DU’A YA MWEZI WA RAMADHANI 3
  • Kichwa: DU’A YA MWEZI WA RAMADHANI 3
  • mwandishi: al-islam.org
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 12:1:4 14-9-1403

DU’A YA MWEZI WA RAMADHANI (SEHEMU YA 3

اللّهُمَّ أَشْبِعْ كُلَّ جَائِعٍ

Ewe Mola Mshibishe Kila Mwenye Njaa

KUJIZOESHA NJAA
Moja ya falsafa za kufunga katika Mwezi wa Ramadhani ni kujizoesha njaa, na hivyo kufahamu hali ya wale ambao wana njaa na hawana uwezo wa kujitosheleza ipasavyo. Hadithi ifuatayo iliyonukuliwa na Faidh Maulā Kāshāni kutoka kwenye kitabu ‘Man lā yahdhuru’l Faqih’, inazungumzia jambo hili hili. Imām al-Sadiq (a.s.) katika hadithi iliyo sahihi, wakati anapoelezea falsafa ya kufunga anasema:-.
أَرَادَ اللّه عَزَّ و جلَّ أنْ يُسَوِّيَ بَيْنَ خَلْقِهِ و أَنْ يُّذِيْقَ الْغَنِيَّ نَيْلَ الْجُوْعِ وَالأَلَمِ لِيَرِقَ عَلى الضَّعِيْفِ وَيَرْحَمَ الْجَايِعَ
“[Allah (s.w.t.) alitaka kufanya usawa baina ya viumbe vyake kwa kumuonjesha tajiri njaa na uchungu ili amuonee huruma alie dhaifu na amhurumie mwenye njaa.]”1
YANAYO SABABISHA NJAA
Njaa ni tatizo lililo enea katika ulimwengu wa leo na kuna sababu mbalimbali ambazo zaweza kuainishwa katika (sababu) aina mbili: aina ya kwanza (ya sababu) zinamhusu mtu binafsi na aina ya pili (ya sababu) zinatokana na mambo ya nje. Chanzo cha sababu zinazomhumsu mtu mwenyewe, hutokana na muathiriwa mwenyewe, ambapo sababu za nje huanzia kwenye jamii na matukio asilia mengineyo. Aina hizi mbili za sababu hatuwezi kuzijadili kwa sasa kwa kuwa zitatutoa nje ya eneo la ufafanuzi huu mfupi.
Hata hivyo ni muhimu kujifunza mipaka ya sababu hizi ili tujitahidi kujiepusha nazo au kuziondolea mbali kwa urahisi. Suala hili ambalo liko chini ya mjadala, kama linavyoweza kuonekana kwa uwazi, vile vile linauhusiano wa karibu na umaskini.
Mwanzoni tulionyesha ukweli kwamba, kitu kinacho jitegemea husimama kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo ikiwa Mwenyezi Mungu hakutaka mtu apatwe au aathiriwe na msiba hakuna kitakacho mpata. Kanuni hii kama ilivyotajwa mwanzoni, sio tu inatajwa na ufunuo (wahyi), bali pia huthibitishwa na akili.
HAKIKISHO LA KUPATIKANA KWA RIZIKI
Baada ya kujua ukweli huu ulio muhimu tuziangalie aya hizi za Qur’an zinavyo tuambia:-
1. (Sura ya A’raf - 7:96)
وَلَوْ أَنَّ أَهْلَ الْقُرَىٰ آمَنُوا وَاتَّقَوْا لَفَتَحْنَا عَلَيْهِمْ بَرَكَاتٍ مِنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ وَلَٰكِنْ كَذَّبُوا فَأَخَذْنَاهُمْ بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ
“Na lau watu wa miji wangeliamini nakumcha Mwenyezi Mungu tungeliwafungulia baraka kutoka mbinguni na ardhini…”
2. (Sura Talaq - 65: 2-3)
وَمَنْ يَتَّقِ اللَّهَ يَجْعَلْ لَهُ مَخْرَجًا.  وَيَرْزُقْهُ مِنْ حَيْثُ لَا يَحْتَسِبُ ۚ وَمَنْ يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّهِ فَهُوَ حَسْبُهُ ۚ إِنَّ اللَّهَ بَالِغُ أَمْرِهِ ۚ قَدْ جَعَلَ اللَّهُ لِكُلِّ شَيْءٍ قَدْرًا.
