NDOA YA MUDA
  • Kichwa: NDOA YA MUDA
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 18:22:56 1-9-1403

BSMILAHI AR-RAHMANI AR-RAHIIMI

NDOA YA MUDA

Ni nini tofauti kati ya ndoa ya muda na kitendo cha zina? - Hussein Muigai Waweru wa Malindi Kenya. Katika kujibu swali hili, ni vyema tukumbushe hapa kwamba, kama unavyojua, dini tukufu ya Kiislamu ndiyo dini ya pekee iliyokamilika katika kila upande wa mahitaji ya maisha ya mwanadamu humu duniani na huko Akhera.

Kwa ibara nyingine ni kwamba, dini hii ina majibu kwa kila mahitaji na matatizo yanayomkabili mwanadamu katika maisha yake humu duniani, bila ya kusahau kwamba, inazingatia pia mahitaji yake katika maisha yake ya baada ya kuondoka humu duniani. Mahitaji hayo ni pamoja na ya kiuchumi, kisiasa, kijamii, kiutamaduni na yanayomhusu mtu binafsi.
Ndoa ni mojawapo ya mahitaji muhimu sana ya mwanadamu ambayo ni rehema kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa waja wake humu duniani, na kwa lengo la kuleta utulivu na usalama katika jamii ya mwanadamu.

Kama tulivyoliashiria suala hili katika vipindi vyetu vilivyopita, kuna ndoa aina mbili katika dini ya Kiislamu, ya kudumu na ya muda. Ndoa ya kudumu kama jina lake linavyoashiria, ni mkataba na makubaliano yanayofikiwa kati ya pande mbili za mume na mke kwa lengo la kuendelea kuishi pamoja daima katika maisha ya ndoa na familia.

Mkataba au makubaliano hayo hubatilika pindi pande hizo zinapoamua kutengana kindoa au kupeana talaka au pale mmoja watu hao waliooana kindoa anapoaga dunia. Kutokana na kuwa tutajishughulisha zaidi na kujibu suala linalohusiana na ndoa ya muda, tunajiepusha kuzungumzia kwa urefu suala la ndoa ya daima kutokana na kuwa hatuna nafasi ya kutosha ya kujadili ndoa zote mbili kwa pamoja.

Ndoa ya muda kama inavyobainika wazi, ni makubaliano kati ya mume na mke kwa madhumuni ya kuishi pamoja kwa muda na wakati maalum ulioainishwa na kuafikiwa na pande husika kama mume na mke, na kwa hivyo ni wazi kwamba, ndoa hiyo humalizika kwa kumalizika muda ulioainishwa katika makubaliano ya ndoa, na wala hakuna haja yoyote ya kusoma ibara za kubatilisha ndoa hiyo.

Muda unapokwisha huo, ndio huwa mwisho wa ndoa hiyo. Suratu Nisaa inaashiria suala hilo kwa kusema; "Basi wale mnaowaoa wapeni mahari yaliyolazimishwa. Wala si vibaya kwenu katika (kutoa) yale mliyoridhiana badala ya yale yaliyotajwa." Neno Istimtaa' lililotumika katika matini ya Kiarabu ya aya hiyo inaashiria ndoa hii ya muda.

Baadhi ya masahaba, na wafuasi wa masahaba wa Mtume kama vile Ibn Abbas, Abi bin Kaab, Jabir bin Abdallah na wengineo miongoni mwa wafasiri wa Kishia wa Qur'ani Tukufu na vilevile wa Kisunni kama vile Fakhru Razi na Tabari wote wanatoa tafsiri ya aina hiyo kuhusiana na aya hiyo.

