TAWASSULI (SEHEMU YA TATU)
  • Kichwa: TAWASSULI (SEHEMU YA TATU)
  • mwandishi:
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 23:42:10 1-9-1403

TAWASSULI (SEHEMU YA TATU)
MUENDELEZO WA MAKALA ILIYOPITA
TAWASSULI NDANI YA HADITHI ZA MTUKUFU MTUME (S.A.W.W.)
Zimepokewa Hadithi mbalimbali zikionyesha ruhusa ya kutawasali kupitia Nabii au Mawalii Wema.
(I) Toka kwa Uthman bin Hunaif amesema: “Mtu mmoja kipofu alikwen- da kwa Mtume akasema: ‘Niombee kwa Mwenyezi Mungu aniponye.’ Mtume akamwambia: ‘Ukipenda nitaomba na ukipenda vumilia na ndiyo bora.’ Yule mtu akamwambia Mtume: ‘Muombe Mwenyezi Mungu.’ Basi Mtume akamwamuru atawadhe vizuri na aswali rakaa mbili na aombe kwa kutumia dua hii: “Ewe Mwenyezi Mungu, hakika mimi nakuomba na ninaelekea kwako kupitia kwa Mtume wako, Mtume wa Rehema. Ewe Muhammad, hakika mimi naelekea kwa Mola Wangu Mlezi kupitia kwako katika haja yangu ili ikubaliwe. Ewe Mwenyezi Mungu mfanye Muhammad kuwa mwombezi wangu.”1
Hadithi hii haina dosari katika usahihi wake mpaka Ibnu At-Taymiyya ameiona kuwa ni sahihi na akasema: “Abu Jafar anayekusudiwa aliyomo ndani ya njia ya upokezi wa Hadithi hii ni Abu Jafar Al-Khatwamiyu, na yeye ni mwaminifu.”
Ama Ar-Rifai yeye amesema: “Hamna shaka kwamba Hadithi hii ni sahihi na ni mashuhuri. Na imethibiti bila wasiwasi wala mashaka kuwa macho ya kipofu yule yalirudia kuona kwa sababu ya dua ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.).”2
Hadithi hii wameileta An-Nasaiy, Al-Bayhaqiy, At-Tabaraniy, At-Tirmidhiy na Al-Hakim ndani ya Al-Mustadrak yake.3
Kwa Hadithi hii inazidi kuthibiti Sheria ya Tawassuli, kiasi tunamkuta Mtume wa Mwenyezi Mungu amemfunza kipofu namna ya kutawasali kwa Mwenyezi Mungu kupitia Nabii Wake, Nabii wa Rehema, na kum- wombea ili kukidhi haja yake. Na makusudio ya Nabii ni Nabii mwenyewe si dua yake. Na kuelekea kwa Mwenyezi Mungu kupitia jaha ya Mtume na njia yake.
(II) Atwiyatu Al-Awfi amepokea kutoka kwa Abu Said Al-Khidri kwam- ba Mtume (s.a.w.w.) amesema: “Yeyote atakayetoka nyumbani kwake kwenda kuswali akasema:
“Ewe Mwenyezi Mungu hakika mimi nakuomba kwa haki ya wanaokuomba na ninakuomba kwa haki ya mwendo wangu huu, kwani mimi sikutoka kwa maringo na majivuno, wala kujionyesha wala kutaka kusifiwa, nimetoka kwa kuogopa ghadhabu zako na kutafuta radhi zako; basi ninakuomba uniepushe na moto na unisamehe madhambi yangu, kwani hakuna anayesamehe madhambi isipokuwa Wewe.”
Basi Mwenyezi Mungu atamwelekea mtu huyo kwa dhati yake na watam- takia msamaha Malaika
elfu sabini.”4
Hakika Hadithi hii inaonyesha ruhusa ya kutawasali kwa Mwenyezi Mungu kupitia heshima ya mawalii wema na daraja zao na cheo chao walichonacho mbele ya Mwenyezi Mungu, basi mtu huwafanya hao ndio viun- go na waombezi ili haja zao zikubaliwe na dua zao zipokelewe.
