AHLUL BAIT NI AKINA NANI?
  • Kichwa: AHLUL BAIT NI AKINA NANI?
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 22:0:30 1-10-1403

AHLUL BAIT NI AKINA NANI?

Swali muhimu kabisa ambalo tungependa kulijibu sasa ni Ahlul Bait ni akina nani? Au Ahlul Bait ni wepi? Hapa pia tutatoa majibu kutoka katika vitabu vya Sunni tu.

1- Muslim anasimulia katika Sahihi yake kutoka kwa Safiya bint Shaibah ambaye aliripoti kuwa: "Siku moja Aisha bint Abubakar alisema: "Siku moja Mtume wa Allah alikuwa amejifunika KISAA (blanket kubwa), kisha akaja Imam Hassan (a.s) na Mtume akamuita na kumfunika na Kisaa. Kisha akaja Imam Husayn (a.s) na pia Mtume akamfunika. Kisha akaja Fatima (a.s) na Mtume akamfunika kwa Kisaa. Kisha akaja Imam Ali (a.s) na Mtume pia akamfunika kwa Kisaa.

Kisha akasema: "INNAMAA YURIIDULLAHU LIYUDH'HIBA ANKUMUR RIJSA AHLAL BAYTI, WA YUTAHHIRUKUM TATHIIRA". Maana yake ni kwamba "Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu enyi Ahlul Bayt na anataka kukutakaseni mtakaso ulio bora kabisa". (Suratul Ahzab 33:33).
Hadithi hii inaonyesha waziwazi kuwa Ali, Fatma, Hassan na Hussein ndio Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) ambao wameteuliwa na Mtume kuwa viongozi wetu, Angalia Sahih Muslim, (Jz. 5, Uk. 287).

2- Katika Sahihi Muslim imeripotiwa kuwa: "Aya ifuatayo iliposhuka nayo inasema hivi: "Na atakayebishana nawe baada ya kukujia elimu, basi mwambie: Tuwaite watoto wetu na watoto wenu, wanawake wetu na wanawake wenu, na nafsi zetu na nafsi zenu, na kisha tuombe kwa unyenyekevu laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie waongo (Aya ya Mubahilah, Aali Imran 3:61); Mtume aliwaiita Ali, Fatima, Hassan, na Hussein na akasema: "ALLAHUMAA HAA'ULAAI AHLII" - Ewe Mwenyezi hawa ndio watu wa nyumbani kwangu, Ahlul Bayt". (Tazama Sahih Muslim, Jz. 5, Uk. 268).

3- Ingawa Mtume alieleza mara nyingi kuwa Ahlul Bayt ni Ali, Fatima, Hassan, na Hussein; na hii imerekodiwa katika vitabu vingi vya Kisunni na wapokeaji thabiti, lakini utakuta baadhi ya wanazuoni wa Kisunni wanajaribu kung'ang'aniza kuwa Ahlul Bayt ni wake za Mtume. Ukweli ni kwamba wake wa Mtume hawamo katika kundi la Ahlul Bayt, kwa sababu Ahlul Bayt kwa mujibu wa Qur'an ni Maasumu (hawana madhambi) na walikuwa wametakasika ambapo wake wa Mtume hawakuwa Maasumu. Mjadala juu ya mada hii utajadiliwa baadaye. Kwa wale wanaoamini kuwa wake wa Mtume ni katika Ahlul Bayt wasome hadithi ifuatayo katika Sahih Muslim, Juz.5, Uk. 274. Muslim amesimulia katika Sahih yake kupitia kwa Zaid bin Arqam ambaye alisema kuwa: "Mtume Muhammad (s.a.w.w) amesema: "Enyi watu! jueni kwamba mimi ni mwanaadamu na Malaika wa Mauti anaweza kunijia hata mimi pia na lazima niitike wito wake. Enyi watu! ninakuachieni vitu vizito (muhimu) viwili; cha kwanza ni kitabu cha Mwenyezi Mungu, ambapo ndani yake mtapata mwongozo na nuru, hivyo shikamaneni na kitabu cha Mwenyezi Mungu na kamwe msikiache; na kizito cha pili ni Ahlul Bayt wangu, ninakukumbusheni juu ya wajibu wenu kwa Ahlul Bayt --- ninakukumbusheni juu ya wajibu wenu kwa Ahlul Bayt ---- ninakukumbusheni juu ya wajibu wenu kwa Ahlul Bayt (alirudia mara tatu)". Kisha tuliuliza: "Ahlul Bayt ni akina nani, Je wake zako nao ni miongoni mwa Ahlu Bayt?" Akasema: "Hapana. Ninaapa kwa jina la Allah, kwa hakika mwanamke huishi na mumewe kwa muda, kisha mumewe akimpa talaka, na mwanamke huyo hurudi kwa baba yake na jamii yake aliyotoka, Ahlul Bayt wa ni watu wake kutoka katika familia yake na ambao kwao sadaka ni haramu baada yake". (Sahih Muslim, Baabu Fadhail Ali (a.s), Juz. 5, Uk. 274).

