JE YAHOVA NA ALLAH NI MIUNGU TOFAUTI
  • Kichwa: JE YAHOVA NA ALLAH NI MIUNGU TOFAUTI
  • mwandishi: Muhibu Said
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 19:14:19 6-10-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

JE YAHOVA NA ALLAH NI MIUNGU TOFAUTI

" Biblia yatofautisha dini ya Yehova na dini ya mungu-mtu
" Ibada za kipagani ni chukizo na najisi kwa Yehova
Na Muhibu Said
KATIKA toleo lililopita tuliona jinsi Biblia tukufu inavyozipambanua dini za Yehova na dini ya Kikristo mungu-mtu ya kwa kudhihirisha uhusiano wa ibada za Kikristo na ibada za dini ya kipagani, ambazo tuliona jinsi Yehova anavyowataka wanadamu wajiepushe nazo mbali kabisa. Baadhi ya ibada hizo za kipagani zilizomo leo katika Ukristo, tuliona kuwa ni pamoja na kuua wana kama kafara ya dhambi, kujishughulisha na pepo na kuwaomba wafu. Tukaona kwamba Wakristo kuzitenda ibada hizo ni uthibitisho wa wazi kuwa hawamwabudu Yehova, Mungu wa Nabii Ibrahim, Ismaili, Isaka, Yakobo, Musa, Yesu, Muhammad na Mitume na Manabii wengine wote aliowatuma duniani. Kwa kuwa (ibada hizo) hazitokani na yeye (Yehova). Endelea.

Kuabudu Sanamu
Hii pia ni ibada ya msingi katika dini ya Kikristo ambapo sala za waumini wake (Wakristo) huwa hazitimii bila ya kuomba na kuabudu sanamu. Masanamu yanayohusishwa zaidi katika ibada hizo ni pamoja na sanamu la mungu-mtu Yesu wa Kikristo akiwa amebebwa na mama yake na kwenye sanamu lingine akiwa amekufa msalabani, sanamu la "Bikira Maria", sanamu la malaika na masanamu mengine mengi ya watakatifu wa Kikristo waliokufa! Kama maandiko ya Biblia tukufu yafundishavyo, ibada hii (ya sanamu) ifanywayo na Wakristo, kiasili imetokana na watu wa mataifa (wapagani). Uthibitisho wa hilo tunaupata katika maandiko yafuatayo: "Bali walijichanganya na mataifa, wakajifunza matendo yao. Wakazitumikia sanamu zao, Nazo zikawa mtego kwao". (Zaburi 106:35-36).

Kwa uchache, maandiko hayo juu yanathibitisha wazi kuwa waasisi na wahusika wakuu wa ibada hiyo (ya sanamu) ni watu wa mataifa, yaani wapagani. Sambamba na ukweli huo, Biblia haikuacha pia kubainisha jinsi Yehova alivyowakemea wanadamu tangu mapema kujaribu kuchonga (kufanya) na kuabudu sanamu, kama ifuatavyo:
"Usijifanyie sanamu ya kuchonga, mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni, au kilicho chini duniani. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi BWANA, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu, nawapatiliza wana uovu wa baba zao; hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao". (Kumbukumbu la Torati 5:8-9).

Katika maandiko hayo juu, tunaona wazi jinsi Yehova anavyowakataza wanadamu kuchonga na kuabudu sanamu ya aina yoyote. Makemeo hayo juu ya Yehova ndio yanayosimamisha amri yake kuu ya pili kati ya amri zake zile kuu kumi ndani ya Biblia tukufu alizowapa wanadamu.

Ingawa alidhamiria kumhubiri Mungu mtu wa dini yake ya Kikristo mwenye desturi na sifa za miungu-watu ya wapagani, lakini Bwana Paulo hakuikubali ibada ya sanamu (tazama Wagalatia 5:19). Hata hivyo, kwa kule kuwawekea Wakristo msingi wa kuzipenda na kuzifuata kwa moyo mkunjufu, imani na ibada za kipagani kamwe hawezi kukwepa dhima kutokana na leo ibada hiyo (ya sanamu) kujaa tele na kujizika mizizi katika dini yake ya Kikristo. Kwa ujumla, ibada hiyo (sanamu) iliyomo katika dini ya Kikristo ni ibada inayotokana na dini ya kipagani ambayo (kama tulivyoona hapo awali) Yehova amewakataza vikali wanadamu kuitenda.

