CHANGAMOTO ZA UMOJA
  • Kichwa: CHANGAMOTO ZA UMOJA
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 0:43:10 2-9-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

CHANGAMOTO ZA UMOJA

Umoja ni mojawapo ya maamrisho matakatifu ya Mwenyezi Mungu yanayotuliza zaidi moyo na ambayo harufu yake nzuri bila shaka huhisika na kila mtu ambaye moyo wake umezama katika dini takatifu ya Uislamu. Maisha ya Waislamu na jamii za Kiislamu zinapasa kujengeka juu ya msingi wa mafundisho na maana ya kuvutia ya neno umoja.

Sauti tamu na ya kuvutia ya aya: 'Na shikamaneni kwa kamba (dini) ya Mwenyezi Mungu nyote, wala msiachane' (3:103), 'Na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake wala msizozane (msigombane), msije mkaharibikiwa na kupoteza nguvu' (8:46), 'Na kwa yakini huu umma wenu ni umma mmoja' (23:52) na aya nyinginezo ambazo huashiria moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja, umuhimu wa kuimarishwa umoja na kuepukwa mifarakano kama zile zinazoanza na ibara, 'Enyi mlioamini' na 'Enyi watu', zote hizi zinaonyesha kwamba Mwenyezi Mungu na mawalii wake wema wanataka kufikiwa kwa jambo hili muhimu kwa upande mmoja na kwa upande mwingine kuonyesha kwamba ndio ufunguo wa kufanikiwa Waislamu maishani mwao.

Ushauri na maamrisho ya Mtume Mtukufu (SAW) na maimamu watoharifu (AS) kuhusiana na umuhimu pamoja na udharura wa kuimarishwa umoja miongoni mwa Waislamu ni jambo ambalo linadhihiri wazi katika mafundisho ya Kiislamu. Kwa msingi huo, jaribio lolote la Muislamu kutaka kuudhuru umoja wa Waislamu kwa kisingizio choche kile ni suala lisilosameheka hata kidogo. Ni wazi kwamba tabia na vitendo vya mtu kama huyo huwa havitofautiana kabisa na vile vinavyotekelezwa na maadui ima kwa siri au kwa uwazi kwa shabaha ya kukabiliana moja kwa moja na mafundisho ya dini kwa visingizio mbalimbali.

Kwa hakika hatima ya watu hao wote ni moja. Kama tulivyoashiria mapema, viongozi watoharifu na watukufu wa dini wamesisitiza na kuwashauri wafuasi wao katika nyakati tofauti kuhusiana na umuhimu wa kulindwa na kuimarishwa umoja miongoni mwa Waislamu. Mtume Mtukufu (SAW) na viongozi wema waliokuja baada yake walikuwa watu wa kwanza kabisa kutoa wito na kusisitiza umoja katika jamii ya Waislamu.

Mtume Mtukufu amesema: Wao (Waislamu ni mkono mmoja dhidi ya wengine (maadui) (Aamali Swaduq uk, Wasail as-Shia j.29 uk75).

Imam Ali (AS) amenukuliwa akimuhutubu Abu Musa Ash'ari kwa kusema; 'kumbuka kwamba hakuna mtu aliye na shauku kubwa zaidi ya kuona umoja ukitawala miongoni mwa wafuasi wa Muhammad (SAW) kuniliko mimi. Natafuta malipo na sehemu tukufu ya kurejea kupitia umoja huo (Nahjul Balagha, barua nambarai 78).' Anasema katika sehemu nyingine: 'Hata kama Waarabu ni wachache leo lakini ni wengi kwa utukufu wa Uislamu na wanaheshimiwa kutokana na utukufu wa ujamaa (umoja) wao.'

Kuna mambo mengi sana yanayoweza kujadiliwa na kusemwa kuhusiana na Uislamu, lakini mjadala wetu katika makala hii ni kujaribu kuchunguza vizuizi na mambo yanayozuia kupatikana kwa umoja unaotamaniwa na Waislamu. Ni matario yetu kwamba baada ya kuyachunguza kwa kina mambo hayo, Waislamu wote ulimwenguni watachukua hatua za lazima kwa madhumuni ya kuondoa vikwazo hivyo ili kuwawezesha kuimarisha umoja na ushirikiano miongoni mwao. Ni matumaini yetu pia kwamba jambo hilo litawawezesha kuboresha uhusiano wao na kushirikiana bega kwa bega kama ndugu wapendwa katika kukabiliana na njama za maadui wao wa pamoja.

