VIZUIZI VYA UMOJA
  • Kichwa: VIZUIZI VYA UMOJA
  • mwandishi: BARAZA
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 19:12:59 1-9-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

VIZUIZI VYA UMOJA

Ulimwengu wa Kiislamu umekuwa ukikabiliwa na matatizo mbalimbali katika juhudi zake za kuleta umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu. Matatizo hayo yamekuwa yakitoka nje na ndani ya ulimwengu wa Kiislamu wenyewe. Waislamu wenyewe ndio wamekuwa wakijisababishia matatizo ya ndani, matatizo ambayo yanatokana na fikra finyu na za upande mmoja.

Fikra hizo finyu kwa hakika zimekuwa zikisababisha harakati na matokeo hatari kwa ulimwengu wa Kiislamu. Vizuizi vya nje vimekuwa vikitokana na ujanja, hila na njama za dhahiri na siri za madola makubwa ya kikoloni ambayo yanautazama umoja wa Waislamu kama hatari kubwa kwao na hivyo kutoustahimili kabisa. Kwa kuzusha mifarakano, ugomvi na fitina miongoni mwa Waislamu, madola hayo yamekuwa yakijaribu kila njia iwezekanayo kuzuia kupatikana umoja wa kutegemewa miongoni mwa Waislamu, umoja ambao unaweza kuwapelekea kuunda harakati moja yenye nguvu duniani.

Ni wazi kuwa mambo na vizuizi vinavyozuia kupatika umoja na nguvu katika ulimwengu wa Kiislamu ni hatari kubwa kwa Waislamu kwa sababu jambo hilo linazuia kabisa kupatikana njia za kielimu za kukabiliana na suala hilo. Pia ni wazi kuwa kughafilika na juhudi za kuleta umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu ni jambo linalopasa kuepukwa kwa kila njia. Pamoja na hayo tunapolinganisha madhara ya vizuizi vya ndani na nje katika kuzuia umoja wa Kiislamu tunaona kwamba vizuizi vya ndani ndivyo vilivyo na madhara makubwa zaidi kwa umoja huo.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kila jamii inayokabiliwa na tatizo hilo la hitilafu na migawanyiko ya ndani hukumbwa na hatari ya kuoza, kuporomoka, kusambaratika na hatimaye kutoweka kutokea ndani. Ni kutokana na ukweli huo ndipo madola ya kibeberu ya Magharibi yakawa yanatumia bejeti na gharama kubwa kwa ajili ya kuwapandikiza viongozi fasidi na kuwalea wanazuoni bandia na vibaraka katika nchi za Kiislamu, wanazuoni ambao badala ya kuhubiri umoja na mshikamano kati ya Waislamu, huhudumia mabwana zao wa Magharibi kwa kueneza chuki na fitina pamoja na kuwakufurisha Waislamu katika ulimwengu wa Kiislamu.

Suala hilo limepelekea nchi za Kiislamu kuwa katika hali ya ugomvi na vita vya mara kwa mara na visivyomalizika, ambavyo huchochewa na kuenezwa na maadui wa Uislamu. Ni wazi kuwa ili kukabiliana na hatari hiyo kubwa kwa ulimwengu wa Kiislamu na kufikiwa lengo tukufu la kuyakurubisha pamoja madhehebu ya Kiislamu pamoja na kuunda harakati yenye nguvu kubwa ya Kiislamu duniani, juhudi kubwa zinapasa kufanyika kielimu ili kuondoa vizuizi na vikwazo vya ndani vinavyozuia kupatika umoja kati ya Waislamu.

Kuhusiana na suala hilo, Shahid Murtadha Muttahari, mwanafikra na mwanafalsafa wa Kiislamu yuko katika mstari wa mbele wa wasomi wa Kiislamu waliofanya na ambao wangali wanafanya juhudi kubwa za kielimu na kiutafiti za kutafuta na kuwasilisha njia za kuondoa vikwazo vya ndani vinavyozuia kupatikana umoja wa Kiislamu. Ustadh Muttahari ametafiti na kuweka wazi vizuizi hivyo na kuwasihi Waislamu wote wafanye juhudi za kuepuka vikwazo hivyo kwa ajili ya kuleta umoja miongoni mwao.

Amewasilisha njia kadhaa za kielimu na kifikra ambazo Waislamu wanaweza kuzitumia katika kuimarisha umoja na mshikamano kati yao. Katika mtazamo wa Muttahari, sutafahumu ni moja ya vizuizi vinavyozuia kupatikana umoja miongoni mwa Waislamu na pia kati ya madhehebu ya Kiislamu. Ili kubainisha zaidi makusudio yake na kuweka wazi hatari kubwa ya kuwepo sutafahumu miongoni mwa Waislamu, Ustadh Muttahari anabainisha kwa ufupi maana ya maelewano na sutufahumu na kuandika: "Maelewano au dhana nzuri ni kuwepo masikilizano kati ya pande mbili na sutafahumu ni kuelewana vibaya pande hizo.

