KUJIFANANISHA NA MAKAFIRI
  • Kichwa: KUJIFANANISHA NA MAKAFIRI
  • mwandishi: MUHAMMAD FARAJ SALEM AL SAIY
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 18:53:11 1-9-1403

BSMILAHI AR-RAHMANI AR-RAHIIMI

KUJIFANANISHA NA MAKAFIRI

Assalamu alaikum ndugu wasomaji Shukrani zote ni zake Mwenyezi Mungu , tunashuhudia ya kwamba hapana mola anaepaswa kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad (SAW) ni Mtume wake , ameufikisha ujumbe na kuifikisha amana aliyopewa , kwa hivyo tunakuomba Mola wetu umsalie na kumsalimu Mtume wako huyu mtukufu pamoja na Aali yake na Masahaba wake watukufu - Aamin.

Amma baad,
Katika mambo yanayosikitisha sana wakati huu ni kule vijana wetu kuzama na kupotea kabisa kwa kuwaigiza makafiri katika kila nyanja za maisha yao. Vijana wa Kiislamu, wengi wao wameipoteza tabia yao , wamekipoteza kitambulisho chao , kama kwamba wanaona haya kusema " Mimi ni Mwislamu". Anasema Sheikh Ahmed Deedat, " Nilipoingia Hong Kong , nilitamani nimuone Mwislamu angalau mmoja amevaa mavazi ya Kiislamu , nione dalili ya Uislamu angalau katika uso wa mmoja wao , nilitamani nimuone angalau mmoja tu anasema , "Mimi hapa Muislamu" natizama huku na kule , sikumuona hata mmoja , wote wamejificha ndani ya mavazi ya Kizungu."

Anaendelea kusema Sheikh Deedat , " Nikawaona Masingasinga wamevaa mavazi yao, huku wakitafakhari kwa usingasinga wao, kama kwamba wanasema " Mimi hapa Mr. Singh" . (Mwisho wa maneno ya Sh.Deedat) Nilipoulizwa na mmoja katika wana Zanzinet, " Kwa nini huandiki juu ya maudhui haya ya vijana wa kiislamu kuwaiga makafiri?" Nikakikumbuka kisa hicho cha Sheikh Deedat na kwa bahati, siku ya pili nilipofungua tu, gazeti la kiarabu liitwalo Al Ittihad, katika makala yake ya dini nikayaona Maudhui haya yameandikwa kwa ufupi na kwa ukamilifu .

Ninaona ni bora niyafasiri kwa lugha yetu ya Kiswahili ili sote tufaidike . Mwandishi anasema :
Maudhui ya vijana wa Kiislamu kuwaigiza makafiri yamekuwa muhimu sana , na tunawaomba Maulamaa wetu wawe wananasihi na kuzungumzia zaidi juu ya jambo hili ili vijana wetu waweze kufahamu maamrisho ya dini yao.

Na katika makosa wanayofanya vijana wa kiislamu ni kule kuvaa mishono ya kisasa ya kizungu isiyokuwa na heshima na kufuata mwenendo wa vijana wa kizungu waliodanganyika na kuhadaika na dunia, na kule kukata nywele zao kwa mikato ya Marines, na kuvaa minyororo ya dhahabu shingoni (chains) na pia kuivaa mikononi mwao au kuvaa herini sikio moja au hata yote mawili. Kwa ajili hii, vijana wetu huonekana kama vikaragosi wakiwa katika hali ya kuwaiga wazungu .

Na mushkila huu upo miongoni mwa vijana wa kike na wa kiume sawa sawa, maana wanawake pia huvaa nguo zisizokuwa za heshima na kujipaka mapoda na michanganyiko ya rangi mbali mbali ili wawababaishe vijana wenzao wa kiume na kuwaingiza katika mitihani mikubwa.

