MATATIZO YA BIBLIA
  • Kichwa: MATATIZO YA BIBLIA
  • mwandishi: X-Paster
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 18:58:48 6-10-1403

BISMILLAHI R-RAHMAANIR-RAHIIM
MATATIZO YA BIBLIA

Tatizo la Kutafsiri
Wataliano wana usemo usemao "Wafasiri ni waongo". Msemo huu una ukweli ndani yake na umetokana na uchunguzi makini. Kuchukua kitu fulani kilichoandikwa katika lugha fulani na kujaribu kukiingiza katika lugha nyingine huwa inaleta matatizo kwa sababu mara nyingi wafasiri hupambana na maneno katika lugha moja ambayo hayamo katika lugha nyingine. Neno jingine badala yake lazima litumike na matokeo yake ni kubadilika kwa maana.

Agano la kale mwanzo kabisa liliandikwa kwa Kiebrania, lakini lilitafsiriwa katika karne ya tatu kwenda katika lugha ya Kigiriki kwa ajili ya Wayahudi waliokuwa wanaishi nje ya Palestina (ambao walikuwa wanaongea Kigiriki - badala ya Kiebrania). Tafsiri hii iliitwa "septuagint" na ilitumika sana hata na wakristo wa mwanzo.

Agano Jipya liliandikwa katika lugha ya Kigiriki lakini maadam Yesu mwenyewe alitumia lugha ya kiaramaiki, hii ina maana kwamba maneno yake yalilazimika kutafsiriwa na hivyo kusababisha uwezekano wa makosa.

Tafsiri ya kigiriki iliyokuwa ikiitwa Septuagint iliunganishwa na maandiko ya Agano Jipya yaliyokuwa katika lugha ya kigiriki katika karne ya nne. Maandiko haya yaliyounda Biblia kamili sasa hivi yanaeleweka kamaCodexsinaiticus" na "Codex Vaticanus" na hizi ndio nakala za maandiko ya zamani kabisa zilizopo leo. Hakuna maandiko ya mwanzo kuliko haya yaliyonusurika kutupiliwa mbali.

Katika karne ya nne, Biblia ilitafsiriwa kwenda katika lugha ya Kilatini na Mt. Jerome. Na hii ilibakia kuwa lugha ya Biblia hadi karne ya kumi na sita ambapo watu wa Mageuzi kama John Wycliffe, William Tyndale na Martin Luther walipoifasiri Biblia katika lugha mbalimbali za watu - jambo ambalo lilikuwa haliruhusiwi kabisa na viongozi wa kanisa wa wakati ule na ili kufanikisha lilimgharimu Tyndale maisha yake. Walifanya hivi ili kuwazuia watu kuyasoma, kuyaelewa au kuyahisi maandiko yao Matakatifu - haya yalifanywa makusudi na viongozi wa kanisa.

Tafsiri nyingine zilifuatia ndani ya muda mfupi. Karibu na mwisho wa karne ya kumi na sita kulikuwa na tafsiri za lugha mbalimbali na tafsiri mbalimbali za lugha moja ambazo zilileta malumbano na mabishano makubwa jambo lililomfanya Mfalme James I wa Uingereza kuteua kamati ya wanazuoni hamsini na nne ili kuandaa toleo "rasmi" na litakalotambulika na mamlaka. Watu hawa (kamati) walizisoma tafsiri zote zilizokuwepo wakati ule na, mnamo mwaka 1611, walitoa toleo lililoitwa "King James Versions of the Bible" yaani toleo la Biblia la Mfalme James - ambalo lilikuwa ndio toleo rasmi miongoni mwa Wakristo kwa mamia ya miaka.

Tatizo la uharibifu na upotoshaji lililoambatana na kutafsiri liliisha mwaka 1611, kwa kupatikana toleo la King James Versions of the Bible, tatizo la marudio... "kuiboresha" au kuifanya kuwa ya "kisasa" limeikabili Biblia leo hii.

Kiwango cha uharibifu na upotoshaji huu ni kama ifuatavyo:
katika mwaka 1952, makala yenye kichwa cha habari "Ukweli kuhusu Biblia" yalionekana katika gazeti la "Look" (Tazama). Makala haya yalisema kwamba kulikuwa makosa zaidi ya 20,000 (elfu ishirini) katika Agano Jipya peke yake. Mashahidi wa Yehova walilizungumzia suala hili katika toleo la Septemba, 1957 la gazeti lao la "Awake" (Amka) ambapo walisema "...Wafasiri walifanya makosa katika kufasiri (Biblia) ambayo yamesahihishwa na wanazuoni wa zama hizi… nao wakasema kuwa biblia ina makosa zaidi ya 50, 000…". Mtu anaweza kujiuliza ni jambo la ajabu wanazuoni hawa walilifanya!!

