ADOPTION - MTAZAMO WA KISHERIA
  • Kichwa: ADOPTION - MTAZAMO WA KISHERIA
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 3:50:57 4-9-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

ADOPTION - MTAZAMO WA KISHERIA
Adoption ni neno la kiingereza lenye maana ya kilugha - kuchukua kitu/ mtu na kukifanya/kumfanya kuwa ni chako/wako. Maana ya kisheria kama ilivyofasiriwa kwenye kamusi la kiingereza la Webster ni: kumchukua na kumlea mtoto wa mtu mwengine( ambae ameshindwa majukumu ya ulezi) na kumfanya wako kwa kufuata utaratibu wa kisheria.

Utaratibu huu wa kuadopt ambapo mtoto huchukuliwa kutoka kwa wazazi wake kama wanajulikana au kwenye nyumba za mayatima, au kutoka mahospitali au hata kwa mawakala na kisha kwa kupitia utaratibu wa kisheria mtoto huyo hutambuliwa rasmi kama ni mtoto halali wa waliomfanya kuwa ni mtoto wao na kuwa na haki zote kutoka kwa "wazazi" wake.

Kuna sababu tofauti kisheria zinazofanya uchukuaji huu wa watoto ukubalike katika jamii zisizokuwa za kiislamu kama, kutojaaliwa kupata mtoto, kuwapatia watoto wasio na uwezo maisha wanayostahiki (kuna utaratibu kwa wasioweza kulea watoto wao kuwapeleka kwa mawakala ambao huwatafutia wazazi.), kuwa na hamu ya kupata mrithi (kwa waliojaaliwa watoto baadae wakafariki) na mengineyo.

Kwa upande mwengine tunao pia foster parents (walezi) ambao hushughulika zaidi na watoto ambao wana wazazi wao lakini wanapigwa au kubughudhiwa (abused) na hivyo kunyan'ganywa wazazi watoto hawa na kupelekwa kwa wazazi walezi wenye ujuzi na kuishi na watoto hawa kwa kuwalea baada ya mzazi kushindwa kutoa huduma hii kikamilifu kwa muda mpaka kupatikane kurekebishika kwa wazazi husika. Lengo la makala hii si kuzungumzia aina hii ya walezi bali ni ya mwanzo - adoption - mtoto wa kupanga.

Imetubidi tuandae makala hii muhimu kwa sababu jamii ya Kiswahili tayari imeshahamia katika nchi za kimagharibi na hivyo kuweza kujikuta kukumbwa katika mfumo huu kwa kuwepo sababu tofauti kama tulivyozieleza hapo juu. Au kutokea jambo linaloweza kutufanya tupatiwe au tuwakose watoto wetu katika mazingira yatakayoweza kuruhusika kwa mujibu wa sheria za nchi hizi lakini kutorohusika katika sheria ya kiislamu. Pia hili lilikuwa ni moja katika masuala yaliyoulizwa katika mojawapo ya mihadhara inayofanyika hapa Uingereza.

ENZI ZA UJAHILIA
MTOTO WA KUPANGA ENZI ZA UJAHILIYA
Uchukuaji watoto kwa njia hii ulikuwepo katika enzi za ujahiliya (kabla ya uislamu) na hata miaka ya mwanzo baada ya kuja uislamu. Waarabu walikuwa na tabia ya kuongeza idadi ya memba wa familia na ilikubalka katika jamii. Mtu humchukua mtoto na kumfanya wake na huitwa kwa kiarabu "tabanna" na hutangaza rasmi na kuchukua jina la "baba" yake mpya na kuwa na haki zote katika familia ile. Na mtoto alifahamika kama "mutabanna" Machifu wa kiarabu waliwagawa watu katika makundi, wale waliachiwa huru kutoka utumwani, wakimbizi walifukuzwa kutoka kwenye koo zao na makundi yaliyokuwa hayana nguvu (kama mayahudi n.k)

