ULIMWENGU ULIVYO ANZA
  • Kichwa: ULIMWENGU ULIVYO ANZA
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 11:48:50 14-9-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

ULIMWENGU ULIVYO ANZA
Profesa Alfred Kroner ni mmoja kati ya maulamaa wakubwa na maarufu sana ulimwenguni katika elimu ya jiolojia ambaye pia ni mwenyekiti wa idara ya jiolojia katika chuo kikuu cha Johannes - Gutenburg huko Ujerumani. Anasema Sheikh Abdul Majeed Al Zindani;

"Tulikuwa katika mojawapo ya mikutano ya kujadili miujiza ya sayansi katika Qurani tukufu uliofanyika katika chuo kikuu cha mfalme Abdul Aziz huko Saudi Arabia, na mmoja kati ya waliohudhuria alinijia akiwa amefuatana na profesa Alfred Kroner, na baada ya kunijulisha naye akanambia kuwa huyu ni mtu asiyeamini Mungu, na kwamba nisije nikahatarisha imani yangu kwa kujadiliana naye juu ya mambo ya dini, kwani yeye ni mwerevu sana katika majadiliano ya namna hii."

Nikamwambia; "Vizuri." Kisha nikamtaka profesa huyo akae na tuanze kujadiliana. Suali la mwanzo nililomuuliza lilikuwa;
"Elimu ya sayansi inasema nini juu ya mwanzo wa dunia, yaani vipi ulimwengu huu ulianza hata zikatokea ardhi na sayari zote hizi" ? Akanijibu ;
"Ulimwengu wetu huu ulianza kiasi cha miaka milioni 20,000 iliyopita, na tuna uhakika uliokwisha thibiti kielimu kuwa ardhi hii tunayoishi juu yake pamoja na sayari zote tunazoziona na tusizoziona huko juu vilikuwa kitu kimoja kilichokamatana na kwamba mada zote ambazo hivi sasa ni asili ya sayari zote hizi (elements) asili yake ni moja. Kwa muda wa miaka milioni nyingi vitu hivi viliendelea kuwa kitu kimoja kilichokamatana mpaka pale ulipotokea mripuko (mlipuko) mkubwa sana uliokuja kujulikana kwa jina la 'The Big Bang', ndipo mkamatano huo ulipogeuka kuwa moshi mwingi na mkubwa sana ulioanza kuzunguka kwa kasi kubwa sana na kwa muda wa miaka mingi sana huku ukijitenga tenga na kujikusanya na kujitengeneza kuwa ardhi yetu hii pamoja na sayari na nyota zinazoelea huko juu zinazokwenda kwa nidhamu ya hali ya juu kabisa".

Sheikh Abdul Majid al Zindani akamuuliza;
"Utasemaje nikikwambia kuwa uhakika huu umekwishatajwa katika Qurani tukufu aliyokuja nayo Mtume Muhammad (SAW) tokea miaka elfu moja mia nne iliyopita?"
Profesa Kroner akasema;
"Haiwezekani kabisa kwa mtu aliyeishi miaka 1400 iliyopita akaweza kuja na uhakika kama huu."

Nikamwambia;
"Mwenyezi Mungu katika Suraul Anbiyaa anasema;
"Je! Hawakuona wale waliokufuru ya kwamba mbingu na ardhi vilikuwa vimeambatana kisha tukaviambua (tukavibandua - tukavipambanua). Na tukafanya kwa maji kila kitu kilicho hai. Basi jee hawaamini?"
Al Anbiyaa - 30
Anasema Sheikh Al Zindani kuwa baada ya kujadiliana naye kwa muda mdogo tu, Profesa Kroner akasema;
"Nikichunguza yote haya ulonambia pamoja na uhakika kuwa Muhammad alikuwa mbedui aliyeishi miaka elfu moja mia nne iliyopita, naona haingewezekana kabisa kwa mtu kama huyo asiyejuwa elimu ya nuclear physics aloishi wakati huo kuweza kujuwa au hata kufikiria kuwa ardhi, sayari na kila kilichokuwemo ndani yake vilikuwa kitu kimoja kilichokamatana, kwani ili mtu aweze kudhania tu juu ya jambo hilo, lazima kwanza awe na elimu ya kutosha pamoja na vyombo vya kisasa vitakavyomwezesha kujuwa kuwa ardhi hii pamoja na sayari zake, vyote vinatokana na asili moja, kwa sababu wana sayansi wameweza kuyajuwa haya miaka ya hivi karibuni tu, tena baada ya kupatikana kwa vyombo vya kisasa kabisa pamoja na teknolojia ya hali ya juu sana."

Neno 'Ratqan' ambalo Mwenyezi Mungu Subhanahau wa Taala amelitumia katika aya hii kuielezea hali ya ulimwengu kabla ya kuipambanua limefasiriwa na Ibni Abbas na Mujahid (RAnhum) kama ifuatavyo; "Mwenyezi Mungu amesema; (Kaanataa ratqan yaani kaanataa multasiqataani - fafataqnaahuma yaani fafaswalnahuma) na maana yake ni kama ifuatavyo; "Mwenyezi Mungu amesema (vilikuwa vimeambatana, yaani vimegandana na akasema fafataqnahuma, yaani tukavipambanua).

Juu ya yote hayo, Profesa Kroner alikataa kukiri kuwa Muhammad (SAW) alijulishwa na Mola wake juu ya matukio hayo, bali alimaliza kwa kusema kuwa; 'Bila shaka ipo nguvu ya ajabu (Supernatural power) inayompa habari hizo.' Na Sheikh Al Zindani alipojaribu kumwambia kuwa; 'Nguvu hiyo ni Allah', Profesa akajibu; ' Mimi sikusema hivyo.'

