KIFO MSALABANI
  • Kichwa: KIFO MSALABANI
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 18:53:58 1-9-1403

KIFO MSALABANI

Mtume Muhammad ndiye aliyekuja kumtukuza Yesu. Aliyapinga madai ya Mayahudi kumshutumu Maryam na kumshutumu Yesu, na akauhakikisha ulimwengu kuwa Yesu ni mwana wa halali, ni Nabii mtukufu aliyetumwa kwa Wana wa Israili, wala si maluuni kama walivyodai Mayahudi, na wala si mungu wa bandia wa kishirikina, kama walivyomfanya Wakristo bila ya wenyewe kutambua nini walitendalo. Kwa watu wanaoamini kuwa Adam alikuwa hana baba wala mama kwa nini ikawa ni vigumu kuamini kuwa Yesu alikuwa hana baba? Yohana Mbatizaji anasema: Mungu aweza katika mawe haya kumwinulia Ibrahimu watoto.
Mathayo 3.9

Je, Mungu awezaye kuinua watoto katika mawe, kama alivyomuumba Adam kutokana na udongo, atashindwa kumzalisha mwanamke bila ya mume? Mtume Muhammad aliwahakikishia maadui wa Kiyahudi kuwa Yesu ndiye Kristo, ndiye Masihi ambaye amebashiriwa katika maandiko yao wenyewe. Aliwakanya Mayahudi walipodai kuwa Yesu amelaanika kwa sababu wao waliweza kumuua kwa kumbandika msalabani. Qur'ani imesema: Hali hawakumuua wala hawakumsalibu, bali walifananishiwa. Na kwa hakika wale waliokhitilafiana katika haya wamo katika shaka nayo. Wao hawana yakini juu yake, isipokuwa wanafuata dhana tu. Na hawakumuua kwa yakini.
(Qur'ani) An Nisaa 4.157

Utafiti wa ilimu za kisasa katika masomo ya Biblia unathibitisha huu ukweli wa Qur'ani. Yajuulikana kuwa zipo Injili nyengine zenye maelezo mbali juu ya mateso ya Masihi yanayokhitalifiana na ya hizi Injili nne zilizokubaliwa na Kanisa. Katika miaka ya karibuni mwangaza mpya umepatikana kutufahmisha nini khasa zilikuwa imani za wale Wakristo wa mwanzo. Zimepatikana nyaraka za zamani sana ambazo ziko katika jumba la kuhifadhi nyaraka huko Istambul, Uturuki. Aliyegundua ni Dr. Samuel Stern wa Chuo Kikuu cha Oxford. Wale Wakristo wa kwanza, ambao wakiitwa Wanasoria au Wanazaria (ambayo yanaelekana na jina litumiwalo katika Qur'ani kuwaita Wakristo "Wanasara") hapo awali ndio waliokuwa wengi na wenye nguvu. Hao Wanasara wakidai kuwa wao wamezalikana na wanafunzi wake Yesu wa kwanza kabisa.

Wakaja wakapambana na Wakristo wamfuatao Mt Paulo. Hao Wanasara wakimuamini Yesu kuwa ni Nabii mtukufu na mwanaadamu mwema mwenye haki. Wakamshutumu Paulo kuwa amezua kwa kutumbukiza mila za Kirumi badala ya mafunzo ya asli ya Yesu, na kumsingizia Yesu kuwa ni Mungu. Walikataa kusherehekea Krismasi kwa kuwa waliona hiyo ni sikukuu ya kikafiri ya kipagani. Hadithi ya mateso ya Yesu iliyomo katika hizo nyaraka za kale ni kuwa Yuda aliwakhadaa Mayahudi kwa kuwaletea mtu mwingine badala ya Yesu. Huyu mtu mwingine alikataa kata-kata mbele ya Hirodi (Mfalme wa Mayahudi) na Pilato (Liwali wa Kirumi) hayo mashtaka kuwa yeye anadai Umasihi. Kwa mujibu wa hadithi hii ilikuwa Hirodi, wala si Pilato (kama isemavyo Biblia) ndiye aliyechukua maji akanawa mikono kuikosha na dhambi ya damu yake, kudhihirisha kuwa yeye hakumwona na kosa. Tena Hirodi akamfungia ndani huyo aliyedhaniwa kuwa ni Yesu usiku kucha; lakini asubuhi yake alishikwa na Mayahudi wakamtesa na mwishoe wakamsalibu.

