KUANZIA NDOA HADI KUWA WAZAZI (SEHEMU YA PILI) A
  • Kichwa: KUANZIA NDOA HADI KUWA WAZAZI (SEHEMU YA PILI) A
  • mwandishi: Ramadhani Kanju Shemahimbo
  • Chanzo: www.islam.org
  • Tarehe ya Kutolewa: 18:36:54 1-9-1403

KUANZIA NDOA HADI KUWA WAZAZI (SEHEMU YA PILI)
MLANGO WA 2: TARATIBU ZA KUJAMIIANA KATIKA UISLAM NO: 1
Kujamiiana na mahusiano ya kijinsia, pamoja na mwenza halali yanatawaliwa na maumbile asilia, na wakati huo huo ni sunnah ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na Ahlul-Bayt wake (a.s.). Yametajwa pia kwamba ndio jambo la kuburudisha zaidi maishani. Kikundi cha marafiki na Shi’a wa Imam as-Sadiq (a.s.) wanasimulia kwamba, Imam alituuliza sisi: “Ni nini kinachoburudisha zaidi?” Sisi tukasema: “Kuna vitu vingi vinavyoburudisha.” Imam akasema: “Kile kinachoburudisha zaidi hasa ni kufanya mapenzi na wake zenu.”1
Imesimuliwa vilevile kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.): “Ama katika dunia hii au katika akhera, mtu hajawahi, na wala hatawahi, kupata starehe yenye burudani zaidi kuliko mahusiano ya kijinsia na wanawake, na hakika haya ndio maelezo ya maneno ya Allah (s.w.t.). ndani ya Qur’an, katika Surat Aali Imran, aya ya 14 Yeye ambapo anasema: “Watu wamepambiwa kupenda matamanio pamoja na wanawake na watoto…..”
Halafu yeye akasema: “Hakika, watu wa Peponi hawapendelei sana katika starehe za Pepo zaidi kuliko Nikah;2 si chakula wala vinywaji ambavyo vina buru- dani kama hiyo kwao.”3
Na kuhusu hali nyingine zote za maisha yetu, Uislam unatoa kutupatia sisi taarifa zote muhimu kwa ajili ya maisha ya kijinsia ya mwanaume na mwanamke. Sababu ya hili ni rahisi; Uislam unatambua hulka ya kimaumbile ya mwanadamu, na umeamuru mahusiano ya kijinsia kwa ajili ya starehe na sio kwa ajili ya kuzaa tu. Matamanio ya ngono hayawezi, na hayapaswi kuzuiwa, bali hasa kurekebishwa kwa ajili ya hali njema ya mtu katika ulimwengu huu na akhera. Endapo kanuni na sheria hizi zitazingatiwa kwa makini na kutekelezwa kwa lengo la burudani na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na kujitenga mbali na maovu ya Shetani, kunahesabiwa kuwa miongoni mwa wema mkubwa kabisa.
UMUHIMU WA MAHUSIANO YA KIJINSIA
Kuna hadithi nyingi sana zinazobeba ule umuhimu wa uhusiano wa kijin- sia. Una kituo cha ibada na sadaka, na umeitwa kuwa ni Sunnah ya Mtume (s.a.w.w.).
Imam as-Sadiq (a.s.) anasimulia kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alizungumza na mmoja wa masahaba zake katika siku moja ya Ijumaa na akamuuliza: “Je, umefunga leo?” Yule sahaba akajibu. “Hapana.” Mtume (s.a.w.w.) akamuuliza tena: “Je, umetoa chochote leo kama sadaka?” Akajibu, “Hapana.” Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akamwambia: “Basi nenda kwa mke wako na hiyo ndio sadaka hasa kwake yeye.”4
Katika hadithi nyingine, Imam as-Sadiq (a.s.) anasimulia kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alimwambia mtu mmoja: “Wewe umefunga leo?” Akajibu akasema, “Hapana.”
