MWALIKO WA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHANI
Tuko katika siku tukufu za ibada ya funga ya mwezi wa Ramadhani na sote tumealikwa kuwa wageni wa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Mtu anapoalikwa kwenye karamu au shughuli yoyote ya ugeni, hali hiyo humsisimua na kumfanya awe ni mwenye furaha wakati wote hadi wakati wa kushiriki karamu au ugeni huo. Sote tunajua ya kwamba jambo linalomfanya mwalikwa kuwa na furaha hiyo ni ile hamu ya kutaka kukutana na mwenyeji wake pamoja na wageni wengine walioalikwa kwenye karamu hiyo ambapo mazingira mapya ya kuonana na kujuliana hali wageni hujitokeza, mapenzi na upendo kudhihirishwa na wakati mwingine zawadi kutolewa na mwenyeji wao. Kabla ya kushiriki kwenye mwaliko, jambo la kwanza ambalo mwalikwa hukabiliana nalo ni jinsi atakavyovalia vizuri, kutembea vizuri na kuzungumza vizuri. Tunapofahamu kuwa mwenyeji wetu atakuwa anatusubiri mlangoni kwa ajili ya kutulaki, hapo kasi ya hatua hatua zetu kumuelekea huongezeka. Mwanzo wa kila mwaliko huwa ni kuzingatia na kufungamana kimawazo na mwenyeji, ambapo kila mara mfungamano huo unapokuwa ni wa kirafiki zaidi, ugeni nao hunoga na kuvutia zaidi. Hivi sasa na kwa mara nyingine tumealikwa na mwenyeji ambaye ni rafiki mwema wa kuvutia, mwenye huruma na anayesamehe zaidi kati ya wenyeji wengine wote tunaowajua sisi wanadamu. Mwenyezi Mungu ni Muumba wa pekee na Mwenye Hekima ambaye jina lake hutuliza nyoyo zinazosononeka na kutaabika.
Kwa mara nyingine tena milango ya mbinguni imefunguliwa wazi mbele ya waumini ili wapate kuzijua nafsi zao na Muumba wao katika mazingira tulivu na yaliyo mbali na mahangaiko na pilikapilika za kila siku maishani. Katika zama hizi za maisha ya kisasa ambapo mwanadamu amepokonywa kabisa fursa ya kufikiria juu ya nafsi yake na hivyo kumfanya kuwa kiumbe anayezingatia tu masuala ya kimaada, Ramadhani ni fursa nzuri ambayo humuandalia mwanadamu huyo mazingira mazuri ya kufikiria juu ya nafsi yake mbali na shughuli zake nyingi za kila siku maishani. Kwa ibara nyingine ni kuwa mwezi huu mtukufu humuandalia mwanadamu fursa ya kufikiria juu ya shughuli za ndani ya nafsi yake kinyume na miezi mingine ya mwaka ambapo huwa anajishughulisha zaidi na masuala ya nje ya nafsi yake. Hali hiyo humuwezesha kuwaza na kufikiria sehemu za ndani ya nafsi yake ambazo anapasa kuzirekebisha na kuziboresha, kuwaza juu ya Muumba wake na kumuomba Yeye tu msaada bila ya kuwategemea viumbe wengine. Mwezi wa Ramadhani kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu na maneno ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) pamoja na Maimamu watoharifu wa Nyumba yake (as), ni mwezi ambao ni bora kuliko miezi mingine yote ya mwaka. Inatutosha kutazama moja kati ya majina ya mwezi huu mtukufu ili tupate kujua heshima na utukufu wake mkubwa. Mwezi huu umetajwa kuwa ni 'Shahrullah' kwa maana ya Mwezi wa Mwenyezi Mungu. Tunafahamu vyema kwamba miezi yote ni ya Mwenyezi Mungu lakini ni mwezi mmoja tu kati ya miezi hiyo ndio umetajwa kuwa ni Mwezi wa Mwenyezi Mungu. Vilevile tunajua kwamba nyusiku (wingi wa usiku) zote ni za Mwenyezi Mungu lakini ni usiku mmoja tu kati ya nyusiku hizo ndio umetajwa kuwa na utukufu mkubwa zaidi kwa kupewa jina la Lailatul Qadr, usiku mtukufu ambao unapatikana kwenye mwezi huu mtukufu wa Ramadhani. Ramadhani ni mwezi wa ugeni ambao mwenyeji wake ni Mwenyezi Mungu mwenyewe, na ambaye amewaalika watu wote kushiriki. Ugeni huu sio kama Hija ambapo waalikwa ni wale tu walio na uwezo wa kushiriki, wala Khumsi na Zaka ambayo hutozwa faida ya ziada kwa mazao, na wala hata Swala ambayo imewajibishwa kwa Waislamu katika siku zote na katika kila hali.
