NGUZO ZA UHAKIKI WA DINI
  • Kichwa: NGUZO ZA UHAKIKI WA DINI
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 3:45:57 2-9-1403

 

BISMILAHI RAHMANI RAHIMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

NGUZO ZA UHAKIKI WA DINI

Uhakiki wa dini unapatiwa ufumbuzi kwa kuzingatia mikondo (mambo) mitatu. Taaluma ya ndani ya dini, taaluma ya nje ya dini, na utendaji wa amali.

Wahakiki wanaotaka kutambua uhakika na haki ya dini wanaweza kuitafiti dini na kuipatia ufumbuzi wake kupitia vigezo hivi vifuatavyo:-

- Kupitia elimu na taaluma ya nje ya dini, yaani kupitia misingi mikuu ya dini, (umbile la nje la dini).

- Kupitia elimu na taaluma ya ndani ya dini, yaani kuzingatia maamrisho, makatazo, hukumu mbali mbali n.k. (umbile la ndani la dini).

- Kuwa na elimu na taaluma katika kuyafanyia amali yote yaliyoamrishwa na Mwenyeezi Mungu kwa kuyafanyia amali kimwenendo na kimatendo, na kujiepusha na yale aliyoyakataza Mola Mtakatifu.

Basi wahakiki wote wanaotaka kuitambua dini inawalazimu kuitafuta dini kupitia mambo hayo matatu yaliyobainishwa hapo juu, mbali ya mambo hayo vile vile inawalazimu kuzingatia na kukuza fikra kiakili katika mambo yaliyomo ndani ya nafsi ya mwanaadamu, kwa sababu baadhi ya mambo ni ya kimaumbile na yanakuwa katika kila nafsi ya mwanaadamu. Kwa upande mwengine wahakiki wanatakiwa kuwa na elimu inayowapa taaluma katika utambuzi wa mambo, inayowapa utambuzi katika kumtambua mwanaadamu, na inayowapa utambuzi katika kutambua viumbe na mambo mbali mbali yanayohusiana na maisha yao, baada ya kupata taaluma hizo muhakiki anaweza kutalii mambo mbali mbali yanayohusiana na taaluma ya dini na elimu kwa ujumla.

Miongoni mwa mambo mengine ambayo wahakiki wa dini wanatakiwa kuyafanya, ni lazima kuuliza masuala mbali mbali yanayowajia akilini mwao wakati wanapofanya uhakiki wao, kila muhakiki anatakiwa kutafakari na kukubali au kupinga mambo kwa mujibu elimu aliyonayo na yale aliyoyatambua kupitia elimu hiyo, hivyo muhakiki anaweza kutoa fikra na mtazamo wake katika Nyanja mbali mbali na sio katika taaluma ya dini tu, muhakiki katika upingaji wa mambo ambayo ana elimu nayo anaweza kutoa fikra au nadharia mpya ambazo zinaweza kuiamsha jamii kifikra na kiakili.

Muhakiki ni lazima awe na hadafu maalumu katika shughuli zake za uhakiki, miongoni mwa hadafu hizo ni kutambua haki na ukweli wa mambo, ingawaje kuna umuhimu mkubwa utakaozingatiwa kutokana na nadharia za wahakiki.

kutokana na ukuwaji wa maendeleo katika dunia na jamii kwa ujumla, na kutokana na masuala au tata mbali mbali zinazotokea kwa sababu tofauti, kumeifanya jamii na watu wote kwa ujumla kutafakari na kukuza fikra zao ili kutambua mambo tofauti yanayowahusu wanaadamu au mambo mengine yoyote, hii imepelekea uwanja wa uhakiki kuenea na kusambazika siku hadi siku, na wahakiki wamekuwa wakifanya jitihada zao ili kupata jawabu ya masuala yao.

Ama ni lazima tuzingatie kuwa sio kila muhakiki anayeingia katika uwanja wa tahakiki ana malengo na hadafu njema katika uhakiki wake, hivyo sio vibaya kubainisha baadhi ya malengo au hadafu za wahakiki.

Jitihada za wahakiki zinaweza zikawa kwa ajili ya malengo na hadafu tofauti: -

-Baadhi ya wahakiki hufanya uhakiki wao kwa ajili ya kueneza na kusambaza ukoloni mambo leo, unaotoka katika mataifa makubwa wenye nia ya kutaka kuutawala ulimwengu kifikra na kiutamaduni.

-Baadhi ya wahakiki hufanya uhakiki wao kuhusiana na dini wakiwa na malengo ya kutaka kutambua ukweli na uhakika wa dini hiyo.

- Baadhi ya wahakiki huingia katika uwanja wa uhakiki wakiwa na malengo ya kuhujumu au kufosi fikra za watu na jamii kwa ujumla, wahakiki kama hao huwa na nia ya kuharibu fikra za watu na jamii kwa ujumla.

- Baadhi ya wahakika huingia katika uwanja wa tahakiki kutokana na udadisi walionao wa kutaka kutambua na kujua mambo tofauti yanayohusiana na dini au mambo mbali mbali.

-Baadhi ya wahakiki huingia katika uwanja wa uhakiki wakiwa na malengo ya kutaka kufahamu uhakika wa mambo na kujua jamii inataka mahitajio gani katika maisha yao, basi wahakiki hao hufanya jitihada zao zote ili kudhamini mahitajio yanayohitajiwa na wanaadamu.

-Baadhi ya wahakiki huingia katika uwanja wa tahakiki kwa ajili ya kuharibu na kuhujumu fikra za watu wenye dini, au walio na itikadi au imani ya dini fulani.

Hayo yalikuwa ni baadhi ya malengo tu ya wahakiki, hivyo ni wadhifa wa kila mtu mwenye fikra salama kuwa makini katika kutambua hadafu na malengo ya uhakiki wake.


MWISHO