WAISLAMU UMAGHARIBINI
  • Kichwa: WAISLAMU UMAGHARIBINI
  • mwandishi: D.K AISHA HAMDAN
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 18:26:49 6-10-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

WAISLAMU UMAGHARIBINI

Baraza la Mahusiano ya Waislamu la Amerika limeripoti kuwa mwaka 2002, kulikuwa na malalamiko 602 ya ubaguzi dhidi ya jamii ya Waislamu. Hili lilikuwa ni ongezeko la asilimia 15 kulinganisha na mwaka wa nyuma yake.

 Mikasa ya ubaguzi ilitokea mashuleni, makazini, kwenye maeneo ya kijamii, kwenye viwanja vya ndege na kwingineko. Mikasa hiyo ilijumuisha ubaguzi katika ajira, bugudha ya maneno, kunyimwa fursa za kidini na kadhalika.

 Matendo haya ya ubaguzi yalihusiana moja kwa moja na rangi au dini ya mtu hasahasa kwa watu ambao utambulisho wa dini yao unabainika kwa vazi la Hijab au shungi.

Je Waislamu wayajibu vipi matukio ya namna hiyo?  Wanawake wa Kiislamu ndio wahanga wakubwa wa aina mbalimbali za unyanyasaji na ubaguzi kutokana na ishara za mavazi yao ya Kiislamu.

Je wanawake hawa wakabiliane vipi na chuki na ubaguzi ambao umekithiri katika nchi inayodai kuheshimu uhuru wa dini na haki za raia? Hebu kwanza tuone, chuki na Ubaguzi ni nini ?

Chuki ina maana ya mwenendo wa hiyana na uwaduwi dhidi ya mtu fulani au dhidi ya jamii fulani ya watu. Ni jambo au ni hukumu inayotolewa kwa mtu kabla hata ya kukutana naye.

Na ubaguzi maana yake ni tendo, mwenendo au hali ya kumyanyapaa mtu au kuinyanyapaa jamii fulani ya watu. Chuki ni hisia na ubaguzi ni utekelezaji wa hisia hizo.

 Hata hivyo, chuki si lazima izae ubaguzi. Chuki inaweza kuwepo bila ya ubaguzi. Na ubaguzi unaweza kutokea pasipo chuki. Mambo haya mawili yana uhusiano lakini si uhusiano wa mara zote.

Chuki na ubaguzi huchukua nafasi kutokana na aina ya jamii (haiba ya kimaumbile kama vile rangi ya ngozi), ukabila (mila, desturi na imani), dini (imani na matendo, jinsia na labda katika jamii nyingine kuna ubaguzi wa hali za utajiri na umasikini.

Kinachozidisha chuki za kijamii ni mtazamo au mwenendo wa watu fulani kujiona bora zaidi kuliko wengine. Watu walio na chuki hufikiri na kuhisi kuwa wao ndio watu bora kuliko makundi mengine ya watu. Na hutumia dhana hii kuwanyanyasa na kuwabaguwa wengine.

Kigezo cha Mtume

Itakuwa busara zaidi kuutazama mfano wa Mtume (saw)s tunapodhamiria kukabiliana na maisha ya chuki na ubaguzi. Mtume (saw) alikumbwa na aina mbaya sana za  chuki, ubaguzi na maonevu.

 Mmoja wa viongozi wa kampeni ya kumpiga vita Mtume alikuwa ni ami yake, Abu Lahab. Bwana huyu alifanya mabaya mengi dhidi ya Mtume (saw) na hiyo ilikuwa ni  chuki na dharau.

Alimpopowa mawe Mtume, alimbeza kwa kifo cha mwanawe wa pili wa kiume, akimwita kuwa ni mtu “aliyekatwa kizazi”, akamfuatilia wakati wa Hija na katika mambo mengine ili kuwashawishi watu wasiitikie mwito wake.

Mke wa bwana huyo,Umu Jamila bint Harb naye pia alishiriki katika kampeni hiyo ya kikatili. Mama huyu alikuwa na tabia mbaya, matusi moto na alikuwa mtu hatari kwa fitna. Alikuwa akifunga malundo ya miba kwa kamba za milala na kuzitega katika njia aliyokuwa akipita Mtume (saw) ili kumdhuru.

Abu Jahl naye alikuwa aduwi mwingine wa Mtume (saw) na Uislamu. Wakati fulani, pale Mtume (saw) alipokuwa anasujudu katika Sala kule Ka’aba, Abu Jahl akaleta mimba iliyoharibika ya ngamia jike na kumwekea Mtume mgongoni. Makafiri waliozunguuka Ka’aba waliangua kicheko cha kuvunja mbavu.

Habari za madhila aliyoyapata Mtume (saw) na wafuwasi wake ni nyingi. Kiasi kwamba Mtume alilazimika kuuhama mji wake na kutafuta hifadhi katika mji wa jirani wa Ta’if.