“Na anaye mcha Mwenyezi Mungu Atampatia njia ya kutokea kwenye matatizo na Atamruzuku kutoka asipo patarajia.”
3. (Sura ya Nuh – 71:10-12)
فَقُلْتُ اسْتَغْفِرُوا رَبَّكُمْ إِنَّهُ كَانَ غَفَّارًا * يُرْسِلِ السَّمَاءَ عَلَيْكُمْ مِدْرَارًا .وَيُمْدِدْكُمْ بِأَمْوَالٍ وَبَنِينَ وَيَجْعَلْ لَكُمْ جَنَّاتٍ وَيَجْعَلْ لَكُمْ أَنْهَارًا .
“Kisha nilisema: muombeni msamaha Mola wenu [kwani] kwa hakika Yeye ni Mwingi wa kusamehe, Atawateremshia mvua kwa wingi na Atawapa mali na watoto na Atawatengenezea mabustani na Atawatengenezea mito.”
Aya hizi zinamhakikishia mwanaadamu njia bora ya kumhakikishia riziki yake na kumuepusha na janga la njaa. Na lau malezi ya uchamungu, na kumuomba Mwenyezi Mungu msamaha yangelizingatiwa ipasavyo, njaa haingekuwa ni shida isipokuwa ile ya mitihani ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.); (Sura ya Baqarah – 2:155)
وَلَنَبْلُوَنَّكُمْ بِشَيْءٍ مِنَ الْخَوْفِ وَالْجُوعِ وَنَقْصٍ مِنَ الْأَمْوَالِ وَالْأَنْفُسِ وَالثَّمَرَاتِ ۗ وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ
“Na bila shaka tutawajaribu na kitu katika khofu na njaa.2
Vile vile tuna hadithi za kutosha zinazomfahamisha mwenye njaa na mwenye shida pamoja na wale ambao wangependa kueneza malezi ya utamaduni wa kujitegemea kuhusu njia za upatikanaji wa riziki. Ifuatayo ni baadhi ya mifano:
UONGEZEKANAJI WA RIZIKI
1. Imam al-Sadiq (a.s.) anasema:
إِنَّ الْبِرَّ يَزِيْدُ فِي الرِّزْقِ
“Hakika wema huzidisha riziki.”3
2. Na kwenye hadithi nyingine pia anasema:
حُسْنُ الْخُلْقِ يَزِيْدُ فِي الرِّزْقِ
“Tabia njema huzidisha riziki.”4
3. Mtume (s.a.w.w.) anasema:
دُمْ عَلى الطَّهَارَةِ يُوَسَّعُ عَلَيْكَ فِي الرِّزْقِ
“Dumisha Tohara (udhu) na riziki yako itaongezwa.”5
Hivyo basi jukumu la ambao wanaoisoma sehemu hii ya du’a kwa ikhlas mbali na kuwasaidia wengine kiukweli, wanapaswa kuwafahamisha yale ambayo moja kwa moja husababisha njaa.
Mwandishi mwenye kuheshimiwa sana wa kitabu ‘Mir’atul Kamal’, marehemu Ayatullah Sheikh Mamaqani ameandika kurasa sita zilizojaa sababu ambazo husababisha umaskini na kuzuia riziki ya mtu. Vile vile, rejea zimetajwa katika ufafanuzi wa toleo lijalo la utungo wa juzuu hizi tatu. Na kwa wale ambao wangependa wangeweza kuangalia kwenye kurasa 569-583. Hata hivyo, hapa tungetaka wenyewe tujitosheleze kwa kutaja baadhi tu ya hizo.
