UZAYUNI KWA MTAZAMO WA IMAMU KHOMEINI
  • Kichwa: UZAYUNI KWA MTAZAMO WA IMAMU KHOMEINI
  • mwandishi: BARAZA
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 15:29:48 1-9-1403

KWA JINA LA MUUMBA MTAKATIFU

UZAYUNI KWA MTAZAMO WA IMAMU KHOMEINI

Iwapo tutalitambua suala la kuasisi serikali ya Kiislamu nchini Iran kuwa lilipewa kipaumbele cha kwanza katika fikra za kisiasa za Imam Ruhullah Khomeini, basi hapana shaka kwamba suala la kukomboa Quds tukufu na ardhi za Palestina kwa ujumla kutoka kwenye mikono ya Wazayuni wa Israel lilipewa umuhimu mkubwa katika fikra na kazi za kisiasa za shakhsia huyo nje ya Iran.

Moja kati ya hitilafu za kimsingi za Imam Khomeini na utawala wa Kipahlavi wa Shah ilikuwa ni ushawishi wa Wazayuni ndani ya Iran na kuwepo Waisraeli katika nafasi za serikali ya wakati huo ya Shah. Kwa maneno mengine ni kuwa, tunaweza kusema kuwa suala la kukomboa taifa la Iran na taifa la Palestina lilikuwa jambo la dharura na lenye kipaumbele cha kwanza katika fikra za kimapinduzi za Imam Khomeini, jambo ambalo linadhihiri wazi zaidi katika maandiko, hotuba na mapambano yake ya kisiasa. Makala hii fupi inaashiria nukta kadhaa kuhusu maudhui hiyo.

A- HISTORIA YA MSIMAMO WAKE
a- Historia fupi ya misimamo ya Imam Khomeini kuhusu Uzayuni Msimamo wa kwanza rasmi wa Imam Ruhullah Khomeini dhidi ya Uzayuni uliambatana na mwanzo wa mapambano ya kisiasa ya kiongozi huyo dhidi ya utawala wa Kipahlawi nchini Iran kuhusu hatua ya utawala huo ya kukataa kuiwekea vikwazo vya mafuta Israel na kukata uhusiano wa kidiplomasia na utawala huo ghasibu. Imam alisema katika mahojiano aliyofanyiwa wakati huo kwamba: "Moja ya mambo yanayotufanya tukabiliane na Shah ni misaada yake kwa Israel. Ameghusubu mafuta ya Waislamu na kuyatoa kwa Israel. Suala hili ni moja ya sababu za upinzani wangu dhidi ya Shah". (1)

Katika ujumbe wake mashuhuri wa sikukuu ya Nouruzi ya 1341 Hijria Samsia, Imam Khomeini alizungumzia mauaji yaliyofanywa na serikali ya Shah dhidi ya Waislamu na wanazuoni wa dini kwa ajili ya kulinda maslahi ya utawala haramu wa Israel nchini Iran. Tangu wakati huo, Imam alikuwa akizungumzia kadhia hiyo kwa nguvu zake zote katika minasaba mbalimbali ndani na nje ya Iran. Kwa mfano katika ujumbe wake kuhusu muswada wa jumuiya za kimkoa, Imam Khomeini alikosoa vikali ushawishi na satua ya Wazayuni katika taasisi za Iran. Mwaka huo huo Imam Khomeini alijibu barua ya jumuiya za wafanyakazi wa mji wa Qum nchini Iran kuhusu muswada wa serikali ya Alam wa kuwa na uhusiano wa kiuchumi na Israel akisema kuwa muswada huo ni hatari kubwa kwa Uislamu na kujitawala kwa taifa la Iran. Mwaka 1342 (19…) Imam Khomeini alijibu barua ya wanazuoni wa mkoa wa Yazd nchini Iran akisema kuwa Israel ni hatari kubwa na akatoa wito kwa wananchi wote kupinga utawala huo ghasibu na serikali ya Shah.

