KUANZIA NDOA HADI KUWA WAZAZI (SEHEMU YA SABA) A
MLANGO WA 6: MIMBA (A)
KUUMBWA KWA MTOTO KWA MUJIBU WA QUR’ANI TUKUFU
Katika aya kadhaa za Qur’an Tukufu, Mwenyezi Mungu ametaja uumbaji wa mtoto na hatua za mabadiliko mtoto. Ni kwa kuchunguza muujiza huu ambapo mtu anapenda bila kupinga, kumshukuru na kumtukuza Yeye, Mbora wa Waumbaji.
Katika Suratul-Mu’minun, aya ya 12 – 14, Yeye anasema:
وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنْسَانَ مِنْ سُلَالَةٍ مِنْ طِينٍ {12}
ثُمَّ جَعَلْنَاهُ نُطْفَةً فِي قَرَارٍ مَكِينٍ {13}
ثُمَّ خَلَقْنَا النُّطْفَةَ عَلَقَةً فَخَلَقْنَا الْعَلَقَةَ مُضْغَةً فَخَلَقْنَا الْمُضْغَةَ
عِظَامًا فَكَسَوْنَا الْعِظَامَ لَحْمًا ثُمَّ أَنْشَأْنَاهُ خَلْقًا آخَرَ ۚ فَتَبَارَكَ اللَّهُ أَحْسَنُ الْخَالِقِينَ {14}
“Bila shaka tulimuumba mwanadamu kutokana na asli ya udongo. Kisha tukamuumba kwa tone la manii, lililowekwa katika makao yaliyohifadhika. Kisha tuliumba tone hilo kuwa pande la damu, na kukalifanya pande la damu hilo kuwa nyama, kisha tukalifanya pande hilo kuwa mifupa, na mifupa tukaivika nyama, kisha tukamfanya kiumbe kingine. Basi ametukuka Mwenyezi Mungu, Mbora wa waumbaji.” (al-Mu’minun; 23: 12-14).
Katika aya hizo hapo juu, Mwenyezi Mungu Mtukufu anataja hatua 7 za uumbaji:
Hatua ya kwanza: Mwanadamu mwanzoni kabisa anaanza kama udongo; kwa maneno mengine, sehemu za udongo zisizo na uhai zinavyotunzwa kwenye mwili hai kwa njia ya chakula.
Hatua ya Pili: Chembehai inajizalisha yenyewe kwa njia ya manii; hivyo mwanadamu anatengenezwa katika mbegu (majimaji ya shahawa), na kuwekwa katika sehemu madhubuti ya kupumzika (tumbo la uzazi la mama).
Hatua ya Tatu: Mabadiliko ya kwanza katika ovari iliyorutubishwa ni ubadilishaji kwenye namna ya donge au mgando mzito wa damu, au bonge lililoning’inia.
Hatua ya Nne: Chembehai za zaigoti hukua kwa ugawanyikaji katika pingili; halafu donge hilo huanza taratibu kupata umbile katika kukua kwake kama kijusi (bonge la nyama).
Hatua ya Tano: Kutokea hapa inaanza mifupa.
Hatua ya Sita: Nyama sasa hukua juu ya mifupa, kama vinavyofanya viungo na mfumo wa neva.
Hatua ya Saba: Hadi hapo ukuaji wa mtoto wa binadamu ni kama ule wa mnyama. Hata hivyo, hatua muhimu sasa inachukuliwa na kile kijusi kinakuwa binadamu kamili. Huu ni ule upuliziaji wa roho ya Mwenyezi Mungu ndani yake. (huu unaweza kuwa sio muda maalum; bali unaweza kuwa sambamba na ule wa ukuaji wa kimwili).