Dr. Abdulla Shahata ambaye ni mkuu wa Sehemu ya Sheria katika Chuo Kikuu cha AL Azhar, anasema ; " Mwenyezi Mungu amemuumba Mwanadamu katika umbo lililo bora kabisa na ameamrisha Waislamu wawe nadhifu . Mtume (SAW) amesema " Kuweni wanadhifu na mjipambe ili muwe mfano wa doa jeupe baina ya mataifa " na akasema , " Hakika Mwenyezi Mungu ni mzuri na anapenda vilivyo vizuri …." Na siku moja mtu mmoja alipoingia katika majlis ya Mtume (SAW) na nywele za mtu huyo zilikuwa Timtim , Mtume (SAW) akamwambia " Mmoja wenu anatuingilia nywele zake zikiwa zimetimka kama shetani kweni nymbani kwako hamna kitana ?".

Kujifananisha na wanawake
Dr. Shahata anaendelea kusema, " Imepokelewa kwamba , Mtume (SAW) amesema " Mwenyezi Mungu amewalani wanaume wanojifananisha na wanawake na (amewalani) wanawake wanaojifananisha na wanaume ". na sisi tunaelewa kwamba Mayahudi ndio wanaofanya kila juhudi kupitia vyombo vya habari na sinema ili kuwabakilisha vijana wetu , na wanaume wanaofuga nywele ndefu na kuzifunga au kuzichana au kukata mikato kama ya wanawake anakuwa ametoka katika heshima za kiislamu , na waislamu lazima wazichunge nia zao na dhamiri zao ".

Kwa kawaida kufuga nywele zikawa ndefu , hapana ubaya ndani yake au kuvaa mavazi mazuri hapana ubaya , isipokuwa ubaya unapatikana pale mtu anapofuga nywele au kuvaa nguo akawa hapana tofauti baina yake na baina ya mwanamke." Mkato wa Marines
Anasema Dr. Abdul Ghafar Hilal Mkuu wa chuo cha elimu za dini katika chuo kikuu cha Al Azhar , " Vijana wengi siku hizi wanapenda kukata nywele sehemu za pembeni na kuacha katikati ya vichwa vyao nywele nyingi na huita mkato huo "Marines" na huku ni kuwafuata makafiri kama kipofu aliyeshikwa mkono , na hakunasibiani kabisa na mafunzo ya dini yetu tukufu ." Vijana wetu badala ya kuwafuata makafiri hawa katika mwenendo wao na kuwafanya kama ni ruwaza njema yao wangelifuata mafundisho ya dini yao na mwenendo wa Mtume wao (SAW)" Kubururwa Na Ustaarab Wa Wazungu

Anasema Dr. Musatafa Mahmoud ambaye ni mmoja ktika wanavyuoni wa kiislamu, " Ni juu ya vijana wetu kuamka kidogo na waweze kutambua kwamba huo ni mwenendo wa mabaradhuli wa kiyahudi ambao wanataka kuangamiza akili za vijana wetu ." "Utakuta kwa mfano , mwanamume amejifananisha na mwanamke akiwa amevaa nguo zenye rangi za kike na marinda ya kike , utamkuta amevaa herini na amezikata na kuzichana nywele zake kama mwanamke na huku amevaa kidani shingoni mwake na mkononi mwake au amefuga nywele mfano wa wale wavuta bangi wa visiwa vya Carribean. Jee Huyu ndiye kijana wa Kiislamu ambaye anatakiwa awe mwanamume kweli kweli ili aweze kuilingania dini yake na kupigana Jihad ?

Kisha utaona baadhi ya kina mama wakijifananisha na wanaume, utawakuta wamekata mikato ya kiume na kuvaa masuti kama wanaume , bali wengine wameingia hata katika kucheza mipira na ngumi na mieleka . Iko wapi dini na ziko wapi haya ?" anauliza Dr, Mahmoud Mustafa.
"Amma kujipaka mafuta na aina mbali mbali za rangi na podari si haramu ikiwa mwanamke atajipamba mbele ya mumewe ama kujipamba na kujitoa nje mbele ya vijana ili awababaishe na kuwatamanisha vijana hao na kuharibu jamii ya kiislamu basi hayo ni Haramu " anasema Dr. Mohammad Ibrahim Fayoumi - Katibu Mkuu Wa Uhusiano Wa Waislamu Huko Misri. MUHAMMAD FARAJ SALEM AL SAIY