QUR-AN INASISITIZA KUVAA HIJABU
  • Kichwa: QUR-AN INASISITIZA KUVAA HIJABU
  • mwandishi: AL-UDII
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 20:18:52 1-10-1403

 BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

QUR-AN INASISITIZA KUVAA HIJABU.

Katika Qur'an kumetaja kwamba, Qur'an inahimiza sana sana kuvaa Hijabu, na katika Aya nyingi za Qur-an umetajwa mkazo wa jambo hili, nasi tutataja baadaye baadhi ya Aya nyingi zinazohusu suala hili na kuzifasiri kwa kifupi.

1. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema; "Ewe Nabii, waambie wake zako na binti zako na wake wa waaminio, wateremshe shungi zao. Kufanya hivyo kutapelekea wao kutambulikana ( kwamba ni wanawake waungwana) hawatakerwa ( na watu waovu), na Allah ni Mwingi wa kusamehe (tena) Mwenye huruma".5

Katika Aya hii tukufu, Mwenyezi Mungu anamuamuru Nabii wake Muhammad (s.a.w), awaamrishe wanawake wa ki-Islamu waki-wemo wakeze, binti zake na wake wa waaminio, wajisitiri kwa kuvaa Hijabu iliyokamilika. Katika zama za mwanzo wa kuja Uislamu wanawake walikuwa wakitoka majumbani mwao bila kujisitiri miili yao kikamilifu, kama vile walivyokuwa wakitoka wanawake wa zama za Jahiliya ( kabla kuja Uislamu). Hali ya kutokujisitiri kikamilifu kwa wanawake, haikuridhiwa na sheria ya ki-Islamu, ndipo Mwenyezi Mungu alipomuamuru Mtume wake Muhammad (s.a.w.w) awaambie wanawake waumini wajisitiri na wavae Hijabu, na awakataze kutoka majumbani mwao bila sitara iliyokamilika kisheria. Akasema Allah s.w.t kumwambia Mtume (s.a.w.w), "Ewe Nabii waambie wake zako na binti zako na wake wa waaminio wateremshe shungi zao." Tamko (Jalabib) ambalo limetumika kwenye Aya ya hamsini na tisa, maana yake kilugha ni ushungi ambao hufunika kichwa cha mwanamke na uso wake na kumkinga asionekane kwa watu kwani kwa mujibu wa Q. 33:59
sheria haifai kuonesha mbele yao baadhi ya sehemu za mwili wake. Bali ilivyo ndivyo, ni mwanamke asitiri sawa maungo yake kama sheria inavyomtaka kuyasitiri.

Ama maana inayopatikana katika kauli ya Mwenyezi Mungu ali-posema; "Kufanya hivyo kutapelekea wao kueleweka ( kwamba ni wanawake waungwana)" Kauli hii inalenga kufahamisha kuwa, Hijabu humfanya mwanamke atajwe kwa utajo wa wema, na katika jamii hupambika kwa sifa ya Uchamungu.

Ni mara chache Wachamungu kukumbwa na mikasa itokanayo na watu waovu, ndiyo maana Mwenyezi Mungu akaendelea kuse-ma katika Aya hiyo ya hamsini na tisa kuwa; "Hawatakerwa na watu waovu".

Hii inamaanisha kwamba, macho ya watu waovu, wajeuri na wenye khiyana, hayamfikii mwanamke ambaye amejisitiri kikamil-ifu tena kisheria, kwa kuwa vazi la Hijabu humlinda dhidi ya aina mbali mbali za uovu, hata kumfanyia maskhara (utani) huwa ni vigumu. Hijabu huwa inasitiri mwili wa mwanamke na kuufanya uzuri wake na mapambo yake kutoonekana, kwani (awapo ndani ya Hijabu) hakuna kinachoonekana katika mwili wake, na mwanamke huyo huwa amesalimika kutokana na shari za aina tofauti. Salama hii hupatikana kwa kuwa, muovu amuonapo na kumtambua kwamba mwanamke huyo ni Mchamungu, tena ni mwenye kujihifadhi barabara hushindwa kumtendea ubaya. Kwa hiyo katika Aya hii tukufu, tuna dalili iliyo wazi inayotujulisha kwamba, kuvaa Hijabu ni lazima, pia inatujulisha kwamba, Hijabu inamhifadhi mwanamke kutokana na ufisadi na aina nyinginezo za uchafu.