Ni wazi kuwa kusikilizana kuna maana ya watu kuelewana na kuishi pamoja kama walivyo, na sutafahumu ni kwa watu hao kutofahamiana kama walivyo, bali wanaishi katika hali ya kudhaniana vibaya. Sutafahumu ni jambo baya katika kila hali na kwa kila mtu. Hii ni kwa sababu jambo hilo huleta upotovu (Kumbukumbu za Ustadh Muttahari, Intisharaat Sadra j. 2 uk 203)."

Shahid Muttahari kisha anazumngumzia sutafahumu kati ya Waslamu na athari zake haribifu katika kuleta mivutano na migawanyiko ambayo huzuia kupatikana umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu. Anasema: "Tukiachilia mbali baadhi ya migawanyiko na tofauti za kiitikadi za Waislamu, tunaona kwamba moja ya misiba mikubwa inayowakumba Waislamu ni sutafahumu nyingi zilizopo miongoni mwao.

Yaani mbali na hitilafu hizo za kiitikadi, Waislamu wanakabiliwa na tatizo kubwa la sutafahumu zisizo na msingi na kudhaniana vibaya. Katika zama za kale na katika hali ya hivi sasa pia kuna watu ambao wamekuwa wakifanya juhudi za kuzidisha hitilafu na dhana mbaya miongoni mwa Waislamu. Hatari inayotokana na sutafahumu isiyo na msingi na kutoelewana vyema miongoni mwa Waislamu ni kubwa zaidi kuliko hatari inayotokana na hitilafu za kimadhehebu (marejeo hayohayo)."

Ustadh Muttahari anazingatia kwa kina masuala matatu muhimu kuhusiana na kadhia hiyo. - Sutafahumu na kutoelewana vyema kifikra Waislamu pamoja na tabia ya kutaka kutilia shaka na kukosoa, bila hoja, mitazamo na matamshi ya watu wengine ni tatizo kubwa lililoenea miongoni mwa Waislamu. Hili si jambo dogo kwa sababu hupelekea kupotea ovyo nguvu, juhudi na jitihada za Waislamu za kuleta umoja na mshikamano miongoni mwao. Tatizo hili huleta madhara na udhaifu mkubwa katika jamii na nchi za Kiislamu na kuwasababishia Waislamu machungu makubwa, machungu ambayo hupelekea watu kutengana, kuzidisha chuki na ugomvi kati ya Waislamu na kupoteza ovyo nguvu kazi, suhula na nishati yao katika mambo ya batili na yasiyo na faida yoyote kwa Waislamu.

- Kuna nyayo za watu fasidi na wafitini katika kila vita, mivutano na ugomvi unaotokea kati ya Waislamu. Watu hao waovu hufanya kila juhudi ili kuhakikisha kwamba moto wa fitina na migawanyiko unaenea kwa kasi kubwa katika kila pembe ya ulimwengu wa Kiislamu kwa madhara ya jamii za Kiislamu. Watu na makundi ya waovu hao hupenya na kuingia katika pande zinazozozana ili kuchochea zaidi mivutano ya pande mbili na hivyo kuweza kusababisha madhara makubwa zaidi kwa umma wa Kiislamu.

Vibaraka na majasusi wao pia huweza kuingia na kupenya katika pande zinazovutana na hivyo kuzidisha hitilafu na migongano kati ya pande hizo. Harakati hizo za fitina huchochea na kuzidisha chuki na uadui kati ya wafuasi wa madhehebu mbalimbali za Kiislamu na hivyo kufunga njia zote za umoja, mshikamano, maelewano na masikilizano kati ya Waislamu. Sutafahumu zilizopo kati ya wafuasi wa madhehebu za Kiislamu ni hatari zaidi kuliko hitilafu zao za kimadhehebu na kwa hivyo kila juhudi zinapasa kufanyika kwa lengo la kuziondoa.

Kama zinazofanyika juhudi za kuondoa tofauti za kimadhhebu na kuwakurubisha pamoja wafuasi wa madhehebu hizo, Waislamu pia wanapasa kufanya juhudi maradufu za kuondoa tofauti na sutafahumu zilizo na madhara makubwa kwa umma wa Kiislamu. Baada ya kusema kuwa madhara ya hitilafu zinazotokana na sutafahumu ni makubwa zaidi kuliko yale yanayotokana na hitilafu za kimadhehebu na kiitikadi, mwanafikra Murtadha Muttahari anatoa dalili ya jambo hilo kwa kusema: "Hakuna hitilafu zozote za kimadhehebu zinazoweza kuwafanya Waislamu wesiwe na umoja na udugu na hivyo kuwa dhihirisho halisi la aya ya Qur'ani inayosema; 'Kwa hakika Waislamu wote ni ndugu.' Hii ni kwa sababu Mwenyezi Mungu anayeabudiwa na watu wote anasema; 'La Ilaha Ila Allah,' yaani hakuna mungu aabudiwaye kwa haki isipokuwa Allah (Mwenyezi Mungu).

Wote wanauamini ujumbe wa Mtume Muhammad (saw) na Aali zake (as) na wanauchukulia utume na dini yake kuwa ya mwisho kwa wanadamu. Wote wanaamini kwamba Qur'ani ni kitabu cha Mwenyezi Mungu, hukisoma na kukichukulia kuwa katiba yao. Wote huswali wakiwa wameelekea kibla kimoja na kunadi adhana moja. Hufunga swaumu katika mwezi mmoja ambao ni mwezi wa Ramadhani.