Moja ya misimamo mikali mno na imara ya kisiasa ya Imam Khomeini dhidi ya utawala ghasibu wa Israel ni hotuba yake mashuhuri katika msikiti wa Aadham mjini Qum, Iran baada ya kuachiwa huru kutoka jela. Imam Ruhullah Khomeini alisema katika hotuba hiyo kwamba: Enyi wananchi! Dini yetu inatuamuru kuwapinga maadui wa Uislamu. Qur'ani inatutaka kutoungana na maadui wa Usilamu mkabala wa safu za Waislamu. Hakika taifa letu linapingana na Shah katika kushikamana kwake na dola la Israel.(2)

Upinzani wa Imam Khomeini dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel ulipamba moto zaidi baada ya mauaji yaliyofanywa na utawala wa Shah katika chuo cha kidini cha Faidhiya mjini Qum. Imam alitoa hutuba kali na ya kihistoria kwa mnasaba huo akisisitiza juu ya kuendelezwa mapambano na kupinga ushawishi wa Wazayuni katika masuala ya Iran.(3)

Katika ujumbe wake wa mwezi Muharram mwaka 1343 (19…) Imam Khomeini alikutaja kuwa na uhusiano na utawala ghasibu wa Israel kuwa ni aibu kubwa na akatoa wito wa umoja na mshikamano kati ya Waislamu kwa ajili ya kupambana na utawala huo. (4) Tarehe 6/6/1347 (28/Agosti 1969) Imam alijibu barua ya kundi moja la wanamapambano wa Kipalestina akisisitiza juu ya udharura na wajibu wa kupambana na utawala haramu wa Israel na akatoa fatuwa akiruhusu kutumia mali za zaka na sadaka kuwasaidia wanamapambano kwa ajili ya kuondoa hatari ya utawala huo ghasibu. (5)

Tarehe 18 Agosti 1969 Wazayuni wa Israel waliuchoma moto msikiti wa al Aqsa. Imam Khomeini alilaani vikali kitendo hicho na akawataka Waislamu wasiujenge upya msikiti huo ili ubakie kama ushahidi wa jinai za Wazauyini mbele ya macho ya Waislamu hadi pale Palestina itakapokombolewa.

Katika kipindi chote cha kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Imam Khomeini aliendelea kutoa taarifa mbalimbali, kujibu maswali ya maulamaa na kutoa fatuwa zinazowawajibisha Waislamu wote kupigana vita vya jihadi kwa ajili ya kuikomboa Palestina na kuyasaidia makundi ya mapambano ya Kipalestina. Imam alihuisha tena maana ya jihadi na kupigania ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.

Kilele cha harakati za Imam za kupinga Uzayuni na kuunga mkono mapambano ya ukombozi wa Palestina kilikuwa ni kuainisha Ijumaa ya mwisho ya kila mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Kuikomboa Quds tukufu na kupambana na Wazayuni. Imam Ruhullah Khomeini alisema katika ujumbe wake kwa mnasaba huo kwamba: Siku ya Quds ni siku ya kimataifa. Si siku ya Quds pekee bali ni siku ya mapambano ya waliodhulumiwa dhidi ya mabeberu. Mataifa yote yanapawa kusimama kidete na kutupa kiini cha ufisadi katika kapu la taka. Siku ya Quds ni siku ya kufanya juhudi za kuikomboa Quds. Ni siku ya Uislamu na kuhuisha dini hiyo tukufu, na siku ya kutekeleza sheria za Kiislamu katika nchi za Waislamu. Siku ya Quds ni siku ya kutengana haki na batili". (6)