SABABU ZINAZOZUIA RIZIKI
1. Kuwa na tamaa.
2. Kulala kati ya Magharibi na Ishaa.
3. Kulala kati ya alfajiri na kuchomoza kwa jua.
4. Kuvunja undugu.
5. Kulala uchi kwa muda mrefu.
6. Mtu kuwalaani watoto wake. (huwazuia watoto kupata riziki)
7. Kula katika hali ya kulala.
8. Kuacha kuwaombea wazazi dua.
9. Kusengenya.
10. Isrāfu (kula kupita kiasi, matumizi ya fujo, nk..)
11. Kutafuta makosa ya watu.
12. Kula ukitembea.
13. Kukojoa au kukutana na mkeo ukielekea kibla.
14. Kukojoa kwenye maji.
15. Kucheka kupita kiasi hasa karibu na makaburi au kwenye mkusanyiko wa wasomi (maulamaa).
16. Kutomkopesha pesa anayehitaji.
17. Hali ya kuonyesha umasikini mbele ya tajiri.
18. Kulala kupita kiasi.
Ayatullah Mamaqani ametaja karibu sababu 175 kwenye kitabu chake. Kwa hivyo ni muhimu kwetu kueneza utamaduni wa taqwā (ucha Mungu) kwenye jamii zile masikini zinazoweza kukubali mafunzo ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.). Taqwā katika kila hali ya maisha inamfanya mtu kupata furaha hapa ulimwenguni na kesho akhera.
KUTAFAKARI KWA MAKINI: MAANA NYINGINE YA NENO CHAKULA
Chakula katika istilahi ya Qur’an siku zote halimaanishi chakula cha kimwili, bali kuna madokezo ya wazi yaliyo fanywa na Maimamu wa Ahlul-Bayt (a.s.) ambao wanawakilisha wafasir wenye ujuzi zaidi wa Qur’an, kwamba ‘ta’ām’ (chakula) katika lugha ya Qur’an wakati mwingine linamaanisha elimu. Kwa maana ya chakula cha roho, na sio tu kile cha mwili. Aya ifuatayo ni mfano:
Katika sura ya ‘Abasa (80:24), Allah (s.w.t.) anasema:
فَلْيَنْظُرِ الْإِنْسَانُ إِلَىٰ طَعَامِهِ
“Basi mwanadamu na aangalie chakula chake.”
Chini ya aya hii tukufu mfasiri wa kishia aitwae Sayyid Hashim Bahrani katika kitabu chake ‘Tafsir al-Burhān’ ananukuu hadithi iliyosimuliwa na al-Kāfi [Jz. 1, uk 39, tr. 8] kutoka kwa Imam al-Sadiq (a.s.) kama ifuatavyo:- “ Zaid al Shaham alimwuliza Imam al-Sadiq (a.s.) ‘chakula cha mwanadamu’6 (kama ilivyotajwa) katika aya liliyopita linamaanisha nini Imam (a.s.) alimjibu:
عِلْمُهُ الَّذِيْ يَأْخُذُهُ عَمَّنْ يَأْخُذُهُ
“Elimu yake anayoipata, anaipata kutoka kwa nani?”7
Kwa hiyo, kama njaa inamaanisha ukosefu wa elimu bila ya shaka wengi wetu tuna njaa. Mwanachuoni ambaye ametumia miaka kumi katika kutafuta elimu, bado atamuomba Mwenyezi Mungu amzidishie zaidi, na zaidi kwa kuwa kutafuta elimu hakuna mwisho. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akimwomba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amzidishie elimu kwa dua hii aliyomfundisha Mwenyezi Mungu kwenye Qur’an (20:114):
فَتَعَالَى اللَّهُ الْمَلِكُ الْحَقُّ ۗ وَلَا تَعْجَلْ بِالْقُرْآنِ مِنْ قَبْلِ أَنْ يُقْضَىٰ إِلَيْكَ وَحْيُهُ ۖ وَقُلْ رَبِّ زِدْنِي عِلْمًا
“Na useme Mola wangu nizidishie elimu”.
Na pia alikuwa akisema:
مَاعَرَفْنَاكَ حَقَّ مَعْرِفَتِكَ
“Hatujakujua haki ya kukujua”. (yaani, hatujakujua kama ipasavyo kukujua)
Ufumbuzi wa njaa hii pia ni taqwā (ucha Mungu). Aya mbili zifuatazo zinathibitisha hoja hii:
1. [Suratu’l Baqara - 2:282]
وَاتَّقُوا اللَّهَ ۖ وَيُعَلِّمُكُمُ اللَّهُ ۗ
“…Mugopeni Allah, na Allah atakuelemisheni…”
2. [Suratu’l Anfal - 8:29]
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنْ تَتَّقُوا اللَّهَ يَجْعَلْ لَكُمْ فُرْقَانًا وَيُكَفِّرْ عَنْكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ۗ وَاللَّهُ ذُو الْفَضْلِ الْعَظِيمِ
“Enyi mlio amini mkimcha Mwenyezi Mungu atawawezesheni kujua haki na batili…..”
