DU’A YA MWEZI WA RAMADHANI (SEHEMU YA 5)
  • Kichwa: DU’A YA MWEZI WA RAMADHANI (SEHEMU YA 5)
  • mwandishi: al-islam.org
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 12:13:39 14-9-1403

DU’A YA MWEZI WA RAMADHANI (SEHEMU YA 5)

اللّهُمَّ اقْضِ دَيْنَ كُلِّ مَدِينٍ

Ewe Mola Mlipie Deni Kila Mwenye Kudaiwa

MAANA PANA YA NENO ‘DENI’

Huenda wengi wakachukulia ya kwamba neno deni ni sawa na mkopo lakini katika sheria za kiislamu lina maana pana kushinda mkopo kwa kuwa mkopo ni sehemu ya deni.
Āyatullāh Shirāzi katika kitabu chake cha ‘Tafsir-e-Nemūne’ amezungumzia jambo hili na akasema kwamba “Mkopo” hutumika mtu anapo lazimika kurudisha kilicho sawa na kilicho chukuliwa, kwa mfano kama atachukua pesa kwa njia ya mkopo atalazimika arejeshe kiasi hicho hicho na lau atachukua aina fulani ya chakula atalazimika arudishe aina hiyo hiyo. Hata hivyo dayn (deni) lina maana pana kwa kuwa linajumuisha aina yoyote ya shughuli, kama vile: kusuluhisha (sulh), mkataba wa kupangisha, (ijāra), kuuza na kununua na kadhalika.1

DENI WAKATI MWINGINE HUMZUIA MTU KUENDELEA KIROHO

Deni wakati mwingine huwa ni kizuizi kikubwa katika njia ya Mwenyezi Mungu. Sababu ya hili ni kwamba hushughulisha akili na moyo wa mtu, na kwamba ni kipengele cha wazi ambacho huzuia maendeleo. Tazama hadithi ifuatayo:
1. Imamu Zaynu’l ‘Abidin katika maombi yake ya kupendeza2 kwa ajili ya kuondokana na madeni anawajulisha wafuasi wake hali ngumu ambayo mdaiwa kwa kawaida huipata:
Ewe Allah!
Mbariki Muhammad na watu wa nyumbani kwake, na uniondolee deni ambalo huchusha uso wangu, huchanganya akili yangu, huvuruga mawazo yangu na hurefusha muda wangu kwa kulishughulikia! Naomba kinga Kwako, ewe Mola wangu, kutokana na wasiwasi na mawazo kuhusu deni, kutokana na uharibifu wa deni na kukosa usingizi; basi mbariki Muhammad na watu wa nyumbani kwake, na unipe kinga kutokana nalo! Naomba hifadhi Kwako, ewe Mola wangu, kutokana na udhalili wa deni katika maisha, na matokeo yake mabaya baada ya kufa…
2. Mtukufu Mtume (saw) amesema:

إِيَّاكُمْ وَ الدَّيْنَ فَإِنَّهُ هَمٌّ بِلّيلِ وَ ذُلٌّ بِانَّهَارِ
“Jihadharini na deni kwani kwa hakika husababisha huzuni wakati wa usiku na udhalilisho wakati wa mchana”.3
Hali nyingine ya dhahiri ambayo yaweza kumzuia mtu anaye daiwa kuendelea kirohoni ikiwa hajali kulipa deni lake.
Zifuatazo ni hadithi ambazo zinafaa mtu kuzitafakari:
1. Imam Ja’far al-Sadiq (a.s.) amenukuliwa akisema:

أَيُّمَا رَجُلٌ أَتَى رًجُلاً فَاسْتَقْرَضَ مِنْهُ مَالاً و فِيْ نِيَّتِهِ أَنْ لاَّ يُؤَدِّيْهِ فَذَلِكَ اللّصُّ العَادِّيْ
“Mtu yeyote ambaye anakwenda kwa mtu na kuchukuwa pesa kama mkopo kutoka kwake wakati ambapo ana nia ya kutomlipa ni mwizi wa kawaida.”4
2. Imam Ja’far al-Sadiq (a.s.) amenukuliwa akisema:

