BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM
FADHILA ZA QURANI
MWENYE KUSIKILIZA QUR'ANI
Imepokelewa kutoka kwa Mohammad bin bashiir [1] kutoka kwa Ali bin Hussen (a.s) na ameipokea hadithi hii kutoka kwa Abi Abdillah (a.s) amesema: Mwenye kusikiliza herufi moja ya kitabu cha Mwenyezi Mungu bila ya kusoma, Mwenyezi Mungu humuandikia jema moja na kumfutia kosa moja na kuinuliwa daraja moja, na mwenye kusoma kwa kuangalia bila ya kusali Mwenyezi Mungu humuandikia kwa kila herufi jema moja na kumfutia kosa moja na huinuliwa daraja moja, na mwenye kujifunza herufi moja ya dhahiri ya kitabu cha Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu humuandikia mema kumi na kumfutia makosa kumi na kuinuliwa daraja kumi, akasema:
Si semi kwa kila aya lakini kwa kila herufi sawa iwe baa au faa au mfano wa hizo, akasema: Na mwenye kusoma herufi moja hali ya kuwa amekaa kwenye sala, Mwenyezi Mungu humuandikia kwa kila herufi hiyo mema khamsini, na kumfutia makosa khamsini, na kumuinua daraja khamsini, na mwenye kusoma herufi moja hali ya kuwa amesimama kwenye sala yake, Mwenyezi Mungu humuandikia mema mia moja na kumfutia makosa mia moja na kumuinua daraja mia moja, na mwenye kuihitimisha, maombi yake ni yenye kukubaliwa, sawa yachelewe au yawahi akasema: Nikasema: Niwe fidia yako mwenye kuihitimisha yote? Akasema: Mwenye kuihitimisha yote.[2]
Na imepokelewa kutoka kwa Is'haq bin Ammar, kutoka kwa Abi Abdillah (a.s) amesema: Mwenye kusoma aya mia moja akisali kwa kisomo hicho kwa usiku mmoja Mwenyezi Mungu humuandikia kwa aya hizo kunuti za usiku na mwenye kusoma aya mia mbili tofauti na kwenye sala ya usiku Mwenyezi Mungu humuandikia kwenye lauhul mahfuudh mema yaliyo sawa na mali nyingi (qintwaar ) na qintwar ni kinaya ya mali nyingi, aukia miamoja, na awqiyah ni kubwa zaidi ya mlima wa Uhudi.[3]
Na imepokelewa kutoka kwa Anas amesema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w): Mwenye kusoma aya mia moja, hataandikwa miongoni mwa wenye kughafilika, na mwenye kusoma aya mia mbili huandikwa miongoni mwa wenye kunyenyekea na watiifu, na mwenye kusoma aya mia tatu Qur'ani haitamtolea hoja, yaani mwenye kuhifadhi kiwango hicho cha aya za Qur'ani, husemwa: Hakika mtoto amesoma Qur'ani: Kwa maana amehifadhi.[4]
SURATUL FAATIHA NA FADHILA ZAKE
Imepokelewa kutoka kwa Hassan bin Ali Al-akariy kutoka kwa baba zake (a.s) (katika hadithi) amesema: Hakika Faatihatul kitaab (yaani Al-hamdu) ni bora zaidi kuliko vilivyomo kwenye arshi (hadi akasema) fahamuni ya kuwa mwenye kuisoma kwa makusudi kabisa kwa ajili ya kumtawalisha Mohammad na Aali zake Mwenyezi Mungu atampa kwa kila herufi aisomayo ya sura hiyo jema moja na kila jema moja ni bora kwake kuliko dunia na yaliyomo ndani ya dunia hiyo kati ya mali za aina tofauti na kheri zake, na mwenye kumsikiliza msomaji akiisoma atakuwa na thawabu mfano wa msomaji, basi ni vema kila mmoja wenu kujilimbikizia kheri hizi zilizo nyingi.[5]
Na mepokelewa kutoka kwa Fudhaili bin Hassan At-twabrasiy (katika majmaul bayan) kutoka kwa Mtume (s.a.w) amesema: Ibada bora kabisa ni kusoma Qur'ani.[6]
Na imepokelewa kutoka kwake (a.s) ya kuwa amesema (katika hadithi): Hakika Qur'ani hii ni kamba ya Mwenyezi Mungu, nayo ni Nuru iliyo wazi na dawa yenye manufaa (hadi akasema): Basi isomeni, hakika Mwenyezi Mungu atakulipeni kwa kuisoma kwa kila herufi mema kumi, ama mimi sisemi ya kuwa Alif laam ni mema kumi lakini Alif ni mema kumi na laam ni kumi na miim ni mema kumi.[7]
Na imepokelewa kutoka kwake (a.s) ya kuwa amesema: Ataambiwa mwenye Qur'ani: Soma na upande juu na soma kwa tartiil kama ulivyo kuwa ukisoma duniani, hakika daraja yako ni mwisho wa aya uisomayo.[8]