Mtume (s.a.w.w.) akamuuliza: “Je, umekwenda kutembelea mgonjwa yoyote?” Akajibu, “Hapana.” Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akamuuliza: “Je, umekwenda kusindikiza jeneza?” Akajibu, “Hapana.” Mtume (s.a.w.w.) akamuuliza: “Je, umetoa chakula kwa mtu masikini?” Akatoa majibu ya kinyume tena. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akamwambia: “Nenda kwa mke wako, na kumwendea mke wako ni sadaka (Mwendee ili upate malipo kwa ajili ya matendo yote hayo).”5
Muhammad bin Khalad anasimulia kutoka kwa Imam ar-Ridhaa (a.s.): “Mambo matatu ni kutoka kwenye sunnah za manabii watukufu na mitume wa Allah (s.w.t.)., na haya ni kutumia manukato, kukata nywele na kijiingiza sana kwenye mahusiano ya ndoa na wake zao.”6
Kukaa mbali na mahusiano ya kindoa ya mtu na mke wake ni matokeo ya minong’ono ya Shetani, na kuna matokeo ya kinyume mengi sana kama vile mabishano na chuki baina ya mume na mke wake.
Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.): Mabibi watatu walikwen- da kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w) kulalamika. Mmoja wao akasema: “Mume wangu huwa hali nyama.” Yule mwingine akasema: “Mume wangu hanusi manukato na wala hatumii manukato.” Na yule wa tatu akasema: “Mume wangu mimi hasogei karibu na wanawake (yaani, hajishughulishi na kujamiiana).”
Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), akiwa hana furaha, katika namna ambayo kwamba joho lake lililobarikiwa lilivyokuwa likiburuzika ardhini, aliondoka na kwenda msikitini na akiwa juu ya mimbari, alimtukuza Mwenyezi Mungu na kisha akasema: “Ni nini kimetokea, kwamba kikundi cha wafuasi wangu hawali nyama, au hawatumii manukato, au hawawaendei wake zao? Ambapo mimi ninakula nyama, ninatumia manukato, na pia ninamwendea mke wangu. Hii ndio sunnah yangu, na mtu yoyote anayekwenda kinyume na sunnah hii huyo hatokani na mimi.”7
Imam as-Sadiq (a.s.) vilevile amesimulia: Mke wa Uthman bin Ma’dhun alikwenda kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, kila siku Uthman anafunga na wakati wa usiku anajishughulisha katika Swala.” Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akaokota makubazi yake na kwa hasira akaenda kwa Uthman (kiasi kwamba hakun- goja kuvaa makubazi yake) na akamkuta katika hali ya Swala.
Kwa vile Uthman alimuona Mtume (s.a.w.w.) aliiacha Swala yake. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akamhutubia akasema: “Allah hakunituma mimi kuwa sufii (anayejitenga peke yake), ninaapa Wallahi, kwamba hilo limenichochea mimi kwenye dini hii safi, yenye imani halisi na rahisi, mimi ninafunga, ninaswali na ninakwenda kwa mke wangu, na yeyote anayependa desturi yangu, ni lazima ashikamane na sunnah yangu na mwenendo wangu, na Nikah8 ni sunnah yangu.9
UMUHIMU WA KUMRIDHISHA MKE WAKO
Kumridhisha mke wake mtu ni jambo muhimu sana katika Uislam, kama lilivyoonyeshwa na hadithi ifuatayo hapo chini; kwa kweli, kukosa kuridhika kwa kipindi cha muda mrefu kunaweza kusababisha kukosa ashiki na chuki ya mke kwa mumewe.
Imesimuliwa kutoka kwa Imam Ali (a.s.): Wakati yeyote kati yenu anapotaka kulala na mke wake, basi asimharakishe kwani wanawake wanayo mahitaji pia.10 Ni muhimu kwa mume kutambua kwamba hamu ya kujamiiana ya mwanamke inachukua muda mrefu kujionyesha yenyewe, lakini mara inapokuwa imevutika, inakuwa na nguvu sana, ambapo kwa mwanaume ni rahisi, anapata ashiki haraka sana na vilevile anaweza kuridhishwa haraka sana.