Katika suala la uumbaji wa kijusi, inasimuliwa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): “Ile mbegu ndani ya tumbo la uzazi la mama inachukua siku arobaini kugeuka kuwa bonge, kisha baada ya siku arobaini linakuwa donge la nyama (kijusi); wakati mtoto anapofikia miezi minne, kwa amri ya Mwenyezi Mungu, Malaika wawili hukipa kile kijusi roho na kuainisha riziki, muda wa kuishi, matendo (Aamaal), ustawi na dhiki za mtoto huyo.1
Huenda ni kwa sababu hii kwamba imeshauriwa kwamba hususan baada ya siku ya arobaini ya kujamiiana, mtu anapaswa kuwa muangalifu zaidi wakati anapoandaa chakula. Chakula hicho lazima kiwe kisafi kiroho (kisiwe najisi) na kiwe halali kwani hili litakuwa na athari juu ya mtoto huyo.2
Imam as-Sadiq (a.s.) vilevile aliielezea hatua ya maendeleo ya uumbaji kama ifuatavyo: “Baada ya kukamilika viungo vya mwili vinavyohitajika, Mwenyezi Mungu anatuma Malaika wawili ambao wana kazi ya uundaji wa mtoto, na kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, wao huunda masikio na macho na viungo vyote vya ndani na vya nje vya mwili huo.”3
Katika Dua ya Imam Husein ya Aarafat, anarejelea kwenye mfuatano wa uumbwaji na anajaribu kuzihesabu zile neema zilizotolewa na Mwenyezi Mungu Mtukufu katika namna ifuatayo:
“Umeniasilisha mimi kwa Rehma Zako
kabla sijawa kitu cha kukumbukwa
Umeniumba kwa udongo,
Kisha ukanipatia nafasi katika migongo ya baba zangu
Salama kutokana wasiwasi wa maangamizi na
matukio ya ajabu ya zama na miaka.
Nilibaki kuwa napita kutoka mgongo hadi tumbo kwa muda
Nisioukumbuka wa siku zilizopita
Na karne zilizokwishapita.
Katika upole Wako, neema na wema kwangu mimi,
hukunipeleka kwenye himaya ya viongozi wa ukafiri,
wale ambao walivunja ahadi Yako na
wakatangaza uongo kwa mitume Wako.
Bali ulinipeleka kwenye ule mwongozo
ambao ulikwishaamuliwa mapema kwa ajili yangu,
namna ulivyoniwepesishia na ulivyonilea.
Na kabla ya hapo ulikuwa na huruma juu yangu
kupitia ufanya mitindo Wako wa hisani na neema tele.
Ulianzisha uumbwaji wangu kutoka kwenye tone la manii
Lililomwagika na ukanifanya nikae kwenye utusitusi mara tatu
miongoni mwa nyama, damu na ngozi.
Hukunipa mimi kushuhudia kuumbwa kwangu,
wala hukuniaminisha mimi na lolote kati ya mambo yangu.
Kisha ukanituma duniani kwa ajili ya mwongozo
ambao ulikwisha kuamuliwa kwa ajili yangu,
kikamilifu na usioharibika.”4
Imam Zainul-Abidiin (a.s.) katika du’a yake baada ya Sala ya usiku – Salatul-Lail ndani ya Sahifah Sajjadiah anakitaja hiki kipindi cha kushangaza cha kijusi na cha wakati wa kunyonya. Anamshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu na kuelezea mshangao wake juu ya jinsi Allah (s.w.t.). alivyoumba kiumbe kizuri kama hicho kutokana na mbegu chache.
“Ewe Mungu Wangu,
Umenifanya nishuke kama maji duni
kutoka kwenye viuno vyenye mifupa myembamba na njia finyu,
kwenda kwenye tumbo la uzazi linalosonga,
ambalo ulikuwa umelifunika kwa mastara;
Umenigeuza geuza kutoka hali hii hadi hali ile
mpaka ukanitengeneza kwenye umbo kamilifu
na ukaweka ndani yake viungo vya kimwili,
kama ulivyoeleza kwenye Kitabu Chako:
Kwanza tone,
kisha bonge,
kisha pande (la nyama),
kisha mifupa,
kisha ukaivisha mifupa kwa nyama,
kisha ukanitoa mimi kama kiumbe mwingine kama ulivyopenda.
Halafu pale nilipohitaji riziki Zako,
na nikawa siwezi kufanya lolote bila ya msaada wa neema Zako,
ulinichagulia kirutubisho kutoka kwenye neema ya chakula na vinywaji,
ambacho ulikiweka mikononi mwa mtumishi Wako,
ambaye kwenye tumbo lake ulinipa mimi mapumziko,
na kwenye makazi ambamo tumboni mwake Wewe ulinihifadhi mimi.