Kwa hali hiyo, ni dhahiri kuwa Wakristo kutenda ibada hiyo ni uthibitisho wa wazi kwamba hawamwabudu Yehova, Mungu wa Nabii Ibrahimu, Ismaili, Isaka, Yakobo, Musa, Yesu, Muhammad na Mitume na Manabii wake wengine wote aliowatuma duniani (a.s.), kwa kuwa ibada hiyo haitokani na yeye (Yehova).

Ubatizo
Hii pia ni ibada kuu na ya msingi katika dini ya Kikristo ambayo hata watoto wachanga nao huusishwa nayo pia! Kwa ujumla wake, ibada hii (ya ubatizo) imeshamiri sana katika Ukristo. Hata hivyo, pamoja na kuwemo katika orodha ya ibada za Kikristo, lakini kwa mujibu wa maelezo ya Biblia tukufu, asili ya ibada hiyo (ya ubatizo) imetokana na dini ya kipagani. Uthibitisho wa hayo tunaupata katika maelezo ya Biblia yafuatayo:

"Ibada ya (ubatizo) kutosa mwili majini ni mfano wa utakaso au wakujitengeneza upya. Ibada kama hiyo ilijulikana na kutendeka katika dini za kale za kipagani na dini ya Kiyahudi pia (kama ubatizo wa waongofu Mdo 2:10; Waesseni)'. (Tazama Biblia ya Wakatoliki, Imprimatur M. Mihayo Archbishop of Tabora, February, 1967, kwenye maelezo ya Mathayo 3:6 uk. 879). Maelezo hayo ya Biblia hapo juu yanathibitisha wazi kwamba ibada hiyo ya ubatizo inatokana na dini za kale za kipagani na kamwe haitokani na dini ya Yehova.

Nasema ibada hiyo (ya ubatizo ya kipagani) katu haitokani na Yehova, kwa sababu tangu mapema Yehova alikwishawakataza na kuwaonya wanadamu kutenda ibada yoyote (kama hiyo ya ubatizo) ya watu wa mataifa (yaani wapagani) kama asemavyo (Yehova) katika maandiko yafuatayo: "Utakapokwisha kuingia katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako, usijifunze kutenda kwa mfano wa machukizo ya mataifa yale". (Kumbukumbu la Torati 18:19).

BWANA, Mungu wako, atakapoyakatalia mbali hayo mataifa mbele yako, huko uingiako kuyamiliki, nawe ukawatwaa, na kuketi katika nchi yao, ujiangalie, usije ukanaswa ukawafuata, wakiisha kuangamizwa mbele yako, wala usije ukauliza habari za miungu yao, ukasema, mataifa haya waitumikiaje miungu yao? Nami nifanye vivyo". (Kumbukumbu la Torati 12:29-30) Kulingana na maandiko hayo juu, hapo Yehova kwa ujumla anawataka wanadamu wajiepushe mbali kabisa na ibada ya watu wa mataifa au wapagani.

Na kwa kuwa Biblia tukufu inakiri kwamba ibada ya ubatizo ni ya kipagani, ni dhahiri kuwa ibada hiyo nayo i miongoni mwa machukizo kwa Yehova ambayo hataki wanadamu kuyatenda. Pamoja na makemeo hayo ya Yehova dhidi ya yeyote anayetenda ibada za watu wa mataifa au wapagani (kama hiyo ya ubatizo), lakini muasisi wa Ukristo, Bwana Paulo kwa kuwa tangu mapema alidhamiria na hatimaye kuamua kufuata mia kwa mia dini ya kipagani, alisema kama ifuatavyo kuhusu ibada hiyo ya ubatizo:

"Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake? Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima". (Warumi 6:3-4). "Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru, nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja". (1Wakoritho 12:13).

Kwa uchache, anachokiri Bwana Paulo katika maelezo yake hayo juu ni kwamba, yeye binafsi pamoja na wafuasi wake wote (Wakristo) huifanya ibada hiyo (ya ubatizo). Kwa lugha nyingine anakiri kwamba ibada hiyo imo katika orodha ya taratibu za dini yake ya Kikristo. Miaka 36 mpaka 45 baada ya Paulo kuifundisha ibada hiyo (ya ubatizo), waandishi wa Agano Jipya nao katika kuuandikia Ukristo wa 'mwalimu wao' (Paulo), walisherehesha mafundisho yake hayo (ya ubatizo) ambayo wamethubutu hata kutunga katika Injili zao kuwa Bwana Yesu naye eti aliwahi kutenda ibada hiyo ya kipagani kwa kubatizwa na Yohana katika mto wa Yordani! (Tazama Mathayo 3:13-17; Marko 1:9-11; Luka 3:21-22; Yohana 1:31-34).

