KISA CHA KUIJENGA L-KA`ABA
  • Kichwa: KISA CHA KUIJENGA L-KA`ABA
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 18:45:10 6-10-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

KISA CHA KUIJENGA L-KA`ABA
Mtume S.A.W. alikuwa na umri wa miaka 35 wakati Ma-Quraishi walipokutana pamoja kuijenga L-Ka`aba. Waliijenga kwa sababu mafuriko ya maji yalibomoa kuta za L-Ka`aba. Kabila zote za Ki-Quraishi zilikusanya mawe ya kujengea. Kila kabila ilijenga sehemu yake maalum bila kuingilia sehemu ya kabila nyingine.

Mpaka ujenzi ulipofikia kwenye jiwe jeusi hapo ulitokea mzozano mkubwa, kwani kila kabila ilitaka iwe yenye kuliweka lile jiwe jeusi. Wakabaki hivi hivi kwa siku wametofautiana mpaka ilitaka kutokea fitina (ugomvi) mkubwa baina yao. Lakini Mwenyezi Mungu S.W.T. akajaalia mmoja wao mwenye akili aliyeitwa Abu Umayya bin Mughiyra L-Makhzuumy kutoa shauri la kuumaliza ugomvi huo;

wakakubaliana wote, na shauri lile lilikuwa kama ifuatavyo: Yeyote yule atakaeingia mwanzo kwenye mlango wa L-Ka`aba (ambao hivi sasa unaitwa Baabu Ssalaami) ndiye atakayekuwa Hakimu wa kuwahukumu baina yao.

Kwa hivyo wote wakaridhika na kulikubali shauri hilo. Na ilitaka hekima ya Muumbaji Mola wa walimwengu wote kuwa mtu huyo atakayehukumu awe Mtume Wake S.A.W.. Mara tu walipomuona yeye ndiye aliyeingia mwanzo wote wakasema, "Huyu mwaminifu tumeridhika naye. Huyu Muhammad (S.A.W.)." Mtume S.A.W. alipowafikia walimueleza lile jambo lililowasababishia kuzozana baina yao, wakamuomba awahukumu.

Mtume S.A.W. alifikiri na kupima kisha akasema: "Nileteeni nguo!" Walimletea nguo baadaye aliitandaza nguo ile kisha akalibeba lile jiwe jeusi kwa mikono yake akaliweka katikati ya hiyo nguo, akasema:

"Kila kabila ishike ncha ya hii nguo halafu inuweni wote kwa pamoja." Walipofanya hivyo na kulifikisha lile jiwe mahali pake, Mtume S.A.W. aliliweka jiwe lile kwa mikono yake yenye baraka kisha wakalijengea. Na hivi ndivyo jinsi Mwenyezi Mungu Mtukufu alivyowaepushia shari ile na ukawa mwisho wa ugomvi ambao ungelisababisha vita baina yao. MWISHO