Katika karne ya kumi na tisa, Wakristo waliamua kuiboresha lugha ilivyotumika katika King James Version. Jitihada zao zilizaa toleo jipya la Biblia liitwalo "American Standard Version" lililotolewa mwaka 1901. Wakristo waliolifanyia kazi toleo hili sio tu kwamba waliikuza na kuiboresha lugha bali pia walifanya mabadiliko katika Biblia yenyewe:

Katika kuuthibitisha ukweli kwamba baadhi ya maneno yaliondolewa na mengine kuongezwa, tunaweza kuangalia katika maandiko ya mwanzo ya Biblia yaliyokuwa katika lugha ya kigiriki toleo la Biblia la King James Version 1Yohana 5:8 ambapo imeandikwa "Baba, Mwana na Roho Mtakatifu". Lakini toleo jipya la American Standard Version, wanazuoni walibadilisha na badala yake wakatumia maneno "Roho, Maji na Damu". (Angalia Nukuu hapo juu kabisa)

Katika kukubali ukweli mwingine juu ya uongezaji na upunguzaji wa baadhi ya maneno katika Maandiko Matakatifu (Biblia), vifungu vya vingi vimefungiwa mabano na katika sherehe yake (maelezo ya ziada) wameeleza kwamba vifungu hivi "havipatikani katika Biblia (Maandiko matakatifu) nyingi za zamani".

Baada ya miaka kadhaa viongozi wa kanisa walikutana wakaamua kuliboresha toleo la Biblia la American Standard Version. Matokeo ya jitihada zao ilikuwa ni kupatikana toleo jingine la Biblia linalojulikana kama "The Revised Standard Version" - yaani toleo la Biblia la kiwango bora na lililofanyiwa marekebisho. Toleo hili lilitoka rasmi mwaka 1952.

Katika dibaji ya Toleo hili kuna maelezo haya: "…Toleo la King James (King James Version) lina makosa na mapungufu mengi mno na hatari sana kiasi kwamba kuna haja kubwa ya kulifanyia marudio na marekebisho toleo zima...". (Tafadhali angalia dibaji ya Revised Standard Version)

Katika toleo la Biblia la 'The Revised Standard Version' tunakuta kwamba aya katika injili ya Marko zinazozungumzia juu ya kupaa kwa Yesu (Marko 16: 9-20) zimeondolewa kwa madai kwamba aya hizi hazipatikani katika Biblia (maandiko) za zamani kabisa.

Katika mwaka 1989, toleo la Biblia la 'The Revised Standard Version' la 1952 liliboreshwa tena na hivyo likapatikana toleo jipya "The New Revised Standard Version". Na katika toleo hili aya zinazozungumzia juu ya kupaa kwa Yesu katika Marko 16 zilirejeshwa. Kwa vile Wakristo wengi hawakufurahia "kumomonyolewa" kwa moja ya imani zao za msingi kulikofanywa na Wahariri wa "The Revised Standard Version", ilibidi aya hizi zirejeshwe ili kuwaridhisha.

Kwa kuhitimisha, tunaweza kusema, kutokana na marudio ya mara kwa mara yaliyofanyika kwa miaka mingi wakati wa kufasiri na "Matoleo" mbalimbali mapya katika Biblia tuliyonayo leo maandiko ya wanadamu ndio mengi zaidi kuliko ufunuo kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Wakristo Wenyewe Wanasemaje Juu ya Tatizo Hili Huko nyuma katika karne ya nne, Mt. Augustino aligundua makosa mengi, ndani ya Biblia. Akizungumzia juu ya suala hili katika barua yake Na. 82 Alisema kwamba… makosa katika uelewaji ndio sababu ya tatizo hili (la kuona aya zinapingana, na nyingine zipo katika toleo hili, lakini katika toleo jingine hazipo na utatanishi mwingine mwingi). Anasema yeye haamini kwamba watu kuongeza, kupunguza na kubadilisha baadhi ya mambo katika Biblia kuwa ni tatizo ila tatizo ni uelewaji mbaya katika usomaji. Kwa maneno mengine anasema kwamba baada ya msomaji kukumbana na mikorogano hii katika Biblia anatakiwa abuni maelezo fulani yatakayokuwa ni msamaha wa makosa haya.