(III) Anas bin Malik amesema: “Alipofariki Fatima binti Asad, Mtume aliingia mahala alipofia akakaa upande wa kichwa chake akasema: “Mwenyezi Mungu akurehemu ewe mama yangu mpendwa baada ya mama yangu mpendwa.” Akataja sifa zake juu yake na kumvisha sanda kwa joho lake, kisha Mtume akamwita Usama bin Zaydi, Abu Ayubu Al-Ansari, Umar bin Al-Khattab na kijana fulani mweusi ili wakachimbe kaburi.
Wakalichimba kaburi lake na walipofikia kuchimba mwanandani Mtume akaichimba hiyo yeye mwenyewe kwa mkono wake na kuutoa mchanga kwa mkono wake. Alipomaliza akaingia kwenye mwanandani kisha akalala ndani yake na akasema:
“Mwenyezi Mungu ndiye anayehuisha na kufisha, na Yeye yu hai wala hatokufa. Ewe Mwenyezi Mungu, msamehe mama yangu mpendwa Fatima binti Asad na uyapanue makazi yake kwa haki ya Mtume Wako na Manabii ambao wamepita kabla yangu.”5
Imepokewa kuwa As-Sawadi bin Qaribi alimsomea Mtume utenzi wake ambao ndani yake alitawasali kupitia Mtume (s.a.w.w.), akasema:
Nashuhudia kwamba hapana Mola isipokuwa Allah.
Na kwamba wewe ndiye mwenye kuaminiwa kuhusu mambo ya kila asiyekuwepo.
Nawe ndiye uliye karibu mno kama njia kwa Mwenyezi Mungu kuliko Mitume wengine, ewe mwana wa watukufu walio wema.
Tuamrishe yale yanayokufikia ewe mbora wa Mitume, japo yatakuwa mazito.
Na uwe mwombezi wangu siku ambayo mwombezi yeyote hatomnufaisha As-Sawadi bin Qaribi japo kwa sehemu ndogo.6
SERA YA WAISLAMU KATIKA TAWASSULI
Sera ya waislamu zama za uhai wa Mtume (s.a.w.w.) na baada ya kufa kwake ni kutawasali kupitia Mtume (s.a.w.w.) na Mawalii wa Mwenyezi Mungu na kuomba shufaa kupitia vyeo vyao na heshima zao mbele ya Mwenyezi Mungu. Ifatayo ni mifano ya sera hiyo ya waislamu:
a) Baada ya kufariki Mtume wa Mwenyezi Mungu Abu Bakr alisema: “Ewe Muhammad tutaje mbele ya Mola wako Mlezi na tuwe ndani ya kumbukumbu yako.”7
b) Al-Hafidh Abu Abdullah Muhammad bin Musa An-Nu’mani ndani ya kitabu chake Misbahu Adh-Dhulami amesema: “Hakika Al-Hafidh Abu Said As-Samuani ameeleza tuliyopokea kutoka kwake kutoka kwa Ali bin Abu Twalib kuwa (a.s.) alisema: “Baada ya siku tatu tangu tulipomzika Mtume wa Mwenyezi Mungu alitujia bedui akajitupa juu ya kaburi la Mtume (s.a.w.w.) na kumwagia sehemu ya udongo wake juu ya kichwa chake na kusema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu ulisema tukasikia kauli yako. Ukatuelimisha kuhusu Mwenyezi Mungu na tukaelimika kuhusu wewe, na miongoni mwa yaliyoteremshwa ilikuwa ni: “Lau wangelikujia walipojidhulumu nafsi zao wakaomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu...”
