HUDUMA ZA HOLLYWOOD
  • Kichwa: HUDUMA ZA HOLLYWOOD
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 13:37:58 4-9-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

HUDUMA ZA HOLLYWOOD

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei leo amukutana na Mwendeshaji filamu na wasanii walioshiriki katika kutengeneza filamu ya Nabii Yusuf (as) akiwashukuru kwa kazi kubwa ya kisanii ya kutengeneza filamu hiyo. Ayatullah Khamenei amesema kuwa filamu hiyo kwa hakika ni mwanzo wa kazi za ubunifu wa kisanii kwa kutumia visa katika majmui ya sanaa za kimapinduzi.

Amesisitiza kuwa Wizara ya Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu, Shirika la Utangazaji la Iran (IRIB) na wasanii wanapaswa kuwekeza zaidi katika medani hiyo. Amesema utumiaji wa sanaa katika kueleza kisa katika filamu ya Nabii Yusuf (as) ni moja ya sifa makhsusi za filamu hiyo ya televisheni. Ameongeza kuwa kwa kawaida katika dunia ya sasa, sanaa ya filamu inatumia baadhi ya masuala kama ngono kwa ajili ya kuwavutia watazamaji, lakini katika filamu hii ya mfululizo ambayo imewavutia watu wengi hapa nchini na katika nchi nyingine, kinyume na aghlabu ya filamu na michezo mingine, maudhui kuu ya kisa chake ilikuwa ni kujiepusha na dhambi na utakasifu wa nafsi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa suala hilo lina umuhimu mkubwa na kuongeza kuwa moja ya sifa nyingine makhsusi za filamu hiyo ni kuonyesha taswira ya shakhsia iliyokusanya pande zote na Unabii halisi wa Mtume Yusuf (as). Amesema shakhsia hiyo ya kidini mbali na masuala ya kiroho na kutilia maanani dua na dhikri, ilikuwa na nafasi kubwa katika kuongoza masuala ya jamii, kutatua mambo mbalimbali, kupambana na dhulma na kusimama kidete mbele ya mashinikizo. Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa leo hii sekta ya utengenezaji filamu inaonekana kidhahiri kuwa ni sekta ya sanaa lakini hakika yake ni sekta inayojihusisha na masuala ya kisiasa. Amesema makampuni na taasisi nyingi za filamu za Hollywood ni kielelezo cha irada na maamuzi ya kisiasa yenye mpangilio na malengo maalumu ambayo yanayohudumia siasa za Marekani, na baadhi ya wakati yanakuwa mapana zaidi ya nchi.

Amesisitiza kuwa maendeleo ya vyombo vya mawasiliano na sanaa yameifanya sekta ya filamu na utengenezaji wake kuwa chombo chenye taathira kubwa kwa ajili ya kubainisha fikra na malengo ya kisiasa. Ameongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina ujumbe na fikra mpya kwa mwanadamu ambao unapaswa kuelezwa kwa kutumia mbinu za kisanii na zenye taathira kubwa. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa demokrasia ya kidini ni moja ya fikra mpya na zisizokuwa na kifani duniani. Amesisitiza kuwa demokrasia inayoambatana na hakika ya dini inatekelezwa nchini Iran na inaweza kuarifishwa kwa walimwengu kwa kutumia mbinu za kisanii.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa kusimama kidete mfumo wa Kiislamu hapa nchini ni moja ya mambo yasiyokuwa na kifani duniani na akaongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina ujumbe na fikra za kuvutia na zinazoungwa mkono na mataifa mbalimbali na kwamba ujumbe na fikra hizo zinaweza kufikishwa kwa wanadamu kupitia filamu fupi au ndefu za visa na kwa kutumia mbinu za kisanii.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza juu ya udharura wa kutumia medani hiyo kwa ajili ya kulingania fikra za mfumo wa Kiislamu na akaongeza kuwa hapana shaka kwamba, kazi kama hizo za kisanii zitakuwa kazi adhimu lakini kamwe hazitatunukiwa tuzo ya Oscar au tuzo ya sanaa na Nobel kwani leo hii imepigwa ngoma ya fedheha na ufuska katika taasisi za kimataifa zinazosimamia sanaa duniani.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa tuzo kama hizo hazina thamani yoyote na kwamba wasanii hawapaswi kufanya kazi zao za kisanii kwa ajili ya kupata zawadi kama hizo.

Akisisitiza kuwa wasanii wanapaswa kutengeneza kazi za sanaa kwa ajili ya haki na hakika, Ayatullah Khamenei amesema, kuna udharura wa kujifunza mbinu za kisanii na kufanya hima kwa shabaha ya kutengeneza sanaa zinazojali hakika na kweli. Amesema lengo hilo haliwezi kufikiwa bila ya kuwepo juhudi za wasanii wanaochunga mipaka ya dini na vijana wenye imani. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa moja ya nukta kuu za udhaifu wa filamu na michezo ya televisheni hapa nchini ni kutotumia visa vizuri na kuongeza kuwa mhimili wa kazi nzuri ya kisanii ni kutumia vyema kisa linachovutia. Ametoa wito wa kuzingatiwa zaidi suala hilo.

Ayatullah Ali Khamenei amemshukuru Bwana Farajullah Salahshur Mwendeshaji filamu ya Nabii Yusuf (as) na akasema ujira wa watu wote walioshiriki kutengeneza filamu hiyo uko kwa Mwenyezi Mungu. Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Iran (IRIB) Izzatullah Dharghami ambaye pia amehudhuria kikao hicho alitoa hotuba fupi akisema kuwa filamu ya Nabii Yusuf ni moja ya filamu za televisheni zilizokuwa na mafanikio makubwa za chombo hicho cha taifa. Amesema kuwa miongoni mwa sifa za kipekee za fimalu hiyo ni kujenga daraja kubwa la mawasiliano na matabaka yote ya wananchi, kuwa na idadi kubwa ya watazamaji iliyopita asilimia 85, kuridhisha asilimia 90 miongoni mwao, utafiti wa kina na mkubwa wa kisa chake, timu mahiri ya wasanii na kuvutia idadi kubwa ya watazamaji katika nchi mbalimbali duniani.

Kwa upande wake Mwendeshaji filamu ya Nabii Yusuf (as) Farajullah Salahshur ameashiria suala la kuvutiwa watu wengi na filamu hiyo ndani na nje ya nchi na kasema kuwa kisa cha kuvutia cha filamu hiyo, matukio yake ya kweli, ibra na mafunzo ya kisa chenyewe, utajiri wa mafundisho yake ya Kiislamu na masuala ya kiufundi na sanaa ya uchukuaji wa filamu ni miongoni mwa mambo yaliyopelekea kufanikiwa kwake. Bwana Salahshur ametoa wito kwa viongozi wa serikali na wasanii kutilia maanani zaidi hakika na kweli katika filamu na kazi za kisanii na kutumia visa vya Qur'ani tukufu katika sanaa hiyo.

MWISHO