Huenda swali hili likaulizwa na baadhi ya watu kwamba je, ni ugeni wa aina gani huu ambao waalikwa na wageni hutakiwa kujizuia kula na kunywa? Tunajibu kwa kusema kwamba Mwenyezi Mungu hakuandaa ugeni huu wa Ramadhani kwa ajili ya kunufaisha na kushibisha miili ya waja wake kwa sababu miili hiyo, kama ilivyo ya viumbe wengine, daima huwa kwenye ugeni wa Mwenyezi Mungu kupitia riziki anazoipa kila siku. Ama katika ugeni wa mwezi mtukufu wa Ramadhani ni nyoyo ndizo huwa zinapata faraja na kunufaika na ugeni huo nayo miili kupata fursa ya kupumzika na hivyo kuwa salama zaidi. Taratibu na ratiba za kimaanawi za mwezi wa Ramadhani humuandalia mja fursa ya kupanga, kurekebisha na kudhibiti matamanio yake ili kumuwezesha kulea vyema utu wake wa asili. Kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa lengo kuu la mwezi mtukufu wa Ramadhani linahusiana na jinsi ya kutakasa roho na nafsi ya mwanadamu kuliko jambo lingine lolote. Katika mwezi huu, funga, dua, kusoma Qur'ani, kusamehe na kutenda mema, kuwasaidia wanadamu wenzetu na kufanya matendo mengine mema, yote hayo husafisha roho ya mwanadamu na kumuandalia njia ya kustawi na kukamilika kimaanawi. Huu ni ugeni ambao hakuna mtu yoyote anayetambua thamani yake isipokuwa Mwenyezi Mungu mwenyewe. Ni wazi kuwa kusifiwa Ramadhani kuwa ni 'ugeni' sio neno lililobuniwa na kutumiwa na wanalugha pamoja na wanairfani hivi hivi tu na kwa msingi wa mapendeleo yao, bali ni neno lililotumiwa na Mtume Mtukufu mwenyewe (saw) kuhusiana na Ramadhani, Mtume ambaye anajua hakika zote za dunia. Anasema katika maneno ya mwanzo kabisa ya hutoba yake mashuhuri ya mwezi mtukufu wa Shaaban: "Ni mwezi ambao mmealikwa kwenye ugeni wa Mwenyezi Mungu.' Hivyo tunapasa kutumia vyema fursa iliyojitokeza na kunufaika vilivyo na ugeni wa mwezi huu mtukufu wa Ramadhani kwa kuzingatia na kuchunguza kwa makini ibara na sifa hii ya 'ugeni' ambayo imetumika kuhusiana na mwezi huu wenye utukufu na baraka nyingi.