Na imepokelewa kutoka kwake (a.s) amesema: Mwenye kusoma Qur'ani ni kama vile ameuweka utume pembezoni mwake ispokuwa ni kwamba yeye si mwenye kutelemshiwa wahyi.[9]
Na imepokelewa kutoka kwa Ahmad bin Fahdi (katika kitabu Uddatud-daaiy) kutoka kwa Mtume (s.a.w) amesema: Amesema Mwenyezi Mungu alie takasika: Mwenye kuacha kuniomba na kujishughulisha na kusoma Qur'ani nitampa thawabu bora zaidi za watu wenye kushukuru.[10]
MWENYE KUSOMA QUR'ANI KISHA AKAISAHAU
Imepokelewa kutoka kwa Abi Baswiir [11] amesema: Amesema Abu Abdillah (a.s) mwenye kusahau sura moja ya Qur'ani itamtokea ikiwa katika sura nzuri yenye kupendeza na itamjia ikiwa na sura ya daraja la juu kabisa peponi, pindi atakapo iona atasema: wewe ni nani? Uzuri ulioje ulio nao? Laiti unge kuwa wangu mimi, nayo itasema je hunifahamu? Mimi ni sura fulani na fulani na lau kama usinge nisahau ninge kuinua hadi mahala hapa.
Na imepokelewa kutoka kwa Yaakuub Al-ahmar, amesema: Nilimuuliza Aba Abdillahi (a.s): hakika mimi nina madeni mengi na hakika nimeingiwa na mambo ambayo huenda Qur'ani ikanikimbia na kunitoka, Abu Abdillah (a.s) akasema: Qur'ani Qur'ani hakika aya moja ya Qur'ani na sura ya Qur'ami itakuja siku ya kiama na zita panda hadi kwenye daraja elfu moja yaani peponi na zitasema lau kama unge tuhifadhi basi tunge kufikisha hapa kwenye daraja hii.[12]
Na imepokelewa kutoka kwa yaakub Al-ahman amesema: Nilimwambia Aba Abdillah (a.s) Niwe fidia yako hakika nimepatwa na mambo na hima, hakukubakia kheri yoyote isipokuwa sehemu fulani imeniponyoka na kunikimbia hata Qur'ani hakika sehemu yake fulani imeniponyoka na kunikimbia, akasema: basi akahuzunika na kufazaiaka kwa wakati huo pindi alipo taja Qur'ani kisha akasema: Hakika mwenye kusoma sura moja ya Qur'ani itamjia siku ya kiama na kumuangalia ikiwa kwenye daraja mojawapo kati ya daraja za peponi na itasema: Amani iwe juu yako, nae atasema:
Amani iwe juu yako pia, (yaani Assalaam alykum) wewe ni nani? Itasema: Mimi ni sura fulani na fulani ulinipoteza na kuniacha, ama lau kama unge shikamana na mimi ninge kufikisha kwenye daraja hili, kisha akaashiria kwa vidole vyake, kisha akasema:
Basi ni juu yenu kushikamana na Qur'ani jifunzeni Qur'ani hiyo hakika kati ya watu kuna wanao jifunza Qur'ani ili watu waseme fulani ni msomaji wa Qur'ani na kuna wanao jifunza Qur'ani hiyo na kuisoma kwa sauti au kuitafutia sauti ili watu waseme:
Fulani anasauti nzuri, na katika hayo hakuna kheri yoyote, na kuna wanao jifunza Qur'ani na kuitumia kusimama usiku na mchana na hamjali mwenye kuifahamu na asie ifahamu.[13] Na imepokelewa kutoka kwa Said bin Abdallah Al-aaraj amesema: Nilimuuliza Aba Abdillahi kuhusiana na mtu mwenye kusoma Qur'amni kisha akaisahau, kisha akaisoma na kuisahau, je kuna tatizo juu yake kwa kufanya hivyo? Akasema hapana.[14] Na riwaya iliyo pokelewa kutoka kwa Hussein bin Zaidi kutoka kwa Swaadiq (a.s) katika (hadithi ya makatazo) ya kuwa Mtume (s.a.w) alisema: Fahamuni ya kuwa mwenye kujifunza Qur'ani kisha akaisahau atakutana na Mwenyezi Mungu siku ya kiama akiwa amefungwa minyororo na Mwenyezi Mungu kumuwekea juu yake nyoka kwa kila aya aliyo isahau na kuwa ndie mwenza hadi motoni isipokuwa ikiwa atamsamehe. Makusudio yake ni kuwa ikiwa ataacha kutekeleza hukumu zake.[15]
MIONGONI MWA ADABU ZA KUSOMA QUR'ANI
Imepokelewa riwaya kutoka kwa Mohammad bin Fudhail kutoka kwa Abil Hassan (a.s) amesema: Nilimuuliza: Ninasoma msahafu (qur'ani) kisha ninabanwa na mkojo nikasimama nikakojoa na kustanji na kuosha mikono yangu na kurudi kusoma msahafu huo? Akasema: Hapana mpaka utawadhe kwa ajili ya sala.
