JICHO LA MATUMAINI
  • Kichwa: JICHO LA MATUMAINI
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 19:11:39 1-10-1403


BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

JICHO LA MATUMAINI

Kwanza kabisa kuna masuala mawili yanayopaswa kuzingatia kwa kina na kupewa haki yanayostahiki bila ya moja kufanywa muhanga wa jingine. La kwanza ni umuhimu wa kulindwa umoja na mfungamano wa Umma wa Kiislamu na jingine ni kulindwa kiini cha Uislamu wenyewe. Umoja na mfungamano wa Waislamu haupaswi kupewa umuhimu na kuzingatiwa zaidi kwa madhara ya ukweli unaotawala ndani ya Uislamu wenyewe na kuchukuliwa tu kuwa suala lenye umuhimu mdogo.

Kwa msingi huo, kusema ukweli na hakika ndilo linalopaswa kuwa jambo la msingi. Pamoja na hayo, mambo ambayo yamekuwa yakichochea uadui na chuki miongoni mwa Waislamu yanaweza kujumulishwa kama ifuatavyo:
1- Kujitenga na kupuuza mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu, Qur'ani Tukufu na ushauri wa wataalamu wa vitu viwili hivi. 2- Kuwategemea watu ambao wameharibu na kuchafua sura ya mafundisho ya Qur'ani tukufu na sunna za viongozi watoharifu wa dini. 3- Imani zisizo za kimantiki wala msingi. 4- Ukabila na ubaguzi wa rangi. 5- Tamaa ya masuala ya kidunia na kuvutiwa na mambo kama vile uchu wa madaraka, umashuhuri na mali. 6- Sera na siasa za mifarakano za madola makubwa kwa lengo la kubana na kuwadhibiti Waislamu, kupora mali na akili zao.

Ni muhimu kuashiria hapa kwamba, mambo mengi yaliyotajwa hapo juu yanaweza kusuluhishwa na kutatuliwa katika kivuli cha Tauhidi na Utume. Lakini kabla ya jambo lolote lile, tunapaswa kwanza kujua maana halisi ya neno umoja. Umoja una maana ya kuwa, huku tukiwa tumelinda imani zetu zisizo na makosa, tunapasa kuwa na msimamo wa pamoja na kusimama imara katika kukabiliana na maadui wetu wa pamoja na hatupasi hata kidogo kupuuza na kughafilika na njama za maadui hao. Hii haina maana kuwa tunapa kukwepa na kujiepusha kushiriki katika mazungumzo na mijadala mizuri ya kielimu inayojiepusha na ushabiki usio na misingi kwa lengo la kufikia ukweli wa mwisho. Kwa ibara nyingine ni kuwa, Umoja ni kutayarishwa kwa mazingira ambayo yanawezesha kupatikana muungano na usawa wa maslahi miongoni mwa watu wanaomwani Mwenyezi Mungu mmoja, Mtume Muhammad (SAW) na kitabu kiitwacho Qur'ani. Lengo la mwisho ni kuleta wongofu miongoni mwa wanadamu na kuwafanya wawe karibu na Muumba wao Allah. Imam Khomeini (MA) anasema hivi kwa maneno ya kuvutia: 'Umoja wa kalima unaweza kupatikana chini ya bendera ya Tauhidi.'

Huku akizungumzia kwa msimamo thabiti na wa kimantiki suala la umoja wa Kiislamu, Muhammad Ashur, Naibu-Kansela wa Chuo Kikuu cha al-Azhar nchini Misri ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mazungumzo baina ya Madhehebu za Kiislamu, anasema 'fikra ya kuyakurubisha pamoja madhehebu mbalimbali ya Kiislamu haina maana kwamba madhehebu hayo yote yanapaswa kufanywa kuwa dhehebu moja, wala haina maana kwamba wafuasi wa madhehebu mbalimbali wanapaswa kuyaacha madhehebu haya na kujiunga na madhehebu mapya. Kwa hakika huku ni kupotosha maana ya ukurubishaji. Ukurubishaji unapaswa kuenezwa na kuimarishwa kwa misingi ya majadiliano ya kielimu ili kuiwezesha silaha hiyo muhimu kushinda imani potofu zisizokuwa na msingi wowote wa kidini wala kielimu. Katika mazungumzo na majadiliano ya kielimu, wasomi wa kila madhehebu wanapaswa kubadilishana uzoefu na ulimu yao na wenzao ili kuwawezesha kujifunza, kujua, kusema na kupata matokeo ya kuridhisha katika mazingira yenye utulivu na salama.'