Wakati alipokuwa njiani akirudi kutoka katika mji huo, alishambuliwa vibaya sana. Lakini nini lilikuwa jibu la Mtume (saw)? Hebu mtu aangalie tu duwa aliyoomba kuhusiana na tukio hili la mwisho.

Akiwa amejeruhiwa, akivuja damu, akiwa na njaa na kiu, Mtume (saw) aliinuwa mikono juu mbinguni na kuomba:

“Ewe Allah! Kwako wewe pekee ndiko ninakoelekeza sononeko langu la unyonge, uchache wa nguvu zangu na udhalili wangu mbele ya walimwengu, Wewe ndiwe Mwenye huruma zaidi ya wenye huruma. Wewe ndiwe Mola wa wasiojiweza na wanyonge, Ewe Mola wangu! Ni  mikononi mwa nani utaniacha mimi: je mikononi mwa ndugu wa mbali asiye na huruma ambaye atanikunjia uso au je utaniacha kwa adui ambaye amepewa mamlaka juu yangu. Lakini kama ghadhabu zako haziniangukii, basi sina cha kutilia shaka. Naomba ulinzi kwa nuru ya paji lako inayoangaza mbinguni na kuondosha giza na inayoendesha mambo yote katika dunia hii na Akhera. Naomba nisipatwe na ghadhabu Zako au usinighadhibikie. Na hakuna uwezo wala nguvu isipokuwa ya kwako pakee.” (Ar-Rahiiq al-Makhtum)

Mafunzo yanayopatikana

Ni jambo muhimu kukumbuka kuwa wakati ule ambapo kulikuwa na nguvu kuwa ya uwaduwi, chuki na upinzani bado madhila haya hayakujibiwa na Mtume (saw). Wasiwasi wake mkubwa ulikuwa ni je Allah angeurudi vipi mwenendo wake yeye. Yeye alihofia kumuudhi Allah.

Mazingatio yake hayakuwa juu mwenendo wa watu waovu bali yeye aliangalia namna gani akabiliane na uovu. Mtume (saw) aliomba duwa kwa MwenyeziMungu amsaidie katika kazi yake na ampe nguvu ya kutimiza utume wake.

Kwa Mtume, Allah ndiye aliyekuwa kila kitu ambapo upinzani wa dunia nzima haukuwa chochote. Katika riwaya nyingine, inaelezwa kuwa Mtume alimuomba Allah awasamehe wanaume na wanawake waliomnyanyasa na kumuumiza na awaongoze katika nuru ya Uislamu.

Hiki ndicho kigezo cha Mtume (saw) ambacho tunapaswa kukifuata katika nyakati za misukosuko na madhila. Hii ni sehemu ya mchakato wa utakasaji wa nafsi kwani MwenyeziMungu anatupa mitihani hii ili tujitakase. Kuna malipo ya Allah kwa wale wanaojizuia na kusamehe waliotenda dhambi.

Ni vigumu kufanya jambo hili lakini lina matokeo bora. Kulipiza  kisasi na kuumizana kutazidisha tu mfarakano na chuki kubwa zaidi. Hilo litazidi kuchochea hisia za chuki na ubaguzi.

Jibu baya la Muislamu linaweza kuzidisha imani na tabia mbovu za mtu mwenye dhambi. Mwenendo bora wa muumini, kwa upande mwingine, huwaonesha watu uzuri wa Uislamu. Kimsingi, hii ndiyo njia bora ya Da’wa.

 Badala ya kuonesha picha ya upande muovu wa silika ya mwanadamu, itawapa wengine picha ya amani na maelewano inayotokana na mtu kuwa Muislamu. Yawapasa Waislamu kuishi kwa amani na viumbe vyote wakiwemo wanadamu wengine.

Jambo hili lifanyike bila kujali tunatendewaje na wengine. Ujumbe wa Uislamu ulienea huku na kule duniani kutokana na ukweli huu. Funzo jingine linalopatikana ni kuwa tusione haya kuwa waislamu.

Uislamu ndiyo neema kubwa kabisa ambayo kila mtu angepaswa kuwa nayo maishani mwake. Lazima tuwe na imani thabiti juu ya Allah na juu ya dini yetu. Tusijifiche majumbani kwa hofu ya bughudha ya wengine wala tusivuwe Hijab zetu kwa sababu hiyo.

Lazima tuwe washupavu, majasiri na tujitokeze kifua mbele kufikisha ujumbe wa Allah ulimwenguni kote kama walivyokuwa Mitume wote (rehema na amani ziwe juu yao).

Hatuna tunachopoteza tunapofanyiwa madhila, bali wanaotufanyia hayo ndio wanaodhulumu nafsi zao wenyewe. Wao ni wajinga wasiojuwa ukweli juu ya maisha haya ya muda ya dunia.

Ni wajibu wetu kujitahidi kuwaokoa wao wasiendelee kudhulumu nafsi zao wenyewe. Hii ndiyo kazi ya muumin na hapa ndipo yalipo mafanikio yake halisi.

MWISHO