Na nimeshaidhulumu nafsi yangu na nimekujia uniombee msamaha.” Basi akaitwa toka kaburuni: Hakika Yeye (Mwenyezi Mungu) ameshakusamehe.”8
c) Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa keshamfunza mtu fulani namna ya kuomba awe anamwomba Mwenyezi Mungu, kisha awe anamse- meza Mtume na awe anatawasali kupitia yeye (s.a.w.w.), kisha amwombe Mwenyezi Mungu akubali shufaa yake, aseme:
“Hakika mimi nakuomba na natawasali kwako kupitia Nabii wako Nabii wa Rehma. Ewe Muhammad; ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu; hakika mimi ninatawasali kupitia wewe kwa Mola Wangu Mlezi katika haja yangu ili nikidhiwe. Ewe Mwenyezi Mungu mfanye awe mwombezi wangu.”9
d) Ndani ya Sahih Bukhari imekuja kuwa: Umar bin Al-Khattab alikuwa kila wanapopatwa na ukame huomba mvua kupitia Abbas bin Abdul-Mutwalibi (r.a.) na kusema: “Ewe Mwenyezi Mungu tulikuwa tuk- itawasali kwako kupitia Mtume wetu na ukitupa mvua, basi sasa tunatawasali kwako kupitia ami ya Mtume wetu basi tupe mvua.” Bukhari amesema: “Basi hupewa mvua.”10
e) Al-Mansur Al-Abasiyu alimuuliza Malik bin Anas –Imam wa madhehebu ya Maliki - kuhusu namna ya kumzuru Mtume (s.a.w.w.) na namna ya kutawasali kupitia yeye…. Akamwambia Malik: Ewe Abu Abdullah, nielekee Kibla niombe au nimwelekee Mjumbe wa Mwenyezi Mungu? Malik akajibu: Kwa nini unampa kisogo Mtume wakati yeye ndiyo njia yako na njia ya baba yako Adamu Siku ya Kiyama? Bali mwelekee na umwombe akuombee na Mwenyezi Mungu atakubali maombi yako, kwani Mwenyezi Mungu anasema: “Na lau walipozidhulumu nafsi zao….”11
f) Shafi’i amesoma beti hizi mbili za shairi lake akitawasali kupitia Kizazi cha Mtukufu
Mtume (s.a.w.w.):
“Kizazi cha Mtume, wao ni njia yangu na wao ni wasila wangu kwa Mwenyezi Mungu. Kwao wao kesho nataraji kupewa kitabu changu kwa mkono wa kulia.”12
Baada ya maelezo yote yaliyotangulia miongoni mwa dalili, hoja na ushahidi wa kihistoria inawezekana kusema kwamba: Manabii na watu wema miongoni mwa waja Wake wanahesabiwa kuwa ndio njia za kishe- ria ambazo alizikusudia Mwenyezi Mungu kwenye kauli yake: “Enyi mlioamini mcheni Mwenyezi Mungu na tafuteni njia ya kumfikia.”13
Na hapa njia inajumuisha mambo ya Sunna na wala haikomei kwenye kutekeleza mambo ya faradhi na kujiepusha na mambo ya haramu pekee.
TAWASSULI KWA MUJIBU WA KIZAZI CHA MTUME
Maimamu wa Ahlul-Baiti wamehimiza sana kutawasali kupitia Qur’ani tukufu, Mawalii wa Mwenyezi Mungu na mengineyo. Atakayerejea kwenye vitabu vya Shia Imamiya, vitabu vyao vya Hadithi na vitabu vyao vya dua atalikuta ni jambo la wazi kabisa kiasi kwamba haiwezekani kulishakia. Ifatayo ni baadhi ya mifano:
a) Al-Harith bin Al-Mughira amepokea, amesema: “Nilimsikia Abu Abdullah akisema:
“Iwapo mmoja wenu anataka kumwomba Mola Wake Mlezi kitu kati ya haja za kidunia, basi asianze mpaka aanze kumhimidi na kumsifu Mwenyezi Mungu Mtukufu na kumtakia rehema Mtume (s.a.w.w.) kisha amwombe Mwenyezi Mungu haja zake.”14
b) Kutoka kwa Abu Jafar (a.s.) amesema: Jabir Al-Answari amesema: “Nilimwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.): Unasemaje kuhusu Ali bin Abu Twalib? Akasema: “Yeye ni nafsi yangu.”