Kama ungeniaminisha mimi katika hatua zile, Ewe Mola Wangu,
kwenye bidii zangu au ungenisukuma kupata msaada
kwenye nguvu zangu mwenyewe
bidii ingeniondoka na nguvu zingechukuliwa mbali kabisa.
Hivyo umenilisha kupitia neema Zako
kwa chakula cha wale Wema na Wapole;
Umefanya hivyo kwa ajili yangu kwa fadhila kwangu
hadi kwenye hatua yangu hii ya sasa
Mimi siukosi wema Wako
wala fadhila Zako haziniweki mwenye kusubiri.
Bado pamoja na yote hayo,
imani yangu haijawa thabiti vyakutosha,
kwamba ningeweza kujikomboa mwenyewe
kwa kile ambacho kinapendelewa zaidi na Wewe.”5
Katika moja ya Hadith al-Qudsi, Mwenyezi Mungu Mtukufu anazungumza na wale wasio na shukurani na anasema: “Ewe mwanadamu! Hujanitendea Mimi haki! Niliufanya uzito wako kuwa mwepesi ndani ya tumbo la mama yako!
Baada ya hapo nilifanya njia ya kuzaliwa kwako kutoka kwenye sehemu finyu na ya giza kuwa laini (na inayovumilika). Pale ulipoweka mguu duniani nje ya tumbo hilo, niliona kwamba ulikuwa huna meno ya kulia chakula; niliweka matiti yaliyojaa maziwa katika kifua chenye joto cha mama (yako). Niliufanya moyo wa mama yako kuwa wenye huruma juu yako, na moyo wa baba yako wenye upendo, kiasi kwamba wanabeba uzito wa kukupa wewe chakula, na hawalali mpaka wahakikishe kwamba wewe umelala.
“Ewe mwana wa Adam! Fadhila zote hizi hazikuwa kwa sababu uliziom- ba kutoka Kwangu, wala kwamba Mimi nilikuhitaji wewe. Na pale hali ya uundwaji wako wa kimwili ilipokuwa tayari, na meno yako yakaota, nilik- ufanya ufurahie (na ufaidike) kutokana na aina tofauti za vyakula na matunda ya kiangazi na kipupwe.
Hata hivyo! Licha ya huruma zote hizi, baada ya kuwa hukunitambua Mimi (kama Muumba Wako na Mpaji Wako), ukaniasi Mimi.”6
Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w.) amesema kwamba: “Pepo ya mtu iko chini ya nyayo za
mama yake.”7
Mwenyezi Mungu Mtukufu anaeleza ndani ya Qur’ani Tukufu, katika Surat al-Faatir, aya ya 11 hivi:
وَمَا تَحْمِلُ مِنْ أُنْثَىٰ وَلَا تَضَعُ إِلَّا بِعِلْمِهِ ۚ {11}
“….. Na mwanamke yeyote hachukui mimba wala hazai ila kwa elimu Yake …..” (Surat Al-Faatir; 35:11).
Imesimuliwa pia kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): “Kama imea- muliwa kwamba Mwenyezi Mungu atafanya mtoto azaliwe, Yeye atamuumba katika umbile lolote lile alipendalo.”8
Hii inatuonyesha sisi kwamba uzazi wa mtoto ni neema ya moja kwa moja kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na ambako kunapaswa kutolewa shukurani endelevu juu yake. Kwa kweli kuwepo kwa mtoto kumefananishwa na tunda la mti, ambako kunamsogeza mwanamke na mwanaume karibu zaidi na kila mmoja wao.
Na kuhusu akina mama, Uislamu umewafanyia dunia nzuri ya kupendeza, ambamo kila mmoja lazima awaheshimu na kuwaenzi. Mwenyezi Mungu Mtukufu anayatambua na kuyataja matatizo yanayobebwa na akina mama: Katika Surat Luqmaan, aya ya 14, Yeye anasema:
حَمَلَتْهُ أُمُّهُ وَهْنًا عَلَىٰ وَهْنٍ {14}
“….. Mama yake amembeba kwa udhaifu juu ya udhaifu….. (Surat Luqmaan; 31:14).