Mwisho, inatia moyo kuona kwamba umuhimu uliowekwa na Uislam juu ya kuridhika kwa wote, mwanaume na mwanamke ni kiashirio cha wazi cha uadilifu na wema wa Mwenyezi Muntu (s.w.t.), kwa kweli, imerudia kukaririwa ndani ya Qur’ani kwamba mwanaume na mwanamke waliumbwa kutokana na nafsi moja,11 na huu ni mfano mmoja tu wa hili.
VITENDO VILIVYOPENDEKEZWA
Hakuna kanuni maalum kwa ajili ya kujamiiana; chochote ambacho kinawaridhisha wawili hao ni sawa, kadhalika, chochote ambacho hakiwaridhishi wawili hao ni lazima kiepukwe; kikwazo pekee kwenye kanuni hii ni kile ambacho Shari’ah inakikataza kwa uwazi kabisa. Hata hivyo, kuna vitendo kadhaa vilivyopendekezwa ambavyo, kama vikifuatwa, vitatarajiwa kuongozea kwenye hali ya kuridhisha zaidi.
KABLA YA KUJAMIIANA
1. Piga mswaki meno yako na tafuna kitu chenye harufu nzuri ili kuondoa harufu mbaya yoyote mdomoni. Kadhalika, jaribu kutokula vyakula vyenye harufu isiyopendeza kabla ya kukutana pia, kama vile kitunguu na kitunguu saumu.
2. Hakikisha unanukia vizuri – harufu safi zaidi ni ile ya mara tu baada ya kuoga au kujisafisha kwa haraka, na harufu mbaya zaidi ni ile ya jasho! Hususan wanawake wanahisia kali sana juu ya harufu.
Matumizi ya manukato, mafuta mazuri na vitu kama hivyo vinapendekezwa sana, ingawa ni muhimu sana kutambua kwamba kutumia vitu vya asili ni bora sana, ambavyo havina mchanganyiko na kemikali ambazo zinaweza kusababisha madhara mwilini.
Hasa, wanja (kuhl) umependekezwa sana juu ya wanawake. Imesimuliwa kutoka kwa Imam al-Baqir (a.s.): “Kupaka wanja kuyazunguka macho kunakipa kinywa harufu nzuri, na kunazifanya kope za macho kuwa na nguvu na kunaongeza nguvu na mvuto wa kujamiiana.12
Imesimuliwa pia kutoka kwa Imam as-Sadiq (s.a.): Kupaka wanja nyakati za jioni kuna manufaa kwenye macho na nyakati za mchana ni katika sunnah.13
Jalizo: Ingawa hadithi zinapendekeza matumizi ya wanja (kuhl), haziruhusu matumizi
yake katika maeneo ambayo yanaweza kuonekana kwa wanaume na yakaweza kuwa chanzo
cha mvuto na ushawishi.