Walioachiwa huru kutoka utumwani mara nyingi huchukuliwa na mabwana zao na kuwa katika memba wa familia ile wakiwa na haki sawa na watoto wa kuzaliwa na mzazi yule. Pia wakimbizi huhifadhiwa na wadhamini wao na wao pia kuwachukua kama watoto wao. Kwa hivyo enzi za ujahiliya uhalali wa mtoto ulipatikana ima kwa njia ya kuzaliwa au kwa njia ya mtoto wa kupanga.Tofauti iliyopo wakati huo ni kwamba mtoto hakuweza kutumia jina la baba yake mlezi hadi baba mwenyewe akubali. Ila baba alikuwa na haki ya kumtambua na kumkana mtoto atakapo hasa kama mtoto yule ataenda kinyume na amri za baba yake mlezi au kabila lake. Hata hivyo mtoto huyu pia alikuwa na uwezo wa kumkana au kujitenga na baba mlezi huyu na kujiunga na koo/kabila nyengine ambapo hupokelewa hasa kama akiwa shujaa au ana uwezo wa aina fulani.

KUHARAMISHWA UTOTO WA KUPANGA (ADOPTION) MWANZONI MWA UISLAMU
Utamaduni huu ulikwisha ota mizizi katika jamii ya waarabu na hata ulipokuja uislamu ilikuwa ni vigumu kwa wale walioingia katika dini ya kiislamu kuachana nao kwa mara moja.

Ushahidi huu unapatikana kutoka kwa Mtume Muhammad(Salla Allahu 'ALayhi Wasallam) hata kabla ya kupewa utume aliwahi kumchukua mtoto alietekwa kutoka kwenye kabila lake, Zaid Ibn Haritha na akaletwa Makkah na kuuzwa kama mtumwa. Hakim bin Hazim alimnunua Zaid na kumzawadia shangazi lake bibi Khadija bint Khuwaylid. Bibi Khadija alipoolewa na Mtume Muhammad (Salla Allahu 'ALayhi Wasallam) chuo cha tatu akampa Mtume (Salla Allahu 'Alayhi Wasallam) Zaid kama mtumishi wake .

Baba yake Zaid alipopata taarifa hizi alihuzunishwa sana na kufanya jitihada za kumtafuta mwanawe mpaka akapata taarifa za kuwepo mwanawe Makkah.akiwa mtumwa kwenye nyumba moja iliyoheshimika enzi hizo. Akafanya safari na ndugu yake hadi Makkah ili kumkomboa mwanawe.Walipofika Makkah Mtume Muhammad (Salla Allahu 'Alayhi Wasallam) aliwapa chaguo kama Zaid atakubali kurudi kwa baba yake hatowalipisha kitu(gharama za kumkomboa mtumwa) na kama ataamua kubaki basi hatoachana na mtu ambaye anapenda kukaa nae

Wazazi wa Zaid wakapendezwa na uamuzi huu na pale alipoitwa Zaid na kuulizwa kama anawajua waliokuja pale na akajibu kwamba anawafahamu vyema. Hapo Mtume (Salla Allahu 'Alayhi Wasallam) akampa chaguo Zaid la ima kubaki au kurudi kwa wazazi wake. Zaid pale pale akajibu kwamba atabaki kwa Mtume(SAW) na kumwambia Baba na Ami yake kwamba: "nimeona mambo kwa mtu huyu ambayo yamenifanya nisiachane nae maishani kwangu" Baada ya kutamka Mtume (Salla Allahu 'Alayhi Wasallam) akamchukua Zaid hadi Al Kaabah na kuwahutubia waliokuwepo kwamba: "Shuhudieni kuanzia leo Nimemchukua Zaid kama mwanangu na atanirithi na nitamrithi."