Na katika kitabu Al-khiswaal imepokelewa kwa sanadi na upokezi wake kutoka kwa Ali (a.s) -katika hadithi ya mia nne- amesema: Asisome mmoja wenu Qur'ani ikiwa hayuko kwenye twahara mpaka ajitwaharishe.
Na imepkelewa kutoka kwa Ahmad bin Fahd katika kitabu (Uddatud-daiy) amesema: Amesema (a.s): Mwenye kusoma Qur'ani hali ya kuwa amesimama kwenye sala, anayo mema mia moja kwa kila herufi aisomayo, na akiisoma kwa kukaa anayo mema khamsini, na akiisoma hali ya kuwa ni mwenye twahara na akiwa kwenye sala, anayo mema ishirini na tano (25), na ikiwa kama hakuwa ni mwenye twahara atapata mema kumi (10), ama mimi sisemi ya kuwa (Alif laam miim) ni kumi, bali ninasema Alif ni kumi, na laam ni kumi, na miim ni kumi, na Ree ni kumi).
Na imepokelewa kutoka kwa Hassan bin Ali Al-askariy (a.s) katika tafsir yake amesema: Ama kauli yake ambayo alikuitia na kukuhimiza kuitekeleza na akakuamuru kuitekeleza wakati wa kusoma Qur'ani ni, Audhu billahis samiul aliim minash-shaitwanir rajiim, hakika Amirul muuminiin (a.s) amesema ya kwamba: Kauli yake Mwenyezi Mungu isemayo (Audhu billahi, yaani ninajizuilia na kujikinga kwa Mwenyezi Mungu-hadi akasema- na istiiadha ni kule kuamuru Mwenyezi Mungu waja wake wakati au pindi wanapo taka kusoka Qur'ani pale aliposema:
Na pindi utakapo taka kusoma Qur'ani basi jikinge kwa Mwenyezi Mungu kutokana na shetani alie laaniwa), na mwenye kufuata adabu ya Mwenyezi Mungu atampeleka na kumfikisha kwenye mafanikio ya milele na milele, kisha akataja hadithi ndefu kutoka kwa Mtume wa Allah (s.a.w) amesema kwenye hadithi hiyo: Ukitaka usipatwe na sharri yao (mashetani) na usipatwe au kufikwa na vitimbi vyao, basi sema unapo amka asubuhi: Audhu billahi minash-shaytwanir rajiim, hakika Mwenyezi Mungu atakulinda na kukukinga na sharri zao.
QUR'ANI NI AHADI YA MWENYEZI MUNGU BASI KUWENI NAYO WAKATI WOTE
Na imepokelewa kutoka kwa Harizi kutoka kwa Abi Abdillah (a.s) amesema: Qur'ani ni ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa viumbe wake kwa hiyo basi inampasa kila Muislaam aangalie kwenye ahadi yake na asome ahadi hiyo kwa kila siku aya khamsini. Na imepokelewa kutoka kwa Zuhriy amesema: nilimsikia Ali binil Hussen (a.s) akisema: Aya za Qur'ani ni hazina, kwa hivyo basi kila inapofunguliwa hazima inakupasa uangalie yaliyomo kwenye hazina hiyo.
Na imepokelewa kutoka kwa Muammar bin Khali, kutoka kwa Ridhaa (a.s) amesema: Nilimsikia akisema: Mtu anapo amka asubuhi inampasa baada ya kusoma nyuradi na dua baada ya sala asome aya khamsini (50).
Na imepokelewa kutoka kwa Abdul-aalaa Aali Saam, kutoka kwa Abi Abdillah (a.s) amesema ya kuwa: Nyumba ambayo huishi Muislaam na kusoma Qur'ani ndani yake huonekana kwa watu wa mbinguni kama nyota yenye kung'ara mbinguni ionekanavyo kwa watu wa Ardhini.