Katika Surat al-Ahqaf, aya ya 15, Yeye anaelezea hivi:
حَمَلَتْهُ أُمُّهُ كُرْهًا وَوَضَعَتْهُ كُرْهًا ۖ {15}
“….. Mama yake amechukua mimba yake kwa taabu, na akamzaa kwa taabu …..
(Surat Al-Ahqaf; 46:15).
Kwa hakika hadhi ya akina mama ni hali ya juu zaidi hata kuliko ya baba kama inavyoonyeshwa na hadithi zinazofuata:
Mtu mmoja alikuja kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na akamwambia, “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, je nifanye wema kwa nani?” Mtume (s.a.w.w.) akasema, “Kwa mama yako.” Hivyo, yule mtu akasema, “Na baada ya hapo nifanye wema kwa nani?” Mtume (s.a.w.w.) akasema, “Mama yako.”
Halafu yule mtu akauliza tena, “Na halafu tena nifanye wema kwa nani?” Mtume (s.a.w.w.) akajibu. “Mama yako.” Halafu yule mtu akasema tena, “Baada ya hapo, nifanye wema kwa nani? Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akasema, “Kwa baba yako.” 9
Imesimuliwa vilevile kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) aliulizwa, “Ni yupi kati ya wazazi wawili ambaye ana cheo kikubwa?” Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akajibu, “Yule ambaye, kwa muda wa miezi tisa yeye amekuwe- ka katikati ya pande mbile (tumbo la uzazi), na kisha akakuleta duniani humu na akakupa maziwa kutoka kwenye matiti yake.” 10
Kuna ahadith nyingi kuhusu umuhimu wa akina mama wajawazito na wanaonyonyesha, baadhi yake ambazo zitasimuliwa hapa chini. Hata hivyo, inapasa kuzingatiwa akilini kwamba hizo zinakwenda bega kwa bega pamoja na majukumu ambayo yanapasa kubebwa kwa kadiri ya uwezo wake wote mtu.
Majukumu hayo kwa kawaida yanakuwepo wakati mtu anapokuwa na dhamira ya kufikia daraja za juu za Akhlaq na ukaribu kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na akapenda kufanya bidiii kuelekea kwenye lengo hili la kimaadili. (Haya yatajadiliwa kwa kina zaidi katika sehemu zinazofuata.).
a) Imesimuliwa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): “Malipo ya mwanamke, kuanzia wakati wa ujauzito hadi wakati wa kuzaa kwake na kunyonyesha, ni sawasawa na yale ya mtu aliyeko kwenye njia (jihadi) ya Allah, na iwapo mwanamke anafariki dunia katika muda huo kwa sababu ya matatizo na machungu ya uzazi, anakuwa na malipo ya shahidi.”11
b) Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.): “Wakati wowote mwanamke atakapoiacha dunia hii kwa sababu ya maumivu ya uzazi, katika Siku ya Kiyama Mwenyezi Mungu atamfufua kutoka kwenye kaburi lake akiwa msafi bila ya hesabu (ya dhambi); kwa sababu mwanamke kama huyo ameyatoa maisha yake kutokana na matatizo na uchungu wa uzazi.”12
c) Imesimuliwa vilevile kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.): “Kila wakati mwanamke anapokuwa na mimba, katika muda wote wa kipindi cha ujauzito anakuwa na cheo cha mtu anayefunga, mtu anayefanya ibada wakati wa usiku, na mtu anayepigana katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa uhai na mali yake. Na wakati anapojifungua, Mwenyezi Mungu humpa thawabu nyingi sana kiasi ambacho hakuna anayeweza kujua mpaka wake kwa sababu ya ukubwa wake.