Tokea siku hiyo Zaid akajulikana Makkah nzima kama Zaid ibn Muhammad. Baadae Mtume (Salla Allahu 'Alayhi Wasallam) alimuoza Zaid mtoto wa shangazi lake, Zainab bint Jahsh..Bi Zainab alikubali ndoa hii shingo upande kwa ajili ya kumridhisha Mtume(Salla Allahu 'Alayhi Wasallam) na hivyo iliingiwa na mitihani kwani kila mara Zaid alikuja kumshtakia Mtume (Salla Allahu 'Alayhi Wasallam) kuhusu mkewe na mara zote Mtume humrudisha na kumwambia: "kaa na mke wako na muogope Allah(SW)" Mpaka mwishowe ikabidi Zaid amuache mkewe. Hapa ikatoka amri kutoka kwa Allah (SW) kwa Mtume (Salla Allahu 'Alayhi Wasallam) amuoe Zainab na hivyo kuondoa kabisa ule utamaduni uliokuwa ukikataza mtu kuoa mtalaka wa "mwanawe wa kupanga" Al Ahzaab/37
وَإِذْ تَقُولُ لِلَّذِى أَنعَمَ اللَّهُ عَلَيْهِ وَأَنْعَمْتَ عَلَيْهِ أَمْسِكْ عَلَيْكَ زَوْجَكَ وَاتَّقِ اللَّهَ وَتُخْفِى فِى نِفْسِكَ مَا اللَّهُ مُبْدِيهِ وَتَخْشَى النَّاسَ وَاللَّهُ أَحَقُّ أَن تَخْشَـهُ فَلَمَّا قَضَى زَيْدٌ مِّنْهَا وَطَراً زَوَّجْنَـكَهَا لِكَىْ لاَ يَكُونَ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ حَرَجٌ فِى أَزْوَاجِ أَدْعِيَآئِهِمْ إِذَا قَضَوْاْ مِنْهُنَّ وَطَراً وَكَانَ أَمْرُ اللَّهِ مَفْعُولاً
Na ulipo mwambia yule Allah aliye mneemesha, nawe ukamneemesha: Shikamana na mkeo, na mche Allah. Na ukaficha nafsini mwako aliyo taka Allah kuyafichua, nawe ukawachelea watu, hali Allah ndiye mwenye haki zaidi kumchelea. Basi Zaid alipo kwisha haja naye tulikuoza wewe, ili isiwe taabu kwa Waumini kuwaoa wake wa watoto wao wa kupanga watapo kuwa wamekwisha timiza nao shuruti za t'alaka. Na amri ya Allah ni yenye kutekelezwa.

MTAZAMO WA KISHERIA
"ADOPTION" KATIKA MTAZAMO WA KISHERIA
Kuchukua mtoto wa kupanga ni haramu katika sheria ya kiislamu. Kwa sababu kinachopatikana hapa ni kuharamisha jambo lililokuwa ni halali na kuhalalisha jambo lililo haramu. Na kama muislamu atapata "mtoto" kwa njia hii basi sheria ya dini ya kiislamu haimpi haki zozote mzazi yule kuwa kama baba aliemzaa kwani kwa mujibu wa Quraan mtoto hawezi kuwa bin au binti kwa sababu ya tamko tu (declaration). Tamko hili liweze kuzifanya hisia za mzazi mlezi kuwa kama za baba halisi , mapenzi yaliyo moyoni ya mzazi mlezi yaweze kuwa sawa na ya mzazi halisi, Kufanana kwa tabia kwa mzazi mlezi kuweza kuwa sawa na mzazi halisi n.k Suuratul Ahzaab /4-5
وَمَا جَعَلَ أَدْعِيَآءَكُمْ أَبْنَآءَكُمْ ذَلِكُمْ قَوْلُكُم بِأَفْوَهِكُمْ وَاللَّهُ يَقُولُ الْحَقَّ وَهُوَ يَهْدِى السَّبِيلَ - ادْعُوهُمْ لاًّبَآئِهِمْ هُوَ أَقْسَطُ عِندَ اللَّهِ فَإِن لَّمْ تَعْلَمُواْ ءَابَاءَهُمْ فَإِخوَانُكُمْ فِى الدِّينِ وَمَوَلِيكُمْ وَلَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ فِيمَآ أَخْطَأْتُمْ بِهِ وَلَـكِن مَّاتَعَمَّدَتْ قُلُوبُكُمْ وَكَانَ اللَّهُ غَفُوراً رَّحِيماً

