UTUKUFU WA RAMADHANI
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمْ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِنْ قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ
“Enyi Mlioamini mmefaradhishiwa Saumu kama walivyofaradhishiwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu”. (TMQ 2:183)
Tunaweza kuugawa Utukufu wa Ramadhani katika sehemu mbili kubwa:
1.Utukufu wa ibada ya funga kwa ujumla ndani ya Ramadhani au nje ya Ramadhani. Na kwa kuwa ndani ya mwezi wa Ramadhani imo ibada ya funga, mfungaji hana budi kufaidika na utukufu huo.
2.Utukufu maalum (khasa) wa funga ya Ramadhani na yote yaliyomo ndani yake
UTUKUFU JUMLA WA KUFUNGA SAUMU
Amesema Mtume (SAAW): akipokea kutoka kwa mola wake “Kila Amali ya mwanadamu ni yake, isipokuwa Saumu, hiyo ni Yangu, na Mimi ndie Nitakayelipa” (Bukhar)
Amesema pia SAAW: “Watu Watatu dua zao hazirejeshwi Kiongozi muadilifu, aliyefunga mpaka kufuturu na dua ya mwenye kudhulumiwa” (Ibn Majah)
Pia kasema SAAW: “Hakika katika pepo kuna mlango unaitwa Rayyan wataingia mlango huo wafungaji na hatoingia mwengine yoyote kinyume na wao” (Bukhar)
UTUKUFU MALUMU (KHASA) WA RAMADHANI
وَأَنْ تَصُومُوا خَيْرٌ لَكُمْ إِنْ كُنتُمْ تَعْلَمُونَ (البقرة:
“Na mkifunga ni kheri kwenu ikiwa mnajua” (TMQ 2:184)
Kwa Aya hii Muumba wa kila kitu Anatangaza kwamba kufunga Ramadhani kuna kheri kwetu. Jee kuna kubwa kuliko kauli ya Allah Taala?
Amesema Mtume SAAW: “Swala tano, ijumaa mpaka ijumaa Ramadhani mpaka Ramadhani ni kafara (kifutio) cha madhambi atakapojiepusha mtu na madhambi makubwa/al-kabair” (Bukhari)
Anasema (s.a.w.w) : “Amekula hasara mtu nitakapotajwa asiniswalie, na amekula hasara itakapoingia Ramadhani na ikaondoka hakusamehewa madhambi yake.
Amesema tena SAAW: “Itakapoingia Ramadhani milango ya moto hufungwa, na hufunguliwa milango ya pepo, na hufungwa mashetani (Bukhar)
Amesema tena SAAW: “Atakaefunga kwa imani thabit na matarajio ya malipo husamehewa madhambi yaliyotangulia (Bukhar)
Kasema SAAW: Hakika imekufikieni funga ya Ramadhani, basi atakaefanya sunna ya kisimamo chake, atakaefunga na kusimama kwa ibada kwa imani na matarajio ya malipo atafutiwa madhambi yake kama siku alipozaliwa kutoka katika tumbo la mama yake (Nassai)
Pia kasema SAAW: “Hakika umekudhihirikieni mwezi wa Ramadhani ndani yake umo usiku mtukufu wa laylat-ul-qadr ambao ni bora kuliko miezi alfu. (ibn Majah)
KULETWA MUONGOZO NDIO UTUKUFU MKUBWA ZAIDI WA RAMADHANI
شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِنْ الْهُدَى وَالْفُرْقَانِ
“Mwezi wa Ramadhani (ndio) ambao imeteremshwa humo Quran kuwa ni muongozo kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi” (TMQ 2:185)
Ramadhani ni mwezi ulioshushwa ndani yake Muongozo kumuongoza mwanadamu katika mambo yake yote amma yawe ni mambo yanayomuhusu mwanadamu na Mola wake moja kwa moja, kama utekelezaji wa ibada mbalimbali kama swala, saumu, hijja nk. Au mahusiano ya mwanadamu na nafsi yake, kama atumie aina gani ya chakula, kinywaji, mavazi nk. Au mahusiano ya mwanadamu na wanadamu wenzake kama katika masuala ya kuuziana, ajira, utawala, ndoa, udugu nk.
MUONGOZO LAZIMA UWE NA KIONGOZI/MTAWALA
Muongozo wowote ima uwe wa batili au wa haki yaani Quran kamwe hauwezi kufanya kazi vilivyo bila ya kuwa na msimamiaji mkuu ambae ni kiongozi/ mtawala. Kwa mfano, huwezi tu kutawanya nakala za sheria ya kodi kwa watu ukatarajia watu kulipa kodi wenyewe bila ya kuwa na vyombo vya kusimamia na kuwaadhibu wasiolipa kodi.
RAMADHANI NI KUKAMILISHA IDADI YA SIKU NA KUITIMIZA KIWANGO CHA SAUMU YENYEWE.
Baada ya kutaja fadhila na utukufu mkubwa wa Ramadhani lazima tukubali kwamba leo kwa kukosekana mtawala wa Kiislamu saumu zetu zinapita katika mitihani migumu katika kila hali. Tunafunga ilhali tumezungukukwa na mazingara machafu kuanzia watu kutembea uchi, kula mchana, kubanwa kiuchumi nk. Leo tunahitaji tuwe na mtawala ili kuja kuwafunga minyororo mashetani wa kibinadamu baada ya kufungwa minyororo mashetani wa kijini. Aidha, tukumbuke kuwa Quran ilipotuwajibisha kufunga Ramadhani imetuwajibisha pia kukamilisha idadi ya siku za kufunga, na imetuwajibisha pia tuitimize saumu. Maana ya kukamilisha ni kwa upande wa idadi ya kitu (quantitiy). Na maana ya kutimiza kitu ni kiwango cha kitu husika ikihusisha kila sifa iliyomo ndani ya kitu chenyewe. Leo saumu zetu zinapata idadi inayotakikana katika kukamilisha siku, lakini ina mushkeli katika kutimiza kiwango chake. Hatusemi kuwa tusifunge, lakini haya lazima tuyatafakari kwa kina.
Zaidi ya yote hayo wakati sisi tukifunga, sehemu ya umma wetu dunia nzima kuanzia Somalia, Iraq, Afghanistan, Burma, Syria nk. wanaingia ndani ya mwezi huu mtukufu wa Ramadhani wao wakikabiliwa na mashaka mbali mbali ya umasikini, mateso, kudhalilishwa na kuuwawa na makafiri na vibaraka wao nk. Jee nani atadhamini Waislamu kufunga kwa furaha na utulivu? Yote haya majibu yake ni uwajibu wa Waislamu sote kufanya kazi ya kurejesha tena dola ya Kiislamu ya Khilafah ili ije kutawala kwa Uislamu na kusimamia muongozo wetu katika maisha ya kila siku ikiwemo kuisimamia ipasavyo ibada hii tukufu ya Ramadhani.
MWISHO