Na imepokelewa kutoka kwa ibnul-qaddah, kutoka kwa Abi Abdillah (a.s) amesema: Amesema Amirul muuminiin (a.s): Nyumba ambayo husomwa Qur'ani ndani yake na Mwenyezi Mungu alie takasika kutajwa ndani ya nyumba hiyo baraka zake hukithiri na malaika huja kwenye nyumba hiyo na mashetani kuiacha na kuikimbia, na huwaangazia watu wa mbinguni kama nyota ziwaangaziavyo watu wa ardhini, kwa hakika nyumba ambayo haisomwi ndani yake Qur'ani na wala hatajwi Mwenyezi Mungu alie takasika ndani yake basi baraka zake hupungua na malaika huikimbia na kuihama nyumba hiyo na huhudhuriwa na mashetani.
Na imepokelewa kutoka kwa Abi Abdillah (a.s), kutoka kwa baba yake (katika hadithi) amesema: Alikuwa akitukusanya na kutuamuru kumtaja Mwenyezi Mungu mpaka linapo chomoza jua na humuamrisha kusoma Qur'ani kila yule ambae alikuwa ni msomaji wa Qur'ani kati yetu, na yule ambae hakuwa msomaji kati yetu akimuamuru kuvuta au kusoma nyuradi, na nyumba ambayo husomwa Qurani ndani yake na hutajwa Mwenyezi Mungu ndani yake baraka zake huongezeka.
Na imepokelewa kutoka kwa Laythi bin Abi Saliim ameiinua kwa kusema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w): Yatieni nuru majumba yenu kwa kusoma Qur'ani na wala msiyafanye kama makaburi kama walivyo fanya Mayahudi na Wakiristo, wali salia kwenye Makanisa na Masinagogi na kuziacha nyumba zao, hakika nyumba inapo somewa sana ndani yake Qur'ani basi kheri zake huongezeka na kukithiri na watu wake kuongezeka na kupanuka, na huwaangazia watu wa mbinguni kama nyota ziwaangaziavyo watu wa duniani.
Na imepokelewa katika (Uddatud-daiy) kutoka kwa Ridhaa (a.s) akiinua hadi kwa Mtume (s.a.w) amesema: Ziwekeeni nyumba zenu sehemu fulani ya Qur'ani, hakika nyumba inaposomewa ndani yake Qur'ani basi huwa njema, nyepesi na pana kwa watu wake na kheri zake hukithiri na wakazi wake huongezeka wakati wote na kama haikusomwa Qur'ani ndani yake basi huwa finyu na mbaya kwa watu wake na kheri zake kuwachache (kupungua) na watu wake au wakazi wake huwa ni wenye kupungua.
MFANYA BIASHARA NA QUR'ANI
Imepokelewa kutoka kwa Fudhaili bin Yasaar kutoka kwa Abi Abdillah (a.s) amesema: Ni lipi linalo mzuia mfanya biashara miongoni mwenu anae shughulika katika soko lake pindi anapo rejea nyumbani kwake asilale mpaka asome sura moja ya Qur'ani, akaandikiwa kwa kila aya aisomayo mema kumi na kufutiwa makosa kumi.
Na imepokelewa kutoka kwa Saad bin Twaarif, kutoka kwa Abi Jaafar (a.s) amesema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w): Mwenye kusoma aya kumi usiku hataandikwa kati ya watu wenye kughafilika na mwenye kusoma aya khamsini huandikwa miongoni mwa wenye kumtaja Mwenyezi Mungu wakati wote, na mwenye kusoma aya mia moja huandikwa miongoni mwa wenye kumtii Mwenyezi Mungu na mwenye kusoma aya mia mbili huandikwa miongoni mwa wanyenyekevu na mwenye kusoma aya mia tatu huandikwa miongoni mwa wenye kufaulu na mwenye kusoma aya mia moja huandikwa miongoni mwa wenye kufanya kujitahi (kufanya jihadi) na mwenye kusoma aya elfu moja huandikiwa Qintwarah elfu kumi (sawa na elfu khmasini ya tembe za Dhahabu, na mithqaali ni sawa na Qintwar ishirini na nne na ndogo kabisa ni kama mlima wa uhudi na kubwa yake ni kati ya mbingu na Ardhi.
Na imepkelewa kutoka kwa Abi hamzah At-thamaliy, kutoka kwa Abi Jaarar (a.s) amesema: Mwenye kuhitimisha Qur'ani katika mji wa Makka kuanzia ijumaa hadi ijumaa au kwa siku chache ya hizo au zaidi ya hizo na akaihitimisha siku ya ijumaa Mwenyezi Mungu humuandikia malipo mema kuanzia ijumaa aliyokuwa duniani mpaka ijumaa ya mwisho atakayo kuwa duniani na ikiwa ataikhitimisha katika siku zingine ni vinyo hivyo. Na imepokelewa kutoka kwa Jaabir, kutoka kwa Abi Jaafar (a.s) amesema: kila kitu kina msimuwake wa kushamiri (Rabii'i) na msimu wa kushamiri Qur'ani ni mwezi wa Ramadhani.