Anasema Sh Al Zindani;
"Nikaacha kuendelea na mjadala huo kwani nilikwishatahadharishwa kuwa yeye ni mtu hodari sana wa kugeuza maneno. Nikamuuliza suali la pili; "Mnazo habari zozote zinazosema kuwa bara ya Arabu (Arabian peninsula) hapo zamani ilikuwa ardhi iliyojaa miti na mabustani na mito?"

Akanambia;
"Ndiyo, huu ni uhakika ambao wanavyuoni wote katika elimu ya jiolojia wanaujuwa vizuri, na kama utachimba sehemu yoyote ile katika ardhi hii utaona dalili nyingi zinazouthibitisha uhakika huu, na dalili maarufu ni ile iliyogunduliwa katika kijiji cha Fao kilichopo ndani ya jangwa linalojulikana kwa jina la Empty Quarter (Roboa al khali - yaani robo tupu isiyokaliwa na mtu)." Anasema Al Zindani;
"Nikamuuliza tena; Mnazo habari zozote kuwa bara ya Arabu itarudi tena kuwa ardhi iliyojaa miti na mabustani na mito?" Akanijibu; "Huu ni uhakika tunaoujuwa vizuri sisi wataalamu wa jiolojia na tumeufikia kwa vipimo na hesabu madhubuti. Tunaweza kukisia kuwa jambo hili litatokea hivi karibuni." Nikamuuliza; 'Vipi?'
Akanambia;
"Tumeichunguza historia tukaona kuwa sehemu hii imepitiwa na zama inayoitwa 'Zama za theluji', na maana yake ni kuwa maji ya bahari yanageuka kuwa barafu. Na hivi sasa barafu hiyo inajikusanya katika North Pole (ncha ya kaskazini ya dunia) huku ikijisogeza kuelekea kusini, na kila inapojisogeza, hali ya hewa ya sehemu iliyo karibu nayo inabadilika, na bara ya Arabu itakumbwa na hali hiyo na kugeuka kuwa sehemu yenye utajiri mkubwa wa ardhi ya kilimo na mvua na mito."

Anasema Shekh Al Zindani;
"Alipokuwa akisema hayo, mimi nilikuwa naunganisha maneno yake na mvua kali zinazonyesha wakati ule katika sehemu ya Abha (Saudia) na sehemu mbali mbali za Arabuni na pia kuanguka kwa barafu." Nikamuuliza;
"Unaweza kutuhakikishia juu ya jambo hili?"
Akanambia;
"Bila shaka! Huu ni uhakika usiokuwa na shaka yoyote ndani yake. Dhoruba za theluji zinashambulia sehemu mbali mbali za ulaya kaskazini na Marekani. Na wanasayansi wana dalili nyingi zinazowajulisha kuwa zama za theluji zinakaribia kurudi tena katika eneo hili la Bara ya Arabu,."

Nikamwambia;
"Nyinyi mumeweza kuyajuwa haya kwa kutumia vyombo vyenu vya kisasa pamoja na ndege na meli na vifaa mbali mbali vya majaribio. Unaonaje nikikwambia kuwa Mtume Muhammad (SAW) ametuambia yote haya miaka elfu moja mia nne iliyopita, katika hadithi iliyo ndani ya Sahih Muslim aliposema;
"Haitosimama Saa (hakitosimama Kiama) mpaka kwanza irudi tena ardhi ya waarabu kuwa mabustani na mito". Nikamuuliza; "Nani aliyemuambia Muhammad (SAW) kuwa ardhi hii ilikuwa mabustani na mito?"
Kwa vile hakutaka kuukubali ukweli Profesa Kroner akasema; "Warumi. Warumi ndio waliomwambia hivyo." Anasema Sheikh Al Zindani;
"Nikamuuliza;
"Nani aliyemuambia kuwa itarudi tena kuwa mabustani na mito?"
Hapo akashindwa kubabaisha, akakiri na kusema; "Kutoka juu." Kisha nikamwambia aandike kwa mkono wake. Akaandika yafuatayo;

"Uhakika wa kisayansi uliomo ndani ya Qurani na Sunnah umenishangaza. Sisi hatukuyajuwa hayo hapo mwanzo mpaka tulipoweza kupata vyombo vya kisasa vya sayansi pamoja na elimu ya juu, na hii ni dalili kuwa Mtume Muhammad (SAW) amezipata habari hizi kutoka kwa Allah kwa kufunuliwa wahyi utokao kwa Allah."

"Ndugu zangu Waislam!" anaendelea kusema Sheikh Al Zindani, "Huu ni msimamo wa Mjerumani asiyeamini Mungu. Nchi za kiislamu zingeubeba mzigo huu wa kuwafahamisha wanavyuoni hawa, bila shaka maulamaa wakubwa wakubwa wa elimu za sayansi wangeingia katika dini hii baada ya kuuona ushahidi ulio wazi. Kama mlivyoona, si kuwa wanakubali tu, bali wanaandika kwa mikono yao na kuyatangaza yale waliyoshuhudia. Na kama dola za Kiislamu zitafanya juhudi tena kwa uaminifu, basi haitopita miaka kumi na mitano isipokuwa tutawaona mmoja katika kila wanasayansi watatu ulimwenguni wakiingia katika dini ya Kiislamu."

MWISHO