Nasema waandishi hao (Wainjilisti) wametunga kwa kuwa kama tulivyoona Biblia tukufu ielezeavyo kwamba ibada ya ubatizo imetokana na dini za kale za kipagani, ni dhahiri kuwa Nabii Yesu na Nabii Yohana kamwe hawawezi kutenda ibada potofu za wapagani (kama hiyo ya ubatizo) ambazo zimekemewa vikali na Yehova aliyewatuma (rejea Kumbukumbu la Torati 18:9). Na hata ukiyasoma masimulizi ya waandishi hao juu ya nadharia hiyo ya Yesu na Yohana kubatizana, licha ya maelezo yao kutofautiana na hivyo kutojua ni mwandishi gani anayeelezea kiusahihi, bado utaona kuna utata mkubwa na wa kimsingi wa kutendeka kwa tukio hilo.

Kwa mfano, waandishi hao wamesimulia kuwa ubatizo wa Nabii Yohana (a.s.) waliouelezea kuwa ni wa maji, ulikuwa ni kwa ajili ya utakaso wa kumwondolea mtu dhambi (tazama Marko 1:4-5). Kwa shuhuda hiyo, waandishi hao wasingeonekana kuwa wanasherehesha ibada ya Paulo (ya ubatizo) iwapo wangetusimulia katika Injili zao kuwa Nabii Yohana (a.s.) alipombatiza Yesu (a.s.) Yehova alisahau kumjulisha kuwa ubatizo wake haukumstahili Yesu kwa kuwa (Yesu) hakuwa na dhambi (tazama Yohana 8:45-46).

Aidha, kauli inayosimuliwa na waandishi hao kutolewa na Nabii Yohana (a.s.) akimshangaa Yesu (a.s.) alipomjia hapo katika mto wa Yordani ili ambatize kwa kumwambia: " Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu?", Kisha Yesu (a.s.) eti akamjibu Yohana (a.s.) na kumwambia: "Kubali hivi sasa, kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote" (Mathayo 3:13-14), inaonyesha Yesu hapa akipinga wazi maelekezo ya Nabii Yohana (a.s.) jambo ambalo kamwe haliwezi kufanywa na Yesu (a.s.) kwani Yesu (a.s.) anajua wazi kuwa Nabii yoyote wa kweli (kama Yohana) hasemi neno ila ni wahyi (ufunuo). (Tazama 2 Petro 1:21). Aidha, kumpinga Nabii kama Yohana (a.s.), Bwana Yesu (a.s.) anajua pia kuwa ni kukiuka ile ahadi yake kwamba: "Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua Torati wala Manabii..." Tazama Mathayo 5:17-19)

Kwa upande mwingine wa masimulizi ya waandishi hao, yaonyesha kwamba, kumshangaa kwake kule Yesu (a.s.), Nabii Yohana (a.s.) hakujua alitendalo hata ikabidi Yesu amkosoe kwa kupinga maelekezo yake (Yohana) yale! Jambo ambalo siyo kweli. Kwani Nabii kama Yohana kamwe hawezi akathubutu kutoa maelekezo ya uongo kama hayo anayodaiwa (katika masimulizi ya waandishi hao) kuwa eti alisema kwamba "alitakiwa Yesu ndiye ambatize yeye (Yohana) na kukosolewa kwa kupingwa vikali na Yesu! Kwa uchache, huo ndio utata wa kimsingi unaotia shaka kuwepo (kutendeka) kwa tukio la kubatizana Yesu na Yohana (a.s.) katika mto wa Yordani kama isimuliwavyo na waandishi wa Agano Jipya katika Injili zao. Kwa uchambuzi zaidi juu ya utata huo rejea makala za "Je, Yesu alibatizwa" na upo utata wa Yesu kubatizwa". (ANNUUR namba 183 Uk. 15 na namba 190 Uk. 15).