UNYEGERESHANO (KUTIANA ASHIKI)
UMUHIMU WA UNYEGERESHANO
Kama ilivyosisitiziwa mapema, mume kumridhisha mke wake ni muhimu sana, na kujiingiza kwenye kujamiiana haraka na kwa pupa sio njia sahihi. Kuna wastani wa tofauti ya dakika nane kati ya muda ambao mume na mke wanafikia kileleni; mwanaume kwa kawaida anachukua dakika mbili kufikia kileleni na mwanamke anachukua dakika kumi kufikia kileleni. Kwa hiyo, ili kumridhisha kikamilifu mke wake, mwanaume lazima ampapase na kumchezea kimapenzi na kujishughulisha katika kunyegereshana (kutiana ashki) ili wote wafikie kileleni kwa pamoja kwa wakati mmoja.Uislam unatilia mkazo sana umuhimu wa unyegereshano, kama unavyoashiriwa katika hadithi zifuatazo hapa chini:
Imesimuliwa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): “Usijishughulishe katika kujamiiana na mkeo kama kuku; bali kwanza kabisa jishughulisha katika kutiana ashiki kwa unyegereshano pamoja na mke wako na kuchezeana naye halafu ufanye mapenzi naye.”14
Imesimuliwa pia kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): “Starehe na michezo yote haina maana isipokuwa kwa mitatu tu: Upanda farasi, kurusha mishale na unyegereshano na mke wako, na hii mitatu ni sahihi.”15
Imesimuliwa kutoka kwa Imam Ali (a.s.): “Yeyote anayetaka kuwa karibu na mke wake lazima asiwe na papara, kwa sababu wanawake kabla ya kuji- ingiza kwenye tendo la kufanya mapenzi lazima wajiingize kwenye unyegereshano ili kwamba wawe tayari kwa ajili ya kufanyiwa mapenzi.16
Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.): “Malaika wa Mwenyezi Mungu na wale ambao ni mashahidi juu ya matendo yote ya wanadamu wanawaangalia katika kila hali isipokuwa wakati wa mashindano ya kupanda farasi na ule wakati ambapo mwanaume anajiingiza katika kujishughulisha na unyegereshano na mke wake kabla hawajajihusisha katika kujamiiana.” 17
TARATIBU ZA KUNYEGERESHANA
Kuna vikwazo vichache sana kwenye taratibu zinazotumika katika unyegereshano; kupigana mabusu, kukumbatiana na kadhalika yote haya yanaruhusiwa. Hapa chini ni baadhi ya mbinu zinazofaa kwenye taratibu maalum:
A) UPAPASAJI KWENYE MATITI
Imesimuliwa kutoka kwa Imam ar-Ridhaa (a.s): “Usijiingize kwenye kujamiiana isipokuwa kwanza ujishughulishe katika unyegereshano, na ucheze naye mkeo sana na kumpapasa matiti yake, na kama ukifanya hivi atazidiwa na ashiki (na kusisimka kwa upeo kamilifu) na maji yake yat jikusanya. Hii ni ili ule utoaji wa majimaji uchomoze kutoka kwenye mati- ti na hisia zinakuwa dhahiri usoni mwake na kwenye macho yake na kwamba anakuhitaji kwa namna ileile kama wewe unavyomhitaji yeye.” 18
B) MAPENZI YA MDOMO (MAONGEZI)
Imam al-Kadhim (a.s.) aliulizwa: “Kuna tatizo kama mtu atabusu sehemu za siri za mke wake?” Imam alijibu akasema: “Hakuna tatizo.”19
DOKEZO: Ingawa kupiga punyeto (kujisisimua mwenyewe uchi wako mpaka ukatoa manii) kunakatazwa, katika suala la watu waliooana hakuna tatizo kama mke anasisimua tupu ya mume wake mpaka kutokwa na manii, au mume anasisimua tupu ya mke wake hadi anafikia kilele cha raha ya kujamiiana. Hili linaruhusiwa kwa sababu haliingii kwenye (kujisisimua mwenyewe;) ni kujisisimua kwa njia ya mwenza halali
C) MENGINEYO
Iliulizwa kwa Imam as-Sadiq (a.s.) “Endapo mtu atamvua nguo mke wake (na kumuacha uchi) na halafu akawa anamwangalia, je kuna tatizo lolote katika hilo?” Yeye akajibu akasema: “Hapo hakuna tatizo, hivi kuna stare- he bora kuliko hiyo ambayo inaweza kupatikana?” Likaulizwa swali jingine tena: “Kuna tatizo lolote iwapo mume atachezea sehemu za siri za mke wake?”
Imam akajibu: “Hakuna tatizo, kwa sharti kwamba hatumii kitu chochote mbali na viungo vya mwili wake (asitumie kitu cha nje cha ziada).”