B- UZAYUNI
Kujitokeza Uzayuni katika sura ya dola ghasibu la Israel na tishio la pande zote la dola hilo dhidi ya Waislamu hususan katika eneo la Mashariki ya Kati kumeleta mabadiliko mengi katika eneo hilo. Hali hiyo na matokeo yake katika kamusi ya uhusiano wa kimataifa imepewa jina la "Mgogoro wa Waarabu na Israel'. Hata hivyo katika fikra za Imam Khomeini, Uzayuni umepewa jina la harakati dhidi ya Uislamu na Waislamu. Imam alifanya jitihada za kifikra za kuondoa mgogoro huo katika duara finyu la Kiarabu la kuupa sura yake halisi ya mpambano baina ya Uzayuni na Uislamu. (7) Hapana shaka kwamba jitihada hizo za Imam Khomeini zilitokana na fikra za kutaka kuleta umoja na mshikamano wa Kiislamu. Katika upande wa kisiasa na kijeshi pia jitihda hizo za Imam Khomeini ziliuweka utawala ghasibu wa Israel mkabala wa Waislamu bilioni moja na nusu badala ya Waarabu milioni mia moja.

Imam alitambua fikra zinazoupiga vita Uislamu na Waislamu za Uzayuni kuwa ndiyo sifa kuu ya harakati hiyo ya kibaguzi inayoendesha shughuli zake kwa kuungwa mkono na nchi kubwa za kikoloni. Imam Ruhullah Khomeini aliutambua Uzayuni kuwa ni harakati ya kisiasa na kikoloni isiyokuwa na uhusiano na dini wala jamii ya Kiyahudi. (8) Alitangaza waziwazi kwamba upinzani wake dhidi ya Israel na Uzayuni hauna mfungamano wowote na dini ya Kiyahudi na Wayahudi na akaeleza heshima yake kwa dini nyingine.

(9) Aliamini kwamba Uzayuni ni mwana wa ukoloni na ubeberu ambao daima unapewa himaya na misaada ya Marekani. Akiashiria uhusiano mkubwa wa Wazayuni na ubepari na mabepari wa nchi za Magharibi hususan Marekani, Imam Khomeini anaeleza chanzo na sababu ya kujitokeza Israel akisema: Israel iliundwa kutokana na njama na ushirikiano wa serikali za kikoloni za nchi za Magharibi na Mashariki kwa shabaha ya kuyakandamiza na kuyakoloni mataifa ya Kiislamu na hii leo inaungwa mkono na kusaidiwa na wakoloni wote. Uingereza na Marekani zimeuimarisha kijeshi na kisiasa utawala ghasibu wa Israel na kuuhamasisha dhidi ya Waarabu na Waislamu kwa kuupa silaha hatari za mauaji". (10)

Miongozi mwa sifa makhsusi za Uzayuni ambazo zinaonekana sana katika hotuba za Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) ni aidiolojia yake ya "Kuanzia Nile Hadi Furati". Imam alikuwa akiamini kamba uvamizi wa Israel dhidi ya nchi za Kiislamu hautaishia Palestina, Lebanon na katika miinuko ya Golan huko Syria, bali Wazayuni wanakusudia kuunda dola wanaloliita Israel Kuu na hatari yao inazilenga nchi zote za Kiislamu za Mashariki ya Kati. Imam alikuwa akizitahadharisha nchi za Kiarabu na kuziusia zijizatiti kwa silaha kwa ajili ya kutokomeza utawala huo bandia na ghasibu katika jiografia ya kisiasa na eneo la Mashariki ya Kati. (11)

Imam Khomeini alikuwa akikumbusha kuwa mipango ya mapatano ya Marekani na Israel ni mchezo wa kisiasa wa kutaka kupata fursa zaidi ya kutekeleza njama za baadaye za kufikia malengo maovu ya Uzayuni yaani kuzidhibiti nchi za Kiislamu kuanzia mto Nile hadi Furati (Euphrets). (12) Imam Khomeini ameitaja harakati hiyo ya Israel kuwa ni sawa na mwendo wa pole wa joka hatari lenye sumu kali na tishio linalotaka kupora utajiri wa eneo hili. (13)

Kwa ujumla Uzayuni katika mtazamo wa Imam una maana ya vita dhidi ya Uislamu na dini, kupenda kujitanua, mwana wa ubeberu, kiini cha ufisadi na wenzo wa kisiasa kwa ajili ya kupora ardhi na maliasili tajiri za nchi za Kiislamu ambao unataka kutimiza malengo ya kikoloni kupitia mpango habithi wa "Kuanzia mto Nile hadi Furati",.