4 -Katika Sahih Tirmidhi imeripotiwa kutoka kwa Umru bin Abi Salama ambaye amesema: "Aya hii: INNAMA YURIDULLAHU LIYUDH HIBA ANKUMUR RIJSA AHLAL BAYTI WA YUTAHHIRUKUM TAT-HIIRA" - "Kwa hakika, Mwenyezi Mungu anataka kuwaondeleeni kila aina ya uchafu, enyi Ahlul Bayt, na kuwatakasani kwa mtakaso ulio bora kabisa (33:33)", ilishuka katika nyumba ya Ummu Salma, Mke wa Mtume; hapo basi Mtume aliwaita Fatima, Hassan, Hussein na Ali na aliwafunika kwa Kisaa (blanketi); kisha akasema : "Ee Mwenyezi Mungu! hawa ni Ahlul Bayt wangu, hivyo waondolee kila aina ya uchafu na watwaharishe kwa tohara iliyo bora kabisa". Ummu Salma akasema: "Je na mimi ni pamoja nao (Ahlul Bait) Ewe Mtume wa Allah?" Mtume alijibu: "Hapana, wewe una nafasi yako na upo katika njia iliyonyooka". Alikataliwa kuingia! Hadithi hii pia imo katika Musnad Ahmad bin Hambal (Juz 6, Uk. 306), na Sahih Tirmidhi (Juz. 2 , Uk. 209).

5 - Katika aya ya Tathiir: "INNAMAA YURIDULLAHU LIYUDH-HIBA ANKUM AR-RIJSA AHLAL BAYTI WA YUTAHIRUKUM TATHIIRA (Ahzab 33:33), dhamiri ya Kiarabu iliyotumika kwa Ahlul Bayt ni "ANKUM......, YUTAHHIRUKUM....". Wakati katika sura hiyo hiyo katika aya zilizotangulia (Ahzab 33:32-34) dhamiri iliyotumika kwa wake za Mtume ni "KUNTUNNA....., MINKUNNA........., n.k." ambayo ni dhamiri ya kike kwa kiarabu. Badiliko hili la ghafla la dhamiri kutoka dhamiri ya kike kwenda dhamiri ya kiume katika Aya (Ahzab 33:33), inathibitisha kuwa wake za Mtume hawamo katika Ahlul Bayt ambao wanatakiwa kufuatwa, kwa sababu wakati Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alipotaka kuwazungumzia wake za Mtume alitumia dhamiri ya kike "KUNTUNNA ......, MINKUNNA.......", lakini alipoanza kuwazungumzia Ahlul Bayt "Ali, Fatma, Hassan na Hussein", dhamiri ilibadilika. Huu ni ushindi dhahiri kwa wale wanaojua sarufi ya lugha ya Kiarabu.
Wapendwa wasomaji , mmeona kwamba hadithi ya Thaqalayn (vizito viwili) : Quran na Ahlul Bayt imeripotiwa katika vitabu vingi sana vya Kisunni, lakini umewahi kumsikia mwanazuoni wa Kissuni akiizungumzia hadithi hii inayozungumzia - Kushikamana na Qur'an na Ahlul Bayt - ambao ndio ulikuwa wasiya wa mwisho wa Mtume. Kwanini wanazuoni wa Kisunni wanaupuuza wasia wa mpendwa kiongozi na Mtume wetu? Je kuna sababu yoyote ya maana ya kuupuza wasia huu (jambo ambalo ni dhambi kubwa) zaidi ya kuwa ni ujinga, ugumu wa mioyo, kujiegemeza upande wa imani zetu tulizonazo, wivu na manufaa yetu binafsi? Tunamuomba Mwenyezi Mungu atupe tawfiiq ya kushikamana na Qur'an na Ahlul Bayt baada ya Mtume (s.a.w.w). Amin.

MWISHO