BSMILAHI AR-RAHMANI AR-RAHIIMI
HAKI ZA MAJIRANI
Tuanze na kujiuliza, jirani ni nani? Jirani tunayemkusudia hapa ni yule mtu aliye karibu yako kimakazi, yaani nyumba zenu zinakurubiana. Mtu mwenye wasifu huu ana haki kubwa juu yako, ewe muislamu. Itakaposadifu kwamba jirani yako ni ndugu yako wa nasabu na akawa ni muislamu mwenzako. Basi jirani huyu atakuwa ana haki tatu kwako; haki ya ujirani, haki ya udugu na haki ya Uislamu. Na akiwa jirani yako ni muislamu lakini si nduguyo wa nasabu, huyu atakuwa nazo kwako haki mbili; haki ya ujirani na haki ya Uislamu. Na iwapo jirani yako huyu si muislamu na hapana udugu baina yenu, jirani huyu atamiliki kwako haki moja tu nayo ni haki ya ujirani. Hivi ndivyo anavyotufundisha Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie:
"Majirani ni watatu; jirani mwenye haki moja naye ndiye mwenye haki ndogo kuliko wote. Na jirani mwenye haki mbili na jirani mwenye haki tatu. Ama yule ambaye mwenye haki moja ni jirani mushriki (kafiri), na ama ambaye mwenye haki mbili ni jirani muislamu (ana) haki ya Uislamu na haki ya ujirani. Na ama yule mwenye haki tatu ni jirani muislamu aliye ndugu, (ana) haki ya Uislamu, haki ya ujirani na haki udugu". Al-Bazzaar & Abuu Nuaim.
Muislamu anakiri, anaikubali na kuichunga haki ya jirani akiamini kuwa kufanya hivyo ni kuitekeleza amri ya Mola wake: "MWABUDUNI ALLAH WALA MSIMSHIRIKISHE NA CHO CHOTE NA WAFANYIENI IHSANI WAZAZI WAWILI NA JAMAA NA MAYATIMA NA MASKINI NA JIRANI WALIO KARIBU NA JIRANI WALIO MBALI--- [ 4 : 36]
Naye Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kama mfasiri mkuu wa Qur-ani, anauelezea uzito wa haki hii ya jirani iliyotajwa ndani ya Qur-ani anasema: "Hakuacha Jibril kuniusia juu ya jirani mpaka nikadhani kwamba atampa na haki ya kurithi". Bukhaariy & Muslim.
Miongoni mwa haki za jirani kama zilivyoelezwa na Uislamu ni kumtendea wema kiasi cha uwezo wa mtu. Mtendee wema jirani yako kwa mali yako, cheo chako na kila chako chenye kuweza kumnufaisha kwa namna moja au nyingine. Hivi ndivyo anavyo tufundisha. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie- kutokana na kauli yake: "Jirani bora mbele ya Allah ni yule aliye mwema kwa jirani yake". Tirmidhiy.
Na akasema tena Bwana Mtume: "Mwenye kumuamini Allah na siku ya mwisho basi na amtendee wema jirani yake". Muslim. Kauli hii ya Mtume wa Allah kama inafahamisha jambo, basi jambo hilo si jingine bali ni kuwa ukitaka kumjua muumini wa kweli basi muangalie anavyoishi na jirani yake. Imepokelewa kutoka kwa Muawiyah Ibn Jundub-Allah amuwiye radhi-kwamba alimuuliza Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: "Ewe Mtume wa Allah, ni ipi haki ya jirani kwa jirani yake? Mtume akamjibu:-
Akiugua mkague (mtake hali), Akifa msindikize (nenda kamzike), Akikuomba mkopo, mkopeshe, Akienda utupu (hana nguo), msitiri ( mvike ), Akipatwa na kheri, mpongeze, Akipatwa na msiba, muizi (mfanyie ta'azia), Wala usinyanyue nyumba yako zaidi kuliko nyumba yake ukamzibia hewa/upepo, Na wala usimuudhi kwa harufu ya chungu chako ila umchotee kidogo". Twabaraaniy
Kumtendea wema jirani alikokueleza Bwana Mtume katika hadithi tulizozitaja ni pamoja na kumpelekea zawadi katika furaha mbali mbali anazozipata. Mithili ya kufaulu katika mtihani, kupata cheo, kuzaliwa mtoto, kuoa/kuozesha, kujenga nyumba na kadhalika. Falsafa na siri ya kupeana zawadi ni kujenga mapenzi na kuondosha chuki na uadui kama anavyolibainisha hilo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: "Peaneni zawadi mtapendana, na peaneni mikono itakuondokeeni chuki baina yenu". Ibn Asaakir.
Na katika jumla ya haki za jirani ni kutokumuudhi kwa kauli au matendo. Siku moja Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie- alisema: "Wallahi hawi muumini, Wallahi hawi muumini, Wallahi hawi muumini. Maswahaba wakamuuliza: Ni nani huyo ewe Mtume wa Allah? Akajibu: Huyo ni yule ambaye jirani yakke hasalimiki na shari/uovu wake". Bukhaariy Mtu mmoja alimuendea Mtume wa Allah na kumuambia: "Hakika mwanamke fulani anatajwa sana kwa wingi wa swala zake, kutoa kwake sadaka kwa wingi na wingi wa kufunga kwake. Isipokuwa kwamba yeye anamuudhi jirani yake kwa ulimi wake. Mtume akasema: "(Pamoja na ibada zake zote hizo, mwanamke) huyo ataingia motoni". Ahmad, Al-Bazzaar, Ibn Hibbaan & Al-haakim.
Kauli hii ya Mtume wa Allah inaonyesha uzito wa dhambi ya kumuudhi jirani na kwamba ibada ya mtu anayemfanyia maudhi jirani yake haitamsaidia kuingia peponi jirani huyo mbaya. Na kinyume chake, kutokumuudhi jirani ni sababu tosha inayoweza kumuingiza mtu peponi, kwani kukaa kwa wema na jirani bila ya kumuudhi kwa maneno au matendo ni kielelezo cha wema wa mja. Imepokelewa kwamba mtu mmoja alimwambia Mtume wa Allah- Rehema na Amani zimshukie-nijulishe amali ambayo nitakapoitenda nitaingia peponi. Mtume akamjibu: "Kuwa mwema". Akasema mtu yule: Ewe Mtume wa Allah, nitajuaje kwamba mimi ni mwema?
Mtume akamwambia: Waulize jirani zako, wakikuambia kwamba wewe ni mtu mwema basi fahamu kwamba wewe ni mwema (kweli). Na wakikuambia kwamba wewe ni mtu mbaya (muovu), basi fahamu kwamba wewe ni mbaya (kweli )". Al-Baihaqiy
Huyu ndiye jirani na haki yake katika Uislamu, lakini watu wengi miongoni mwetu hawaijali haki hii ya ujirani. Kutokuitambua haki hii ya ujirani ndio imekuwa sababu kuu ya magomvi uadui na mizozo mitaani mwetu. Utawaona majirani daima wakigombana kwa mambo ya kipuuzi kabisa kiasi cha kuwafanya wasijuliane hali na kutokushirikiana katika furaha wala huzuni. Huu si Uislamu aliokuja nao Bwana Mtume kutoka kwa Allah, muislamu wa kweli haishi hivyo na jirani yake hata kama si muislamu mwenziwe(kafiri )
MWISHO