Mambo yanayoleta Umoja Baada ya utangulizi huo mfupi sasa tanaashiria baadhi ya mambo muhimu ambayo yana nafasi muhimu katika kuleta umoja na utengemano miongoni mwa Waislamu. 1- Qur'ani Takatifu
Kitabu hiki kitakatifu na kilichokamilika katika kila upande, kikiwa kimegawanyika katika sehemu tatu za maadili, imani na sheria, daima kimekuwa kikibeba mabegani bendera ya uokovu na mwongozo kwa binadamu. Kimekuwa kikiwahubiria wanadamu kwamba iwapo watakusanyika wote chini ya kivuli cha bendera hii, bila shaka watadhaminiwa furaha na saada ya humu duniani na ya huko Akhera. Kuna aya nyingi katika Qur'ani Takatifu zinazosisitiza haja ya Waislamu kuishi kwa amani na waumini wa dini nyinginezo. Hata kama neno 'umoja' halijatajwa moja kwa moja katika kitabu hiki kitakatifu lakini maneno mengine yametumiwa ambayo yanashiria maana ya neno hilo. Baadhi ya aya hizo ni kama ifuatavyo:
Aya ya Kwanza: Na Kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu. (Zamani) mlikuwa maadui; naye akaziunganisha nyoyo zenu; hivyo kwa neema yake, mkawa ndugu.

Mbinu na njia inayotumiwa na Mwenyezi Mungu ni kuwa, kwa upande mmoja huwanasihi na kuwataka waja wake wafuate njia ya saada ya milele, elimu na matendo mema na kwa upande mwingine kuonya dhidi ya upumbavu, ujinga, uigaji usio wa kimantiki, tabia za mifarakano na uadui. Uadui ulikuwa umekita mizizi miongoni mwa Waarabu kutokana na taasubu na ushabiki wa kikabila lakini kwa kudhihiri Uislamu, jambo hilo lilisahaulika na kuwa ni la kuzungumziwa kihistoria tu. Ulimbainishia mwanadamu sababu za kuumbwa kwake na haja yake ya kufuatilia mambo yanayomkurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Uliyachukulia maisha ya humu duniani kuwa utangulizi tu wa kufikiwa maisha mengine mema zaidi ya kudumu milele huko Akhera. Uliwataka waishi pamoja kwa amani na kama mandugu walio sawa, kama yalivyofanywa makabila ya Aus na Khazraj ambayo hatimaye yalifanikiwa kutiliana saini makubaliano ya amani baadda ya miaka mingi ya kuwa maadui wakubwa.

Aya ya Tatu: Na shikamaneni kwa kamba (dini) ya Mwenyezi Mungu nyote, wala msiachane (msitengane). Mtume amenukuliwa akisema: Uislamu ni wasila (chombo) ambao mwisho wake mmoja uko mikononi mwa Mwenyezi Mungu na mwingine uko mikononi mwenu. Shikamaneni nao kwa nguvu ili msije mkapotoshwa wala kuwapotosha wenzenu.'

Imenukuliwa katika riwaya nyingine kwamba, kamba hii takatifu ni Qur'ani tukufu ambayo iliteremshwa ardhini na Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni. Pia Mtume (SAW) amenukuliwa akisema kuwa, kamba hiyo ni kizazi chake kitoharifu (AS) ambacho wanadamu wameamrisha kukiheshimu, kukitii na kukifuata katika masuala yote yanayowahusu humu duniani kwa ajili ya kupata saada ya milele huko Akhera. Tunafahamu kutokana na maneno 'nyote' na 'wala msitengane' kuwa kama ambavyo Qur'ani Tukufu inawaamuru Waislamu kushikamana wote kwa kamba ya Mwenyezi Mungu ambacho ni kitabu hichohicho kitakatifu na sunna za Mtume (SAW), pia inawataka Waislamu kuwa kitu kimoja katika masuala yao ya kijamii. Kama Waislamu wangetekeleza maamrisho ya aya hii, bila shaka hii leo wangekuwa ndio wanauunda nguvu kubwa zaidi ambayo haijawahi kushuhudiwa ulimwenguni.