Utafiti unaojaribu kuangalia na kuonyesha makosa katika Maandiko Matakatifu, tofauti na watu wengi wanavyofikiri, umeanza hivi karibuni. Kwa mamia ya miaka Biblia ilikubalika tu "kama ilivyo". Ilichukuliwa kuwa ni dhambi kubwa sana kujaribu kukosoa kosa, hata dogo lililomo ndani ya Biblia na viongozi wa kanisa walifanikiwa sana kuyazima majaribio yoyote ya kujaribu kuikosoa Biblia.

Kitabu cha kwanza kuonyesha na kukosoa makosa katika Biblia kilichoandikwa na Richard Simon kiitwacho Critical History of the Old Testament (Historia inayojaribu kuonyesha na kukosoa makosa yaliyomo katika Agano la kale), kilitoka mwaka 1678. Kitabu hiki kilileta tafrani na mtafaruku mkubwa lakini kilisaidia sana kufungua njia kwa wale waliokuja baadaye katika karne ya 18 na 19 kwa dhumuni la kufanya utafiti juu ya makosa yaliyomo katika Agano la Kale.

Kutokana na ukweli mwingi usiopingika uliotolewa na watu mbalimbali, Halmashauri ya awamu ya Pili ya Vatican (1962- 1965) ilitoa maelezo yanayoshangaza juu ya jambo hili "…Vitabu vya Agano la Kale vina (ndani yake) habari zisizo sahihi na zenye mapungufu mengi..."

Agano Jipya pia lina kasoro na mapungufu mengi. Ingawa Halmashauri ya awamu ya pili ya Vatican inashikilia kwamba Injili "kihistoria ni ya kweli " na kwamba wao "kwa uaminifu kabisa wanaeneza yale ambayo Yesu alifanya na kufundisha watu wakati wa maisha yake". Wanazuoni wengine wamekuwa na maelezo ambayo ni kinyume kabisa na msimamo wa Vatican.

Katika kitabu chake "The Call of the Minaret" (Wito kutoka katika mnara wa msikiti, Adhana), Dr. Kenneth Cragg anasema kwamba kuna "mambo yaliyoongezwa na kupunguzwa" katika Agano Jipya Injili na ni kazi ya akili ya viongozi wa kanisa ikiongozwa na waandishi, na kwamba katika kazi zao wanatumia uzoefu na historia."
Padre Kannengiesser, Profesa katika taasisi ya kikatoliki katika mji wa Paris, alionya katika kitabu chake "Faith in Resurrection" (Imani juu ya ufunuo), kwamba watu wasijaribu "kuyatafsiri na kuyaelewa maneno kama yalivyo" juu taarifa za kweli kuhusiana na Yesu katika Injili - onyo ambalo pia lilitolewa na Padre Rognet wa Paris katika kitabu chake "Initiation to the Gospels".

Carl Andrey, profesa wa falsafa na masomo ya dini katika Chuo kikuu cha Ball State kilichopo Indiana anasema kwamba vitabu vinne vya Injili: "…viliandikwa na watu wenye shauku wa harakati za mwanzo za kikristo na kwamba wanatupatia nusu tu ya habari kamili na kwa kiasi kikubwa ni mazao ya fikra za waandishi wao"

Mwisho tuna maelezo ya Dr. W. Graham Scroggie wa "Prestigious Moody Bible Institute" ambaye anasema: "Ndiyo, Biblia ni zao la kazi iliyofanywa na binadamu …vitabu hivyo vimetokana na akili za watu, vimeandikwa kwa mikono ya watu, na fani ya uandishi wake ni ya kibinadamu.

Kama huu ndio msimamo wa wanazuoni wa Biblia, wakristo wa "kawaida" watakuwa na lipi la kusema juu ya jambo hili?

Wengi (wa wakristo wa kawaida) hata hawajui lolote juu ya kasoro nyingi zilizomo ndani ya Biblia kwa sababu waandishi wa utangulizi na washereheshaji (wanatoa maelezo ya ziada) wa Biblia. Wanatumia mbinu mbalimbali za kijanja ili kuwafanya Wakristo wasiyajali na wajisahaulishe na maswali ambayo wangejiuliza juu ya kasoro nyingi zilizomo ndani ya Biblia. Pamoja na mambo mengine, waandishi hawa:

1) Wanaandika mambo kama ukweli uliothibitika wakati ukweli na uthabiti wake una mashaka, na

2) Wanayafunika makosa na kasoro zilizomo ndani ya Biblia kwa kutoa nyudhuru na kuomba radhi mbinu ambayo inaondoa umakini wa msomaji kutoka kwenye dosari na kasoro zilizomo ndani ya Biblia na badala yake kuangalia mambo mengine.