Wala hakuwafanya watoto wenu wa kupanga kuwa ni wana wenu khasa. Hayo ni maneno ya vinywa vyenu tu. Na Allah ndiye anaye sema kweli, naye ndiye anaye ongoa Njia

Waiteni kwa baba zao, maana huo ndio uadilifu zaidi mbele ya Allah. Na ikiwa hamuwajui baba zao, basi ni ndugu zenu katika Dini, na rafiki zenu. Wala si lawama juu yenu kwa mlivyo kosea. Lakini ipo lawama katika yale ziliyo fanya nyoyo zenu kwa makusudi. Na Allah ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu

Na kumfanya "baba" huyu awe na hisia juu ya mtoto huyu kama aliyemzaa au kuweza kuwa na tabia, khulka kama za baba yake mzazi ambazo hupatikana kwa kurithiwa kwenye "genes".. Mahusiano kati ya mlezi na mtoto kwa mujibu wa sheria ya kiislamu yako tofauti ukilinganisha na mahusiano ya jamii nyengine.kama ifuatavyo:

1 Kama mtoto atachukuliwa kulelewa basi hatakiwi kubadilisha jina la baba/babu yake.na kujipachika/kupachikwa jina la mlezi .
2 Mtoto anamrithi baba aliyemzaa na wala harithi kwa baba wa kupanga (kama anataka kumuachia chochote amuachie wakati wa uhai wake)
3 Mtoto akishakuwa mkubwa basi wale anaoishi nao katika nyumba wanakuwa si mahrum wake tena kwa hivyo atakuwa na haki ya kuoa/kuolewa na pia itabidi iwepo stara baina yao.
Kwa ufupi baba wa kupanga kwa mtazamo wa sheria ya kiislamu anakuwa ni mlezi tu wa mtoto na si baba halisi na kazi hii anayoifanya ni moja katika mambo yaliyohimizwa katika Jamii ya kiislamu. Na hapa ieleweke kwamba hata kama muislamu atakuwa amemchukua mtoto kwa njia ya Adoption atatakiwa azingatie athari zake kisheria na kidini na afahamu msimamo wa kiislamu kwa jambo hilo.

MTOTO WA KUPANGA
ATHARI ZA UTARATIBU HUU WA MTOTO WA KUPANGA KATIKA UISLAMU.
Kuna athari nyingi zinapatikana endapo muislamu atachukua /kuchukuliwa katika utaratibu huu nazo ni kama zifuatazo:
1 Kukosekana malezi sahihi kwa mtoto kwani atakapokuwa na wazazi wa kupanga hatokuwa na mapenzi halisi kama yale atakayoyapata kutoka kwa wazazi wake halisi.
2 Kuathirika kwa watoto kisaikolojia hasa watakapogundua kwamba wazazi wale ni wa kupanga na si halisi au wazazi wake halisi hawajulikani kabisa.
3 Kuweza kupotea kabisa kwa watoto hasa katika nchi za kimagharibi wakipatiwa wazazi wasiokuwa waislamu. Dini si kigezo kinachoangaliwa katika Adoption.
4 Kuweza kurithi/kurithishwa mali asiyostahiki.
5 Kukatika kabisa kwa ukoo na nasaba ya mtoto ambao moja kwa moja hupewa nasaba mpya ya wazazi wa kupanga na hivyo kupoteza asili yake.
6 Mtoto kujikuta katika hali ya mtafaruku ya kuwa na aina mbili za wazazi , wa kupanga na halisi na hivyo kujikuta ashindwe kugawa mapenzi kuwapa wale wanaostahiki/wasiostahiki.

KULEA MAYATIMA
KULEA WATOTO YATIMA NI JAMBO LILILOHIMIZWA KATIKA UISLAMU
Moja katika sifa za familia za kiislamu (jambo ambalo halipatikani katika familia za kimagharibi) ni kuwepo mfumo wa "extended family" Koo zilizotanuka.. Familia za jamii za kimagharibi hujengwa na baba,mama na watoto tu na mara chache kuingia babu na bibi na si zaidi ya hapo. Familia za kiislam zinakwenda mbali sana kujumuisha ami, mjomba ,shangazi, kaka,dada, binamu n.k.