Vikwazo vya umoja Kutokana na kuwa umoja na ushirikiano limekuwa ni suala muhimu zaidi ambalo limekuwa likijadiliwa na kuzungumzwa katika kipindi chote cha historia ya Uislamu, na kuwa na athari pamoja na matokeo nyeti kwa Waislamu, daima maadui wamekuwa wakifanya jitihada za kuweka vizingiti na vikwazo katika njia na juhudi zinazolenga kuleta umoja huo miongoni mwa Waislamu. Vingi vya vikwazo hivyo hutoka nje ya mipaka ya nchi za Kiislamu.

Mikono miovu ya wageni inaweza kuonekana wazi katika kila mgogoro na ugomvi unaoendelea kati ya Waislamu. Kwa bahati mbaya kutokana na uadui mkubwa walionao dhidi ya Uislamu, njama za maadui hazijaishia tu katika juhudi kubwa za kiuhasama ambazo zimekuwa zikifanywa na maadui kwa lengo la kuwagombanisha na kuwatenganisha Waislamu.

Hali imekuwa mbaya kwa Waislamu kiasi kwamba, maadui hawahitajii tena kuwa katika nchi za Kiislamu ili kueneza fitina, mifarakano na chuki miongoni mwa Waislamu. Waislamu wenyewe hivi sasa ndio wanaochukua jukumu na nafasi ya kuwahudumia maadui wa Uislamu kwa kueneza fitina na uhasama miongoni mwao.

Kwa maneno mengine ni kuwa, madhara yanayoenezwa dhidi ya Uislamu katika ulimwengu wa Kiislamu hii leo yanatokana na Waislamu wenyewe ambao wengi wameghafilika na njama hatari za maadui dhidi yao. Hali inatatiza na kusikitisha mno tunapotambua ukweli kwamba, kuna magenge ya watu ambao daima wanatekeleza njama za kuwatenganisha na kuwafarakanisha Waislamu na kuzusha hofu na wasiwasi katika safu zao.

Kuna mambo kadhaa yanayozuia kupatikana kwa umoja na ushirikiano miongoni mwa Waislamu ambayo ni:
" Ushabiki na uigaji wa kijinga na usio na muelekeo ambao hudhihirisha kichwa chake kibovu katika ushabiki wa kidini na kibaguzi.
" Matovuti ya kigeni
" Waislamu kujiweka mbali na mafundisho aali na adhimu ya Uislamu, kudhihiri kwa ujahili, imani za ushirikina na kidhana zisizo na msingi wowote, bidaa na uigaji usiofaa.
" Wanazuoni walio na mifungamano ya kisiasa katika upande mmoja na wanasiasa pamoja na watawala kwa upande wa pili.
" Tofauti za kielimu ambazo hatimaye huruhusiwa kupenya na kuingia katika hadhara ya watu wa kawaida.
" Fikra za kindoto na mielekeo ya kibaguzi.
" Kutoelewana.
" Kutokuwa na habari Waislamu.
" Tuhuma zisizo na msingi, uzushi na kuharibiana majina.
" Uzayuni.
" Ukomunisti.
" Upenyaji na ueneaji wa utovu wa adamu na maadili miongoni mwa Waislamu.
" Migawanyiko ya kidini na ugomvi.
" Serikali vibaraka na zenye uchu wa madaraka.

Tunaashiria hapa baadhi ya mambo mengine yanayoleta vizuia katika njia ya Waislamu kutaka kuwa na umoja na ushirikiano kati yao.

Njama za kikoloni Mojawapo ya vikwazo ambavyo daima vimekuwa vikizuia kupatikana umoja miongoni mwa Waislamu ni udikteta na ukoloni. Tatizo hili limechangia kwa kiwango kikubwa katika kuwatenganisha Waislamu kwa njia mbalimbali. Uadui dhidi ya umoja wa Kiislamu umekuwepo tangu jadi na mizizi yake inaweza kufuatiliwa tokea mwanzoni mwa kudhihiri Uislamu huko katika mji mtakatifu wa Madina. Hii ni kwa sababu, baadhi ya watu waliuchukulia Uislamu ambao ulipatikana kutokana na irada ya Mwenyezi Mungu na juhudi kubwa na za muda mrefu za Mtukufu Mtume (SAW), kuwa hatari na tishio kubwa kwa maslahi yao haramu ya kimakundi.