Kina wanachokwenda washereheshaji (Commentators) katika kujaribu kutetea kasoro na dosari zilizomo ndani ya Biblia ni alama na ushahidi tosha juu kutojisikia kwao vizuri na ugumu wanaoupata katika jitihada zao za kujaribu kutetea makosa, dosari na kasoro zilizomo ndani ya Biblia.

Pamoja na ukweli huu juu ya kasoro na dosari zilizomo ndani ya Biblia, ajabu ni kwamba mtu anapojaribu kuzionyesha hataambulia chochote kutoka kwa wakristo isipokuwa uadui.
Watu wengi waliwahi kupeleka makaratasi yenye utafiti juu ya kasoro na dosari mbalimbali zilizomo ndani ya Biblia katika mishenari ya kikristo, lakini wanacho ambulia kushutumiwa kwa kufanya "uvamizi dhidi ya Biblia, na utawasika wakisema "Biblia imefanyiwa uvamizi (imevamiwa) kwa karne nyingi, lakini bado ipo. Imestahimili vishindo (vyote) vya nje na ndani".

Nastaajabu vipi mtu awe na msimamo kama huu mbele ya mifano tele inayoweza kuthibitishwa, sielewi anamaanisha nini katika neno "vishindo". Labda linaendeleza lile linalopatikana katika "kazi bora " ya vitabu vinavyotetea dosari na kasoro zilizomo katika vitabu vya Kikristo iliyomo katika kitabu kiitwacho "Is Bible Reliable. (Je, Biblia inaaminika?).

Katika kitabu hiki, mwandishi Bjug Horstal anasema kwamba Mungu "aliwashawishi" waandishi wa Maandiko Matakatifu " …kuandika kasoro na dosari zilizoambatana (zinazotokana) na lugha, na kwamba tunatakiwa tuliache jambo hili kwa Mungu mwenyewe, awe huru kutumia idadi yoyote ile ya fani na hata udhaifu wa kibinadamu kama anavyotaka mwenyewe…".

Mashahidi wa Yehova wameandika kitabu kizima kiitwacho:
Bible: God's Word or Man's? (p. 97) (Biblia: Ni neno la Mungu au la Mwanaadamu?), ambacho kinazungumzia kasoro na dosari zilizomo ndani ya Biblia. Katika kitabu hiki, wamelizungumzia suala hili kwa namna tofauti na ya pekee kwa kusema kwamba: 'kuna baadhi ya "kasoro na dosari za wazi" katika Biblia ambazo "ni vigumu kuzitetea". Hata hivyo tusizichukulie dosari na kasoro hizi kuwa ni kugongana na kupingana kwa aya za Biblia; mara nyingi ni kwa sababu ya ukosefu wa taarifa na habari kamili'.

Nilibahatika kupata nakala ya tafsiri ya Biblia ya Mashahidi wa Yehova "The New World Translation of the Holy Scriptures". Nilimuuliza mjumbe mmoja wa ngazi za juu kuwa ana maelezo gani juu ya aya ya Mathayo 17:21, ambayo inasomeka: "Hakuna aya, kuna namba tu mstari mrefu ulio wazi". Mjumbe yule alibabaika sana alipoangalia sehemu hiyo. Akaahidi kuwa angekuja kuniona kwa mara nyingine tena ningependa kujua anasemaje kuhusiana na suala hili.

Kwa kifupi, Wakristo hawako tayari kuukubali ukweli kwamba Maandiko yao Matakatifu yamepotolewa kwa madai kwamba, ikiwa msingi utayumba na kutokuwa na uhakika, je tutasimama juu ya nini katika siku za masaibu na mashaka?" (Is the Bible Reliable?)

Sio hayo tu, bali kuna aya inayozungumzia juu ya kuyabadilisha maandiko matakatifu katika maandiko hayo hayo:

"...ikiwa mtu yeyote ataongeza (au kufuta) neno lolote katika kitabu hiki, Mungu atamuongezea balaa zilizoandikwa katika kitabu hiki".
(Ufunuo 22:18,19)

Ushahidi uko hapo, upo wazi na rahisi kwa kila mtu kuelewa. Ikiwa Mungu aliwaongoza kwa ufunuo kuandika vitabu vya Biblia, hakuna shaka kwamba wanadamu wameingilia na kubadilisha mambo mengi. Swali muhimu kabisa la kumuuliza Mkristo ni kwamba: Inawezekanaje kwa neno la Mungu kubadilishwa, kuondolewa na hata kutupiliwa mbali kwa matakwa ya mwanaadamu??

MWISHO