Na mfumo huu wa kuunga ukoo katika uislamu bado una nguvu na athari kubwa sana katika jamii na ndiyo maana si rahisi kupata watoto wa kupanga katika jamii zetu. Kwani mtoto hawezi kabisa kukosa mtu wa kumlea hata kama wazazi wake wamefariki, au kutokea kwa jambo litakalomfanya mtoto asilelewe na wazazi wake.

Hakuna mfano bora hapa kama wa kipenzi chetu Muhammad (SAW) ambae tumeona katika maisha yake jinsi alivyopitia mikono tofauti katika malezi kama historia ya kiislamu inavyotubainishia. Alizaliwa yatima baba yake tayari alikuwa amefariki, akalelewa na mama yake na alipofariki alichukuliwa na babu yake naye alipofariki alilelewa na ami yake. Suuratu Dhuhaa/6-11

أَلَمْ يَجِدْكَ يَتِيماً فَآوَى - وَوَجَدَكَ ضَآلاًّ فَهَدَى - وَوَجَدَكَ عَآئِلاً فَأَغْنَى - فَأَمَّا الْيَتِيمَ فَلاَ تَقْهَرْوَأَمَّا السَّآئِلَ فَلاَ تَنْهَرْ - وَأَمَّا بِنِعْمَةِ رَبِّكَ فَحَدِّثْ
Kwani hakukukuta yatima akakupa makaazi? Na akakukuta umepotea akakuongoa? Akakukuta mhitaji akakutosheleza? Basi yatima usimwonee! Na anaye omba au kuuliza usimkaripie! Na neema za Mola wako Mlezi zisimlie.
Na Allah(SW) anasema katia Suuratul Baqarah/220

وَيَسْـَلُونَكَ عَنِ الْيَتَـمَى قُلْ إِصْلاَحٌ لَّهُمْ خَيْرٌ وَإِن تُخَالِطُوهُمْ فَإِخْوَنُكُمْ وَاللَّهُ يَعْلَمُ الْمُفْسِدَ مِنَ الْمُصْلِحِ وَلَوْ شَآءَ اللَّهُ لأَعْنَتَكُمْ

Na wanakuuliza juu ya mayatima. Sema: Kuwatengenezea ndio kheri. Na mkichanganyika nao basi ni ndugu zenu; na Allah anamjua mharibifu na mtengenezaji. Na Allah angelitaka angelikutieni katika udhia

Na Mtume Muhammad (Salla Allahu 'Alayhi Wasallam) anasema katika hadithi iliyopekelewa na Sahl ibn Saad kwamba:
أنا وكافل اليتيم في الجنة هكذا وقال بإصبعيه السبابة والوسطى
رواه البخاري

Mimi na mwenye kulea yatima tutakuwa peponi kama hivi, huku akionesha kidole chake cha kati na kati na cha shahada.
Imesimuliwa na Bukhari
Anasema Ibn Battwaal kama ilivyonukuliwa na Ibn Hajr katika kitabu chake cha Fat-hul Baariy katika kuisherehesha hadithi hii kwamba :
حق على من سمع هذا الحديث أن يعمل به ، ليكون رفيق النبي صلى الله عليه وسلم في الجنة
Ni haki ya kila atakaeisikia hadithi hii, kuifanyia kazi vilivyo ili kuwa pamoja na Mtume(SAW) peponi.
MTOTO WA KUPANGA NA MTOTO WA KULELEWA
TOFAUTI KATI YA KULEA MTOTO KIISLAMU NA MTOTO WA KUPANGA MTOTO WA KUPANGA MTOTO WA KULELEWA
Hulelewa na kunasibishwa na nasaba ya mlezi Hulelewa mtoto bila ya kunasibishwa na nasaba ya mlezi Hatoweza kumuoa/kuolewa na ndugu yake Wataweza kuoana na ndugu ya waliolelewa pamoja Huchukuliwa na kuwa mtoto halali wa mzazi na kupoteza nasaba na ukoo wa wazazi halisi. Huchukuliwa kwa ajili ya kulelewa tu na kubaki chini ya wazazi waliomzaa kiukoo na kinasaba.