Katika Ijumaa ya mwisho ya mwezi wa Shaaban, Mtume Mtukufu (saw) alitoa hutuba muhimu sana ambapo aliwabashiria Waislamu fadhila na utukufu wa mwezi wa Ramadhani. Alisema katika sehemu ya hotuba hiyo: Enyi watu! Hakika mwezi wa Mwenyezi Mungu umekufikieni kwa baraka, rehema na msamaha. Mwezi ambao mbele ya Mwenyezi Mungu, ni mwezi ulio bora zaidi, siku zake ni siku bora zaidi, nyusiku zake ni nyusiku bora zaidi na saa zake ni saa bora zaidi. Ni mwezi ambao ndani yake mmealikwa kuwa wageni wa Mwenyezi Mungu (katika dhifa yake) na kufanywa kuwa miongoni mwa watu wanaonufaika na ukarimu Wake. Pumzi zenu katika mwezi huu ni tasbihi, usingizi wenu ibada, amali zenu zinakubaliwa na dua zenu kujibiwa. Hivyo mwombeni Mwenyezi Mungu kwa nia njema na roho safi ili akupeni taufiki ya kufunga kwa ajili yake na kukisoma Kitabu chake (Qur'ani).....Enyi watu! Ndani ya mwezi huu milango ya Pepo umefunguliwa wazi. hivyo mwombeni Mwenyezi Mungu asikufungieni, na milango ya Jahannam katika mwezi huu imefungwa hivyo mwombeni asikufungulieni (milangohiyo). Mashetani katika mwezi huu wamefungwa minyororo hivyo mwombeni Mwenyezi Mungu asiwafanye wakudhibitini."
Kwa mujibu wa kauli ya Mtume Mtukufu (saw), katika mwezi huu amali ndogo zaidi za waja hupata thawabu kubwa na Mwenyezi Mungu kuwapa neema nyingi hata kama watafanya ibada ndogo tu. Kwa uzingatiaji mdogo tu, dhambi kubwa za waja hupata msamaha na mazingira kuandaliwa kwa ajili ya kuwawezesha wafanye ibada zao kirahisi na kuweza kufikia ukamili wa kweli na saada ya kudumu, kuliko wakati mwingine wowote. Hiyo ndiyo fursa nzuri na bora zaidi ambayo mja anaweza kuandaliwa katika karamu na ugeni wowote ule wa kimaanawi. Ikiwa mja atafunga kwa nia safi na kama inavyotakiwa, bila shaka atakuwa ameshiriki vilivyo kwenye ugeni huu wa Mwenyezi Mungu na kuweza kufikia kiwango cha juu zaidi cha ukamilifu na manufaa ya kimaanawi kutokana na msaada wake Mungu Muumba. Riwaya zinatwambia kwamba siku moja, Nabii Musa (as) Alisema: "Ewe Mungu Wangu! Nina bahati iliyoje kuweza kukukaribia na kuzungumza na wewe moja kwa moja kwa namna hii bila ya kuwepo wasila (kiunganishi)! Je, kuna mtu mwingine yeyote aliye na bahati kama hii niliyonayo? Mwenyezi Mungu akasema: Eeh Musa! hivi sasa unazungumza na mimi baada ya kupitia pazia (vizuizi) elfu sabini, lakini katika Zama za Mwisho, kuna watu watakaokuwa wakifunga funga ndefu za kuchosha kwa ajili ya kupata radhi zangu na watakapokuwa wakifuturu, nitakuwa nikiwakaribia bila kuwepo pazia (vizuizi) hizo."
Kwa kuwaalika waumini kwenye karamu yake, Mwenyezi Mungu amewafanya waachane kwa muda na maisha yao ya kimaada na kuwakurubisha kwake kupitia karamu hiyo ya kimaanawi. Ni kwa msingi huo ndipo viongozi wa dini na riwaya zikatuusia tuwe wageni wema na wazuri wa Mwenyezi Mungu katika mwezi huu. Tulindeni heshima na utukufu wa Mwenyezi Mungu kwa kujiepusha na madhambi. Tutambueni funga ya kweli ili tuweze kufikia kiwango cha takwa ya kweli, kama anavyosema Mwenyezi Mungu katika aya ya 183 ya Suratul Baqarah:
Enyi mlioamini! Mmeandikiwa kufunga kama walivyoandikiwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kuwa na takwa.
Salamu ziwe juu yako ewe mwezi mtukufu wa Ramadhani! Mwezi wa maghfira, baraka na ugeni wa Mwenyezi Mungu. Salamu kwa dua, usiku wa Leilatul Qadr, minong'ono na sauti za al-ghauth! Al-ghauth! Za waja wa Mwenyezi Mungu, salamu kwa Idul Fitr, wakati wa kujibiwa dua, funga na kutakabaliwa maombi yenye ikhlasi ya waja mbele ya Mwenyezi Mungu.
MWISHO