Hadithi hii ya kusalibiwa walau inatupa sura njema kuliko ile iliomo katika Biblia inayomueleza Yesu kuwa aliyayatika kama asiye na imani ya kutosha, pale alipokuwa msalabani. Kwani katika Injili ziliomo katika Biblia, yaani zile walizozikubali wakuu wa Kanisa, yasimuliwa kuwa Yesu alilia: "Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?" Kwa mtu wa hivi hivi, mchache wa imani, aweza kusamehewa akifanya hivyo, lakini hayamuelekei hayo mwenye kuongoza watu, seuze Nabii, seuze Mwana wa Mungu, kama tunavyoambiwa. Tena Mwana Mungu wenyewe ambaye amekuja makusudi huku duniani kwa kazi hiyo ya kutundikwa msalabani ili waokoke viumbe vyake. Ikiwa aliyesalibiwa ni Yesu, na Yesu ni Mungu, hadithi hiyo haingii akilini. Upton Sinclair anaandika katika kitabu chake A Personal Jesus (Yesu Mtu): "Waona kuwa wale wanaosimulia hadithi hii hawawezi kukata shauri katika akili zao kuwa Yesu ni Mungu au ni mtu. Kwa hakika ni tatizo zito mara unapokubali kuwa yamkinika Mwenyezi Mungu awe na sura ya mtu na ateremke duniani. Je, pale anapokuwa mtu anakuwa Yeye ni mtu au bado ni Mungu? Na vipi anaweza kusalitiwa, na hali Yeye anajua kuwa anakwenda kusalitiwa? Masimulizi hayo hayatubainishii waziwazi, kwani kwa msingi wa mambo, yote hayo ni muhali, hayaingii akilini, na hatuwezi kupata jawabu, wala hayumkini kuweza kuyafikiri vilivyo mambo namna hii.

Ikiwa Yesu ni Mungu, basi anajua mbele kila kitu. Lakini kwa hivyo yote hayo ni upuuzi mtupu kwake; Yeye anakuwa kama mwenye kucheza mchezo wa kuigiza sinema, na bila ya shaka mchezo kama huo ni wa kumnyon'gonyesha Mwenyezi Mungu Mjuzi wa kila kitu. Je, anafanya haya kufurahisha watoto wadogo? Ikiwa ni hivyo, kwa nini hawasaidiwi watoto wakue akili zao waweze kuukabili vilivyo ukweli wa mambo? Upande wa pili, ikiwa yeye ni mtu, na ana akili ya kiutu, basi hajui hakika ya mambo, hana ile raha ya kujua kila kitu, ambayo ni sifa ya Kiungu. Hizo hadithi za kitoto zatutaka sisi tuamini yote mawili kwa wakati mmoja; lakini ni wazi kabisa, kuwa mtu hawezi kujua kitu na wakati huo huo akawa anapapasa- papasa kama asiyeona baraabara, kama tutendavyo sisi katika maisha yetu yote."

Kitandawili kinacho watatanisha wasomaji wenye akili zao kama Upton Sinclair kinatatuliwa na vile wale Wanasara wa kale wanavyoeleza kile kisa cha kusalibiwa. Kwa maelezo yao Yesu anatakasika na tuhuma ya woga na ukosefu wa imani ya rehema ya Mwenyezi Mung, kama alivyoonyesha yule mtu aliyesalibiwa. Hali kadhaalika tunaweza kuelewa kwa nini wanafunzi wa Yesu aliowateuwa mwenyewe walivyomkana na sote tukaona wamefanya kitendo cha woga na ukhaini. Wakati ule wa shida vipi wafuasi wake wote wamkatae? Wangapi waliokhiari kufa kwa ajili ya waja wa kawaida kama sisi tuliojaa dhambi, itakuwa wanafunzi aliowateuwa mwenyewe Yesu kuwa ndio watakao eneza mafunzo yake wamtupilie mbali kama tambara bovu mara baada ya kuingia matesoni? Na miongoni mwa watu hao awemo Petro ambaye Yesu alimwita mwamba ambaye juu yake atajenga Kanisa lake? Kudai kuwa yote hayo ni kutimiza bishara ziliomo katika Agano la Kale ni kutumwagia mchanga wa macho. Lakini walivyoeleza wale Manasara wa mwanzo yanaingia sana akilini. Ni kweli yule aliyekamatwa na kubandikwa msalabani akayayatika kama mtu asiye na imani si Yesu, siye Bwana wao, siye mwongozi wao, siye Mwalimu wao. Ni kweli hawamjui mtu yule. Yule mtu waliyemsaliti, waliyemkataa, waliyemwacha ateseke na auliwe bila ya kunyanyua kidole kumtetea, wala kutoa kauli kumsemea wala dua kumwombea, ni kweli hawamjui.