Aya ya Tatu: Wala msiwe kama wale waliofarikiana na kukhitalafiana baada ya kuwafikia dalili zilizo wazi (za kuwakataza hayo). Na hao ndio watakaokuwa na adhabu kubwa.
Khitilafu hapa ina maana ya kutengana kiimani. Mfarakano umeitangulia hitilafu hapa kutokana na kuwa ndio unaoandaa uwanja wa kutokea hitilafu. Hali hii inatokana na ukweli kwamba, kadiri watu wanapoungana na kuwa na uhusiano mzuri na wa kidugu katika jamii, hapo ndipo imani zao zinapoimarika na kukurubiana. Lakini wanapotengana na kuwa mbalimbali bila shaka jambo hilo hupanua pengo la kutengana kwao na kuondoa kabisa mambo yanayoleta umoja na mfungamano miongini mwao. Aya ya 213 ya Surat al-Baqarah inauchukulia mfarakano kuwa dhulma mbaya zaidi ambayo huwatenganisha watu. Kwa hivyo njia bora zaidi ya kuepuka mfarakano na kuimarisha umoja miongoni mwa Waislamu ni kushikamana na kamba ya Mwenyezi Mungu na kutegemea hoja zilizo wazi. Aya ya Nne: Kwa hakika Waislamu wote ni ndugu.

Aya ta Tano: Na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Wala msizozane (msigombane), msije mkaharibikiwa na kupotea nguvu. Kwa hakika ugomvi na uhasama usio na lengo tena katika mazingira yasiyo mazuri huwa hauna matokoe mengine isipokuwa mfarakano, chuki, ushabiki potofu na hitilafu za mara kwa mara. Qur'ani huyachukulia majadiliano yoyote yanayozusha mfarakano na ugomvi kuwa yasiyofaa na yale yanayoelekeza katika umoja na mfungamno kuwa mazuri na yanayopaswa kushajiishwa. Aya ya Sita: Kwa yakini huu umma wenu ni umma mmoja na mimi ni Mola wenu (mmoja), kwa hivyo Niabuduni.

Taifa ni kundi au jamii yoyote ile ambayo imefungamanishwa pamoja na hatima au lengo moja. Aya hii inayajumuisha mataifa yote ya mwanadamu na katika zama na vizazi vilivyo na Mungu mmoja pamoja na hatima moja ambayo ni Akhera. Aya nyingine za Qur'ani kama vile Aali Imran: 152, Nisaa: 71, An'am: 159, Tauba: 36 An'biyaa 92 Mu'minun: 52 Rum: 31 na 32 na Swaf: 4 zote hizi zinasisitiza umuhimu wa kuimarishwa umoja na mfungamano miongoni mwa wanadamu. Pamoja na hayo, lengo la aya hizi sio kupuuza na kufunika haki. Mbali na kusisitiza umuhimu wa kuwepo umoja miongoni mwa Waislamu Qur'ani pia inawashauri kufuatilia na kuimarisha umoja na wafuasi wa dini nyinginezo: Sema: "Enyi watu mliopewa Kitabu cha Mwenyezi Mungu. (Mayahudi na Manasara)! Njooni katika neno lililo sawa baina yetu na baina yenu: ya kwamba tusimwabudu yoyote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe (Mwenyezi Mungu) na chochote; wala baadhi yetu tusiwafanye wengine kuwa waungu badala ya Mwenyezi Mungu (au pamoja na Mwenyezi Mungu)."

Aya hii inaashiria imani ya pamoja ya Waislamu na Watu wa Kitabu, yaani kuhusiana na Tauhidi na umoja wa Mwenyezi Mungu na kuashiria kuwa imani hii inaweza kutumiwa kama chombo kizuri cha kuleta umoja na ushirikiano miongoni mwa wafuasi wa dini mbalimbali.
2 -Utume wa Mtume (SAW)
Jambo jingine linaloweza kuwaunganisha Mashia na Masunni ni utume wa Mtume Mtukufu (SAW) ambaye Mwenyezi Mungu amemuarifisha na kumsifu kwa kusema kuwa ni 'rehema kwa walimwengu wote.' Pia amemuarifisha kama mmbeba bendera ya amani na urafiki kati ya Waislamu na mataifa mengine ya ulimwengu. Kwa kipindi cha miaka 23, Mtume Mtukufu (SAW) alikuwa ndiye nembo halisi ya mapambano kwa ajili ya udugu na usawa na pia mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi na ukoloni. Yeye ndiye nembo ya wazi ya aya: Basi aongozaye katika haki siye anayestahiki zaidi kufuatwa au (anastahiki) yule asiyeongoka (hata yeye mwenyewe) isipokuwa aongozwe?