مَنْ اسْتَدَانَ دَيْنًا فَلَمَ يَنْوِي قَضآءَهُ كَانَ بِمِنْزِلَةِ السَّارِقِ
“Yeyote yule achukuae mkopo na akaweka nia ya kutokulipa, ni sawa sawa na mwizi.”5
Katika hadithi hizo hapo juu watu kama hao wametajwa kama wezi. Kwa maana yake basi, dhana ile ya ‘kuendelea kiroho’ iko mbali mno nao.
Wale ambao wana tabia ya mara kwa mara ya kuchukuwa mikopo hapa na pale, ni lazima vile vile watambue hatimaye hatari ambayo inayowangoja. Hadithi za Ahlul-Bayt (a.s.) zimedokeza baadhi ya hatari hizo kama ifuatavyo:
1. Imamu ‘Ali (a.s.) amenukuliwa akisema:

كَثْرَةُ الدَّيْنِ تُصِّيْرُ الصَّادِقَ كَاذِبًا و المُنْجِزَ مُخْلفَا
“Madeni yakizidi humgeuza muaminifu kuwa muongo na mtu anaye tekeleza ahadi kutokuwa muaminifu.”6
2. Imamu Muhammad al-Baqir (a.s.) amenukuliwa akisema:

كُلُّ ذَنْبٍ يُكَفِّرُهُ الْقَتْلُ فِيْ سَبِيْلِ اللّهِ إلاَّ الدَّيْنَ، لاَ كَفَّارَةَ لَهُ إِلاَّ أَدآءُهُ أَوْ يَقْضِيْ صَاحِبُهُ أَوْ يَعْفُو الَّذِيْ لَهُ الحَقُّ
“Shahidi katika njia ya Allah hufutiwa dhambi zote isipokuwa deni, kwani halina fidia isipokuwa malipo yake, au kulipwa na warithi (sāhibuhu) au kusamehewa na mdai…”7
3. Imamu Ja’far al-Sadiq (a.s.) amenukuliwa akisema:

خفِّفُوْا الدَّيْنَ فَإِنَّ فِيْ خِفَّةِ الدَّيْنِ زِيَادَةُ العُمْرِ
“Punguzeni deni kwani katika kupunguza deni kuna nyongeza ya umri.”8

NI WAKATI GANI MTU ANAPASWA KUCHUKUA MKOPO?
Hata hivyo isije ikaeleweka vibaya kwamba hadithi hizi zinamaanisha mtu asikope kabisa kwa vyovyote vile. Bali wakati wa shida waumini wanaruhusiwa kuchukuwa mikopo kwa mujibu wa sheria za kiislamu. Ma’asumin, kizazi cha Mtume (s.a.w.w.) walichukua mikopo katika zama zao. Lakini kilicho muhimu ni kufahamu vizuri ‘mazingira sahihi ya kuchukua mkopo’. Watu wengi huchukua mikopo ili waishi maisha ya starehe au ufujaji. Kadiri ambavyo mu’umini atakuwa hachungi adabu (nidhamu) za kiislamu siku zote ataishi maisha ya matatizo.
Imam Zainu’l ‘Ābidin (a.s.) katika dua yake namba 30 ya ‘Sahifatul Sajjadiyya’ anawafunza wafuasi wake njia bora ya kuishi na ili kujiepusha na deni na kuwa huru kutokana nayo:
Ewe Mola,
Mbariki Muhammad na watu wa nyumba yake, na uniepushe na ubadhirifu na kupitisha kiasi, na uniwezeshe kutumia kwa ukarimu na kwa kadiri na unielimishe njia bora ya matumizi na kwa upole wako unizuie kufanya ubadhirifu, na upitishe riziki yangu kwenye sababu za halali na uelekeze matumizi yangu kwenye milango ya kheri na uchukue kutoka kwangu mali ambayo yatanisababishia majivuno au kunielekeza kwenye uasi au kunifanya niwe dhalimu.
Ewe Mola,Nijaalie nipende kusuhubiana na maskini, na unisaidie kwa subira nzuri katika kusuhubiana nao na wakati wowote uchukuapo kutoka kwangu mazuri ya ulimwengu huu unaokwisha niweke kwenye hazina yenye kubaki.
Na ujalie ulichonipa na ukaniharakishia katika mapambo yake kuwa ni njia ya kufikia ujirani (ukuruba) wako na wasila wa kukufikia na sababu ya kupata pepo Yako.
Hakika Wewe ni Mwenye fadhila kubwa na Wewe ni Mkarimu.
Kwa uzuri kabisa Imam (a.s.) amewaeleza wafuasi wake kuhusu sababu ya hali zao kudhalilika kwa deni. Kila nukta katika dua hiyo hapo juu ni njia ya fahamu. [wasomaji wanaombwa kuviangalia vifungu hivi kwa makini ili kuzitambua sababu].
Kwa upande mwingine waumini walio matajiri wanahimizwa ipasavyo kuwapa mikopo ndugu zao na kuwasaidia wanapokuwa na shida. Kwa kweli baadhi ya riwaya zimeelezea wazi wazi kwamba thawabu anazozipata mtu kwa kukopesha ni zaidi ya thawabu anazo zipata kwa kutoa sadaka ingawa katika hali ya pili hakuna malipo yanayotarajiwa, ambapo katika hali ya kwanza mkopeshaji anatarajia kurudishiwa. Zifuatazo ni hadithi ambazo zinafaa tafakari:
1. Imamu Ja’far al-Sadiq (a.s.) amenukuliwa akisema:

مَكْتُوْبٌ عَلَى بَابِ الْجَنَّةِ: إِنَّ الصَّدّقَةَ بِلْعَشْرةِ وَ الْقَرْضُ الْوَاحِدُ بِثَمَانِيَةَ عَشرَة.
“(Maneno yafutayo) yameandikwa katika mlango wa pepo: ‘Hakika malipo ya sadaka hufikia mara 10, na mkopo mmoja malipo yake hufikia mara 18.”9
2. Imamu Ja’far al-Sadiq (a.s.) amenukuliwa akisema:

مَنْ أَقْرَضَ مًؤْمِنًا قَرْضًا ينْظر بِهِ مَيْسُوْرَهُ كَانَ مَالُهُ فِيْ زَكَاةٍ، وَكَانَ هُوَ فِيْ صَلاةٍ مِنَ الْمَلآئِكَةِ حَتَّى يُؤَدِّيْهِ
“Yeyote yule anayemkopesha mu’umin na akategemea wepesi wake kwa mkopo huo mali yake itakuwa ni yenye kuongezeka, na malaika watamuombea du’a mpaka atakapolipwa.”10

SHEIKH BAHAI NA DUA YA KUONDOLEWA DENI
Katika kitabu chake maarufu cha tafsiri ya hadithi arbaini (Arba’una Hadithan) Sheikh Baha’i anaelezea kisa cha ajabu kilicho mpata baada ya kunukuu hadithi ifatayo:
Sheikh Saduq Muhammad bin Babawayh al-Qummi amepokea hadithi yenye mlolongo wa wapokezi kutoka kwa Imam Baqir (a.s.) akaipokea kutoka kwa baba zake (a.s.) walioipokea kutoka kwa Amirul Mu’uminiin (a.s.) alisema:
“Nilimlalamikia Mtume (s.a.w.w.) kuhusu mkopo niliokuwa nadaiwa, naye aliniambia: “Ewe Ali, sema:
أَللَّهُمَّ أَغْنِنِيْ بِحَلَالِكَ عَنْ حَرَامِكَ وَ بِفَضْلِكَ عَمَّنْ سِوَاكَ
“Ewe Mola nitajirishe kwa halali Yako ili nisihitajie haramu Yako na kwa fadhila Zako ili nisimuhitajie asiyekuwa Wewe.”
Baada ya hapo Sheikh Baha’i anasema:-
Miaka mingi katika maisha yangu nimekuwa katika deni lililozidi 1500 mithqali ya dhahabu na wakopeshaji walikuwa wanazihitajia pesa zao. Hali ilifikia mahali pabaya kiasi cha kunitoa katika baadhi ya shughuli zangu na sikuwa na njia ya kuzilipa. Basi nilianza kujizoesha kusoma du’a hii iliyotajwa hapo juu na nikawa nikiirudia baada ya kila swala ya asubuhi na wakati mwingine baada ya swala nyinginezo. Matokeo yake ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliniwezesha kuyalipa hayo madeni kwa muda mfupi kwa njia nisizo zijua.11

