shaaban.
2. Kwa kuonekana mwezi mwandamo siku ya 29 ya mwezi wa Shaaban. Imepokewa hadithi na Abu Hurayrah (Radhiya Allahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi Wasallam) amesema: {Fungeni kwa kuonekana kwake (mwezi mwandamo) na fungueni kwa kuonekana kwake}. (Al Bukhariy na Muslim).
Na mwezi wa kuingia Ramadhani inatosha kuonekana na Muislamu mmoja mwadilifu ama mwezi wa kumalizika Ramadhani ni lazima uonekane na Waislamu waadilifu wawili au zaidi.
Yanayobatilisha (kuharibu) Funga
Mambo yafuatayo hubatilisha (huharibu) funga. Nayo ni:
1. Kula au kunywa kwa kukusudia.
2. Kila kinachoingia tumboni au kooni kwa kukusudia.
3. Kukutana kimwili (kuingiliana) kati ya mume na mke.
4. Kujitoa manii (mbegu za uzazi) au kusababisha kutokwa na manii (kwa kujichezea sehemu za siri, kukumbatiana au kupigana mabusu na kadhalika).
5. Kujitapisha kwa makusudi. Imepokewa hadithi kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allahu ‘anhu) amesema: Amesema Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi Wasallam): {…na mwenye kujitapisha basi inamuwajibikia kulipa}
(wameipokea maimamu watano).
6. Kutokwa na damu ya mwezi (hedhi) au damu ya uzazi (nifasi).
Wakati wowote yanapomtokea mwanamke mawili hayo, funga yake ya siku hiyo itakuwa imeharibika na itamlazimikia kuilipa siku hiyo baada ya mwezi wa Ramadhani.
Yasiyofunguza
1. Kula au kunywa kwa kusahau. Imepokewa hadithi kutoka kwa Abu Hurayrah amesema, {amesema Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi Wasallam): {Mwenye kusahau naye amefunga, basi akila au akinywa na aikamilishe funga yake….} ( Al Bukhariy na Muslim ).
2. Kusukutua au kupandisha maji puani wakati wa udhu (bila ya kubalighisha).
3. Kuoga au kujiburudisha kwa kujimwagia maji katika kiwiliwili (hasa katika maeneo yenye joto kali).
4. Kuonja chakula kwa mpishi (kwa sharti ya kutokumeza alichokionja).
5. Kutokwa na mbegu za uzazi (manii) katika usingizi (ndoto) au bila ya kukusudia.
6. Kuamka na janaba. Imepokewa hadithi kutoka kwa Mamama Aishah na Ummu Salamah (Radhiya Allahu ‘anhuma) kwamba Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi Wasallam) alikuwa akiamka na janaba kutokana na kukutana kimwili na wake zake, kisha anaoga na kufunga (Al Bukhariy na Muslim).
7. Kupiga mswaki (wakati wowote).
8. Kuchoma sindano ya kawaida ya tiba.
9. Kung’oa jino na mfano wake.
10. Mwanamke kuamka kabla ya kuoga kwa hedhi au nifasi.
MWISHO