Halafu tena Imam akaulizwa: “Kuna tatizo lolote kufanya ngono ndani ya maji?”
Imam akajibu: “Hakuna tatizo.” 20
Dokezo: Hadithi hiyo hapo juu inasisitizia makatazo ya kutumia vitu vya nje.
BAADA YA KUJAMIIANA:
1. Ni mustahabu kwamba josho la janaba ‘Ghusl al-Janaabat’ linafanywa mara tu baada ya tendo la ndoa, na linapochukuliwa mapema zaidi ndio bora. Vilevile, kama mtu angependa kufanya ngono zaidi ya mara moja katika usiku mmoja, ni bora kwamba kila mara waoge josho la janaba. Hata hivyo, kama hilo litakuwa haliwezekani kutendeka, inapendekezwa kwamba mtu atawadhe kabla ya kila tendo.21
2. Mara tu baada ya kumaliza tendo la ngono, mume hana budi kuoga josho na wakati huohuo ale sehemu ya nta ya nyuki (inayosifika kwa kuponya aina zote za majeraha, hususan mipasuko na mivunjiko) iliyochanganywa na asali na maji au iliyochanganywa na asali safi, halisi, kwani hii itafidia yale majimaji yaliyopotea.22
3. Kama nguvu za kiume za mtu zikiisha haraka baada tu ya kujamiiana, hana budi kujipasha mwili moto na kisha kulala.23
4. Mume na mke hawana budi kutumia mataulo tofauti katika kujisafisha wenyewe. Imesimuliwa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kwamba kama litatumika taulo moja tu, hii itasababisha uadui na utengano baina ya wawili hao.24
REJEA:
•    1. Wasa’ilush-Shi’a, Juz. 20, Uk. 23, namba 24927
•    2. Nikah kwa maneno halisi ina maana ya kujamiiana
•    3. Wasa’ilush-Shi’a; Juz. 20, Uk. 23, namba 24929
•    4. Wasa’ilush-Shi’a; Juz. 20, Uk. 109, namba 25163
•    5. Wasa’ilush-Shi’a; Juz. 20, Uk. 109, namba 25163.
•    6. Wasa’ilush-Shi’a; Juz. 20, Uk. 241, namba 25537
•    7. Wasa’ilush-Shi’a; Juz. 20, Uk. 107, namba 25158
•    8. Nikah ina maana ya kuingiliana (na mkeo).
•    9. Wasa’ilush-Shi’a; Juz. 20, Uk. 106, namba 25157
•    10. Wasa’ilush-Shi’a; Juz. 20, Uk 118, namba 25184
•    11. Suratun-Nisaa; 4:1, Surat al-Zumar; 39:5, Surat Luqman; 31:28, Suratun-Nahl; 16:72
•    12. Halliyatul-Muttaqin, Uk. 91
•    13. Niyaazha wa Rawabith Jinsi wa Zanashui, Uk 38
•    14. Halliyatul-Muttaqiin, Uk. 110
•    15. Wasa’ilush-Shi’a, Juz. 20, Uk.118, namba 25186
•    16. Halliyatul-Muttaqiin, Uk. 115
•    17. Ibid., Juz. 20, uk. 188, namba 25185
•    18. Mustadrak al-Wasaa’il, Juz. 2. Uk.545
•    19. Niyazha wa Rawabith Jinsii wa Zanashuii, Uk. 55
•    20. Halliyatul-Muttaqiin, Uk. 111
•    21. Niyazha wa Rawabith Jinsii was Zanaashuii, Uk. 52
•    22. Tib wa Behdaasht, Uk. 200
•    23. Niyazha wa Rawabith Jinsii was Zanaashuii, Uk. 24
•    24. Halliyatul-Muttaqiin Uk. 112.
ITAENDELEA KATIKA MAKALA IJAYOI