Katika siku za mwanzoni mwa utume wake, Mtume aliwaandikia watawala na wafalme barua nyingi akiwawajulisha mambo mengi yanayofanana kati ya dini ya Uislamu na imani za watu wa mataifa mengine tofauti. Baada ya kuzungumzia umoja na urafiki, alibainisha ukweli na haki ya Uislamu. Pia alishauri na kuimarisha utiwaji saini wa mikataba ya kidugu na kirafiki miongoni mwa Waislamu na hivyo kuvunja kivitendo sura mbovu ya migogoro na ugomvi katika jamii ya Kiislamu. 3-Kutegemea shakhsia ya Imam Ali (AS)

Mashia na Masunni wanaweza kuimarisha kwa kiwango kukibwa umoja miongoni mwao kwa kuamua kusoma na kutalii kwa undani shakhsia ya Imam Ali (AS). Huyu ndiye shakhsia anayezungumziwa na Bin Abil Hadeed anaposema: 'tuseme nini kuhusiana na mtu ambaye aliwatangulia wenzake katika uokovu, imani na kumwabudu Mwenyezi Mungu katika hali ambayo watu wengine wote walikuwa wakiabudu mawe?!'

Imam Ali mwenyewe anasema katika hotuba ya tano ya Nahjul Balagha kwamba, umoja wa Waislamu huleta maendeleo, uchanuaji, baraka, nguvu na heshima. Daima alikuwa akitoa wito wa kuimarishwa umoja miongoni mwa Waislamu. Mashia na Masunni wanaamini kwa kauli moja kwamba aya kadhaa zikiwemo zinazozungumzia utoaji zakaa katika hali ya rukuu kwenye swala, usiku ambao Mtume alihajiri kwenda Madina, utakasaji, upendo na uwalii ziliteremshwa kwa heshima ya Imam Ali (AS), mmbeba bendera ya elimu, wema na ambaye alilelewa katika shule ya Mtume Mtukufu (SAW). Uzingatiaji mahsusi wa shakhsia huyu mtukufu bila shaka unaweza kuwa na manufaa na nafasi nzuri katika kuimarisha umoja miongoni mwa Waislamu.

4-Mazungumzo ya Kielimu, Msingi wa Umoja

Kuwepo kwa watu wanaochukizwa kuwaona Waislamu, licha ya makundi na madhehebu yao tofauti, wakiishi pamoja kwa amani na ushirikiano chini ya mwavuli wa Tauhidi na Utume, bila shaka hufanya majukumu na mzigo wa wanazuoni wa Kiislamu kuwa mzito zaidi. Mtazamo wa harakaharaka tu wa wafuasi wa madhehebu yoyote ile kuhusiana na masuala mengi yanayowaunganisha Waislamu unawafanya wapate moyo wa kuimarisha ushirikiano miongoni mwao kwa maslahi ya umma mzima wa Kiislamu.

Katika upande wa pili, kuchunguzwa kitaalamu na kielimu masuala yanayowatenganisha Waislamu bila shaka huchochea hisia za kutaka kuelewa zaidi kielimu sababu za jambo hilo, na hivyo kuwafanya waweze kufikia ukweli na jinsi ya kuvumiliana na kukubali maoni ya upande wa pili.

Kwa kutilia maanani maudhui mbili hizi tunapasa kuutayarisha umma wa Kiislamu katika kuandaa mazingira yanayofaa ya kupatikana umoja kwa lengo la kufikia malengo mamoja kama vile, umoja katika kukabiliana na maadui, kukabiliana na mielekeo inayochochea mifarakano, kunyanyua kiwango cha elimu, maendeleo ya kiviwanda, kiutamaduni pamoja na kuimarisha usawa na udugu miongoni mwa Waislamu.