KUSOMA QUR'ANI NDANI YA MSAHAFU
Imepokelewa kutoka kwa Yaakub bin Yaziid [16] ameiinua hadi kwa Abi Abdillahi (a.s) amesema: Mwenye kusoma Qur'ani katika msahafu hustareheshwa kwa macho yake kwa kuviona vitu vyenye kupendeza na wazazi kupunguziwa adhabu hata kama wote wawili watakuwa ni makafiri.
Na imepokelewa kutoka kwa Mtume (s.a.w) amesema: Hakuna kitu kilicho kikubwa na kigumu zaidi kwa shetani kuliko kusoma Qur'ani kwa kuangalia kwenye msahafu.[17]
Na imepokelewa kutoka kwa is'haq bin Ammar, kutoka kwa Abi Abdillah (a.s) amesema: Nilimwambia niwe fidia yako hakika mimi ninahifadhi Qur'ani kimoyomoyo, na kuisoma kimoyomoyo ni bora zaidi au kuisoma kwa kuangalia kwenye msahafu? Akasema: akaniambia bali isome na uangalie kwenye msahafu hilo ni bora zaidi je hufahamu ya kuwa kuangalia msahafuni ni ibada.[18] Na imepokelewa kutoka kwa Abi Dharri (katika hadithi) amesema: Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu akisema: Kumuangalia Ali bin Abi Twalib ni ibada na kuwaangalia wazazi wawili kwa huruma na upole ni ibada na kuangalia kwenye msahafu (kwenye kurasa za Qur'ani) ni ibada na kuiangalia Al-kaabah ni iabada.
Na imepokelewa kutoka kwa Hammad bin Issa, kutoka kwa Abi Abdillah (a.s), kutoka kwa baba yake amesema: Hakika ninafurahishwa na kupendezewa sana msahafu kuwa ndani ya nyumba na Mwenyezi Mungu kuwafukuza mashetani kwa msahafu huo.[19]
Na imepokelewa kutoka kwa Abi Abdillah (a.s) amesema: Vitu vitatu vitamshitakia Mwenyezi Mungu alie takasika: Msikiti ulio haribika na ambao hauswaliwi ndani yake na Watu wa msikiti huo, na mwanazuoni alie kati ya majahili na msahafu ulio tundikwa na umefunikwa au ulio jawa na vumbi na hausomewi msahafu huo.[20]
KUISOMA QUR'ANI KWA KISOMO CHA TARTIIL
Imepokelewa kutoka kwa Abi Abdillah bin Sulaiman[21] amesema: Nilimuuliza Aba Abdillah (a.s) kuhusiana na kauli ya Mwenyezi Mungu alie takasika isemayo:
ورتل القرآن ترتيلا [22]
akasema: Amesema Amirul muuminiin (a.s) Ameibainisha kwa uwazi kabisa na wala usiisome haraka haraka kwa kuikatakata kama mashairi na wala usiitawanye kama utawanyavyo mchanga lakini idonyoeni mioyo yenu kwa Qur'ani hiyo iliyo migumu na wala hima ya yeyote kati yenu isiwe mwisho mwa sura. Na imepokelewa kutoka kwa Saliim Al-farrai, kutoka kwa alie mhabarisha, kutoka kwa Aba Abdillah (a.s) amesema: Isomeni Qur'ani kwa kiarabu kwani Qur'ani ni kiarabu. [23] Na imepokelewa kutoka kwa Mohammad bin Fudhail amesema: Amesema Abu Abdillah (a.s): Ni makruh kusoma Qul-huwallahu ahad katika mpumuo mmoja.[24] Na imepokelewa kutoka kwa Abi Baswiir, kutoka kwa Abi Abdillah (a.s) kuhusiana na kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu:
ورتل القرآن ترتيلا
akasema: Tartiil ni kuisoma aya taratibu kwa kuipendezesha sauti yako. [25] Na imepokelewa kutoka kwa Ummu Salamah ya kuwa amesema: Mtume (a.s.w) katika usomaji wake alikuwa akikata kisomo chake kwa kusoma aya baada ya aya. Na imepokelewa kutoka kwa Ibn Abi Umayri, kutoka kwa alie itaja kutoka kwa Abi Abdillahi (a.s) amesema: Hakika Qur'ani imekuja kwa huzuni kwa hivyo basi isomeni kwa huzuni.[26]
