BSMILAHI AR-RAHMANI AR-RAHIIMI
DUNIA SI CHOCHOTE SILOLOTE
Wakati unayoyoma na hakuna awezaye kuuzuia usiende. Hakuna tofauti nyengine baina yetu na wale waliotangulia mbele ya haki ila ni wakati tu. Hakika wakati ndio unaomfanya mtu kuwa mtoto, kijana au kizee. Haukuwepo wakati na hii ni Neema Zake Muumba. Ni wakati huu ndio unaoufanya mchana ukaondoka kwa kuupisha usiku. Hakika, kwetu sisi Waislamu hii Dunia si chochote ila ni wakati tu unaoiweka kuwepo hadi sasa. Matokeo yake ni baina ya mawili; ama tutaiacha sisi ama utatufikia wakati ambao Dunia itabidi iondoke na kila vilivyo Ulimwenguni tukiwemo sisi viumbe. Ni kitu gani, chatufanya kuhangaika na kuruka juu na chini bila ya kuchagua kilicho haramu au halali? Kibri chetu kitatufikisha wapi enyi ndugu wa Kiislamu? Tumefikia kupotozwa na kushughulishwa kwenye sinema na mambo ya michezo. Nani amekusanya mali zaidi ya Qaaruun? Mali yake yote aliyoikusanya haikumsaidia kuondoka hapa Duniani! Haujatufikia wakati wa sisi kuacha mzaha na Mola Wetu?
Tambua kwamba Ibliys (Laana za Allaah Ziwe juu yake), ametoa ahadi ya kutupotosha kwa kuifanya Dunia kuwa tamu. Alisema Ibliys: {{Kisha nitawafikia kwa mbele yao na nyuma yao na kuumeni (kuliani) kwao na kushotoni kwao; wengi katika wao Hutawakuta (Hutawaona) ni wenye kukushukuru}} [Suratu al-A'raaf: 17] Basi yule mwenye kumfuata Ibliys kwa kupotezwa muda wake wote kwenye pumbazo, michezo, ufuska na maovu mengine hatokuwa miongoni mwa wenye kupata Rahma Zake Muumba.
{{Atakayekufuata miongoni mwao, (Nitamtia Motoni) Niijaze Jahannamu kwa nyinyi nyote}} [Suratu al-A'raaf: 18] Basi tambua ya kwamba vyoote vilivyomo Duniani Si Chochote Si Lolote, chenye thamani mbele ya Mola Mlezi ni yale matendo mema yatakayobaki Kwake. Kumbuka Qawl Yake:
{{Na chochote mlichopewa, basi ni matumizi kwa maisha ya dunia na mapambo yake tu; lakini kilichoko kwa Mwenyezi Mungu ndicho bora na kitabaki; basi je, hamfahamu?}} [Suratu al-Qasas: 60] Jee hatujaona namna Shaytwaan alivyotukalia pembe zote nne? Ukianza Magharibi kuna pombe, mashariki kuna uzinifu, kusini kuna fitina na kaskazini kuna umwagaji damu. Na bado Shaytwaan hajatosheka, ametuwekea ligi za mipira zenye mzunguko kama wa ibada ya Swalaah, sinema zisizokwisha, nyimbo za kila aina na kila staili, na michezo ya barazani ili kutufanya wapofu wa Akhera yetu tukiishughulikia Dunia.
MWISHO