Na pale anakumnyonyesha mwanawe, kwa kila mfyonzo mmoja wa mtoto huyo, Mwenyezi Mungu humpa malipo ya kumuachia mtumwa mmoja kutoka kwa wana wa Isma’il, na wakati kile kipindi cha kumnyonyesha mtoto kinapokamili- ka, mmoja wa Malaika wakuu wa Mwenyezi Mungu humgusa upande wake mmoja na kusema: “Anza matendo yako upya, kwani Mwenyezi Mungu amekwisha kukusamehe makosa yako madogo madogo yote.”13
d) Katika wakati wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), mtu mmoja alikuwa anafanya Tawaf (ya Ka’ba Tukufu), akiwa amembeba mama yake mabegani mwake. Wakati alipomuona Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), alimuuliza, “Kwa kufanya hivi, je, nitakuwa nimelipa haki za mama yangu?” Kwa hili Mtume (s.a.w.w.) alijibu, “Hapana, hujalipa hata angalau moja ya vile vilio vyake vya wakati ule wa kukuzaa wewe.” 14
e) Mtu mmoja alikuja kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na akauliza: “Ninaye mama yangu mzee, ambaye kwa sababu ya umri wake wa uzee hawezi hata kusogea. Ninambeba kwenye mabega yangu na kumuwekea vipande vya chakula mdomoni mwake na kumsafisha. Je, nimelipa haki zake?” Kwa swali hili Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alijibu, “Hapana, kwa sababu tumbo lake lilikuwa mahali pako wewe, na katika muda wote huo, aliyapenda maisha yako.” 15
f) Imesimuliwa kutoka kwa Imam Zainul-Abidiin (a.s.): “Haki ya mama yako ni kwamba ujue kwamba yeye alikubeba mahali ambapo hakuna mtu anayembeba yoyote. Amekupa kutokana na tunda la moyo wake ambalo hakuna mtu anayelitoa kwa yeyote, na amekulinda kwa viungo vyake vyote. Yeye hakujali kama angekuwa na njaa ilimradi wewe uwe umekula umeshiba, au kama alikuwa na kiu madhali wewe umekunywa, hakujali iwapo angetembea bila nguo ilimradi wewe umevaa, kama alikuwa juani madhali wewe ulikuwa kivulini. Aliusamehe usingizi wake kwa ajili yako. Alikulinda kwenye joto na baridi, vyote ili uweze kuwa ni wake yeye. Hutaweza kumuonyesha yeye shukurani, isipokuwa Mwenyezi Mungu akusaidie na upate mafanikio.” 16
Hadithi hiyo hapo juu inapaswa kuwapa wanawake wajawazito matumai- ni, ambao bila shaka yoyote watakabiliana na tatizo moja au jingine katika kipindi hiki.
Kwenye nyakati za shida, mtu lazima ajue kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu amewaandalia wanawake vyote, uwezo na tamaa ya kuzaa na kulea watoto, kwani kama vile Imam as-Sadiq (a.s.) anavyosimulia: “Allah (s.w.t.). amempa kila mwanamke subira ya wanaume kumi, na wakati wa ujauzito Mwenyezi Mungu humpa uwezo wa wanaume kumi wengine zaidi.17
REJEA:
1. Tafsiir Gaazar, Jz. 6, Uk. 235
2. Niyaazhaa wa Rawaabith Jinsii was Zanaashuii, Uk. 36
3. Biharul-Anwaar, Jz. 6, Uk. 334
4. http://alIslam.org/masoom/writings/duas/arafah.html
5. http://al-Islam.org/sahifa/dua32.html
6. Biharul-Anwaar, Jz. 60, Uk. 362
7. Mustadrakul-Wasaail, Jz. 15, uk.180
8. Niyaazha wa Rawabith Maadaraa wa Janiin, Uk. 10
9. Al-Kafi, Juz. 2, Uk. 159-160
10. Mustadrakul-Wasaail, Jz. 2, Uk. 628
11. Makarimul-Akhlaq, Uk. 238
12. Bihaarul-Anwaar; Juz. 101, Uk. 108
13. al-Kafi, Jz. 5, uk. 496
14. Tafsiir Fi Dhilaalil-Qur’ani, Jz. 5, Uk. 318
15. Mustadrakul-Wasaa’il, Jz. 2, Uk. 628
16. Treatise of Rights, Sahifatus-Sajjadiyyah
17. Mustadrakul-Wasaa’il, Jz. 10, Uk . 46
ITAENDELEA KATIKA MAKALA IJAYO