UMRI WA MWANAADAMU
  • Kichwa: UMRI WA MWANAADAMU
  • mwandishi: AL-UDII
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 19:1:3 1-9-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

UMRI WA MWANAADAMU

Umri Haurudi kwa maana miaka unayoishi huisha tena tunavyoishi na muda wetu ni siri hakuna ajuaye ila aliyetuumba. Viungo hunyongonyea umri ukiwa mkubwa, nuru hupungua ya macho au kutoweka kabisa, Sauti hubadilika, na sisi hupinda mgongo kama tulikuwa ni warefu wa kimo hurudi kidogo. Nguvu zile za ujana na wingi wa starehe ama huzitamani tungekuwa nazo wakati wote au kwa uzee tunaofikia tukijipima na tukazihesabu amali zetu tulizozitenda ujanani zisizokuwa na kheri, baadhi yetu hulia hata katika sala au yakihadithiwa yale yetu na vikundi katika jamii, basi si hasha tukabadili hata njia maana pengine watu wakati huo wanafinyana masikio, “ndo huyo kiumbe” zama zimepita, alitamba zama zake. Basi baadhi yetu hatupendi kuyasikia yakikumbushwa yetu “yanatia haya” yanatufanya tujute, lakini pia yanawanyanyasisha wana wetu wanaposikia baba yao hatajwi kwa wema.
Maneno haya tunayasema ili tujue kwamba ni tabia ya Wanaadam wengi kuhifadhi maovu ya watu kuliko yale mema tuliyoyatenda. Si vizuri kusemana na wakati mwengine huambizana wenyewe kwa wenyewe “tusifukue makaburi yaliyopita yamepita au ndoo ujana” na wengine husema “dah nimepoteza wakati sana”. Tunasema umri haurudi lakini umbile jipya linaloweza kurudi kama yeyote kaandikiwa Umri mkubwa, basi ni ule umri wa uadilifu na huu unahitaji sana kuchungwa ili usiwe mbaya kwa kuandaliwa, bali uwe wakuoteshwa jua huku tukisema Masha’Allah Mzee kala chumvi, lakini Bwana au Bibi huyu alikuwa Mtu wa ibada Mcha Mungu, mtu wa msaada kwa watu, alikuwa na mdomo mzuri kwa watu na alikuwa mpole na mlezi mzuri kwa wanawe, basi huyu kwa umri wake ambao hufikia hata majira ya sala yaingiapo au usiku na mchana au kutojijua kuwa sasa kalala au yumacho au kutowatambua tena wanawe kwa ukongwe alionao na kumbukumbu za mambo huja na kutoka, basi naiwe fakhari na akhitimike vyema mjaa huyu. Wapo wazee wa aina hii kama kioo kwa wazee wenziwao, waige, wajirudi na waangalie khatima zao. Vizazi vyao kwa bahati njema hupewa huruma na Mola mtukufu wasione taklifah hata chembe kumhudumia, kumpa maneno ya matumaini na kumtambulisha yapitayo japo hayaoni kwa kuwa haoni vyema au hayatambui, lakini mahaba yale yanamuandama hadi siku yake ifike.
Kwa kuwa hayo ni ya umri ambao tunasema haurudi ambao usipoutumia vyema utakuangusha na ukiutumia vyema utakunyanyua daraja, basi si haki ya tajiri pekee au mwiko kwa maskini, lakini kote kiwiliwili kinahusika maana kipato hakijengi tabia wala ufukara si sababu ya kupotoka tabia ni mawazo ni fikra zenye kujirejea. Jee fikra hurudi? Naam hurudi kwa Yule ajuae kufikiri ni tofauti na umri. Mwenye kujua kufikiri hujiuliza nilianza anzaje hadi nikafika hapa nilipo. Alie tajiri hujitathimini kabla ya kuwabeza walio maskini vyenginevyo hatakuwa na marejeo wala kinga pale dunia itakapo mrudi ghafla kwa kiburi chake. Si tunawaona humu waliochezea pesa na ulwa walivyo dhalili baadae, lakini umri umewapita, basi waliomahiri wa kufikiri wanajutia kimoyo moyo wanapojifikiri walivyo na wapi walitokea, lakini jee wale walomuonya kama wapo huwaangalia vipi na jee wale aliowabeza wakati ule na sasa wametononoka, moyo wake huuma kiasi gani aonapo wamestawi na yeye amerudi nyuma hatua kumi. Basi fikra zina nafasi ya kurudi kama mtu haja changanyikiwa bado kwa yaliyo mfika. Wapo wajuao kuwa M/Mungu yupo, dunia inapowapa kisogo, lazima hawa wawe kioo kwetu tusiwacheke au kuwabeza ni mtihani, si hadithi tena ni hali ya kawaida miaka yetu hii.
Baadhi yetu tukimuona Yule anachomoza hatutoi noti zetu kuhesabu au kununua kitu maana ni zamu yake kuonja shida. Tusiwakimbie tushukuru na tuwasaidie, bali tusome kutokana na makosa yao na tusitakabar. Mtu wa aina hiyo kama unamuelewa namna alivyokuwa Muombee M/Mungu amsamehe maana mtihani huo si wa mmoja usipotanabahi dunia ikakutia kamba ya sheiytani unaweza ukasahau umri wako kwa kudhani ulikosa mengi yaliyowafaidisha wenzio ujanani mwao . kwa vijana wa leo wanakila sababu ya kujiepusha kuutumia umri wao vibaya kwani wana mengi ya kujifunza, wanasikia, wanaona na wachambuzi zaidi hata kwa kupima, lakini walichozidiwa na wakongwe waliopita, waliona bila miwani na vijana waleo sharti kila kitu tukione kikijiri kwa darubini kuliko ukweli wa maumbile na mkatiko wa uhai. Akili zetu zipo na asilimia kubwa na kuishi zaidi kuliko kuondoka wakati wowote, badala kuikanyaga ardhi hutufukia sisi.

MWISHO