Nikasema: Unasemaje kuhusu Hasani na Huseini? Akasema: Wenyewe wawili ni roho yangu na Fatuma mama yao ni binti yangu, kinanichukiza kile kinachomchukiza na kinanifurahisha kile kinachomfurahisha. Nashuhudia kwa Mwenyezi Mungu kuwa hakika mimi ninapigana na wanaopigana nao na nina amani na wale wanaokaa nao kwa amani. Ewe Jabir, ukitaka kumwomba Mwenyezi Mungu na akujibu ombi lako mwombe kupitia majina yao, hakika yenyewe ni majina vipenzi kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.”
c) Kutoka kwa Mtume (s.a.w.w.): “Ewe Mwenyezi Mungu hakika mimi naelekea kwako kupitia Muhammad na Kizazi cha Muhammad na naku- rubia kwako kupitia wao na ninawatanguliza huku nikiwa na haja.”15
d) Imam Ali Kiongozi wa waumini (a.s.) ndani ya dua yake alikuwa akisema: “……..kwa haki ya Muhammad na Kizazi cha Muhammad iliyo juu yako, na haki Yako tukufu juu yao wapelekee Rehema kama unavyostahiki na unipe kilicho bora mno kuliko vile ulivyowapa waombaji miongoni mwa waja wako waumini waliotangulia na kilicho bora mno kuliko vile utakavyowapa waja wako waliosalia miongoni mwa waumini.” 16
e) Imam Abu Abdullah Husein (a.s.) katika dua yake ya Arafa amesema: ‘Ewe Mwenyezi Mungu hakika sisi tunaelekea kwako - jioni hii ambayo umeifaradhisha na kuitukuzakupitia Muhammad Nabii wako na Mteule wako miongoni mwa viumbe vyako.17
f) Imam Zainul-Abidin amesema ndani ya dua yake ya munasaba wa kuingia Mfungo wa Ramadhani: …..Ewe Mwenyezi Mungu, hakika mimi nakuomba kupitia haki ya Mfungo huu na haki ya atakayejibidisha humu kwa Ibada, mwanzo wake hadi mwisho wake; kuanzia Malaika uliyemkurubisha au Nabii uliyemtuma au mja mwema uliyempenda…..”18
•    1. Sunanu Ibnu Majah 1: 441, Hadithi ya 1385. Musnad Ahmad 4: 138 Hadithi ya 16789. Mustadrak Asw-Swahahain cha Al-Hakim An-Naisaburi 1: 313. Al- Jamius-Swaghir cha As-Suyutwi: 59. Minihajul-Jamiu 1:286.
•    2. At-Tawassuli cha Subhani: 69. Amenukuu kutoka kwenye At-Tawassulu ila Haqiqatu At-Tawassul cha Ar-Rifai: 158.
•    3. Sunanut-Tirmidhi: 5/ 531 Hadithi ya 3578. As-Sunanu Al-Kubra cha An-Nasai: 6, 169, Hadithi ya 10495.
•    4. Sunanu Ibnu Majah 1: 256 Hadithi ya 778, mlango wa kwenda kwenye Sala
•    5. Kashful-Irtiyabi: 312, amenukuu toka kwenye Wafaul-Wafai na Ad-Duraru As-Saniyatu: 8..
•    6. Ad-Duraru As-Saniyatu: 27. At-Tawassulu ila Haqiqatu At-Tawassuli: 300. Fat'hul-Bari 7: 137
•    7. Ad-Durarus-Saniyatu fi Radi A'lal-Wahabiyya: 36.
•    8. Wafaul-Wafai cha As-Samuhudiyu 2: 1361.
•    9. Majumuatu Ar-Rasaili Wal-Masaili cha Ibnu At-Taymiyya 1: 18.
•    10. Sahih Bukhari: Mlango was ala na kuomba mvua 2: 32, Hadithi ya 947.
•    11. Kutoka kwenye Wafaul-Wafai cha As-Samuhudiyu 2: 1376.
•    12. As-sawaaiqul-Muhriqa: 274.
•    13. Al-Maida: 35.
•    14. Biharul-Anwar: juzuu 93, kitabu cha utajo na dua, mlango wa 17, Hadithi ya 19 kutoka kwenye Iddatu Ad-Dai: 97.
•    15. Biharul-Anwar, Juz 94, mlango wa 28, Hadithi ya 19. Kutoka kwenye Da’awatul-Qutubi Ar-Rawandiyu.
•    16. As-Swahifatul-Alawiyya cha As-Samahijiyu: 51.
•    17. Iqbalul-Amali cha Ibnu Twawusi 2: 85.
•    18. As-Swahifatus-Sajadiyya: Dua namba 44.
ITEANDELEA KATIKA MAKALA IJAYO