MAZINGATIO
  • Kichwa: MAZINGATIO
  • mwandishi: UMMU IYYAAD
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 22:48:16 1-9-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM
MAZINGATIO

Maafa mengi yamezidi siku hizi duniani na baada ya kutokea maafa ya mitetemeko ya ardhi baharini inayoitwa Tsunami, ambayo ni makubwa mno kuwahi kutokea, inatupasa tuelewe kuwa kuna mazingatio makubwa ndani yake. Mengi tumesikia, na kuona kwa kila aina ya rangi katika televisheni na radio na kusikitika sana kuona maafa yaliyowapata wenzetu. Lakini tujiulize maswali yafuatayo: Je, nini sababu ya kutokea maafa hayo? Au mazingatio gani yanatupasa tuyatie akilini mwetu? Au mafundisho gani tumepata kwa matukio hayo? Na baada ya kujuwa yote hayo je, inatupasa tufanye nini?

Sababu kubwa ni kuwa watu wamezidi kufanya maasi na ufisadi duniani. Na katika maafa haya kuna waliokuwa hawamjui kabisa Mola wao, na kuna waliokuwa wanamjua lakini hawafuati amri Zake na makatazo kwa hiyo Allaah  سبحانه وتعالى huwateremshia ghadhabu Yake ili watanabahi wajirekebishe na warudi Kwake.

{{Uharibifu umedhihiri barani na baharini kwa sababu ya yale iliyofanya mikono ya watu, ili Awaonjeshe (adhabu ya ) baadhi ya mambo waliyoyafanya, huenda wakarudi (wakatubia kwa Mwenye Enzi Mungu) }} Ar-Ruum 30:41 Na ghadhabu Yake Allaah ni kali hapa duniani, na akhera ni zaidi.

{{Na namna hivi ndivyo inavyokuwa kutesa kwa Mola wako anapowatesa (watu wa) miji wanapokuwa wameacha mwendo walioambiwa. Hakika teso lake (Mwenye Enzi Mungu) linaumiza (na) kali kabisa }} Hud 11:102 Maafa kama haya sio mageni katika ulimwengu, bali ni marudio tu ya yaliyokwishatokea kabla yetu kutokana na hadithi za mitume wa kabla yetu. Ukisoma kisa cha Nuuh Alayhis salaam utapata picha iliyokaribiana na maafa haya ya watu kuangamizwa katika mawimbi makubwa mno ya bahari.

Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema kuwa ni desturi Yake kuwaadhibu watu na kuwaletea maafa katika miji yao na mateso mbali mbali wanapovuka mipaka Yake:
{{Kwa ajili ya kutakabari kwao katika ardhi, na kufanya vitimbi vibaya vibaya, na vitimbi vibaya havimteremkii ila yule aliyevifanya. Basi hawangoji ila dasturi (ya Mungu) iliyokuwa, (aliyoipitisha) kwa watu wa zamani! Hutapata mabadiliko, katika kawaida (dasturi) ya Mwenye Enzi Mungu (aliyoiweka) wala hutakuta mageuko katika kawaida ya Mwenye Enzi Mungu}} Fatir 35:43 Wala Allaah  سبحانه وتعالى
hamdhulumu mtu bali watu wenyewe hujidhulumu nafsi zao kwani haangamizi mji, au watu, au kuwapa adhabu bila ya kuwatumia Mitume kuwaonya. Wanapoendelea kufanya maasi hapo tena ndio huwaadhibu. Na hakuna umma wowote ila Ametuma Mtume kuwaonyesha njia iliyo sawa:

{{Na tumeiangamiza miji mingapi iliyojifaharisha juu ya maisha yao! Hayo maskani yao yasiyokaliwa baada yao tena ila kidogo tu hivi; na sisi tumekuwa Warithi (wa hayo) }} {{Na Mola wako haangamizi miji mpaka ampeleke Mtume katika mji wao mkuu, awasomee Aya zetu, (wakatae ndio waangamizwe) wala hatuiangamizi miji mpaka watu wake wamekuwa madhalimu }} Al-Qasas 28:58 & 59