Wote husherehekea idi za Fitr na Adh'ha, huhiji kwa namna moja katika Nyumba ya Mwenyezi Mungu na kuwapenda Watu wa Nyumba ya Mtume. Mambo haya yanatosha kuwaunganisha Waislamu na kuwafanya kuwa kitu kimoja katika udugu wa Kiislamu. Lakini kwa bahati mbaya na masikitiko makubwa, makundi na madhehebu tofauti ya Kiislamu yamekumbwa na tatizo sugu la sutafahumu na dhana mbaya. Mwenyezi Mungu atuepushe na watu wasio na kazi nyingine ya kufanya isipokuwa kuvuruga na kuharibu uhusiano wa Waislamu!"

Moja ya dalili zinazofanya hatari ya hitilafu za sutafahumu miongoni mwa Waislamu kuwa mbaya zaidi kuliko hatari ya hitilafu zao za kimadhehebu na kiitikadi ni kuwa, tofauti za kimadhehebu hazibadiliki na wakati bali ni zilezile katika zama zote, ilhali tofauti zinatokana na sutafahumu hubadilika sambamba na kubadilika wakati na zama. Kwa msingi huo, moto na madhara yanayotokana na hitilafu kama hizo pia ni makubwa zaidi.

Kwa msingi huo, watu wanaoeneza fitina na migawanyiko kati ya Waislamu pia wametambua vyema kwamba hitilafu za kimadhehebu na kiitikadi kama vile uimamu na ukhalifa, ambazo ni thabiti, haziwezi kuzuia kupatikana umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu na kwa hivyo, wameamua kuchochea hitilafu zinazozushwa na sutafahumu ambazo hubadilika mara kwa mara sambamba na kubadilika wakati.

Jambo hilo linawawezesha maadui wa Uislamu kubuni na kuzusha sutafahumu mpya zinazoambatana na zama tofauti. Kwa kuzingatia hatari hiyo, Waislamu wote wanapasa kufanya juhudi maradufu kwa lengo la kuondoa tofauti, sutafahumu na fikra finyu na potovu ambazo huzuia Waislamu kuwa na umoja na mshikamano.

Huku akisisitiza kwamba si tofauti na vizuizi vyote vinavyozuia kupatikana umoja na mshikamano wa Kiislamu, vinatokana na sutafahumu, Ustadh Muttahari anaamini kwamba dhana mbaya na zisizo sahihi ni miongoni mwa matatizo makubwa ambayo hutumiwa vibaya na maadui pamoja na vibaraka wao katika kuzusha hasara na maafa katika jamii za Kiislamu.

Kwa msingi huo anasisitiza kwamba mambo yanayozusha kutoelewana na sutafahumu kati ya Waislamu yanapaswa kutambuliwa na kuondolewa mara moja, na madhehebu ya Kiislamu kufanya juhudi za kufahamiana na kuelewana kama yalivyo. Waislamu wanawajibika kuwaelewa ndugu zao wa Kiislamu kama walivyo na kuondoa kabisa dhana mbaya kwenye fikra zao kuhusiana na upande wa pili. Ili kufikia lengo hilo tukufu, mwanafikra Shahid Ustadh Muttahari anawasilisha njia tatu muhimu kama ifuatavyo.

- Kuchunguza aina ya dhana zisizo na msingi na sutafahumu zinazoelekezwa kwa Mashia na hasa Wairani.
- Kuchunguzwa aina ya dhana zisizo na msingi na sutafahumu za Mashia kuhusu wasiokuwa Mashia.
- Kuchunguzwa njia za kivitendo za kupunguza na kuondoa kabisa sutafahumu.
Njia hizi ambazo zina pande mbili za 'kifikra na kielimu' na 'kivitendo' zinapaswa kufuatiliwa kwa juhudi kubwa zenye ikhlasi na zinazoambatana na fikra huru zilizo mbali na kila aina ya taasubi zisizo na misingi ya kisheria wala mantiki. Juhudi hizo zinapasa kutekelezwa kwa kutilia maanani maslahi ya ulimwengu wa Kiislamu na njama ambazo zinatekelezwa na madola makubwa ya kibeberu kwa ushirikiano wa vibaraka wao wa dhahiri na wa siri dhidi ya Waislamu. Maadui hao wanafanya kazi mchana na usiku kwa ajili ya kuvuruga kabisa umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu.

Njama za maadui hao wa Uislamu huongezeka kila siku na hivyo kuhatarisha Uislamu na usalama wa mataifa ya Kiislamu. Ni matarajio yetu kuwa juhudi hizo muhimu za kuunusuru Uislamu kupitia kuimarishwa umoja na udugu miongoni mwa Waislamu, juhudi ambazo zinafanywa na wanafikra, wasomi walio na ikhlasi pamoja na kila Muislamu anayehisi kuwa na jukumu kuhusiana na suala hilo, zitazaa matunda ya kuridhisha katika siku zijazo.

MWISHO