Kwa maelezo hayo, jiwe la msingi la uadui dhidi ya umoja wa Kiislamu kwa lengo la kuuzuia usije ukatengeneza jamii nzuri ya kupigiwa mfano ulimwenguni, liliwekwa katika siku hizo za mwanzoni mwa Uislamu. Huo ndio wakati ambao juhudi kubwa za taratibu, lakini zisizo na kikomo, zilipoanza kufanywa na maadui kwa shabaha ya kudhoofisha, kutenga na kuwafarakanisha Waislamu. Walianza kufuatilia na kudhoofisha viungo vya kuimarisha umoja ambavyo vilianzishwa na kuimarishwa na Mtume (SAW) tokea siku ya mwanzo ya utume wake. Njama hizo za kiuadui hazikutekelzwa tu katika ardhi za Bara Arabu na Hijaz katika kipindi cha mwanzoni mwa Uislamu bali chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu ilienezwa kwa njia na mbinu mbalimbali sambamba na kuenea kwa Uislamu ulimwenguni.

Ni lazima tuseme kwa masikitiko makubwa kwamba, katika zama zetu hizi, chuki na uadui huu umechukua sura mpya kabisa ambapo unaendeshwa kwa mpangilio maalumu usiofahamika kirahisi na kwa kutumiwa zana na suhula ambazo ni za kisasa kabisa. Chuki na uadui huo umepewa msukumo mpya na zana mpya za kileo ambapo jambo hilo limetoa na lingali linatoa pigo kubwa kwa umoja wa jamii nzima ya Kiislamu katika pembe mbalimbali za dunia.

Kuna nukta muhimu hapa inayopaswa kuzingatiwa kuhusiana na suala hili. Nukta hiyo ni kwamba, lengo la mwisho la ukoloni wa zamani na wa hivi sasa ni kuutokomeza na kuufuta kabisa Uislamu halisi na usiopotoshwa katika sura ya dunia. Hiyo ni ikiwa utakuwa na uwezo wa kufanya hivyo.

Kama kuna jambo lolote wanaloliafiki maadui kuhusiana na Uislamu, basi bila shaka hali hiyo hutokana na kukata kwao tamaa na kutokuwa na njia nyingine ya kufuata katika kuharibu jina zuri la Uislamu au huwa ni katika moja ya mbinu zao za kufanya hila za kuwahadaa Waislamu na kisha kuwatumbukiza katika mtego bila ya wao kutambua.

Huenda wakaafikiana kiujanja na Waislamu ili wapate imani na uungaji mkono wao na kisha kutekeleza njama hatari dhidi yao. Kwa kuchunguza kwa makini maneno na harakati za maadui kuhusiana na suala hili, mtu yoyote anaweza kujua kirahisi kwamba lengo lao la mwisho ni kuusambaratisha na kuufuta kabisa Uislamu halisi ulioletwa na Mtume pamoja na viongozi wengine watukufu wa dini hii ya Mwenyezi Mungu.

Kwa uchunguzi huo anaweza kutambua kwamba kama maadui watapata fursa ndogo tu ya kuuharibu Uislamu, hawawezi kusita hata sekunde moja katika kutekeleza njama zao hatari na za chuki dhidi ya Uislamu.

Kwa kutilia maanani suala hili, bado Waislamu hawajachelewa sana kusoma malengo hasa ya maadui na kuchukua hatua za dharura na zinazofaa katika kuondoa uhasama na chuki isiyohalalishwa kwa kisngizio chochote kile miongoni mwao kwa maslahi ya ulimwengu mzima wa Kiislamu. Kwa kushikamana na misingi inayoimarisha umoja na utengemano na ambayo inakubalika na makundi yote ya Kiislamu, Waislamu wanapaswa kusimama imara kwenye misingi hiyo katika kukabiliana na adui mjanja na asiye na huruma. Kuna maneno ya kuvutia ambayo amenukuliwa akiyasema Sayyid Sharaf ad-Deen kuhusiana na suala hili katika moja ya mazungumzo yake na watu wa Misri.

