NI NANI AHLULBAYT (A.S) 1
  • Kichwa: NI NANI AHLULBAYT (A.S) 1
  • mwandishi: HASSAN BUSS
  • Chanzo: busihassan@gmail.com
  • Tarehe ya Kutolewa: 19:7:37 1-9-1403

AHLUBAITI RASUL AS, KILUGHA NI KUNDI KUBWA SANA LAKINI KISHERIA NI WATU MAALUM WASIOZIDI 14 AMBAO MWENYEZI MUNGU NA MTUME WAKE SAWW WAMETIA MKAZO WA KUWATII NA KUFUATA, KWENDA KINYUME NA WAO NI KUMUASI MWENYEZI MUNGU NA MTUME WAKE SAWW.

WANAZUONI WAKUBWA WA AHLISUNA NA SHI'AH WANA MAKUBALIANO YA PAMOJA KATIKA KUWATAMBULISHA HAO AHLUBAITI RASUL AS KATIKA VITABU VYAO VYA HADITHI, TAFSIRI NA HISTORY

Sunnah na Nyumba ya Mtume saww, Ahlul Bayt.

Ni nani wanaunda Nyumba ya Mtume saww Ahlul Bayt?

Swali jingine linahusu ile maana ya "Nyumba ya Mtume saww" katika hadithi nyingi zinazotuagiza kushikamana na Nyumba ya Mtume saww, wao wanarejelewa kwa jina la Ahlul Bayt au al Itrah. Maneno haya yanatumika juu ya nini na ni watu gani wamezungukwa na nafasi hiyo ya watu wa Nyumba ya Mtume saww? Je, inajumuisha yeyote na ndugu wote wa Mtukufu Mtume Saww?

Hoja tatu tofauti zitatolewa katika kujibu maswali haya, ingawa kila hoja inaweza kuonekana yenye kujithibitisha yenyewe. Kama mambo yalivyo hakuna shaka miongoni mwa waislamu kwamba Fatimah, bint ya Mtukufu Mtume saww, Imamu Aliy as, na watoto wao Imamu Hassan na Imamu Hussein walitokana na Nyumba ya Mtukufu Mtume saww.

Swali pekee ni iwapo ndugu wengine wa Mtukufu Mtume Saww wanaweza kujumuishwa katika kundi hilo au hapana, na kama ni hivyo, je ni kwa kiasi gani.

Baadhi ya waislamu wa Ahlisuna wanaamini kwamba ndugu wote wa Mtume saww wanapaswa kujumuishwa, ukiwaondoa, wale ambao hawakuukubali uislamu, kama vile Abu Lahab, ami yake Mtume saww ambaye wakati wote huo huo alikuwa mmoja wa maadui zake wakubwa na kwa sababu hiyo alikuwa amelaaniwa ndani ya Quran tukufu.

Waislamu wa Shi'ah, kinyume chake, wao wanaamini kwamba Nyumba ya Mtume saww ni wale watu ambao wana viwango vya imani na elimu ambavyo vinafanya iwezekane wao kutajwa pamoja na Qur-an katika Thaqalayni na katika hadithi nyinginezo. Zaidi ya hayo, Shi'ah wanaamini kwamba Mtukufu Mtume saww mwenyewe amenainisha watu wa Nyumba Yake.

HOJA YA KWANZA :

Wakati wowote tunapokuwa na shaka kuhusu upeo wa jambo lolote lile, kama vile kanuni au dhana, lakini tukawa tunajua kwamba ni ukweli wenye kujuzu kwa ukomo fulani, ambao zaidi ya hapo unaingia kwenye mjadala, ni lazima tutumie Tahadhari na tufate tu lile la chini kabisa. Kwa mfano, tuseme kwamba mtu hana uhakika iwapo katika swala yake pale mwanzoni mwa rakaa mbili za awali anaweza kusoma Surat al Fatiha tu au kama anaweza kusoma sura zingine za Qur-an pia. Akili inaamua kwamba anapaswa kutahadhari na lazima asome kile ambacho ana uhakika nacho, ambacho ni Surat al Fatiha.