Tukiachilia mbali utata huo, jambo la kuzingatia ni kwamba ibada hiyo (ya ubatizo) kama Biblia ielezavyo imetokana na wapagani. Kwa shuhuda hiyo ni dhahiri kuwa Bwana Yesu (a.s.) na Nabii Yohana (a.s.) kamwe hawawezi kutenda ibada hiyo kwa kuwa ni ibada ya kipagani ambapo Yehova aliyewatuma amewakataza wanadamu kutenda ibada zote za wapagani. Na ni wazi kuwa Wakristo kutenda ibada hiyo ni uthibitisho kuwa hawamwabudu Yehova, Mungu wa Nabii Ibrahimu, Ismaili, Isaka, Yakobo, Muhammad na Manabii wengine wote.

Msimamo wa Yehova kuhusu ibada za watu wa mataifa (wapagani)
Kulingana na mafundisho ya Biblia tukufu, msimamo wa Yehova au Allah (s.w.) kuhusu ibada za watu wa mataifa au wapagani, ni "ubatili", ni "chukizo" na ni "najisi" tupu. Msimamo wake huu unathibitishwa na maandiko yafuatayo ya Biblia tukufu kama yalivyomkariri Yeye mwenyewe (Yehova au Allah s.w.) akisema: "BWANA anasema hivi, Msijifunze njia ya mataifa, wala msishangae kwa sababu ya ishara za mbinguni, maana mataifa hushangaa kwa sababu ya ishara hizo. Maana desturi za watu hao ni ubatili; maana mtu mmoja hukata mti mwituni, kazi ya mikono ya fundi na shoka". (Yeremia 10:2-3).

"Msijitie unajisi katika mambo hayo hata mojawapo, kwa maana hizo taifa nitakazozitoa mbele zenu zimekuwa najisi kwa mambo hayo yote; na hiyo nchi imekuwa najisi, kwa ajili ya hayo naipatiliza uovu wake juu yake, na hiyo nchi yatapika wenyeji wake na kuwatoa. Kwa hiyo mtazishika amri zangu na hukumu zangu, wala msifanye machukizo hayo mojawapo; yeye aliye mzalia, wala mgeni aketiye kati yenu; kwa kuwa hao watu wa nchi wameyafanya machukizo haya yote, hao waliotangulia mbele zenu, na hiyo nchi imekuwa najisi... kwani mtu awaye yote atakayefanya machukizo hayo mojawapo, nafsi hizo zitakazofanya zitakatiliwa mbali na watu wao. Kwa ajili ya hayo yashikeni mausia yangu, ili kwamba msifanye kabisa desturi hizi zichukizazo mojawapo zilizotangulia kufanywa mbele zenu, wala msijitie unajisi katika mambo hayo, mimi ndimi BWANA, Mungu wenu". (Mambo ya Walawi 18:24-30 ).

"Na wa mataifa BWANA aiwaambia wana wa Israeili, msiingie kwao, wala wasiingie kwenu; kwa kuwa hakika wataigeuza mioyo yenu kuifuata miungu yao..." (1 Wafalme 11:3) "Msiwape mbwa kilicho kitakatifu, wala msitupe lulu zenu mbele ya nguruwe, wasije wakazikanyaga chini ya miguu yao, wakageuka na kuwararua". (Mathayo 7:6). Kwa uchache, huu ndio msimamo halisi wa Yehova kuhusu ibada za watu wa mataifa au wapagani; kwamba ni chukizo, najisi na ni ubatili mtupu kwake (Yehova).

Hitimisho
Pamoja na ukweli wa shuhuda hizo juu, jambo la kuzingatia hapa ni kwamba, ibada zote ambazo zimefundishwa na Ukristo, Biblia imetuonyesha kuwa ni ibada za kipagani. Pia Biblia imetuonyesha kuwa mungu-mtu wa Kikristo ni mungu wa kipagani. Kwa kuwa sifa zake zitofauti kabisa na za Yehova. Na bila shaka wenzetu wameona na wameelewa kwa nini Waislamu wanasema kwamba Wakristo hawamwabudu Yehova, Mungu wa Nabii Ibrahimu, Ismaili, Isaka, Yakobo, Musa, Yesu, Muhammad na Mitume na Manabii wengine wote.

Ni kwa sababu imani yao (ya mungu-mtu) na ibada zao kamwe hazitokani na Yeye (Yehova). Na kwa ujumla, mradi ibada kuu zinazotekelezwa na Wakristo ni hizo za watu wa mataifa au wapagani, ni dhahiri kuwa mbali ya kutomtambua kwa kutojua sifa zake tukufu na takatifu, Yehova daima siye Mungu anayeabudiwa na Wakristo.

MWISHO