Amenukuliwa akisema: 'siasa zamewatenganisha wawili hawa kwa hivyo zinapaswa pia kuwaunganisha.' Alikusudia kusema kuwa tokea mwanzoni ni siasa ndizo zilizowatenganisha Mashia na Masunni na kwa hivyo siasa hizo hizo ndizo zinazopaswa kutumika katika kuwaunganisha tena. Anaongeza kuwa, kutokana na ukweli kwamba tokea mwanzoni Waislamu wamegawanywa na siasa na mipango madhubuti ya wageni, na kwa ujumla na ukoloni, kwa hivyo wao pia wanapasa kuchukua jukumu la kupanga mipango madhubuti na makini na inayozingatia maslahi ya Kiislamu kwa lengo la kuimarisha umoja na mshikamano wao.

Kwa kutumia vyema suhula ulionazo, ukoloni umekuwa ukisonga mbele kwa kasi kubwa katika medani za uchumi, siasa na utamaduni. Tunaweza kufupisha harakati za kikoloni katika kujaribu kuleta mgawanyiko na chuki miongoni mwa Waislamu katika mambo yafuatayo:
1- Kubuni makundi yenye misimamo inayopindukia mipaka.
2- Kuunga mkono watu wa kutiliwa shaka na wasioaminika katika jamii za Kiislamu.
3- Kuwasilisha masuala yanayozusha chuki na mtengamano kati ya Waislamu.
4- Kufanya tofauti na ugomvi miongoni mwa Waislamu kuwa mkubwa zaidi kuliko ulivyo hasa.
5- Uandishi na usambazaji wa vitabu, majarida na magazeti yanayoleta mgawanyiko miongoni mwa Waislamu.
6- Kuanzisha matovuti kwa nia mbaya
7- Uvumi na uenezaji wa masuala yanayotiliwa shaka
8- Uundaji na uungaji mkono wa serikali zinazopinga dini.
9- Kuzuia Waislamu Wasijuane Baada ya kugundua kuwepo Uislamu wa aina mbili yaani Uislamu halisi na ule uliopotoshwa, maadui wamekuwa wakifanya kila wawezalo ili kusambaza na kueneza Uislamu uliopotoshwa. Wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa katika kueneza fikra mbovu kwamba Uislamu halisi ni ule ulio na mtazamo finyu kuhusiana na masuala mbalimbali na hivyo kuwanyima Waislamu haki yao ya kuujua na kunufaika na Uislamu halisi. Wanatambua vyema kwamba, Uislamu halisi una maana ya kuwa macho na muamko na kwamba kwa kuenea Uislamu wa sampuli hiyo katika nchi za Kiislamu, wakoloni hawatakuwa tena na nafasi ya kuzidhibiti nchi hizo.

Kwa hivyo, kwa kuunga mkono Uislamu uliopotoshwa, au kwa ibara ya Imam Khomeini (MA), 'Uislamu wa Kimarekani' maadui wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuendelea kulinda maslahi yao haramu katika nchi za Kiislamu kwa madhara ya ulimwengu mzima wa Kiislamu. Kwa kueneza fikra potofu ya kutenganisha dini na siasa, wameweza kuwaweka mbali Waislamu na kiti cha nguvu na madaraka ili kuwawezesha maadui kutekeleza kwa mafanikio njama zao dhidi ya Waislamu bila ya kukabiliwa na upinzani wowote wa maana. Adui amekuwa akitumia njia zifuatazo katika kufikia lengo lake hili ovu. 1- Uundaji wa makundi yenye misimamo inayopindukia mipaka.

Katika vipindi tofauti, ukoloni umekuwa ukibuni makundi tofauti yanayonasibiana na malengo yao na kuyasambaza katika nchi za Kiislamu ili kufanya uharibifu humo na kuwagonganisha vichwa Waislamu. Matokeo ya njama hizo ni kudhihiri katika nchi za Kiislamu makundi yanayojiita kuwa ni ya Kiislamu, lakini yenye mitazamo finyu kuhusiana na Uislamu, makundi ambayo yanapinga akili, filosofia, irfan na fatwa za kifikhi.

Kwa kutegemea maana ya dhahiri ya riwaya na hadithi za Kiislamu zilizopokelewa kutoka kwa viongozi wa kidini hadi kufikia karne ya tatu hijria, makundi hayo potofu yanapinga vikali kutafsiriwa na kubainishwa kwa maana halisi ya hadithi hizo yakisema kwamba hiyo ni bidaa na uzushi katika dini..