Na imepokelewa kutoka kwa Abdallah bin Sinan, kutoka kwa Abi Abdillah (a.s) amesema: Hakika Mwenyezi Mungu alimteremshia wahyi Mussa bin Imran (a.s) akasema: Utakapo simama mbele yangu basi simama kisimamo cha mtu dhalili (mnyenyekevu au mnyonge) na muhitaji (fakiri) na pindi utakapo soma taurati basi nisikilizishe taurati hiyo kwa sauti yenye huzuni.[27] Na imepokelewa kutoka kwa Hafsi amesema: Sikumwona yeyote mwenye khofu zaidi juu ya nafsi yake kuliko Mussa bin Jaafar (a.s) na mtu mwenye matarajio zaidi kati ya watu kuliko yeye na usomaji (kisomo) wake ulikuwa ni wa huzuni, na pindi anapo soma ni kana kwamba anamzungumzia mtu fulani.[28]
KUSOMA QUR'ANI KWA SAUTI YA JUU NA KUISOMA KIMYAKIMYA
Imepokelewa kutoka kwa Saif bin Umayrah [29] kutoka kwa Mtu fulani, kutoka kwa Abi Jaafar (a.s) amesema: Mwenye kusoma Inna anzalnahu fii lailatil qadri kwa sauti kubwa au kwa sauti ya juu atakuwa kama yule ambae ameuchomoa upanga wake kwa ajili ya kupigana katika njia ya Mwenyezi Mungu, na mwenye kuisoma kimia kimia atakuwa kama yule alie tapakawa na damu yake katika njia ya Mwenyezi Mungu, na mwenye kuisoma mara kumi atapitiwa na msamaha wa madhambi elfu moja kati ya madhambi yake.
Na imepokelewa kutoka kwa Muawia bin Aammar amesema: Nilimwambia Abi Abdillah (a.s): Mtu ambae haoni kana kwamba amefanya chochote katika kusoma dua na Qur'ani mpaka ainue sauti yake, akasema: Hakuna shaka yoyote, hakika Ali bin Hussein (a.s) alikuwa ni mwenye sauti nzuri sana kati ya watu pindi anaposoma Qur'ani, na alikuwa akiinua au kupaza sauti yake pindi anapo soma Qur'ani mpaka watu wa nyumbani mwake wanasikia na kwamba Aba Jaafar (a.s) alikuwa ni mwenye sauti nzuri pindi anapo soma Qur'ani na alipokuwa akisimama usiku kwa ajili ya sala na kusoma Qur'ani alikuwa akisoma kwa sauti ya juu, na anapo pita mpita njia kati ya wauza maji au wachota maji na wengine husimama na kusikiliza usomaji wake.[30]
Na imepokelewa kutoka kwa Abi Dharri, kutoka kwa Mtume (s.a.w) katika usia wake amesema: Ewe Aba Dharri! Punguza sauti yako kwenye jeneza na wakati wa mapigano na wakati wa kusoma Qur'ani.[31]
Na imepokelewa kutoka kwa Abdallah bin Sinan, kutoka kwa Abi Abdillah (a.s) amesema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w): Someni Qur'ani kwa naghma za kiarabu na sauti zake na ole wenu na naghma za mafasiki na watu wenye madhambi makubwa, hakika watakuja watu baada yangu na kuisoma Qur'ani kwa sauti za nyimbo na sauti za kuomboleza na za kipadiri, haivuki Qur'ani hoyp kwenye mishipa yao ya shingo, nyoyo zao zimegeuzwa na nyoyo za wenye kupendezewa na sauti hizo ni kama wao. [32]
Na imepokelewa kutoka kwa Ali bin Mohammad An-nawfaliy, kutoka kwa Abil hassan (a.s) amesema: Nilitaja sauti nilipo kuwa mbele ya yake nae akasema: Hakika Ali bin Hussen (a.s) alikuwa akisoma na pengine alikuwa akipitiwa na mpita njia na kuzimia kutokana na uzuri wa sauti yake-Hadith. [33]
Na imepokelewa kutoka kwa Abdallah bin Sinan kutoka kwa Abi Abdillah (a.s) amesema: Amesema Mtuume wa Allah (s.a.w) kila kitu kina pambo lake na pambo la Qur'ani ni sauti nzuri.[34] Na imepokelewa kutoka kwa Hassan bin Abdallah At-tamiimiy, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa Imam Ridhaa (a.s) amesema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) ipambeni Qur'ani kwa sauti zenu hakika sauti nzuri huizidishia Qur'ani uzuri. [35]
ADABU ZA KUSOMA QUR'AN NA KUISIKILIZA