Kwa hiyo sababu mojawapo ni madhambi ya watu kama walivyoadhibiwa watu waliopita kutokana na dhambi zao: {{Basi kila mmoja tulimtesa kwa sababu ya dhambi zake, miongoni mwao wako tuliowapelekea kimbunga cha changarawe, na miongoni mwao wako waliotolewa roho kwa ukelele mkubwa (uliopigwa na Jibriil); na miongoni mwao wako tuliowagharikisha. Na hakuwa Mwenyezi Mungu Mwenye kuwadhulumu, lakini walikuwa wakijidhulumu (wenyewe nafsi zao) }} Al-'Ankabut 29:40 Atauliza mtu au atawaza: "lakini mbona kuna watu wema humo, au watoto ambao hawana dhambi zozote?" Majibu ni kuwa : 1) Allaah hutupa mitihani yote ya shari na ya kheri kama Alivyotuambia katika:

... na tunakujaribuni kwa mtihani wa shari na kheri  (Suratul-Anbiyaa 21:35). Pia hadithi Inatokana na Bibi Aisha kuwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kasema: (Jeshi litaelekea Kaaba na litakapofika uwanja ulio sawa,(ardhi iliyo tambarare) wa mwanzo wao na wa mwisho wao wote watamezwa na ardhi. Akauliza "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Kwanini wote watamezwa na hali wamo humo walio sokoni na wengine wasio miongoni mwao? Akajibu : "Wa mwanzo wao mpaka wa mwisho wao watamezwa na ardhi lakini watafufuliwa kila mmoja na nia yake " (Bukhari na Muslim).

Kwa hiyo wale waliokuwa watu wema au waliokuwa hawana dhambi kabisa kama watoto waliofikwa na maafa pengine ni bora kwao kuwa na mwisho mzuri kuliko wangeliishi zaidi pengine wangelichuma madhambi. Na Mwenye Enzi Mungu ndie Mwenye kujua.

MAZINGATIO NA MAFUNDISHO
Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika aya ifuatayo:

Kwa hakika katika haya yapo mazingatio kwa wanao ogopa. (An Nazi'aat 79:26). Lakini sio kila mtu atakuwa na khofu isipokuwa wale wenye imaani hasa kwani japokuwa mtu ataona kwa macho yake, au kusikia kwa masikio yake, lakini huenda akawa hajaathirika kabisa ndani ya imani yake. {{Miji mingapi tuliiangamiza iliyokuwa ikidhulumu, ikaanguka juu ya mapaa yake; na visima (vingapi) vilivyoachwa; na majumba (yaliyokuwa) madhubuti?}}

{Je! Hawatembei katika ardhi ili wapate nyoyo, (akili) za kufahamia, au masikio ya kusikilia? Kwa hakika macho hayapofoki (yakadhuru katika dini) lakini nyoyo ambazo zimo vifuani ndizo zinazopofoka (zikadhuru katika dini} Al Hajj : 25:45 & 46 Yafuatayo ni mazingatio au mafundisho niliyoyaona katika maafa haya: Binaadamu wote ni dhaifu mbele ya Allaah  سبحانه وتعالى hata kama ana cheo, au utajiri, au elimu kubwa au nguvu. Mwenyewe peke yake ndiye Mwenye nguvu

{{Enyi watu! Nyinyi ndio wenye haja kwa Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu Mkwasi (na nyinyi - hakuhitajieni). Asifiwaye (kwa neema zake juu ya viumbe vyake vyote}} Faatwir 35:15 2. Dunia haina thamani yoyote:

{{... Sema : Starehe ya dunia ni ndogo. Akhera ni bora zaidi kwa hao wenye kumcha Mungu}} An-Nisaa 4:77 3. Tujitayarishe na mauti wakati wowote, na popote {{ ….. Na nafsi yeyote haijui ni nini itachuma kesho, wala nafsi haijui itafia ardhi gani, bila shaka Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi (ndiye) Mwenye habari (ya mambo yote) }} Luqmaan 31:34 4. Hakuna teknolojia ya kuweza kuzuia mitetemeko ya ardhi, au kimbunga, au mafuriko, au aina yoyote ya maafa ardhini wala hawezi mtu kujua mambo ya ghaibu ya Mwenye Enzi Mungu. Na yote Ameshayakadiria katika Lawhun Mahfuudh:

{{Na ziko Kwake (Mwenyezi Mungu tu) funguo za siri, hakuna azijuaye ila Yeye tu. Na anajua yaliyomo barani na baharini. Na halianguki jani ila analijua. Wala (haianguki) punje katika giza la ardhi (ila anajua). Wala (hakianguki) kilichorutubika wala kilichoyabisika (ila anakijua). (hapana chochote) ila kimo katika Kitabu kidhihirishacho (kila jambo) }} Al-An'aam 6:59 5. Qiyama kipo karibu kwa kuzidi mitetemeko ya ardhi juu ya kuwa alama karibu zote ndogo alizotaja Mtume صلى الله عليه وسلم  zimeshatokea kwa mujibu wa Maulamaa.  Anasema Mtume rahma za Allah na amani ziwe naye:
(Qiyama hakitosimama mpaka mitetemeko ya ardhi izidi) Bukhari 6. Mitetemeko ya ardhi hii sio sawa na mtetemeko wa siku ya Qiyama kwani wa duniani watu hufa na kupata misiba ya kufiwa na watu wao na kupoteza mali zao na baada ya muda yanasahaulika, lakini mtetemeko wa Qiyama siku hiyo mama atamtupa mwanae, kila mtu atamkimbia mwenzake, kila mmoja atakuwa na lake litakalomshughulisha:

Enyi watu! Mcheni Mola wenu, hakika mtetemeko wa Kiama ni jambo kubwa (kabisa ) Siku mtakapokiona (hicho Kiama) kila mwanamke anyonyeshaye atamsahau amnyonyeshaye, na kila mwenye mimba ataizaa mimba yake (kabla ya wakati kufika) . Na utawaona watu wamelewa; kumbe hawakulewa, lakini ni adhabu ya Mwenyezi Mungu (tu hiyo) iliyo kali }} Al-Hajj : 1-2

Watu wote watafufuliwa makaburini:
{Itakapotetemeshwa ardhi mtetemesho wake (huo mkubwa)} {Na itakapotoa ardhi mizigo yake (hiyo) (2) }} Az-Zalzalah 99:1& 2 Mtetemeko sio sehemu moja tu ya ardhi bali dunia nzima na vilivyomo ndani yake vyote: kama tunavyoona katika sura zifuatazo: {{Jua litakapokunjwakunjwa (1) Na nyota zitakapopukutika (2) Na Milima itakapoendeshwa (angani kama vumbi) (3) Na ngamia wenye mimba pevu watakapoachwa, (wasishughulikiwe) (4) Na wanyama wa mwitu watakapokusanywa (5) Na bahari zitakapowashwa moto (6) }} Attakwiir 81: 1- 6 {{Mbingu zitakapo pasuka (1) Na nyota zitakapo pukutika (3) Na bahari zitakapopasuka (3) Na makaburi yatapo fukuliwa (4)}} Al-Infitaar 82:1 - 4

{{(Msiba) ugongao nyoyo (yaani Kiyama) (1) (Msiba) ugongao nyoyo ni upi huo? (2) Na ni jambo gani litakalokujulisha (hata ukaujua) ni upi huo (Msiba) ugongao nyoyo? (3) Siku ambayo watu watakuwa kama madumadu (watoto wa nzige) waliotawanywa (4) Na milima itakuwa kama sufi zilizochambuliwa (zikawa zinapeperuka) (5) }} Al-Qaariah 1 - 5 Baada ya mazingatio na mafundisho hayo inatupasa tufanye nini?
" Kumtii Allaah na Mtume Wake
" Kutubia kwa maasi au dhambi zozote
" Kumshukuru Allaah سبحانه وتعالى kutuweka katika neema Zake
" Kuwaombea dua Waislamu wenzetu waliofikwa na maafa na kujiombea sisi wenyewe Allaah  سبحانه وتعالى
Atuhifadhi nayo. Mazuri yote niliyoandika yanatoka na Allaah سبحانه وتعالى na mabaya yote ni kutoka kwangu na kwa shetani.
MWISHO