WAJIBAT
Kuwaondolea watu madeni ni jambo muhimu kwa kuwa linahusiana na ukamilifu wao. Hatimaye, kifungu hiki cha du’a hujenga wajibat aina mbali mbali kwa watu mbali mbali:
• Wale ambao wana uwezo wa kuwaondolea watu aina yoyote ya deni wanatakiwa kujitahidi kufanya hivyo. Mkopeshaji wa pesa aliye mkarimu baada ya kujua uaminifu na kutokuwa na uwezo wa aliyekopeshwa anaweza kumsamehe (kiasi au lote) na hapo atakuwa kimatendo ameifasiri sehemu hii ya du’a.
• Wale ambao wana uwezo wa kujiondolea deni katika dalili yoyote waliyojifunga, lazima wajitahidi kufanya hivyo, vinginevyo kitakuwa ni kilio kisicho cha uaminifu kutoka kwao. Ni tamaa iliyoje kwa mwenye uwezo wakujilipia, lakini akawa anangojea kusaidiwa na huomba msaada kutoka nje.
• Jamii za kiislamu ambazo zina mfumo ulioungana zinaweza kulitatua tatizo hili zito la madeni katika dalili zake mbali mbali kwa kukusanya japo michango midogo kutoka kwa watu.

KUTAFAKARI KWA MAKINI
Du’a walizotufunza maimamu wetu (a.s.) zina mambo mazito lakini zinahitaji mtazamo mpana ili zieleweke. Katika sehemu nyingine tumejaribu kuonyesha kwa kiasi fulani undani wa yaliyomo katika kila kifungu cha hii du’a. Hapa pia tunadhani itakuwa bora kufanya hivyo.
Moja katika kanuni muhimu zilizoko kwenye ulimwengu wa lugha ni kwamba maneno yamewekwa kulingana na maana ya kiroho. Jambo hili ni kinyume na baadhi ya dhana kwamba maneno yamewekwa kwa mujibiu wa uhusiano ulioko wa kimaada na sio kwa maana ya kiroho.
Wanataka kusema kwa mfano neno ‘balance’ lina maana tu ya mizani ya kawaida tunayoijua (ya kupimia vitu) ambapo siyo sawa, Qur’an Tukufu pia inajulikana kama ‘Mizani’. Imam ‘Ali (a.s.) pia anajulikana kama Mizani kwa kuwa waumini wanahukumiwa na kupimwa kulingana na hali yake ya kiroho. Na wanachuoni wengi wanaamini ya kwamba maneno yamefungamanishwa na maana ya kiroho na sio lazima yawe yametokana na maana ya kimada. Kwa utafiti zaidi kuhusiana na jambo hili mtu anaweza kuangalia kwenye dibaji ya kitabu ‘al-Mizan’ cha Allama Tabatabai na kifungu cha kwanza cha kijitabu kiitwacho (Kukutana na Mwenyezi Mungu) cha Ayatullah Malik Tabrizi, mwanachuoni mashuhuri wa kishia. Nadhani sii vibaya tukinukuu kifungu kutoka kwenye kitabu hiki:
“Mbali na hayo kutokana na utafiti uliofanywa maneno yamefungamanishwa na maana ya (kiroho) kwa mfano neno mizani. Mizani linamaana chombo cha kupimia vitu vingine lakini kuwepo sehemu mbili za kupimia au viungo vingine vya kupimia haina uhusiano wowote na maana ya hilo neno. Kwa hiyo kutumia neno mizani kwa maana ya aina mbalimbali za mizani zilizovumbuliwa itakuwa ni sawa. Kwa hiyo neno mizani linakusudia chombo cha kupimia bila ya ufafanuzi wa chombo chenyewe au kile kinachopimwa. Siku hizi chombo kinachotumiwa kupimia joto na hali ya mwili, na hewa na hali ya damu na mwendo wa magari na aina nyingine ya vyombo vya kupimia zifikiazo mamia au maelfu zote ni kwa maana ya mizani. Na kutumia neno mizani kwa vyombo hivi itakuwa ni sawa kabisa. Na hivyo hivyo kuhusiana na maneno mengineyo kama vile njia (sirat) Mwanga (nur) malipo (thawab) Adhabu (‘iqab) na nyinginezo.12
Baada ya kujua jambo hili tujaribu kuangalia maana ya kiroho ya neno ‘deni’ ili tuweze kufumbua mifano mbali mbali inayohusiana nayo ambayo itatusaidia kujiepusha na kuwa huru kutokana nayo.
Kwa mujibu wa kitabu ‘Mu’ujam Maqayis al-Lugha’ ambacho ni kamusi ya lugha ya kiarabu, siri ya neno deni, lina maana ya ‘kujisalimisha’ (inqiyad). Maneno yote yaliyotokana na asili ya neno ( dayn) yaani (dal – ya - nun) yana maana ya kujisalimisha na utumwa kwa hivyo deni kwa njia fulani humfunga mkopaji na kumfanya akawa mtumwa mpaka atakapojikomboa kutokana nalo.
Maneno yafuatayo ya Imam ‘Ali (a.s.) yanafaa kuzingatiwa:
1. Imamu ‘Ali (a.s.) amenukuliwa akisema:

الدِّيْنُ رِقٌّ، الْقَضآءُ عِتْقٌ
“Deni ni utumwa na kulipa ni uhuru.”13
2. Imamu ‘Ali (a.s.) amenukuliwa akisema:

الدَّيْنُ أَحَدُ الرِّقّيْنِ
“Deni ni moja ya njia mbili za utumwa.”14
3. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amenukuliwa akisema:

لا تَزَالُ نَفْسُ الْمُؤْمِنِ مُعَلَّقّةً مَا كَانَ عَلَيْهِ دَيْنٌ
“Moyo wa mu’umin hubakia ukiwa umeangikwa muda akiwa na deni”15
Tunapochukua mkopo huwa kwa kweli tunajiingiza katika utumwa mpaka tutakapo jikomboa kwa kulipa. Na hivyo ndivyo ilivyo kuhusiana na aina ya nyongeza nyingine za deni.
Halikadhalika matendo yale ya ibada ambayo Mwenyezi Mungu huyatarajia kutoka kwa mwanadamu ni mfano wa ‘deni’. Kwa hiyo mwanadamu anatakiwa ajitahidi kuyatekeleza ilikwamba yasiwe mzigo juu ya mabega yao. Katika hadithi angavu ifuatayo, Salaat imechukuliwa kama nyongeza ya deni:
Imepokewa kutoka kwa Imam Ja’far al-Sadiq (a.s.) akisimulia kwamba, Luqman amesema:

إِذَا جآءَ وَقْتُ الصَّلاَةِ فَلاَ تُأَخِّرْهَا لِشَيءٍ، صَلِّهَا وَاسْتَرِحْ، فَإِنَّهَا ديْنٌ
“Wakati wa salat unapofika usiicheleweshe kwa jambo loloteو swali upumzike kwa kuwa Salaat ni deni.”
•    1. Āstāne Qudse Radawi, Sharh-o Tafsire Luhgāte Qur’an Bar Asāse Tafsir-e Namūne.
•    2. Sahifat al-Sajjādiyya, Du’a ya 30.
•    3. Muhammad al-Rayy Shahri, Mizān al-Hikma, j. 2, uk. 958.
•    4. Al-Shaykh al-Hurr al-’Āmili, Wasā’il al-Shi’a, j. 18, uk. 329.
•    5. Ibid, j. 18, uk. 328.
•    6. Marhūm Āmadi, Ghuraru’lHikam Wa Duraru ‘l Kalim, uk. 368.
•    7. al-Shaykh al-Hurr al-’Āmili, Wasā’il al-Shi’a, j. 2, uk. 324.
•    8. Muhammadi al-Rayy Shahri, Mizān al-Hikma, j. 2, uk. 958.
•    9. Āyatullāh Mamaqāni, Mir’ātu’l Kamāl, uk. 146.
•    10. al-Shaykh al-Hurr al-’Āmili, Wasā’il al-Shi’a, j.18, uk.330.
•    11. Shaykh Bahā’i, Arbu’ūna Hadithan, uk. 243.
•    12. Āyatullāh Maliki Tabrizi, Risaleye Liqa’ullah.
•    13. Marhūm Āmadi, Ghuraru’l Hikam wa Duraru’l Kalim, uk. 368.
•    14. Ibid.
•    15. al-Shaykh al-Hurr al-’Āmili, Wasā’il al-Shi’a, j.18, uk. 317.

MWISHO