Kwa ibara nyingine ni kuwa, wasomi na wataalamu wa ulimwengu wa Kiislamu wanapasa kupanua uwanja wa ustawi na utafiti wa kielimu pamoja na mijadala inayohusiana na jinsi ya kuimarisha umoja na utulivu katika jamii ya Kiislamu. Hii ni kutokana na kuwa, huko nyuma masuala kama hayo yamekuwa na athari kubwa nzuri katika kunyanyua kiwango cha maisha ya Waislamu, athari ambazo tungali tunazishuhudia hata katika zama zetu hizi.

Kwa mfano ni mazingira hayo mazuri ndiyo yaliyompelekeka mwanazuoni mashuhuri wa Kisunni na Kansela wa Chuo Kikuu cha Al-Azhar Sheikh Muhammad Shaltut kuanza kufanya utafiti na uchunguzi wa kina kuhusiana na imani ya Kishia. Utafiti wake huo hatimaye ulimshawishi kutoa fatwa mashuhuri ambayo sehemu yake inasema hivi: 'Madhehebu ya Ja'fari ambayo ni mashuhuri kwa jina la Shia Ithna Asheri ni madhehebu ambayo ufuasi wake unaruhusiwa kisheria kama yalivyo madhehebu mengine ya Kisunni. Kwa hivyo Waislamu wanashauriwa kuifahamu vyema na kujiepusha na taasubu ya kishabiki dhidi ya madhehebu fulani.'

Bila shaka fatwa hiyo ya Shaltut ilitolewa katika msingi wa utafiti na katika mazingira ya utulivu na umoja. Hili ndilo jambo lililowapelekea wanazuoni wengine mashuhuri katika ulimwengu wa Kiislamu kama vile Dr. Muhammad Fahham, Sheikh Muhammad Ghazali, Abd ar-Rahman Najjar - Mwenyekiti wa Bodi ya Wasimamizi wa Msikiti wa Cairo, Profesa Ahmad Bek, Profesa Sheikh Shaltut na Abu Zahra, Profesa Mahmoud Sartawi - mmoja wa mamufti wa Jordan na Dr. Hamid Hanafi Dawoud - mhadhiri wa lugha ya Kiarabu katika Chuo Kikuu cha Cairo kuunga mkono fatwa hiyo ya Sheikh Shaltut. Walilalamika kuwa hali ya kusikitisha na kuhuzunisha inayoukumba ulimwengu wa Kiislamu hivi sasa inatokana na mfarakano wao na kutofahamiana. Walisema kuwa walikuwa na imani thabiti kwamba kutekelezwa kwa fatwa hiyo kungesaidia sana katika kutatua tatizo hilo na kuleta maendeleo na ushirikiano miongoni mwa Waislamu.

Neno la mwisho Katika kipndi cha karne nyingi zilizopita, Waislamu wamefanywa kubaki nyuma ya mataifa mengine kutokana na migawanyiko yao wenyewe ya kimadhehebu. Kabla ya kugunduliwa bara la Marekani nao Wazungu kuishi chini ya tawala ndogondogo za kijamii zilizokuwa zikizozana mara kwa mara, Waislamu walikuwa tayari wamepiga hatua kubwa katika nyanja za kielimu, kiviwanda , kiutamaduni na uadilifu wa kijamii. Kwa masikitiko makubwa adui alifanikiwa kwa kiwango kikubwa katika kutumia silaha ya kuwatenganisha na kuwagonganisha Waislamu katika misingi ya kimadhehebu.

Njama hizo za maadui hazikukomea hapo bali ziliendelea hadi wakati wa kubuniwa kwa pote potofu la Mawahabi lililoasisiwa na Muhammad bin Abdul Wahhab. Mara tu baada ya kuasisiwa kwake, kundi hilo hatari lilitekeleza mauaji ya kutisha dhidi ya Mashia na Masunni. Katika siku ya Idul Ghadir Mwaka 1216 kundi hilo potofu liliwachinja kinyama Waislamu wasio na hatia wapatao 5000 katika mji mtakatifu wa Karbala nchini Iraq. Adui pia alifanya njama ya kuasisi kundi jingine kibaraka la Mabahai nchini Iran chini ya uongozi wa Muhammad Ali Bab na kumuarifisha kuwa ndiye Imam wa Zama wa Mashia.