NJAA (KWA) NA MTAZAMO WA KI-’IRFANI
Marehemu mwanachuoni wa mambo ya ‘irfani na pia mwalimu wa Imam Khomeini (r.a.) Ayatullah Malik Tabrizi katika kitabu chake “al- Murāqabāt” anaelezea faida nyingi za njaa kwa msafiri wa kiroho kwa kutaja baadhi ya hadithi zifutazo:
أَفْضَلُكُمْ عِنْدَ اللّهِ مَنْزِلَةً يَوْمَ الْقِيَامَةِ أَطْوَلَكُمْ جُوْعًا و تَفَكُّرًا فِي اللّهِ سُبْحَانَهُ
“Mbora wenu kwa cheo mbele ya Mwenyezi Mungu siku ya kiama ni yule akaaye na njaa kwa muda mrefu na kutafakari kumhusu Mwenyezi Mungu.(s.w.t.)8”.
2. Imepokewa kwamba Mtume (s.a.w.w.) alimuambia Usama:
إن اسْتَطَعْتَ أَنْ يَأْتِيَكَ مَلَكُ الْمَوتَ وَبَطْنُكَ جَايِعٌ وَكَبِدُكَ ظَمْآن فَافْعَلْ، فَإِنَّكَ تُدْرِكَ بِذَلِكَ أَشْرَفَ الْمَنَازِلِ وَتَحُلُّ مَعَ النَّبِيِّيْنَ وَتَفْرَحُ بِقُدُوْمِ رُوْحِكَ الْمَلآئِكَةُ وَيُصَلِّ عَلَيْكَ الْجَبَّارُ
"Lau kama utaweza atakapokujia Malaika wa mauti akukute katika hali ya njaa na kiu basi fanya hivyo kwa kuwa utapata cheo kitukufu mno na utakuwa pamoja na Mitume na watafurahi Malaika kwa roho yako kuwasili na Mwenyezi Mungu atakuteremshia rehema."9
3. Imepokewa pia kwamba Mtume (s.a.w.w.) amesema:
أَجِيْعُوْا أكْبَادَكُمْ و أَعْرَوا أجْسَادَكُمْ، لَعَلَّ قُلُوْبُكُمْ تَرَي اللّه عَزَّ وَ جَلَّ
“Ziwekeni tumbo zenu katika hali ya njaa na miili yenu muiweke uchi (mjiepushe na mavazi ya ufakhari) kwa kuwa huenda nyoyo zenu zitamwona Mwenyezi Mungu aliye Mtukufu.”10
4. Vile vile Mtume (s.a.w.w.) anasema:
مَنْ أَجَاعَ بَطْنَهُ عَظُمَتْ فِكْرَتُهُ
“Anaye liweka tumbo lake na njaa fikra na akili yake itapanuka”.11
5. Mtume (s.a.w.w.) wakati wa Mi’iraji (alipopelekwa mbinguni alimwuliza Mwenyezi Mungu (s.w.t.):
يَارَبِّ مَا مِيْرَاثُ الْجوْعِ
“Ewe Mola wangu njaa inarithisha nini (ina faida gani)”? Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akamjibu.
الْحِكْمَةُ وَ حِفْظُ الْقَلْبِ...
“Hurithisha hekima na hifadhi ya moyo…”12
Kwa hiyo njaa ina jukumu la msingi la kufanya katika kumjenga mwanadamu kiroho. Hata hivyo, hiyo haiwezi ikachukuliwa kumaanisha kwamba ‘njaa’ inapendekezwa kwa wote na kila kitu, pamoja na wale wasioweza kuvumilia njaa, ambao huenda wakaugua au wakafa.