Kwa kupinga akili na mantiki, makundi hayo yenye misimamo finyu yamechukua mfumo na sura ya kijeshi na kama walivyokuwa Mabedui, wamebuni makundi ya wanamgambo ambao hutembea yakivunja athari za utamaduni wa Kiislamu na kuwaua ovyo na kinyama wapinzani wao. Jambo la kusikitisha ni kwamba, watu hao waovu hutekeleza jinai zote hizi kwa kisingizio cha kukabiliana na ushirikina pamoja na bidaa katika dini.

Uadui wao dhidi ya Ushia na Mashia unaweza kuchunguzwa katika mtazamo huo. Baadhi ya harakati katika nchi za Kiislamu tokea mwanzoni, zilibuniwa kwa ajili ya kuhudumia ukoloni wa Uinegerza ima kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja kwa madhara ya ulimwengu wa Kiislamu na madhehebu za Kiislamu na hasa madhehebu ya Kishia. Maakundi hayo ya upotofu ambayo hayajawahi kupinga ukoloni au nchi adui za Magharibi katika shughuli zao, yalibuniwa kwa lengo la daima kuchunga na kudhibiti kuenea kwa Uislamu halisi na wenye harakati ili kuzuia kabisa kupatikana umoja na ushirikiano miongoni mwa Waislamu. Hii ni kwa sababu, Uislamu wa aina hiyo unachukuliwa kuwa tishio kubwa kwa maslahi ya wageni wa kikoloni katika nchi za Kiislamu.

2 - Kuunga mkono watu wa kutiliwa shaka na wasioaminika
Tumekuwa tukishuhudia kuwepo kwa watu wa kutiliwa shaka na wasioaminika katika nchi za Kiislamu, watu ambao hawawezi kutegemewa kabisa kutokana na kutokuwa kwao makini kitabia na kimaadili. Kwa kuahidi kuwapa zawadi na malipo ya kuvutia, watu hao huwa ni chombo kizuri cha maadui kutekelezea njama zao katika ulimwengu wa Kiislamu. Hutumiwa vibaya a maadui kwa lengo la kueneza propaganda sumu na uandishi wa vitabu ambavyo kidhahiri huonekana kuwa ni vya mafunzo kumbe vina sumu kali dhidi ya Waislamu. Vitabu kama hivyo ambavyo husambazwa kwa wingi katika nchi za Kiislamu kwa hakika huwahudumia mabwana wao wa kikoloni ambao hufuatilia siasa za mifarakano na fitina katika ulimwengu wa Kiislamu.

3- Kuwazuia Waislamu wasijuane
Kwa kutumia zana na suhula nyingi za kisasa kabisa, ukoloni umekuwa ukifanya juhudi kubwa na zisizo na kikomo za kuwazuia Waislamu wasijuane vyema. Daima hufanya njama za kupotosha nia yao njema katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano wao. Kwa yakini ni jambo lisilowezekana kwa Waislamu kukurubiana na kuwa na umoja miongoni mwao bila ya kwanza kutambuana na kujuana vyema. Kwa mfano katika kongamano moja la kimataifa lililofanyika hivi karibuni huko Istambul Uturuki, mwanachama mmoja wa bodi ya elimu inayohusika na masuala ya kidini aliwasilisha makala moja kuhusiana na nguzo za dini ambapo alitoa tuhuma kumi zisizo na msingi dhidi ya Mashia, tuhuma ambazo kwa hakika Mashia wenyewe hawana habari nazo. Jambo hili linaonyesha wazi ni jinsi gani Waislamu hawafahamiani wala kujua imani za wenzano. Mtazamo wake kuhusiana na Ushia ulikuwa kama ifuatavyo:

1- Mashia wana mitazamo inayofurutu mipaka kuhusiana na sifa za Mwenyezi Mungu. Wao ima huwa ni maanthropormofia wanaomuhusisha Mweneyzi Mungu na sifa za kibinadamu au maagnostiki wasadikio kuwa hatuna habari za Mwenyezi Mungu wala hatuwezi kuzijua.