2. Mwenyezi Mungu anasema tena kwamba; "Na mnapowauliza (kitu wakeze Mtume), waulizeni nyuma ya pazia, kufanya hivyo kutatakasa nyoyo zenu na nyoyo zao".
Aya hii inawaamuru Waislamu wanapouliza au kuomba kitu kuto-ka kwa wake wa Mtume (s.a.w.w) waulize hali ya kuwa wako nyuma ya pazia. Hapa wametajwa wake wa Mtume, lakini matu-mizi ya amri hii ni kwa wanawake wote ambao sheria ya ki-Islamu hairuhusu kuonana nao bila ya kuwepo kizuizi kwa ujumla.

Maana inayojitokeza katika Aya hii, ni kupatikana wajibu wa kuwepo sitara, yaani Hijabu baina ya wanaume na wanawake. Siyo sawa wanaume na wanawake kukosa mipaka ya mawasil-iano, lazima papatikane muongozo utakaoeleza mipaka hiyo.

Ndani ya Aya hii ya hamsini na tatu, Mwenyezi Mungu aliposema; "Kufanya hivyo kutatakasa nyoyo zenu na nyoyo zao". Kilichokusudiwa ni kwamba, suala la Hijabu kwa maana yake halisi ni jambo jema kwa pande zote mbili yaani wanaume na wanawake. Hapana shaka kwamba mwanaume anapomuangalia mwanamke, jambo hilo huamsha hisia za kijinsia, na kumpa shetani nafasi ya kumsukumiza mwanaume huyo katika mambo ya haramu na ufisadi. Na kwa upande wa mwanamke, pindi anapokosa kuwa ndani ya mazingira ya Hijabu, tayari huwa anai-weka heshima yake na utu wake katika hatari ambapo wakati wowote ule anaweza kuvunjiwa heshima yake. Hivyo basi vazi la Hijabu ni utakaso kwa wanaume na wanawake, na ikiwa kizuizi cha wanawake na wanaume kuchanganyika kitaondolewa, hali hiyo inaweza kusababisha ufisadi na fitna ndani ya jamii, mambo ambayo Mwenyezi Mungu ameyakataza na kuyaharamisha. Hali hii ya uovu ndani ya jamii inajitokeza kwa wingi mno ndani ya maeneo yasiyozingatia kanuni hii ya Hijabu.6

° Ni mara nyingi mno tunasikia wanawake wakivunjiwa heshima zao ndani ya misongamano isiyozingatia tofauti zilizoko baina ya wanawake na wanaume, k.m. ndani ya vyombo vya usafiri, sokoni na maeneo mengine mengi. Kumbuka ndugu msomaji, hapa kwetu Tanzania kutokana na hali hii ya kuhuzunisha dhidi ya wanawake ilipata kutokea msamiati unaoitwa mfadhaiko. Yote haya hayakuja kwa bahati mbaya, bali ni kutokana na kupuuzwa kwa mafunzo ya Mwenyezi Mungu na kuyapa mgongo. Basi ni kwa nini tusiadhirike? Mtarjumi.
Wakati huo huo ni lazima tufahamu ya kwamba, Mwenyezi Mungu ameyakemea maovu na ufisadi kwa aina zake na vyanzo vyake vyote.

Baada ya maelezo haya yatupasa tujiulize, je ni kwa nini Mwenyezi wakati akilielezea suala la Hijabu tamko lake akalielekeza kwa wakeze Bwana Mtume ((s.a.w))? Jawabu lake ni kwamba, wakeze Mtume wanayo daraja maalum ndani ya jamii ya ki-Islamu, kadhalika wao ni Mama wa Waumini wote, na kwa ajili hiyo wanatarajiwa mno kuwa na ziada katika utekelezaji wa sheria za Mwenyezi Mungu Mtukufu, na miongoni mwa sheria muhimu ni hii kanuni ya Hijabu. Kutokana na ukweli huu, mwan-zoni tu mwa Aya hii Mwenyezi Mungu ameanza kwa kusema:

"Enyi Wake wa Mtume, ninyi si kama yeyote miongoni mwa wanawake".7 Maana ya maneno haya ni sawa na kumwambia mtu mwenye elimu, "Wewe Bwana ni mwanachuoni usiseme uongo". Sasa basi, maneno kama haya huwa hayamaanishi kuruhusu kusema uongo kwa asiyekuwa Mwanachuoni, bali maana yake ni kuwa sifa ya kuwa mkweli inamsatahikia mno mtu huyo na uongo kwake ni jambo baya sana. Bali ukweli ulivyo ni kuwa, jambo lolote ambalo huwa ni sababu ya mwanaadamu kuingia ndani ya makosa, huwa ni haramu kwa mujibu wa sheria ya ki-Islamu. Ni wazi kabisa kwamba, wanawake wengi walikuwa wakienda kwa wake wa Mtume (s.a.w.w) na kujifunza mambo mengi waliliyokuwa wakiyaona kwao.