Imepokelewa kutoka kwa Jaabir [36] kutoka kwa Abi Abdillah (a.s) amesema: Nilisema: Hakika watu fulani linapo tajwa jambo lihusianalo na Qur'ani au aya fulani au ikizungumziwa Qur'ani mmoja wao hupigwa na butwaa (huzimia) mpaka hufikia hali ya kuwa hata mmoja wao akikatwa mkono wake au mguu wake hahisiii hali hiyo akasema: Utakasifu ni wa Mwenyezi Mungu hili ni katika shetani, hawakusifiwa kwa hilo bali wamesifiwa kwa ulaini (kuto kuwa wagumu wa nyoyo) uliaji na khofu.[37] Na imepokelewa kutoka kwa Abdillah bin Abi Yaafur, kutoka kwa Abi Abdillah (a.s) amesema: Nilimwambia: Mtu fulani akisoma Qur'ani je ni wajibu kwa mwenye kuisikia kunyamaza na kuisikiliza? Akasema: Ndio, inaposomwa mbele yako Qur'ani ni wajibu kwako kunyamaza na kusikiliza.[38]
Na imepokelewa kutoka kwa Ali bin Mughirah, kutoka kwa Abil Hassan (a.s) amesema: Nilimwambia: Hakika baba yangu alimuuliza babu yake kuhusiana na kuihitimisha Qur'ani katika kila usiku, babu yako akamwambia, katika kila usiku, akasema: katika mwezi wa Ramadhani, babu yako akamwambia: katika mwezi wa Ramadhani, babu yangu akamwambia, ndio kiasi utakacho weza, kwa hivyo baba yangu alikuwa akiihitimisha mara Arobaini (40), katika mwezi wa Ramadhani kisha nikaihitimisha baada ya baba yangu, na huenda nilizidi Arobain au nilipunguza kutokana na nafasi niliyo kuwa nayo na kutokana na shughuli zangu na uchangamfu nilio kuwa nao na uvivu, na inapofika siku ya iddil fitri huihitimisha kwa ajili ya Mtume, na Ali kumuwekea hitima yake na Fatuma (a.s) humhitimishia nyingine kisha huhitimisha kwa ajili ya maimam mpaka nikafika kwako na kukuwekea moja tangu nilipo kuwa katika hali hii, basi ninakitu gani kwa kufanya hivyo? Akasema: ulicho nacho kwa kufanya hivyo ni kuwa utakuwa pamoja nao siku ya kiama, nikasema: Allahu akbar mimi nina hilo (yaani nitakuwa pamoja nao)? Akasema: ndio mara tatu.[39]
Na imepokelewa kutoka kwa Sulaiman bin Khaalid, kutoka kwa Imam Swaadiq (a.s) amesema: Hakika Mtume (s.a.w) aliwajia vijana wa kianswari akasema: Hakika mimi ninataka kukusomeeni yeyote atakae lia basi anayo pepo, basi akaanza kusoma aya za mwishi mwa surat Zumar, hadi mwisho wa aya isemayo:
(وسيق الذ ين كفروا الي جهنم زمرا)
watu wote wakalia isipokuwa kijana mmoja akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu hakika nimejaribu kulia na kujiliza lakini macho yangu hayakutoa machozi, akasema:" Hakika mimi nitakusomeeni tena mwenye kujiliza anayo pepo, akasema akasoma tena watu wote wakalia na yule kijana akajiliza na wote wakaingia peponi. [40] Na imepokelewa kutoka kwa Jaafar bin Mohammad, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu zake (a.s) amesema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w): Jifunzeni Qur'ani kwa kiarabu chake……..[41]
Na imepokelewa kutoka kwa Salma, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa Abi Abdillah (a.s) amesema: Jifunzeni kiarabu kwani kiarabu ni maneno ya Mwenyezi Mungu ambayo amewazungumzia waja wake na kutamkwa na walio tangulia- Hadith.[42] Na imepokelewa katika kitabu (Uddatud-daaiy) kutoka kwa Abi Jaafar (a.s) amesema: Hawawi sawa watu wawili katika hadhi na dini kamwe isipokuwa mmoja wao atakuwa bora kwa Mwenyezi Mungu nae ni yule mwenye adabu zaidi kati yao, akasema: Nikasema hakika nimefahamu fadhila na ubora wake kwa watu katika kikao au mkusanyiko basi ni ipi fadhila yake kwa Mwenyezi Mungu? Akasema: Ni kusoma kwake Qur'ani kama ilivyo teremshwa na kuomba kwake kiasi kwamba hasemi maneno ya maombolezo wala huzuni kwani dua au maombi ya mwenye kuomboleza hayapandi na kumfikia Mwenyezi Mungu.
