SIFA ZA WATIIFU NO.2
  • Kichwa: SIFA ZA WATIIFU NO.2
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 3:46:47 21-8-1403

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

SIFA ZA WATIIFU NO.2

WAFUASI WAKWELI WA MITUME

* Ni alama gani zinazoonesha ukweli wa wafuasi wa Mitume?.

* Kuna athari gani katika kuwakubali na kuwafuata Mitume?.

Katika makala iliyopita tulielezea kuhusu wafuasi wa kweli wa Mitume ya Mwenyeezi Mungu (s.w) na sifa walizonazo watiifu hao. katika makala hii tutaendelea kuelezea sifa nyengine walizonazo watu hao.

2-2. Kunufaika na rehema zake Mwenyeezi Mungu.

Kumtii Mwenyeezi Mungu na Mitume yake, kunamsaidia na kumuokoa mwanaadamu na ujahili, na pindi mwanaadamu akimtii Mwenyeezi Mungu na Mitume yake hujiepusha na kufanya madhambi, na mwanaadamu huyo hunufaika na rehema zake Allah (s.w). kama inavyosema Qur-ani Takatifu:-

وَاَطِيعُواْ اللّهَ وَالرَّسُولَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ[1]

mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume ili mpate kurehemewa.

*Hapa inabainishwa kuwa rehema ya Mwenyeezi Mungu haiwezi kupatikana ila kwa KUMTII Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, kwa kufuata amri zao kiasi cha uweza wako, na kuwacha makatazo yao kabisa kabisa.

Haipatikani Pepo kwa kuwa wewe ni Muislamu tu (Mwislamu jina), wala kuwa unafuata madhehebu fulani ya Kiislamu au tarika (njia) fulani, kwa kuwa mkubwa wa madhehebu hayo au mkubwa wa tarika hiyo atakushufaia.

Mtume mwenyewe atawapa watu shifaa kwa idhini ya Mola wake tu, seuze wengineo.

Sharia husema, Aso thawabu               Shida na mashaka, yatamsibu.

Shufaa ya Tumwa, Lmahbubu             Huwa mbali naye, na kumwegema.

Salili Jahimu, mambo mazito               Siyahi na zite, katika moto

Sura uwakao, kwa mivukuto                Na kwenda miteo, na kugoroma.

Dhamirini mwako, usisahau                Dhiki za motoni, ukadharau.

Dhurubu mithali, kama hiyau              Wadhurubiyeo, wote Ulama.

Dhalimu wa huku, ulimwenguni           Dhili ya Arishi, haketi tini.

Dhulma humpa, kwenda motoni           Nyumba ya adhabu, zisizokoma.       

Wale ambao humtii Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, hufutiwa madhambi yao waliyoyafanya, na wala hawapunguziwi malipo yao hata chembe kutokana na mambo ya kheri waliyoyafanya.

Kama anavyosema Allah (s.w):-

قَالَتِ الاَعْرَابُ آمَنَّا قُل لَّمْ تُؤْمِنُوا وَلَكِن قُولُوا اَسْلَمْنَا وَلَمَّا يَدْخُلِ الإِيمَانُ فِى قُلُوبِكُمْ وَإِن تُطِيعُوا اللهَ وَرَسُولَهُ لاَ يَلِتْكُم مِّنْ اَعْمَالِكُمْ شَيْئاً إِنَّ اللهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ[2]

Mabedui wamesema: Tumeamini. Sema: Hamjaamini, lakini semeni: Tumesilimu. Kwani Imani haijaingia katika nyoyo zenu. Na mkimt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hatakupunguzieni chochote katika vitendo vyenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.

2-3. Kunufaika na muongozo (usaidizi) wake Allah (s.w).

Mitume, na wafuasi wa kweli wa Mitume hiyo hunufaika na muongozo wake Allah (s.w),  na Mwenyeezi Mungu huwapa msaada watu hao duniani na Akhera. Kama anavyosema Allah (s.w):-

إِنَّا لَنَنصُرُ رُسُلَنَا وَالَّذِينَ آمَنُوا فِى الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَيَوْمَ يَقُومُ الاَشْهَادُ[3]

Hakika bila ya shaka Sisi tunawanusuru Mitume wetu na walio amini katika uhai wa duniani na siku watapo simama Mashahidi.

*Wema wasikate tamaa, watapata nusra tu japo itakuwa vipi – na japo baada ya kufa kwao, ya haki wanayoyalingania yatakuwa tu.

MWISHO

[1] Surat Al-Imrani Aya ya 132

[2] Surat Al-Hujurat Aya ya 14

[3] Surat Al-Ghaafir Aya ya 51