Tunaweza kusema kutokana na aya hiyo kwamba ndoa hiyo ya muda ilikuwa imeenea sana katika zama za Mtume Mtukufu na hiyo ndiyo maana ikajadiliwa na kuzumgumzwa katika kitabu kitakatifu cha Qur'ani. Mbali na Qur'ani, kuna riwaya nyingi sana za Kiislamu ambazo zinabainisha wazi kwamba ndoa hiyo ya muda ilikuwa imeenea sana katika zama za Mtume (SAW), na kwamba iliendelea kutekelezwa na Waislamu hadi kipindi cha utawala wa Khalifa Omar. Hata hivyo khalifa huyo baadaye aliiharamisha ndoa hiyo kutokana na dalili alizoziona mwenyewe kwamba zililazimu kuharamishwa kwa ndoa hiyo.

Lakini kutokana na ukweli huu kwamba ndoa hiyo muhimu iliwekwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe pamoja na Mtume wake mwanzoni mwa Uislamu, ilifaa kutekelezwa katika nyakati zote za uhai wa mwanadamu madamu hakuna dalili yoyote ya wazi kutoka kwa Mtume inayoharamisha ndoa hiyo. Ndoa ya muda, ni ndoa ambayo iwapo itatekelezwa vyema kama inavyotakiwa na Uislamu, si tu kwamba haiwezi kusababisha matatizo yoyote, bali utakuwa ni utatuzi mzuri sana unaoweza kuileta jamii manufaa mengi, na kuikinga na matatizo mbalimbali ya kijamii kama tunavyoshuhudia katika jamii zatu za leo.

Kuna uwezekana kwamba mtu ambaye hajafanikiwa kuoa ndoa ya kudumu asiwe na uwezo wa kufanya hivyo kutokana na sababu mbalimbali za kishughuli ya kimasomo. Kwa ibara nyingine, huenda mtu asiwe na fursa ya kuoa au kuolewa kutokana na matatizo ya kiuchumi, umasikini, au kuwa katika hali ya kuendelea na masomo jambo linaloweza kumzuia asiweze kuwa tayari kulinda familia yake katika mazingira ya kawaida ya kuwa baba au mama katika familia hiyo. Vile vile mtu anaweza kukosa fursa ya kuwa na mke wa daima kutokana na shughuli za kikazi.

Kwa mfano mtu anayefanya kazi katika sehemu ya mbali na mkewe na hivyo kutokuwa na uwezo wa kuishi na mke huyo katika sehemu anayofanyia kazi, hukabiliwa na hali ngumu sana ya kimaisha anapojipata kuwa hana uwezo wa kikidhi mahitaji yake ya kimwili na kimatamanio kutokana na mkewe kuwa mbali naye. Kwa hivyo, katika hali kama hiyo badala ya watu kujihusisha na vitendo vya zina na viovu katika jamii, Uislamu umewaainishia njia ya kukidhi kwa usalama na kisheria majitaji yao ya kijinsia kwa kuwachagulia ndoa ya muda. Jambo hilo husaidia sana katika kuzuia watu kutumbukia katika masuala yanayoenda kinyume na maadili ya kidini na kiakhlaqi katika jamii, na hivyo kuwaepusha na dhambi ya zina.

Kutokana na kuwa ndoa hii hutimia baada ya makubaliano ya pande mbili za mke na mume kukubaliana kuishi pamoja kisheria na kwa muda maalum, uwezekano wa kuenea ufisadi na vitendo viovu vya kijinsia hupungua sana katika jamii, kinyume na kama ambavyo baadhi ya watu hujaribu kuonyesha kwamba ndoa hiyo ni aina moja ya vitendo vya zina.

Ndoa hiyo ni sawa kabisa na ndoa ya kudumu, kwa sababu nafasi ya mume na mke imebainishwa wazi katika ndoa hiyo, na hivyo kuzuia uhusiano mwingine wowote usiokuwa huo nje ya ndoa. Kwa kutekelezwa ndoa hiyo, magonjwa hatari kama vile Ukimwi yanayotokana na uhusiano haramu wa kijinsia baina ya watu wasiojali maadili hupotea kabisa au kupundua kwa kiwango kikubwa.