3.Mwenyezi Mungu anatoa maelekezo zaidi anasema: " Na kaeni majumbani mwenu (enyi wanawake) wala msioneshe mapam-bo yenu kama walivyokuwa wakionesha (mapambo yao) wanawake wa zama za Jahiliyya (kabla kuja Uislamu).8

7.Qur'an 33:32 8Qur'an 33;33.
Ndani ya Aya hii mnapatikana amri ya Mwenyezi Mungu inay-omtaka mwanamke kutulizana nyumbani mwake, ili ashughulikie masuala ya ndani miongoni mwake ni kuhusu ndoa yake na familia, ikiwa ni pamoja na kuwalea wanawe kwa malezi ya kidini na tabia nzuri.
Hii ndiyo maana sahihi ya wanawake kutulizana majumbani mwao. Na iliposemwa katika Aya hii ya 33; "Na wala msioneshe mapambo yenu kama walivyokuwa wakionesha mapambo yao wanawake wa zama za kijahiliya." Maana yake ni kuwataka wanawake wa ki-Islamu wasitoke majumbani mwao kila inapobi-di kutoka, bila ya kujisitiri sawa sawa kama walivyokuwa na tabia hiyo wanawake wa zama zajahiliya. Si sawa mwanamke kuone-sha mapambo yake hadharani. Na inapotajwa mapambo, lazima ieleweke wazi kwamba mapambo ni kama vile hereni, bangili, mikufu n.k. Istoshe kwa vitu hivyo kuwa ni mapambo, bali mwanamke yeye mwenyewe bila kuongeza hereni au mkufu ni pambo. Kwa hiyo basi mwili wake asiuache wazi na kuufanya uonekane kwa kila mtu.
Kitu kingine muhimu kinachojitokeza katika Aya hii ni kwamba, Mwenyezi Mungu anamtaka mwanamke wa ki-Islamu apambike kwa sifa tofauti na wanawake wasio Waislamu katika mavazi na Uchaji Mungu. Hali hii ni kwa sababu wanawake wa ki-Yahudi, ki-Kristo na washirikina huwa hawajilazimishi kufuata hukmu hii ya sheria ambayo ndani yake mna hekima nyingi . Wao hutoka bila kujali kulinda heshima zao kama wanawake na mapambo yao huwa wazi mbele ya kila mtu.
Suala la kutojiheshimu kwa wanawake wa ki-Islamu, Mwenyezi Mungu hapendezwi nalo, ndiyo maana akawatakia utukufu na heshima kwa kuwachagulia vazi litakalowasitiri na kulinda hadhi yao. Kutokana na maelezo haya, linapatikana fundisho ambalolinamtaka kila mwanamke alizingatie kuhusu namna ya kuvaa. Na iwapo mwanamke wa ki-Islamu ataacha kuvaa Hijabu na akaamua kuuacha wazi mwili wake, basi atakuwa kajifananan-isha na wanawake wa kiyahudi kikristo na washirikina. Pia huonekana kama mtu anayekataa heshima na utukufu ambao Uislamu unamtaka awe nao. Si hivyo tu bali huwa anajisogeza taratibu hadi kwenye mwelekeo mbaya unaomchukiza Mwenyezi Mungu. Kuna hadithi isemayo kwamba; Mwenyezi Mungu alimpelekea Wahyi (ufunuo) Mtume fulani miongoni mwa Mitume wake akamwambia, "Waambie Waumini; wasivae mavazi ya maadui zangu, na wala wasile vyakula vinavyoliwa na maadui zangu, na wala wasipite katika njia wanazopita maadui zangu, (ikiwa watayafanya haya niliyoyakataza) basi nao watakuwa miongoni mwa maadui zangu kama walivyo hao ambao ni maadui zangu."

Aya hizi tatu zimekuja kuzungumzia maana ya Hijabu, na kuna Aya nyingine nyingi kuhusu suala hili ambazo hatujazitaja ili kufupisha maelezo.

MWISHO