Injili ya Barnaba ambayo Kanisa limeikataa inaeleza kuwa yule aliyesalibiwa ni Yuda; na madhehebu ya Kikristo ya kale iitwayo Basilidoni ikiamini kuwa ni Simoni Mkirene ndiye aliyesalibiwa, si Yesu. Kwa mujibu wa Injili tatu za mwanzo, yaani Mathayo, Marko na Luka, ni huyo Simoni ndiye aliyebeba msalaba. Ni Injili ya Yohana tu ndiyo inayotwambia kwamba ni Yesu mwenyewe aliyebeba msalaba wake. Jambo hili lafaa kuzingatiwa na kutiwa maanani. Wataalamu wengine, wanaotegemeza utafiti wao juu ya hizi hizi Injili nne zilizokubaliwa na Kanisa na kutiwa katika Biblia, wana mawazo mengine juu ya hichi kisa cha kusalibiwa. Mmoja wao ni Dr. Hugh Schonfield, ambaye ametoa maoni yake katika kitabu chake chenye kuzua majadiliano mengi. Kitabu hicho kinaitwa The Passover Plot (Njama ya Pasaka). Yeye anadai kuwa ni Yesu kweli aliyetundikwa msalabani, lakini hakufa hapo msalabani; alionekana tu kama kwamba kafa, kwa kunywa dawa ya kuzimia inayoelezwa katika Injili ya Mathayo kuwa ni siki.

Basi tangu saa sita palikuwa na giza juu ya nchi yote hata saa tisa. Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Na baadhi yao waliohudhuria, waliposikia, walisema, Huyu anamwita Eliya. Mara mmoja wao akaenda mbio, akatwaa sifongo, akaijaza siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha. Wale wengine wakasema, Acha; na tuone kama Eliya anakuja kumwokoa. Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake.
Mathayo 27.45-50

Hayo ni maelezo ya Injili ya Mathayo. Lakini Schonfield anadai ya kuwa hiyo ilikuwa ni hila tu kumwokoa Yesu asife msalabani. Alipewa hiyo dawa ili aonekane kama aliyekufa. Kwa mujibu wa Injili Yesu alibakia hapo msalabani kwa muda wa saa tatu tu, ilhali ilikuwa ni ada mtu kubaki ananing'inia msalabani kwa siku kadhaa wa kadhaa yupo baina ya uhai na mauti akisononeka. Tena kwa kufuata mpango maalumu uliopangwa, alitokea mfuasi wake Yesu, tajiri mmoja aitwaye Yusufu wa Arimathaya akamwendea Liwali wa Kirumi, Pilato, akamwomba ampe yeye maiti akamzike. Akapewa.

Mtaalamu wa ilimu ya binaadamu (Anthropology) Michael J. Harner wa Chuo Kikuu cha California katika kuthibitisha hayo alisema kuwa ni kweli ilikuwa ikifanywa mvinyo kutokana na mmea wa tunguje mwitu ambayo ikitumiwa kumfanya mtu kuzimia na kuonekana kama kafa ili kumwokoa na kifo cha kusononeka msalabani. Huyo Yusufu tena alimpeleka huyo aliyeonekana kama maiti kwenye pango alilolichonga kama chumba kwenye bustani yake liwe ati ni kaburi. Na jiwe kubwa likawekwa mlangoni. Hakuzikwa katika kaburi liliochimbwa chini kwenye ardhi na kufukiwa kwa udongo.

MWISHO