C-MBINU NA JINSI YA KUKABILIANA NA UZAYUNI
Njia ya utatuzi wa kisiasa na kidiplomasia haikuwa na nafasi katika fikra za Imam Ruhullah Khomeini kwa ajili ya kadhia ya Palestina. Alikuwa akiamini kwamba serikali na makundi ya Kipalestina hayapaswi kupoteza wakati katika mijadala ya kidiplomasia kwa ajili ya kupata haki zilizoghusubiwa za wananchi wa Palestina. Aliamini kuwa njia pekee ya kumuangamiza adui ghasibu na Mzayuni ni mapambano ya silaha na vita vya jihadi. Imam Khomeini alikuwa akiamini kwamba utawala ghasibu wa Israel ni kama donda la saratani ambalo njia pekee ya kulitibu ni upasuaji, kulikata na kulingoa kabisa. Imam alikuwa akiwalaumu watu wanaotumia mbinu za kisiasa kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa kadhia ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na alikuwa akisema: Ninawausia viongozi wa Kipalestina waache kwenda huku na kule kukutana na Wazayuni na wapigane hadi kufa na Israel kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu SW, wananchi wa Palestina na silaha zao wenyewe. Kwani kukutana na Wazayuni kunayavunja moyo mataifa ya wanapambano. Si Magharibi wala Mashariki inayokufaeni nyinyi. Piganeni kwa kutegemea imani yenu kwa Mwenyezi Mungu na silaha zenu wenyewe hadi mtakapopata haki zenu za kisheria na wala msiache mapambano". (14)

Imam Khomeini aliutambua mfarakano na hitilafu kuwa ndio tatizo kuu la Waislamu na kwamba jambo hilo linawadhoofisha mkabala wa Israel. Imam alikuwa akisema, lau Waislamu wataungana na kila mmoja wao akamwaga ndoo moja tu ya maji, basi utawala ghasibu wa Israel utaangamia. (15)

Moja ya mbinu zilipendekezwa na Imam Ruhullah Khomeini kwa ajili ya kukabiliana na Wazayuni wa Israel ni udharura wa nchi za Kiislamu zenye utajiri wa mafuta kutouza bidhaa hii yo kwa Israel na waungaji mkono wake. Imam daima alikuwa akisisitiza kwamba nchi na mataifa ya Waislamu zinapaswa kutumia utajiri wao wa mafuta na suhula nyinginezo kama silaha dhidi ya utawala ghasibu wa Israel na madola ya kikoloni. (16) Ni vema kusema hapa kuwa Imam Khomeini alizungumzia mbinu hiyo ya vikwazo vya mafuta wakati nchi za viwanda zilikuwa bado hazijaanza mjadala juu ya nishati mbadala wala kuweka akiba ya kistratijia. Imam Khomeini alikuwa akisema kuwa tatizo kuu la Waislamu linalosababisha mashaka na masaibu mengine ni serikali vibaraka na tegemezi kwa madola makubwa na kwamba suluhisho la tatizo hilo pia liko mikononi mwa mataifa na wananchi. (17) Kuhusu nafasi ya jumuiya za kimataifa, Imam Khomeini alikuwa kisema: "Waislamu hawapaswi kuketi chini na kusubiri jumuiya za kimataifa ziwafanyie kazi. Mataifa yanapaswa kusimama na kuzilazimisha serikali za nchi zao kupambana na Israel na wala zisitosheke kwa kulaani kwa maneno matupu". (18)