Masuala haya yote yanayafanya majukumu ya wasomi na watafiti wa Kiiislamu kuwa magumu zaidi. Yanawakumbusha kwamba wanapaswa daima kuhubiri umoja, upendo na ushirikiano miongoni mwa Waislamu na kupambana dhidi ya mielekeo na imani mbovu zinazotumiwa na makundi ya kishabiki katika jamii kwa madhara ya Umma wa Kiislamu.

Kwa mfano, ni jambo la kusikitisha kuona kwamba baadhi ya makundi ya Kisunni hufanya sherehe za harusi katika siku ya huzuni ya Ashura ambapo mjukuu wa Mtume Imam Hussein (AS) aliuawa shahidi na dhalimu Yazid. Katika upande wa pili, kuna baadhi ya makundi ya Kishia ambayo hufanya sherehe maalumu ya kumuenzi na kuonyesha mapenzi yao kwa Bibi Zahra ijulikanayo kama Idu Zahra (AS) ambapo katika shehere hiyo hutumia lugha mbaya na isiyo ya heshima dhidi ya baadhi ya viongozi wa Kisunni. Ni wazi kwamba tabia hizo za kijanagenzi huleta mfarakano, chuki na uadui kati ya Waislamu kwa furaha na kicheko cha adui muovu mwenye makri.

MWISHO
MAREJEO: 1- Ulimwengu wa Kiislamu, changamoto na utatuzi, makala zilizowasilishwa kwa kikao cha 12 cha Umoja wa Kiislamu, 1379 (Kalenda ya Kiirani)
2- Swahife-ye- Nour, Imam Khomein, j.1 uk.120
3- Mtazamo mpya wa fikra ya ukurubishaji, Eskandary, pg.32
4- Aali Imran:103
5- Dhariyaat:56
6- Aali Imran:103
7- Durr al-Manthur, Suyuti, chini ya aya 103, Aali Imran
8- Tafsir Ayashi, chini ya aya 103, Aali Imran
9- Tafsir Mizaan, Allama Tabatabai, j.3 uk.602
10- Aali Imran 105
11- Tafsir Mizaan, j.3 uk.608
12- Hujuraat:10
13- Anfaal:46
14- Nahl:125; Ankabut:46
15- Anbiyaa:92
16- 'Mufradaat Raghib, chini ya maudhui 'umma'
17- Tafsir Nemuneh, Makarim Shirazi, j.13 uk.497
18- Aali Imran:64
19- Tafsir Nemuneh, Makrim Shirazi j.2 uk.450
20- Yunus:35
21- Makatib Rasul, j.1 uk.97
22- Shereh Ibn Abil Hadeed, j.3 uk.210
23- Aali Imran:6, Musnad Ahmad j.1 uk.185
24- Baqarah:207, Mustadrak ala as-Swahihein, j.3 uk.4
25- Ahzab:33, Swahih Muslim, j.2 uk.331
26- Shura:23 Durr al-Manthur, Suyuti j.2 uk.239
27- Maida:55, j.2 uk.239
28- Chanzo cha tofauti kati ya Mashia na Masunni katika kutafsiri maana ya aya za Qur'ani kinatokana na riwaya na hadithi.
Wanazuoni wanaweza kutalii silisila ya wapokeaji hadithi na maana ya hadithi zenyewe mbali na hisia za kitaasubu na majivuno yasiyo na msingi ili kufikia ukweli wa Qur'ani and Sunna.
29- Islamuna, Rafi' uk.59, akinukuliwa Ghadir Shanasi, Ali Asghar Rezwani, uk.18
30- Fi Sabil Wahdatil Islamiya uk.64
31- Difa' anil Aqida wa Sharia uk. 257
32- Fi Sabil Wahdatil Islamiya uk.66
33- Taarikhul Madhahibil Islamiya uk.39
34- Risalatu Thaqalain magazine. j.2, mwaka wa kwanza,1413, uk.252
35- Ghadir Shanasi, Ali Asghar Rezwani, uk.10-30
36- Ain Wahabiyat, Ja'far Subhani, uk.29
37- Hambastegi