HADITHUL QUD-SIY
  • Kichwa: HADITHUL QUD-SIY
  • mwandishi: USTADH MASOUD SHANI
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 15:12:43 1-9-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

HADITHUL QUD-SIY

Kila hadithi ambayo Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) ameinasibisha na Mwenyezi Mungu Subhanahau wa Taala inaitwa 'Hadith al Qudusy', na maana ya neno 'Al Qudusiy' ni Kutakasika na kuepukana na kila dosari. Na sababu ya kunasibishwa hadithi hizi na Mwenyezi Mungu ni kuwa maneno yake yanatokana Naye Subhanahu wa Taala.

Na sababu ya kuitwa 'Hadithi', ni kwa sababu Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) ndiye msemaji wa Mwenyezi Mungu ndani yake, tofauti na Qurani ambapo hapana anayetajwa au kuongezwa isipokuwa Mwenyezi Mungu. Kwa mfano tunapozungumza juu ya aya ya Qurani tunasema; "Mwenyezi Mungu anasema." Ama tunapozungumza juu ya Hadith al Qudusiy tunaanza kwa kusema; "Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) amesema, kuwa Mwenyezi Mungu amemuambia." Au kwa maneno mengine yenye mfano huo.

Tofauti iliyopo baina ya Hadith al Qudusiy na hadithi nyengine za Mtume (SAW), ni kuwa; Hadithi hizi moja kwa moja zinanasibishwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) na kwamba yeye ndiye msemaji wa maneno hayo. Ama Hadith al Qudusiy zinanasibishwa na Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala, na Mtume (SAW) anapohadithia huyanasibisha maneno yake moja kwa moja kwa Mwenyezi Mungu, na hii ndiyo sababu zikaitwa 'Hadith al Qudusiy', na nyingine zikaitwa 'Ahadith Nabawiyah, yaani "Hadithi za Mtume.", juu ya kuwa hadithi zote asili yake ni 'Wahyi' anaofunuliwa na Mola wake Subhanahu wa Taala, kwani Mwenyezi Mungu anasema;

"Wala hasemi kwa matamanio (ya nafsi yake). Hayakuwa haya (anayosema) ila ni Wahyi uliofunuliwa (kwake)."
Suratun Najm - 3-4
Inapasa kukumbushana hapa kuwa kupewa hadithi hizi jina la Al Qudusiy hakumtakasi mtoaji wa hadithi au wapokezi wa hadithi za aina hii, kwani wasfu wa "Al Qudusiy' ni wasfu wa hadithi na si wasfu wa wapokezi wake wala wa watoaji wake, kwani zimo Hadith al Qudusiy sahihi na dhaifu na hata hadithi maudhui (zilizopachikwa tu - za uongo).

Mfano wa Hadith al Qudusiy;
Kutoka kwa Abi Dhar (RA) kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) akihadithia juu ya aloambiwa na Mola wake Azza wa Jalla kuwa alisema; "Enyi waja wangu! Hakika mimi nimejiharamishia nasfi yangu dhulma, kisha nikaijaalia kuwa haramu baina yenu (pia), kwa hivyo msidhulumiane."
Muslim Juzu ya nne ukurasa wa 1994
Maulamaa wamezungumza pia juu ya hitilafu iliyopo baina ya Qurani tukufu na Hadith al Qudusiy, wakasema;
1. Qurani tukufu ni muujiza ulohifadhika usoweza kubadilishwa wala kuongezwa wala kupunguzwa ndani yake, na utabaki hivyo mpaka kitakaposimama Kiama, , na mapokezi yake ni Mutawatir (na maana yake ni kuwa; imepokewa maneno yake na herufi zake na njia zake hivi hivi kama ilivyo kutoka kwa wapokezi wengi sana wenye kuaminika, kupitia tabaka mbali mbali na kwa njia nyingi sana)

2. Matamshi na maana ya maneno ya Qurani tukufu yanatokana na Mwenyezi Mungu Subhanahau wa Taala moja kwa moja bila mabadiliko, wakati maneno ya Hadith al Qudusiy matamshi yake yanatoka kwa Mtume (SAW) lakini maana inatoka kwa Mwenyezi Mungu na kwa Wahyi.

3. Kusoma Qurani ni ibada ambayo ndani yake unapata thawabu kumi kwa kila herufi.
4. Qurani lazima isomwe ndani ya Sala, wakati haijuzu kusoma Hadith al Qudusiy ndani ya Sala.
5. Ni haramu kuisoma Qurani kwa kutumia maneno mengine hata kama mneno hayo yanaleta maana sahihi, wakati inajuzu kusoma hadithi ya Al Qudusiy kwa maneno mengine, muhimu yawe yanaleta maana sahihi.
Wallahu taala aalam
Wassalaam alaykum wa Rahmatullahi wa Barakatuh
MWISHO