Imam Khomeini ametaja siri ya ushindi kuwa ni kupigana na kuwa tayari kuuawa shahidi na kulitaja suala hilo kuwa ni siri ya Qur'ani ambayo inamfikisha mwanadamu katika mafanikio zaidi na kutimiza matarajio ya mataifa bila ya kuzingatia maisha ya kimaada na kidunia. Imam alikuwa akiyahimiza mataifa ya Kiislamu kuielewa vyema siri hiyo. (19) Imam Ruhullah Khomeini ametaja mapambano ya Intifadha ya Palestina na harakati ya Kiislamu na ya wananchi kuwa ni mti uliobarikiwa na nyota inayong'ara na kusisitiza kuwa mbinu hiyo ya mapambano ndiyo stratijia kamili zaidi kwa ajili ya kuuangamiza Uzayuni. Ametilia mkazo mno juu ya kuendelezwa na kudumishwa mapambano hayo. (20)

NATIJA
Imam Khomeini hakujuzisha mapatano ya aina yoyote na Wazayuni hata kama watatubia makosa yao ya huko nyuma. Imam alitambua mapambano ya mataifa, wananchi na serikali zinazowaunga mkono wananchi wa Palestina chini ya stratijia ya umoja wa Kiislamu na udugu wa kidini kuwa ni mambo ya dharura katika mapambano dhidi ya utawala ghasibu wa Israel. Alikuwa akisema kuwa msingi wa mapambano hayo ni vita vya jihadi, kusimama kidete wananchi hususan taifa la Palestina na kushikamana na siri ya kuwa tayari kufa shahidi na kumtegemea Mwenyezi Mungu. Intifadha ya wananchi wa Palestina iliakisi vyema fikra na stratijia hiyo ya Imam Khomeini.

MAREJEO
1- Sahifeye Nur, juz-4 mahojiano ya tarehe 16/9/ 1357 Shamsia (7 Disemba 1978)

2- Sahifeye Nur, juz-1 ukurasa wa 77 tarehe 25/2 1343 (15 Mei 1964)

3- Sahifeye Nur, juz- 1 ukurasa 154 na 157 tarehe 13/3/1343 (3 Juni 1964)

4- Sahifeye Nur, juz-1 ukurasa 137

5- Sahifeye Nur, juz-1 ukurasa 134

6- Sahifeye Nur, juz- 10 ukurasa 113, 119

7- Sahifeye Nur, juz 17 ukurasa 29 tarehe 29/6 /1361 (20 Septemba 1982)

8- Sahifeye Nur, juz- 6 ukurasa 164 tarehe 24/ 2 1358 (14 Mei 1979)

9- Sahifeye Nur, juz- 4 ukurasa 219 tarehe 24/10/1357 (14 Januari 1979)

10- Sahifeye Nur, juz- 1 ukurasa 186 tarehe 24/ 2/ 1351 (14 Mei 1972)

11- Sahifeye Nur, juz- 19 ukurasa 6,7

12- Sahifeye Nur, juz- 19 ukurasa 7

13- Sahifeye Nur, juz- 18 ukurasa 12

14- Sahifeye Nur, juz- 16 ukurasa 228 tarehe 25/4/1361 (16 Julai 1982)

15- Sahifeye Nur, juz- 8 ukurasa 235 tarehe 25/5/1358 (16 Agosti 1979)

16- Sahifeye Nur, juz- 16 ukurasa 197 tarehe 24/3/ 1361 (14 Juni 1982)

17- Sahifeye Nur, juz-12 ukurasa 278 tarehe 24/3/1359 (14 Juni 1980)

18- Sahifeye Nur, juz- 15 ukurasa 262 tarehe 25/2/60 (15/ Mei 1981)

19- Sahifeye Nur, juz- 5 ukurasa 262

20- Sahifeye Nur, juz- 20 ukurasa 179 tarehe 21/11/66 (10/02/1988)