Kuongezeka kwa umri wa ndoa, kuongezeka idadi ya wanawake wasioolewa ikilinghanishwa na ya wanaume, urefu wa umri wa wanawake kuliko wanaume, kiwango kikubwa cha matamanio katika wanaume kuliko wanawake, matatizo ya kiuchumi na vita, ni miongoni mwa mambo yanayofanya ndoa ya muda kuwa ya dharura.

Ni wazi kuwa kuwepo kwa matatizo kama hayo na hasa vita, huongeza kwa kiwango kikubwa idadi ya wanawake wasio na ulinzi wa kifamilia, na hivyo kuandaa uwanja wa kuongezeka vitendo vya ufisadi wa kijinsia katika jamii. Kwa hivyo, ili kujitokeza na kulinda wanawake kama hao wanaokabiliwa na hatari kubwa ya kutumiwa vibaya na watu wasiojali wala kuzingatia maadili ya kijamii, wanaume wanaweza kukubaliana na wanawake na kufunga ndoa ya muda ili kulinda usalama wa jamii.

Kwa hakika mojawapo ya faida kubwa za ndoa ya muda ni kuwalinda wanawake wasio na wanaume, wanawake ambao kwa kuwa na watoto pia matatizo yao ya kijamii na kifamilia huongezeka. Kwa hivyo ndoa hiyo hukinga na kuwalinda wanawake kama hayo na mambo maovu ambayo wanaweza kushawishika kuyatenda wasipokuwa na mtu wa kuwalinda na kuwakidhia majitaji yao ya kifamilia.

Ni wazi kuwa, watu waliohitimu umri wa kufunga ndoa iwe ni ya daima au ya muda, wanapoamua kuoana, matatizo yao ya kiroho na kinafsi hutatuka, na hivyo kiwango cha ufasadi wa kijinsia katika jamii kupungua kwa kiwango kikubwa. Jambo hilo huwapa watu wote waliohitimu umri wa kuoana haki yao ya kimsingi na ya kimaumbile yaani ndoa kati ya mume na mke na hivyo kupunguza idadi ya watu wasiooana katika jamii.

Pamoja na hayo yote, lakini nukta tunayopaswa kusisitiza hapa ni hii kwamba Uislamu haujamuhusia Muislamu ndoa ya muda kama njia ya kwanza muhimu ya kutatua matatizo yake ya kijinsia na kifamilia. Yaani watu walio na uwezo wa kujenga familia na kuishi kwa salama katika mazingira yenye furaha ya familia hiyo, wanapaswa kufanya kila wawezalo ili kufunga ndoa ya kudumu na hivyo kubuni jamii safi inayozingatia maadili yote ya kibinadamu na kidini.

Mwishoni, ni vyema kuashiria hapa baadhi ya nukta zinazopaswa kuzingatiwa katika ndoa ya muda. 1- Katika ndoa hii sawa kabisa na ilivyo ndoa ya kudumu, ibara au maneno ya kufunga nikah husomwa kabla ya watu wawili wanaotarajia kufunga kufunga ndoa hiyo, kuchukuliwa kuwa mume na mke. Toauti iliyopo katika ndoa hiyo ni ile ya kudumu ni hii kwamba katika ndoa ya muda, kipindi na muda maalumu wa ndoa hiyo huwa umeainishwa.

2- Katika ndoa ya muda kama ilivyo katika ndoa ya kudumu, mahari inapaswa kuainishwa kabla ya kufungwa ndoa hiyo, na ni jukumu la mume kumpa mke mahari hiyo.

3- Baada ya kumalizika muda ulioainishwa wakati wa kufunga ndoa, watu haoa waliooana wanaweza kuafikiana kuurefusha muda huo au kuachana. 4- Watoto wanaozaliwa kutokana na ndoa kama hiyo ni watoto halali wa wazazi wao na kwa hivyo wana haki ya kuwarithi sawa kabisa na kama ilivyo katika ndoa ya kudumu.

5- Mume na mke wanaofunga ndoa ya muda wanaweza kuafikiana juu ya mume kumpa au kutompa mke nafaka au kwa ibara nyingine chakula na mahitaji ya lazima kama vile mavazi na mengineo.

MWISHO