Sasa katika suala letu sisi kama mtu ana wasiwasi kuhusu upeo wa maneno Ahlul Bayt au maneno kama hayo, kibusara anawajibika kujifanya kwenye kadiri iliyo ndogo ambayo kwamba yeye anao uhakika nayo. Sasa kama mtu ana shaka juu ya iwapo Mwenyezi Mungu anakubali kutajwa kwa watu zaidi ya Fatimah na familia yake pamoja na Qur-an, kama sehemu ya Nyumba ya Mtume saww, akili inamuelekeza mtu kuwa na Tahadhari na kujikomeshea mwenyewe kwa wale watu ambao haswa wamejumuishwa katika upeo wa maneno haya.

Na waliojumuishwa katika upeo wa maneno haya yaani nyumba ya Mtume saww, ni watu maalumu kama ilivyo katika tafsir ya Aya hii ya utakaso

إنما يريد الله ليذهب عنكم الرجس أهل البيت ويطهركم تطهيرا.

Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni (kukukingeni na) uchafu, Enyi watu wa Nyumba ya Mtume, na kuwatakasa kabisa kabisa. 33:33

Ibun Taymiyyah anasema katika kitabu chake "Huquuq Ahlul Bayt baynas Sunnah wal Bidaa,"

Pamoja na Uadui wake wa enzi na enzi juu ya Shi'ah, lakini hapa uzalendo umemshinda kasema ukweli, haya hapa maneno yake :. "Na pindi Mwenyezi Mungu alipobainisha kwamba anataka kuwaondolea (kuwakinga na) uchafu Ahlul Bayt na kuwatoharisha tohara ya kabisa kabisa, Mtukufu Mtume saww aliwaita ndugu zake wa karibu na akawatukuza ili wawe makhsusi kwake, nao ni Ally bin Abi Twalib as, Fatimah (radhiyallahu anhum) na mabwana wa vijana wa watu peponi, Mola aliwatoharisha hao baada ya kukusanyika na du'a ya Mtume saww kukamilika, na hilo lajulisha kuwa kuondolewa uchafu na kutakaswa ni neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Vilevile Ibn Taymiyyah anasema : "Kutoka kwa Ummu salama :" Hakika aya hiyo ilipoteremshwa Mtukufu Mtume saww aliwafunika kishamiya Ally, Fatimah, Hassan na Hussein (r. a) akasema : "Ewe Mola wangu hawa ndio Ahlul Bayt wangu waondolee (wakinge na) uchafu na watoharishe tohara ya kabisa kabisa.

Ahmad Muhammad Subhi Ustadhi wa falsafa naye ni katika Masunni, katika kitabu chake" Nadhariyyatul Imamah "akiweka pambizoni kwenye aya ya Utakaso  Amesema :." Na tafsir hii inafaidisha kwamba AhIul Bayt ni wale ambao wamekusudiwa katika lafudhi ya Qurba katika aya, na hata Ibn Taymiyyah pamoja na upinzani wake juu ya tafsir za ki Shi'ah lakini amesarenda, kwani imepokewa katika vitabu sahihi kwamba Mtume saww alihutubia siku ya Ghadir khom akasema : "Ninawakumbusha kuhusiana na Ahlul Bayt wangu, aliyasema hayo mara tatu".

Rejea :.

Na la kuchunguza na kuzingatia hapa ni kwamba hakuwataja wake wa Mtume saww na hakusema aya ya Utakaso imeteremshwa kwao, wala haikuwajumuisha wake wa Mtume saww na hiyo ni dalili tosha kwamba aya ya Utakaso imeshushwa juu ya watu hao wanne Ally, Fatimah, Hassan na Hussein a.s kutokana na kukiri na kuandika vitabuni mwao wanachuoni wa Ahlisuna.

Fuatana nami sehemu ya kumi ya Sunnah na Ahlul Bayt na ni nani hao? hoja ya pili.

REJEA:

  1. Huquuq A'ali Bayt cha Ibn Taymiyyah UK 12.
  2. Huquuq A'ali Bayt cha Ibn Taymiyyah UK 10.
  3. Nadhariyyatul Imamah UK 184.