Tunapokiangalia kitabu cha fiqhi13 ambacho kipo katika matumizi yetu, tutaona kwamba moja katika adabu za matumizi ya chakula ni kula mara mbili kwa siku:
Sehemu ya mwanzo ya mchana na nyingine sehemu ya mwanzo ya usiku. Mwanya baina ya milo hii miwili lazima iachwe bila kujazwa na chakula cha aina yoyote ile. Wengi wetu wanao uwezo wa kuvumilia chakula hicho, lakini nguvu za matamanio ya nafsi hayaturuhusu kufanya hivyo.
Hata hivyo, kuna watu ambao wanahitaji chakula zaidi, na hivyo chakula kama hicho itakuwa hawatosheki nacho. Hata hivyo, hii isimaanishe kwamba hawashikamani na dini au sio wacha Mungu. Ni kwa kula chakula (kama hicho) ndipo wanaweza kutekeleza ibada zao na kufanya matendo yaliyo bora na kujitahidi katika maisha yao ipasavyo kwa mujibu wa maelekezo ya sheria (dini) ya Mungu.
Hutokea katika maisha ya mtu aliyeitakasa nafsi yake na amepata mkuruba wa Allah, ambapo ana uwezo wa kuvumilia njaa sio tu kwa nyakati fupi bali hata kwa muda usio wa kawaida. Bila ya shaka hoja hii laonekana ya kipuuzi katika lugha ya sayansi na majaribio (ya kimaabara), lakini wajuzi wa elimu ya ndani ya ki-Islam wanamini kwamba wakati moyo wa mtu unaimarika, mambo kama hayo ni ya kuwezekana.
Aviccena (Ibn Sina) mwanafilosofia mkubwa wa ki-Shi’a, ambaye vile vile anajulikana kama Sayyid al-’Uqalā’ (kiongozi wa wasomi) katika kitabu chake kikubwa kiitwacho “Ishārāt wa al-Tanbihāt” anasema:
إِذَا بَلَغَكَ اَنَّ عَارِفًا أَمْسَكَ عَنِ القُوْت الْمَرْزوء لَهُ مَدَّةً غَيْرَ مُعْتَادَةٍ فاسْجَحْ بِالتَّصْدِيْقِ وَ اعْتَبِرْ ذَلِكَ مِنْ مَذَاهِبِ الطّبِيْعَةِ الْمَشْهُوْرَة
“Utakapojua kwamba Arif amejizuia kula kwa muda usio wa kawaida basi uamini kwa kweli na ujue ya kwamba hilo ni katika misingi maarufu ya kimaumbile.”14
Kwa hiyo, njaa kwa wale ambao hawana ukosefu wa riziki na wana uwezo wa kuivumilia njaa hiyo, inapendekezwa sana kwa sababu zilizotajwa hapo juu.
•    1. Mawlā Fayd Kāshāni, al-Mahajjat al-Baydā, j. 2, uk. 124.
•    2. Qur’an Tukufu, 2:155.
•    3. Muhammadi Rayy Shahri, Mizān al-Hikma, j. 2.
•    4. Muhammadi Rayy Shahri, Mizān al-Hikma, j. 2.
•    5. Ibid.
•    6. Tafsiri hii ni yenye kufaa na sahihi, ukweli wa mwanadamu ni roho yake. Kwa umuhimu basi, chakula chake kitakuwa sawa na roho yake. Na chakula hiki hakiwezi kuwa lolote bali ni elimu
•    7. Al-Sayyid Hāshim Bahrani, al-Burhān fi Tafsiri’l Qur’an, uk. 214.
•    8. Āyatullāh Maliki Tabrizi, al-Murāqibāt, uk.154 – toleo jipya.
•    9. Āyatullāh Maliki Tabrizi, al-Murāqibāt, uk.154 – toleo jipya.
•    10. Ibid.
•    11. Ibid, uk. 156.
•    12. Āyatullāh Sa’ādat Parwar, Sirru’l Isrā’, j. 1, uk. 13.
•    13. Āyatullah al-’Uzmā al-Sayyid ‘Alial-Sistāni, Tawdhihu’l Masā’il, uk.495.
•    14. Shaykh al-Ra’is Ibn Sinā, al-Ishārāt wa’l-Tanbihāt, j. 4, uk. 111.

MWISHO