2- Uimamu kwa Mashia ni kama utume ambao huendelea kuwepo kwa kuwepo Uimamu. Wanaamini kwamba wahyi haukukatika kwa kifo cha Mtume bali uliendelea kupokelewa kupitia watoto wake.

3- Mashia Imamia huwalaani masahaba wa Mtume (SAW).

4- Mashia huamini kwamba kuna upungufu na nyongeza katika Qur'ani Takatifu na riwaya zinazozungunzia suala hilo zinapatikana katika marejeo yao ya asilia.

5- Wafuasi wa uimamu wanapatikana tu katika miskiti ambayo wamezikwa humo viongozi wao.
6- Hawazipi thamani yoyote riwaya ambazo zimepokelewa na masahaba mashuhuri wa Mtume katika hali ambayo huzithamini zile ambazo zimepokelewa na maadui wa Uislamu.

Hii ndiyo hali ya makala ambayo imewasilishwa na mtu anayedaiwa kuwa ni msomi wa chuo kikuu kuhusiana na masuala ya kidini! Amepotosha kabisa imani ya Mashia na kuwaelekezea tuhuma za uongo na zisizo na msingi wowote tena katika kongamano la kielimu la kimatiafa bila hata kwanza kufanya chembe ndogo tu ya uchunguzi kuhusiana na imani yao halisi (Abdul Karim Biazar Shirazi - Hambasteghiye Madhahebe Islami uk.49)

Kuhusiana na suala hili, Tassisi ya Ukurubishaji, wasomi mashuhuri na wanazuoni wa Kishia na Kisunni katika ulimwengu wa Kiislamu wameamua kuwafahamisha wafuasi wao kuhusiana na imani za wenzao na hasa katika kuondoa shaka na tuhuma zinazotolewa dhidi ya madhehbu zao. Hii ni kutokana na kuwa, moja ya malengo ya Taasisi ya Ukurubishaji ni kuarifisha na kubainisha sura halisi ya Uislamu pamoja na madhehebu mbalimbali za Kiislamu, ziwe ni za Kishia au Kisunni, kwa mtazamo wa viongozi wa madhehebu hizi wenyewe.

Kwa kufanya hivyo, kizuizi muhimu cha kielimu na kiutamaduni ambacho huimarisha ujahili na kuzuia kufikiwa kwa malengo ya kielimu na kimantiki kitakuwa kimeondolewa na hivyo kuandaa uwanja wa kukurubishwa pamoja madhehebu mbalimbali za Kiislamu. Wanazuoni wa Kishia wamekuwa wakifanya juhudu maradufu kwa lengo la kuondoa tuhuma zisizo na msingi ambazo zimekuwa zikielekezwa na maadui dhidi yao.

Hali hiyohiyo imekuwa ikionekana miongoni mwa wanazuoni wa Kisunni ambao wamekuwa wakifanya juhudi kubwa katika kuwakataza wafuasi wao wasifuate misimamo ya kishabiki na wakati huohuo kufungua kwa kiwango fulani mlango wa ijtihadi, elimu na uwazaji.

4- Kuwasilisha masuala yanayozusha chuki na mtengamano kati ya Waislamu
Hata kama suala hili halijachochewa na wakoloni lakini ni jambo lililo wazi kwamba wamekuwa wakipanga njama na kudhamini mambo yanayozusha ugomvi, chuki na fitina miongoni mwa Waislamu kupitia watu wasiotambua hali halisi ya mambo katika jamii za Kiislamu. Watu hao kwa kawaida ndio hutumiwa na maadui kwa madhara ya Waislamu. Kuna tofauti ambazo zimekuwepo katika jamii za Kiislamu tangu jadi lakini hazijawahi kuzusha mivutano na chuki kama tunavyoshuhudia hii leo katika ulimwengu wa Kiislamu. Kwa hakika tofauti hizo zilikuwepo hata kabla ya kudhihiri wakoloni katika ardhi za Waislamu.

Lakini tofauti hizo zinapotumiwa na maadui kwa lengo la kuzisha fitina na chuki miongoni mwa jamii za Kiislamu, hali hubadilika kabisa na kuwa njama inayolenga kuwadhuru Waislamu. Hali hiyo hubadilika na kuwa njama hatari dhidi ya Waislamu inayopaswa kuvunjwa na kusimamishawa kwa thamani na njia yoyote ile ya kisheria.

MWISHO