Anamrithi baba wa kupanga kama watakavyorithi watoto wake wengine Hamrithi( hata hivyo anaweza kumuusia katika mali yake ) Lazima papatikane tamko na taratibu za kisheria kuweza kuchukua mtoto Hakuna haja ya tamko wala taratibu za kisheria Tamko likishatolewa la kuchukuliwa mtoto basi halibadiliki Mzazi halisi ana haki ya kumchukua mtoto wake apendapo Mzazi( kama yuhai) hupangiwa wakati maalum wa kuweza kumuona(ikiwa kama kutakuwa na maslahi kwa) mtoto wake Hakuna muda ataweza kumuona mtoto wake atakapo
TAATHIRA NDANI YA JAMII ZETU
VIPI JAMII YETU INAVYOATHIRIKA (TUNAOISHI NCHI ZA KIMAGHARIBI)
Moja katika mambo ambayo jamii yetu itakuja kuathirika nayo na sijui kama tumejiandaa ni:
1 Pakitokezea mmoja kati ya watoto wa Kiswahili kuchukuliwa kwa ajili ya kulelewa kama zikitokea moja katika hali tulizozielezea hapo juu.
2 Wazazi wa mmoja wetu kuondoka duniani na kubaki watoto ambao tunaweza kuwakosa kwa kupewa familia zisizokuwa za kiislamu na hivyo kupotea .
3 Kushindwa sisi tuliokuja katika nchi hizi kutumia nafasi ya kuwachukua watoto wa jamaa zetu(waliopo nyumbani) ambao tungeliweza kuwalea na kupata ujira mkubwa wa kumhudumia yatima na kupata kuwa karibu na Mtume (Salla Allahu 'Alayhi Wasallam) peponi
4 Kushindwa kuwachukua watoto yatima wa ndugu zetu wa kiislamu hapa hapa kwa sababu ya kuvunja ukoo wetu wa asili na kujipa unasaba mpya ambao hauoneshi kuwepo uhusiano wowote wa kindugu(ingawa hali halisi upo).

MAMBO YANAYOWEZA KUFANYIKA
Kwa kuwa tayari tunaishi katika nchi hizi na kizazi chetu kuendelea katika miaka ijayo kuna haja ya kutafakari kwa undani zaidi vipi tunaweza kwanza kukitunza kizazi chetu, kukienzi na kuhakikisha kinaendela katika hali ile aliyotuamrisha Allah(Subhaanahu Wata'ala) Al Imraan /102
وَلاَ تَمُوتُنَّ إِلاَّ وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ ...
wala msife ila nanyi ni Waislamu 1 Kujenga mfumo mzuri wa kifamilia na kuwepo koo zilizotanuka ( extended family) kama wanavyofanya ndugu zetu wenye asili ya kiasia ili kuweza kuepukana na kuchukuliwa watoto wetu.
2 Kuhakikisha kama wakitokea ndugu zetu wa kiislamu kupelekwa kwenye adoption kwa kutokea kwa moja ya sababu tulizozitaja ,kuhakikisha wanajiandikisha kwenye mawakala na kuwafuatilia hadi kuwapata hata kwa kutumia mkondo huu haramu . Kwa sababu madhara ya kuwaacha kupotea ni makubwa mno kuliko madhara ya kujiingiza katika mfumo huu wa adoption. Hii ni kwa dharura tu.
3 Kujenga communities zetu wenyewe ambayo zitaweza kuwa na jukumu la kuidhibiti hali hii kwa kutumia jumuia.
4 Kujiondoa katika mifumo ya maisha ambayo (hapa tunakusudia zaidi wale waliotumia ujanja wa kujitenga na familia zao) itaweza kutuingiza katika janga la kuwapoteza watoto wetu kwasababu zisizokubalika kidini na kisheria .
MWISHO