Na imepokelewa kutoka kwa Sukuniy kutoka kwa Abi Abdillah (a.s) amesema: Amesema Mtume wa Mwewnyezi Mungu (s.a.w): Hakika mtu asie kuwa muarabu kati ya umma wangu huisoma Quur'ani kwa lahaja yake na malaika kuiinua ikiwa kwenye kiarabu chake.
MAREJEO YA VITABU
[1]-Wasailush-shia:Kitabus-swalat, milango ya Qiraa'atul Qur'an, mlango wa 11/ h 6-12.
[2]- Wasailush-shia: Mujallad wa 6/188.
[3]- Wasailush-shia: Mujallad wa 6/138.
[4]- Wasailush-shia: Mujallad wa 6/190.
[5]- Wasailush-shia: Mujallad wa 6/190
[6]- Wasailush-shia: Mujallad wa 6/168.
[7]- Wasailush-shia: Mujallad wa 6/191.
[8]- Wasailush-shia: Mujallad wa 6/191.
[9]- Wasailush-shia: Mujallad wa 6/191.
[10]- Wasailush-shia: Mujallad wa 6/191.
[11]- Wasailush-shia:Kitabus-swalat, milango ya Qiraa'atul Qur'an, mlango wa 16/ h 2-8.
[12]- Al-kafiy: Mujallad wa 2/ 608.
[13]- Al-kafiy: Mujallad wa 2/ 608, mlango wa Manhafidhal Qur'ani, thumma nasiyahu.
[14]- Al-kafiy: Mujallad wa 2/ 633, mlango wa An-nawaadir.
[15]- Manlaa yahdhuruhul faqiih: Mujallad wa 4/ 11.
[16]- Wasailush-shia,Kitabus-swalat, milango ya Qiraa'atul Qur'ani, mlango wa 19/ na 20/ h 1-4.
[17]- Wasailush-shia: Mujallad wa 6/ 204.
[18]- Wasailush-shia: Mujallad wa 6/ 205.
[19]- Al-kafiy: Mujallad wa 2/ 613.
[20]-Al-kafiy: Mujallad wa 2/ 613.
[21]- Wasailush-shia,Kitabus-swalat,milango ya Qiraa'atul Qur'ani, mlango wa 21/ na 22/ h 1-5.
[22]- Suratul muzzamil aya ya 4.
[23]- Al-kafiy: Mujallad wa 2/ 615.
[24]- Al-kafiy: Mujallad wa 2 / 616.
[25]- Wasailush-shia: Mujallad wa 6/ 207
[26]- Al-kafiy: Mujallad wa 2/ 614.
[27]- Al-kafiy: Mujallad wa 2/ 606.
[28]- Al-kafiy: Mujallad wa 2/ 606.
[29]- Wasailush-shia,Kitabus-swalat,milango ya Qiraa'atul Qur'ani, mlango wa 23 h 1-3 na mlango wa 24 h 1-7.
[30]- Wasailush-shia: Mujallad wa 6/ 209, mlango wa Jawaazul-qiraa'ati sirran wa jahran.
[31]- Wasailush-shia: Mujallad wa 6/ 210, mlango wa Jawazu qiraa'ati sirran wa jahran.
[32]- Al-kafiy: Mujallad wa 2/ 614, mlango wa Tartiilil Qur'ani biswautin hasan.
[33]- Wasailush-shia: Mujallad wa 6/ 211, mlango wa Tahriimul ghinaa fiil- qur'an.
[34]- Al-kafiy: Mujallad wa 2/ 615, mlango wa Tartiilil Qur'ani biswautin hasan
[35]- Wasailush-shia: Mujallad wa 6/ 212, mlango wa Tahriimul-ghinaa fiil-Qur'ani.
[36]-Wasailush-shia,Kitabus-swalat, milango ya Qiraa'atul Qur'ani, mlango wa 25 h 1 na mlango wa 26 h 4 na mlango wa 28 h 1 na mlango wa 29 h 1.
[37]- Al-kafiy: Mujallad wa 2/ 616, mlango wa Fiiman yudhhirul ghashyaa inda qiraa'atil Qur'ani
[38]- Wasailush-shia: Mujallad wa 6/ 614.
[39]- Al-kafiy: Mujallad wa 2/ 618.
[40]- Wasailush-shia: Mujallad wa 6/ 219.
[41]-Wasailush-shia: Mujallad wa 6/ 220.
[42]-Wasailush-shia: Mujallad wa 5/ 84.
MWISHO